Habari

CUF WEEKLY REPORT: 17/4/2017

CUF WEEKLY REPORT: 17/4/2017

MATAWI YA CHAMA MKOA DAR ES SALAAM YAMTAKA LIPUMBA KUONDOKA OFISI KUU BUGURUNI KWA HIARI KABLA HAWAJATUMIA NGUVU YA UMMA:

THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF–Chama Cha Wananchi)

THE DIRECTORATE OF INFORMATION, PUBLICITY AND PUBLIC RELATION:

TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA MUHIMU ZA WIKI TAREHE 10-17 APRIL, 2017

Hii ni wiki ya saba (11) sasa kukuletea mukhtasari wa taarifa muhimu juu ya masuala mbalimbali kwa lengo la kuwajulisha wanachama, viongozi na watanzania wote kwa ujumla yanayoendelea ndani ya CUF na kuwekana sawia kwa kuwapa “Updates” na aidha kusahihisha taarifa za upotoshwaji, hujuma na au propaganda chafu dhidi ya Chama (CUF Weekly Report).

KURUGENZI YA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA WIKI HII INAWAJULISHA TAARIFA ZIFUATAZO:-

1. KATIBU MKUU, MAALIM SEIF AKAMILISHA ZIARA YA SIKU 10 KISIWANI UNGUJA, WANA-CUF WAMUHAKIKISHIA WAKO TAYARI KUKILINDA CHAMA CHAO:
Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, amekamilisha ziara yake ya siku kumi katika kisiwa cha Unguja. Ziara hiyo iliyoanza Tarehe 1 Aprili, 2017 katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ imekamilika Alkhamis, Tarehe 13 Aprili, 2017 kwa kufanyika kwa kikao cha majumuisho na tathmini katika ofisi ya CUF Kilimahewa Wilaya ya Mjini-Unguja. Ziara hiyo imepata mafanikio makubwa na kufikia malengo yaliyowekwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF. Miongoni mwa kazi alizofanya katika ziara hiyo ni pamoja na kukabidhi majukumu ya kwa waratibu wa Chama, ambapo kwa jumla ya waratibu 4,727 walipatikana, ofisi za Chama zilizinduliwa, mawe ya msingi katika maeneo 6 yaliwekwa, Barza 14 zilizinduliwa na kufungua majengo 6 ya Chama yaliyokamilika, na kukabidhiwa viwanja viwili (2) kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Chama. Wanachama wapya 591 walijiunga na CUF miongoni mwao 124 walikuwa wana-CCM. Katika kuhitimisha ziara hiyo Chama kiliwapatia Nishani maalum wanawake saba (7) walio mstari wa mbele kutumia rasilimali zao kwa ajili ya chama. Aidha, Katibu Mkuu alipata fursa ya kuwajulia hali wagonjwa, kuwafariji wafiwa na kuwapa pole wananchi mbali mbali waliopata matatizo katika maeneo yote aliyoyatembelea. Miongoni mwa ishara za mapenzi waliyonayo wananchi kwa Maalim Seif Sharif Hamad ni zawadi walizomtunukia wakati wa ziara yake. Mbali na zawadi alizokabidhiwa ikiwa ni pamoja na mapambo ya nyumbani, vyakula, mavazi, vifaa vya ofisi, vifaa vya kufanyia ibada, mifugo na Nishani mbali mbali kama sehemu ya kutambua mchango wake na kazi kubwa aliyoifanya katika kukipigania Chama, kuleta na kustawisha demokrasia nchini Tanzania, baadhi ya wananchi walitoa maeneo yao ya ardhi na kumpatia Maalim Seif Sharif Hamad ili ajenge makaazi yake na kuishi karibu na wananchi hao. Hissham Abdukadir Afisa Habari, Makao Makuu, Mtendeni Zanzibar.

Katika hatua nyingine Jumuiya za Chama cha CUF; JUKECUF, JUVICUF na wilaya mbalimbali nchini zimempongeza Katibu Mkuu kwa Hotuba na ujumbe murua alioutoa wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Tarehe 9/4/2017 katika ukumbi wa Ramada Encore, Viongozi hao wakiongozwa na Mhe. Fatma Fereji –Mwenyekiti wa JUKECUF-Taifa walisema wapo tayari kukabiliana na njama zote ovu dhidi ya CUF na Viongozi wake na kwamba watakilinda Chama kwa gharama zozote zile.

2. a) WABUNGE WA CUF WAFANYA ZIARA WILAYA YA KONDOA KUIMARISHA
CHAMA:
Katika utaratibu waliojiwekea kila wiki wakiwa Bungeni Dodoma kufanya ziara za kuimarisha Chama kwa wilaya mbalimbali nchini, kwa niaba ya wenzao Mhe.Masoud Abdallah Salim (Mtambile), Mhe.Saumu Sakala (Viti Maalum), Mhe.Twahir Awezu Mohamed (Mkoani), Mhe.Juma kombo Hamad (Wingwi), Mhe.Mbarouk Salim Ali (Wete) na Mhe.Mussa Mbarouk (Tanga) wameendelea na Programu hiyo kwa kufanya ziara katika wilaya ya Kondoa. Wakiwa Kondoa walikutana na kufanya vikao na Viongozi wa Kata, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji Wilaya pamoja na Madiwani wa CUF na kuweka ratiba ya kuwafikia wanachama wengi zaidi. Katika muendelezo wa Ziara hizo Wilaya/Mikoa itakayofikiwa hivi Karibuni ni Pamoja na Morogoro Mjini, Tanga, Pangani, Shinyanga, Nyamagana Na Ilemela-Mwanza, Lindi Na Tabora. Wabunge wa CUF wamekuwa Ngangari kuhakikisha kuwa Chama chao kinaendelea kuwa Imara na Salama kutoka mikononi mwa Wasaliti na Vibaraka wa CCM.

b) WABUNGE WA CCM WAMSHANGAA MAFTAHA NACHUMA, ASHINDWA KUJENGA HOJA ZINAZOELEWEKA;
Wabunge wa CUF watoka nje ya ukumbi baada ya Maftaha Nachuma kupewa nafasi kuchangia Bungeni Dodoma wiki iliyopita. Anakataa kuwa Jaji Francis Mutungi ndiye aliyetoa barua za kumtambua Lipumba. Wakati Mtungi ameandika katika barua yake amepokea majina ya wajumbe 216 wakilalamika, Nachuma anasema wajumbe 324 ndio walioandika barua na kusaini. Ukaguzi wa majina hayo ulipofanyika zaidi ya majina 74 yamejirudia na saini zake kugushiwa. Wajumbe wa Mkutano Mkuu walikuwa 700. Lipumba hajakataliwa na Maalim Seif, amekataliwa na wajumbe 476 wa Mkutano Mkuu, na baadae kuvuliwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa. Lipumba alijiuzulu mwenyewe kwa hiari yake. Wajumbe 116 kutoka Zanzibar ni wajumbe halali kwa mujibu wa katiba ya Chama Ibara ya 78 (1) (t) ni wajumbe waliokuwepo tangu mwaka 2014 (kukidhi asilimia 30 ya wanawake katika ngazi za maamuzi) na walishiriki kumchagua hata LIpumba kuwa Mwenyekiti wa Chama taifa kwa wakati huo. Si wajumbe wapya. Msajili kuvilea vyama vya siasa haimaanishi kuingilia maamuzi ya vikao halali. Wajumbe 484 hawakupeleka malalamiko kwa Msajili. Akaunti za wilaya zimefungwa na Bodi ya Wadhamini ya CUF kutokana na wizi wa shilingi milioni 369 uliofanyika kwa kutumia akaunti ya wilaya ya CUF Temeke, Tawi la NMB Temeke. Wabunge wa CCM baada ya kumsikiliza baadhi yao wakaanza kuzomea na kumtaka azungumzie ajenda iliyowasilishwa mezani.

3. TAARIFA YA KESI ZA CHAMA:
a) Shauri la msingi namba 23/2016 lililopo kwa Jaji Kihiyo dhidi ya Msajili Jaji Francis Mutungi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Lipumba na wenzake limepangwa kutajwa tena Tarehe 24/4/2017. Taratibu za kisheria kuomba mapitio (Revision) mbele ya Mahakama ya Rufaa zimekamilika.
b) Shauri la wizi wa fedha za Ruzuku limepangwa kusikilizwa Tarehe 20/4/2017 kuhusu zuio la Lipumba na wenzake kupewa fedha za Ruzuku. Na Tarehe 24/4/2017 shauri la Msingi mbele ya Mheshimiwa Jaji Dyansobera. WANACHAMA WOTE TUNATAKIWA TUJITOKEZE KWA WINGI MAHAKAMANI KUHUDHURIA KESI HII KWA TAREHE TAJWA HAPO JUU.

4. MATAWI YA CHAMA DAR ES SALAAM YAMTAKA LIPUMBA KUONDOKA
OFISINI BUGURUNI KWA HIARI KABLA HAWAJATUMIA NGUVU YA UMMA:
Viongozi wa Matawi ya CUF, KOSSOVO, CHECHNIA, OPEC na Mengineyo zaidi ya 50 yaliyopo Kinondoni/Ubungo-Dar es Salaam yamefanya mkutano na waandishi wa Habari na kumtaka Lipumba kuachia ofisi ya Buguruni kwa njia ya amani. Viongozi hao wa matawi waliunga mkono hotuba ya Katibu mkuu, Maalim Seif aliyoitoa wiki iliyopita Ramada Encore. Maalim Seif ataanza Ziara ya Dar es Salaam hivi karibuni, na kuzindua Kamati ya Uratibu Mkoa wa Dar es Salaam itakayoongozwa na Majemedari.

5. MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA MHE. SALIM BIMANI AWAPOKEA MADIWANI WA UKAWA MTENDENI, ZANZIBAR:
Leo tarehe 17/4/2017 Mhe. Salim Bimani aliwapokea madiwani wa UKAWA Dar es Salaam ambao wapo kisiwani Unguja kwa mapumziko ya Pasaka. Madiwani hao walimuhakikishia Mkurugenzi wa Habari kuwa wapo pamoja na CUF na wataendelea kuunga mkono juhudi za kudai Haki na Demokrasia ya kweli nchini. Madiwani hao wameshangazwa sana na Msomi wa Uchumi Lipumba kukubali kutumika kuleta sintofahamu ndani ya CUF/UKAWA bila ya sababu za msingi. Wamedai kuwa kiongozi lazima awe na uoni wa mbali (Visionary Leader) jambo ambalo Lipumba amepoteza sifa hiyo. Inaonekana amezungurukwa na watu wenye uwezo mdogo wa kuyafikiria mambo na waliotanguliza maslahi yao binafsi. Wamshauri Lipumba kupumzika siasa. Kati ya madiwani 27 wa CUF Mkoa wa Dar es Salaam ni madiwani wawili tu ndio wanamuunga mkono Lipumba.

HAKI SAWA KWA WOTE

———————————————-
MBARALA MAHARAGANDE
NMHUMU
MAWASILIANO: 0784 001 408/0715 062 577

Nakala ya kieletroniki -softcopy ya Katiba ya Chama -1992 (toleo la 2014) inapatikana: WhatsApp 0715 062577 or maharagande@gmail.com

FB

Share: