Habari

Bomani amekonga nyoyo za Wazanzibari

Na Abdallah Vuai, Zanzibar

Posted Jumatano,Julai3 2013

Wiki iliyopita, Zanzibar ilipata ugeni mzito wa Mwanasheria Mkuu wa kwanza mzalendo,Tanzania,Jaji mstaafu Mark Bomani ambaye alifika Zanzibar kuungana na wananchi wengine katika kutoa uzoefu wake, maoni yake kuhusu mchakato wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ujio wake uliwafurahisha wengi,hususan vijana waliokuwa wamesheheni katika ukumbi wa Salama pale Hoteli ya Bwawani kumsikiliza mtaalam huyo katika sheria.

Kwa hakika kila aliyefika siku ile aliweza kukubali uwezo,busara,hekima ya Jaji mstaafu Bomani katika kukabili hadhira.

Hakuzunguka, hakutafunamaneno,hakujizonga,alikuwa muwazi, mkweli aliyezikonga nyoyo za Wazanzibari pale alipotamka kuwa mfumo wa muundo wa Muungano unaweza pia kuwa wa mkataba.

“Serikali ya mkataba inawezekana ikiwa watu wanaotaka hilo, si jambo la ajabu, kitu muhimu ni watu wakae kitako kuamua nini wanataka,wasiburuzwe au kufungwa mikono” Alifafanua Jaji Bomani alipokuwa akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na washiriki wa kongamano lililoandaliwa na kamati ya maridhiano Zanzibar.

Furaha katika ukumbi, wapo walioruka ruka,wengine walifikia hata kutamka kuwa Jaji amemaliza kazi. Kwa hakika kongamano lile lilitosha kumvua chui ngozi ya kondooo.

Nini hasa Jaji mstaafu Mark Bomani aliwaambia Wazanzibari?

“Muungano hautakufa kwa kuwa na Serikalitatu(Tanganyika, Zanzibar na ya Muungano),lakini unaweza kufa kwa sababu ya watu wenye tamaa na masilahi binafsi wasiojali wananchi,” alisema Jaji Bomani.

Ubinafsi wa baadhi ya wanasiasa umetugharimu kwenye maendeleo,ufisadi unalalamikiwa na wananchi. Naungana na Mzee Bomani kulizungumzia hili la ubinafsi kuwa ni donda sugu katika siasa za Tanzania.

Hapa Zanzibar tunaendelea kuona kwenye mchakato wa katiba baadhi ya watu na hasa wanasiasa wakichukua ubinafsi kuwa ni muelekeo Sahihi wa kutoa maoni kwenye mchakato wa kupata katiba mpya.

Ndio pale Mzee Bomani alipotamka kwamba Muungano hautakufa kwa kuwa na mfumo wa muundo wa Serikali tatu,ila tamaa ya baadhi ya wanasiasa,maslahi ubinafsi wasiojali wananchi inaweza kuwa sababu ya kuvunjika kwa Muungano.

Jaji mstaafu Bomani amefafanua kwa kina mfumo wa muundo wa Muungano wa Serikali tatu kuwa mbali ya kudumisha kwa kuwa na nguzo imara katika Muungano wetu,lakini pia hauna gharama zaidi ya kupunguza gharama ambazo zipo hivi sasa.

Wananchi waliowengi wanakubaliana na hoja za Mzee Bomani kwamba mifumo miwili, ya Serikali moja,mbili haina nafasi kwenye kizazi cha leo na hata cha baadae.

Kimsingi,mfumo wa Serikali mbili umethibitisha udhaifu katika utekelezaji wake na Watanzania hususan Wazanzibari sasa wanauzoefu wa miaka hamsini ya mazonge ya mfumo huo uliozalisha kero za Muungano.

Jaji Bomani amesema kwamba kwa mtazamo wake, mfumo wa kuwa na Serikali tatu ndio muafaka. “Mfumo wa Serikali moja hauna uwezekano…ili lilibainisha miaka 50 iliyopita,mfumo wa Serikali ndio hivyo tumejionea matatizo na kero zake na ubishi usiokwisha”.

Naam, zimeundwa Tume na Kamati zilizoongozwa na Majaji na watu wenye kuheshimika hapa nchini kuangalia utatuzi wa kero za Muungano,lakini hazikuweza kuzaa matunda,malalamiko yamezidi katika kila upande wa Muungano huu,Zanzibar na Tanganyika.

Bila shaka wengi wanakubali dhana ya mfumo wa Serikali tatu katika Muungano wetu kuwa zitaondoa yale malalamiko sugu yaliyoshindikana katika kipindi cha takriban miaka hamsini sasa.

Mabadiliko ya mfumo wa muundo wa Muungano ni suala lisiloweza kuepukika,hatuwezi kukwepa ukweli wa udhaifu wa muundo wetu tulionao,tunahitaji mfumo madhubuti,tusiogope mabadiliko ni hali ya mwanadamu kupitia vipindi tofauti katika maisha.

Wimbi la Serikali tatu kwa sasa ni kubwa unahitaji kuwa na chombo imara kwani wimbi hilo la tufani linalotishia kulivunja Jahazi la mhafidhina ambapo kwa sasa mabaharia wake wameanza kuweweseka baada ya jitihada nyingi za kuwakatisha tamaa wataka mageuzi kutozaa matunda

Vuguvugu la kutaka mabadiliko kwa kuwa na mfumo wa muundo wa Muungano wa Serikali tatu siyo tu kwa Zanzibar bali ni Tanzania halikamatiki tena, hakuna njia mbadala wala hekima inayoweza kuwatuliza wananchi zaidi ya kukubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba kupendekeza Serikali tatu katika Muungano wetu.

Kizazi cha leo na hata cha baadae cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kitaendelea kuwaheshimu wazee makini wa aina ya Jaji Marki Bomani ambao hawakutaka kujizonga,hawakutaka kuficha uchafu kwenye zuria.

Mwanasheria Bomani ataingia kwenye kumbukumbu ya watu waliosimama imara katika kutetea mfumo wa muundo wa Serikali tatu,lakini hakusita kueleza hisia zake kwamba hafungiki na wazo moja,ikiwa wananchi watataka mfumo fulani hakuna budi kukubali matakwa yao.Alisema serikali tatu zitatoa nafasi kwa kila nchi mwanachama kuendesha mambo yake jinsi wananchi wake wanavyotaka.Jaji Bomani alisema ni vigumu kuunda mfumo wa muundo wa Muungano ambao utamfanya mdogo kuwa na hofu.

“Kwa kuondoa shaka hiyo, tuwe na Serikali tatu, ya Zanzibar,ya Tanganyika zote zikiwa na madaraka kamili na kwa kuwa sisi ni wamoja lazima tuwe na kitu kinachotuunganisha nacho

Aidha, alishauri mjadala wa kupata katiba mpya uwe huru, wananchi wafungue mioyo yao,wasifungwe na mawazo au itikadi fulani na badala yake kila mmoja atoe alichonacho moyoni

Mwananchi

Share: