Habari

CUF ya Lipumba yadai itamzuia Maalim Seif

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akiwa na baadhi ya viongozi na walinzi wake wa Chama na Serikali kwenye moja ya maeneo ya mjini Unguja katika ziara yake ya Unguja mjini, iliyomalizika wiki hii.

Elizaberth Zaya – Nipasehe
14 Aprili 2017

KURUGENZI ya Ulinzi ya Chama cha Wananchi (CUF), upande wa Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, imedai itazuia ziara za Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ambazo amepanga kufanya Dar es Salaam, ikiwa hataishirikisha kurugenzi  hiyo kwa ajili ya ulinzi.

Kurugenzi hiyo imetoa tamko hilo siku chache baada ya Maalim Seif kusema anakusudia kufanya ziara wakati wowote katika mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kurugenzi ya CUF Bara, Athuman Hamad alidai kwa mujibu wa katiba ya CUF, kiongozi yeyote wa chama hicho anapofanya mikutano lazima alindwe na walinzi wa chama.

Alidai wameapa kukilinda chama na wako tayari kumlinda Maalim Seif katika ziara zake, lakini anatakiwa afuate utaratibu kwa kupitia ofisi za chama na kuwashirikisha walinzi wa chama.

Alisema ni vema Maalim Self akaondoa hofu na kufika katika ofisi hizo kwa ajili ya kuendelea na shughuli zake kama kawaida na wao wako tayari kumlinda kama wanavyofanya kwa viongozi wengine.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Bara, Masoud Omari alidai chama chao hakiendeshwi kiholela, hivyo hawawezi kumruhusu Maalim Seif kufanya ziara bila ya walinzi wa chama.

Nipashe lilipomuuliza  Ofisa Habari na Mawasiliano wa chama hicho  Zanzibar, Hisham Abdukadir alisema ziara za Maalim Seif zitafanyika kama zitakavyopangwa na kamati husika kwa mujibu na taratibu za chama na hakuna wa kuzuia.

Alisema ratiba ya ziara za Maalim Seif kwa upande wa Tanzania Bara inatarajiwa kutolewa wakati wowote baada ya kumalizika kwa tathmini ya ziara zake alizozifanya Zanzibar (Pemba na Unguja).

“Ratiba ya ziara za Katibu Mkuu zilipangwa kufanyika Bara baada ya kumalizika kwa ziara zake alizokuwa anazifanya upande wa Zanzibar, ambazo zilimalizika jana (juzi),” alisema na kuongeza:

“Kwa hivyo kinachofanyika kwa sasa ni tathmini na baada ya hapo itatolewa ratiba ya ziara zake wakati wowote kwa upande wa Tanzania Bara na zitafanyika kama zitakavyopangwa,” alisema Abdulkadir.

Share: