Habari

CCM yaanza kukabiliana na ukosefu wa ajira Zanzibar

NA MWINYI SADALLAH
18th May 2013

Chama cha Mapinduzi (CCM), visiwani hapa,  kimeanza kukusanya takwimu za vijana wasiokuwa na kazi kwa lengo la  kuandaa mipango ya  kuwajengea uwezo ili kuwawezesha kujiajiri wenyewe.

Mpango huo umetangazwa na viongozi wa Jumuiya za  CCM za Umoja wa Vijana ( UVCCM) , Umoja wa Wanawake (UWT) na ile ya  Wazazi walipozungumza na wanahabari mjini Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Amour Shaka, alisema takwimu hizo zitakusanywa kutoka  mikoa mbalimbali bila kujali itikadi ya chama kwa vile umaskini unawaumiza vijana bila ya kujali  vyama vya kisiasa.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema tatizo kubwa linaloikabili Zanzibar ni kukosekana tafiti za kutambua vijana wasiokuwa na ajira na kuwawekea mazingira ya kutumia fursa za sekta binafsi kujiajiri.

Alisema serikali imeanzisha mifuko ya kuwasaidia wajasiriamali wakiwamo vijana na kuwataka kutumia nafasi  hiyo ambayo imelenga kupambana na umaskini.

Naibu Katibu Mkuu wa UWT Salama Aboud Talib,  alisema ziara ya Rais wa Zanzibar Dk . Ali Mohamed Shein ya  mwezi  uliopita  katika mikoa sita ya kichama  ya Zanzibar imesaidia kuwaelimisha vijana kuhusu mpango wa kujiajiri kupitia sekta binafsi.

Alisema iwapo vijana watajengewa njia bora ya kutumia fursa ya sekta binafsi, mpango wa kukuza uchumi na kupambana na umaskini utafikiwa kwa wakati  visiwani Zanzibar.

Tatizo la ajira Zanzibar limekuwa na mjadala mpana na kuelezwa kuwa ndiyo chanzo cha vijana wengi kujiingiza kwenye uhalifu na utumiaji wa dawa za kulevya.

CHANZO: NIPASHE
Share: