CCM yatoa mwelekeo wa sera 2010-2020
Chama Cha Mapinduzi kimetoa mwelekeo wa sera zake kwa kipindi cha 2010 hadi 2020, ambapo mageuzi ya mfumo wa elimu yatakayotoa nafasi kwa sayansi na teknolojia kuingizwa katika mfumo rasmi yamepewa kipaumbele.
Hayo yalisemwa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Kingunge Ngombare-Mwiru, wakati akiwasilisha taarifa ya mwelekeo huo kwa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliomalizika jana mjini hapa.
Akisoma mwelekeo huo, Kingunge alisema hakuna mafanikio katika sekta za maendeleo yanayoweza kufikiwa, pasipo kuwepo mfumo bora wa elimu unaotoa kipaumbele kwa sayansi na teknolojia.
Kingunge alisema viashiria vya maendeleo nchini vinaonyesha kuwa uchumi wa Tanzania bado unategemea kilimo ambacho hata hivyo, kinatekelezwa kwa kutumia teknolojia duni na isiyoendana na wakati.
Alisema utekelezaji wa mwelekeo huo unaoainishwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2010 hadi 2015, utailazimu wizara husika kufanya marekebisho ya mfumo wa elimu.
Alisema hivi sasa kuna mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo, na kutoa mfano wa ongezeko la wanafunzi katika shule za msingi, sekondari, vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu.
Pia, alisema yapo mambo ambayo hayakuwekwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2005-2010, kama vile ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom). Alisema chuo hicho ni matokeo ya ubunifu na dhamira ya Rais Jakaya Kikwete.
Kuhusu mageuzi ya kilimo, alisema mwelekeo unaeleza katika utoaji wa elimu ili kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata maarifa yatakayoboresha utendaji kazi wao.
Alisema mwelekeo huo unatoa mkazo kwa uongezaji thamani ya mazao kupitia uzalishaji viwandani.
Pia, alisema suala la upatikanaji wa nishati ya uhakika iliyo nyenzo muhimu katika kuboresha kuboresha uzalishaji na kukuza uchumi pia limeanishwa kwenye mwekeo huo.
Kwa mujibu wa Kingunge, miongoni mwa rasilimali hizo ni maji, makaa ya mawe, gesi na madini ya uranium ambayo Tanzania inashika nafasi ya saba duniani.
Alisema mwelekeo huo unatoa fursa ya uboreshaji miundombinu ikiwemo barabara, bandari, reli na viwanja vya ndege.
Hata hivyo, alionya kuwa kama jitihada za kutumia vema miundombinu hiyo hasa bandari zisipotekelezwa, kuna hatari ya nchi zenye bandari katika ukanda wa Afrika, zinaweza kuchukua biashara zinazopitia kwenye bandari zilizopo nchini.
Kingunge alisema katika utekelezaji wa sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, mwelekeo umetoa nafasi ya utoaji elimu kwa umma, kuhusu namna bora ya kufanya biashara.
Alisema hivi sasa kuna upungufu wa elimu na maarifa kwa umma, katika kushiriki shughuli za kiuchumi ili wapate tija.
Kingunge alisema mpango huo utahusisha pia mareboresho ya elimu kwa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ili kuwawezesha wahitimu wake kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.
Alisema utekelezaji wa mwelekeo huo utategemea ushiriki wa serikali, CCM na wananchi.
Alitoa mfano kuwa uboreshaji wa kilimo cha kisasa hauwezi kufanikiwa ikiwa viongozi na wanachama wa CCM hawatashiriki.





