Habari

CCM Yahoji Serikali Ya Umoja Zanzibar

Na Mwinyi Sadallah – Mwananchi

Posted Jumatatu Mei 5, 2014 saa 4:15 asubuhi (10:15AM)

MNADHIMU wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Salmin Awadh Salmin (CCM) amesema wawakilishi wa CCM wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza hilo, ili kuwapa nafasi wananchi waulizwe iwapo wanataka kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), au la.

Akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho ulioongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana kwenye Viwanja vya Kibandamaiti, Unguja jana, Salmin alisema wajumbe hao wamefikia hatua hiyo kwa kuwa wanaona kwamba lengo na matumaini ya kuundwa kwake yamefutika na hayana dalili njema katika siku za usoni.

Alisema ni vyema wananchi wakaulizwa kama bado wanautaka mfumo huo au ule wa zamani urejeshwe.Salmin Awadh Salmin ni mwakilishi wa Magomeni, Unguja.

“Kitendo cha viongozi tuliounda nao umoja wa kitaifa kupinga Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar hakivumiliki, tunaona ipo haja kila upande ubaki na msimamo wake kuliko kujenga urafiki wa mashaka,” alisema Salmin.

Alimwomba Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuunga mkono hoja hiyo itakapowasilishwa ili kutoa nafasi mpya ya kidemokrasia kwa wananchi wake kujua kama wanataka mfumo wa sasa au wa zamani.

Wazo hilo liliungwa mkono na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ambaye alisema ni jambo muhimu kuitishwa kura ya maoni ili wananchi wapate nafasi ya kuulizwa kama wanataka mfumo wa Serikali iliyopo au la kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu mwakani.

Kinana amshukia Maalim

Awali, Kinana alisema kwa miaka 20 tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad amekuwa akiwayumbisha Wazanzibari kutokana na tabia yake ya kubadilisha ajenda za kisiasa na kutikisa misingi ya umoja wa kitaifa nchini.

Alisema tabia ya kiongozi huyo imekuwa haifahamiki na haijulikani anatafuta jambo gani licha ya kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa mwaka 2010 na CCM na CUF.

Alisema kwa msingi huo, tabia ya kiongozi huyo mbali na kuonekana kutaka kuzorotesha misingi ya umoja wa kitaifa pia imekuwa ikichafua siasa za Zanzibar na Muungano na kuwataka wananchi kuwa macho hasa katika mjadala wa Katiba unaoendelea nchini.

“Tabia ya Maalim Seif haifahamiki, ni bingwa wa kubadilisha ajenda za kisiasa mara kwa mara akiwayumbisha wananchi. Tokea kuanzisha vyama vingi, ameshabadili ajenda zaidi ya 20, amewaacha wananchi hawajui washike lipi na waamini jambo gani,” alisema.

Alisema Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano lazima ipatikane kwa njia ya amani na isiwe kichocheo cha watu kung’oana macho au kutoana ngeu na kwamba mabadiliko ya katiba si mwarobaini wa maendeleo. Alisema mataifa mengi yamewahi kuandika katiba mpya na bado kuna kero za wananchi.

Aliwataka wabunge na wawakilishi wa CCM kukaa pamoja na kutafakari kwa kina jinsi ya kuondosha kero zinazolalamikiwa na wananchi wa Zanzibar na kuipa Zanzibar nafasi pana ili ijiimarishe kiuchumi..

Tagsslider
Share: