Habari

Cuf yaungana na wanaokosoa mchakato wa Katiba mpya

17th May 2013

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kinaungana na Watanzania walioonyesha shaka juu ya mchakato wa kupata Katiba mpya kwani hakioni nia njema na utayari wa Tume kuwa na Katiba inayotokana na maoni ya wananchi.

Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Irahim Lipumba, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao cha baraza kuu la chama hicho kitaifa.

Alitaka  Rasimu ya Katiba inayoandaliwa iwekwe hadharani kwa wakati ili wananchi waweze kutoa maoni yao kabla haijapelekwa katika Bunge la Katiba na kupigiwa kuwa na wananchi.

Alisema Cuf hakitakuwa tayari kuiunga mkono Katiba ambayo haitakuwa na misingi imara ya kidemokrasia na isiyotokana na maoni ya Watanzania na kitakuwa tayari kuwahamasisha kuikataa katiba hiyo.

Profesa Lipumba ameitaka tume ya kuratibu ukusanyaji wa maoni kuweka mpango wa kuyafikia makundi yenye mahitaji maalumu ikiwa ni wanawake, walemavu, vijana na asasi za kiraia zinazoshughulika na malezi ya watoto ili yaweze kutoa maoni yao.

Alisema pamoja na mchakato wa uandikaji wa katiba kupangiwa miezi 18 muda huo  hautoshi  kwani kuna chaguzi mbalimbali ambazo zinatarajiwa kufanyika mwakani hivyo hakuna sababu za msingi za kuharakisha zoezi hilo na kupata katiba mbovu isiyokidhi matakwa ya wananchi na badala yake kupata katiba ya matakwa ya kikundi kidogo cha watu wenye dhamana.

CHANZO: NIPASHE
Share: