Ama kweli, sikio la kufa……….

Written by  //  06/09/2010  //  Habari  //  1 Comment

Na. B.OLE,

Wakati nikiwa mdogo nilikuwa nikihangaika na kufuatilia sana kutaka kujua baadhi ya methali na maana zake, mara nyingi zilikuwa nikifikiri maana tofauti na hatimae kuniumiza kichwa bila kujua nichukue tafsiri gani, lakini kwa sababu mapenzi yangu yalilenga huko na Waswahili walisema kipendacho moyo hula nyama mbichi, kwa maaana hiyo nilikaza kamba ili na mimi nifahamu siri ya methali na umuhimu wake katika maisha ya kila siku. Wale watu wa Fasihi hawatosita kuonyesha nyoyo zao za bashasha huku wakitabasamu kwa haiba njema yenye kuvutia, ikiashiria njozi njema na baraka nyingi nyusoni mwao.

Licha kwamba ilibidi niwe Mwanafunzi mtiifu na mpole ili nifaidike kwa kile nilichokikusudia kwani sote tunaelewa kwamba mtaka cha mvunguni sharti ainame kinyume chake itakuwa sio rahisi kufanikiwa, kuna wakati hali ilikuwa ngumu lakini sikusita kumfuata Mwalimu wangu ambae alifarijika kila uchao pale anaponiona nanyatia nyatia katika anga zake , kwani alikuwa anajua kwamba atachemsha bongo kwa masuali kede wa kede kutoka Mwanafunzi wake lakini kwake yeye hayakuwa maudhi bali ilikuwa ni furaha na sherehe isiyo kikomo kwake.

Mwisho wa yote nilifahamu kwamba methali zinajukumu kubwa katika jamii yetu ,zinafunza, zinaadabisha na zinatoa changa moto ndani ya jamii kwa wale wanaojua maana kwani asie jua maana haambiwi maana.Hapa tunapata hekima na mafunzo mbali mbali katika jamii zetu.

Leo hii nimekumbuka hii methali inayosema ”Sikio la kufa halisikii dawa” basi imenikumbusha mbali tokea enzi zile za utotoni wakati nikikumbatia mabuku yangu, huku kibaridi nyororo kikipuuliza na majani yakiyumbayumba kama vile yamechelewa kuchanua wakati kijua kinachomoza kwa chati kuashiria asubuhi njema. Nakwezea suruali yangu ya kaki na kukimbilia shule na umande ili nisichelewe na kupata fimbo asubuhi ile yenye kila mahaba na mapenzi kwa Wanaadam.

Lakini wakati nafikiria methali hii ghafla moja nimeanza kubadilika na nikaona nitowe kalamu yangu nianze kuihakiki ili nijikumbushie ya zamani kwani ”old is gold”. Huzuni zimenishika baada ya kupata taaswira mzima ya jamii yangu na si nyengine ni” Wazanzibar” machozi yameanza kunilengalenga na kunitiririka mithili ya bomba ya maji yanayomwaika, huku damu ikinichemka kama vile maji moto kwenye birika ya umeme na mama hakuchelewa kuingia wasi wasi alfajiri hii kulikoni ? baada ya kusikia sauti yenye mguno unayoashiria masikitiko ya moyoni.

Sikusita kumueleza kile kinachonisibu moyoni kwamba si chochote bali ni hii hali tuliyonayo Zanzibar hivi sasa , kuna wenzetu hii hali hawaioni au vipi ? nahisi sote tunaielewa na inatugusa lakini kwa nini wengine wafurahie mama ? Je wao si Wazanzibar na kama ni Wazanzibar hawaumii na hii hali inayoendelea visiwani.

Ni kweli Mwanangu lakini tutafanya nini na wenzetu hata ukiwapigia zumari basi hawageuzi migongo yao kuangalia nyuma au mbele yao kwamba kunakuja kitu gani.

Sikuwa na sumile kumtupia suala la haraka haraka hivi Wazee wangu mulifikiria kwamba iko siku Mzanzibar atakuwa muombaji, mkimbizi,Mzanzibar atakimbia visiwani,biashara itapotea, udugu utakufa,urafiki na usahiba utapotea!,fitina, kejeli, kibri, kebeh zitatawala nyoyoni mwa watu ziwe nyimbo zinaimbwa mitaani!,mabaa ya ulevi ndio sehemu za kupumzikia!,wizi na rushwa litakuwa ni jambo la kawaida!,haki itapingwa kwa bei yeyote!, batili ndio utakuwa utu!, uongo ndio furaha ya wengine!,udanganyifu ndio ibada!,wachache watavaa makoti ya uongozi wawatese wengine!, ubaguzi na uonevu utashamiri !, njaa na maradhi iwe fahari ya wanyonge!, thamani ya dini kupotea na kuonekana kama ni usanii!, wenyeji kuwa wageni katika visiwa vyao!,rasilimali zetu kuwa zao na maamuzi ya nyumba yetu kuamuliwa kwa jirani !,wenye elimu kuonekana wajinga!, Nchi yetu kuonekana na wao si nchi!, Mama kulikoni nini ? kweli haya yanajuzu kwetu sisi ? mbona wamefika mbali.

Mama yote haya yanamuandama Mzanzibar kama vile mtoto wa kambo. Kinachonishangaza na kunisikitisha ni kwamba kuna baadhi miongoni mwetu tunayafurahia haya kama vile hatuna macho basi hata kusikia tumekuwa viziwi ?tunapiga vigeregere wala ngoma hatujaiona hatujui ni sherehe ya nani na wengine hata kualikwa hawakualikwa hivi Wazanzibar tutafika na sisi tuishi kama Wanaadam, mama naomba unijibu.

Tumekaa kwenye uwanda,jua kali tunapiga mayowe sema baba,sema baba, wambie hao, lakini kiumbe huyu hana hata mkate wake na watoto nyumbani, hana kazi, pesa ya matibabu ni mfalme, makaazi yake funika kombe, elimu usiseme mtoto wake haendi shule hana daftari wala kalamu, jamani hivi tutafika mbona tunazidi kuingia porini.

Halafu anakuja Gabachori anavaa kaniki la uongozi anatwambia mumeyaona maendeleo basi munichague niwaongoze ili mupate maendeleo zaidi,bila hisia wala kujali kwamba tayari wameshatuburuza miaka nenda, miaka rudi hadithi na nyimbo ni hizo hizo kila siku, kama hilo halitoshi sasa wanataka watumalize mpaka huu utu wetu sasa wanataka kuufanya kwamba hauna kwao, kisa na mkasa wenzetu wanapata mafupa wanabebenya lakini hata nyama hayana.Ama kweli jirani yetu mbaya mbuzi wote wale alionao anatokwa roho na huyu beberu mmoja, ama kwel;i mambo mengine kinehe.

Mara nikashtuka nilifikiria nilikuwa nimelala naota kumbe niko macho mama ananitazama bila kuamini macho yake na mimi sikuchukua muda nikakumbuka ile methali niliofundishwa shule kwamba sikio la kufa halisikii…………..

One Comment on "Ama kweli, sikio la kufa………."

  1. awammy 06/09/2010 kwa 5:08 um ·

    pole! pole mwanangu haya yote yatakwisha bado kama miezi hii,miwili tu! mwanangu.Wala usiwe na wasiwasi hawatumalizi tushaamka na hao wa vigelegele watanyamaza tu,usijali mwanangu.Hata na mm mzee wako natamani siku hiyoo umalize kwani mwanangu, nitaweka historia ya kufika nusu ya huo unaotutesa!, unaujua ni nn?muungano!!!
    Ahsante kwa utumiaji wako wa tamathali za semi. Mwana ngu we mkali!!!

Comments are now closed for this article.