HabariMakala/Tahariri

DHANA NI KITU KIBAYA, LAKINI KUENEZA TAARIFA USIZO NA UHAKIKA NAZO NI KUBAYA ZAIDI!

TAFAKURI YA BABU.

DHANA NI KITU KIBAYA, LAKINI KUENEZA TAARIFA USIZO NA UHAKIKA NAZO NI KUBAYA ZAIDI!

Na Said Miraji

Ni kweli Abdu Rahman kwamba kumeenea uvumi huo kwamba eti nimeombwa au nimeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar! Binafsi nimepigiwa simu na kuulizwa juu ya jambo hili na nimemshuhudia mtu akinon’gona na swahiba zangu kuwaeleza haya mbele ya uso wangu na alipoondoka nikajuilishwa kuhusu taarifa hizo! Isipokua, siwezi kuwalaumu wale wote walio, wanao na watakao zusha chochote kuhusu maisha yangu hasa ya kisiasa zaidi ya kuwahurumia kwa sababu hawanijui na yawezekana wanatamani kuonekana mbele ya jamii kuwa wananifahamu, jambo ambalo si kweli.
Mimi ni mtu wa misimamo (Principles) na katika maisha yangu yote ya kisiasa sikujali kupoteza marafiki kwa kumchungia murua mtu, waliowahi kufanya kazi nami hili wanalielewa, siwezi kubadili msimamo wangu kwa kua fulani amesema nini au fulani anataka hivi ama vile zaidi ni kwamba naweza kubadilika pale tuu utakapo nidhihirishia kwa hoja kua msimamo wangu si sahihi na ninapogundua jambo hilo sioni aibu wala tabu kubadilika mradi niwe na hoja madhubuti na thabiti katika kufanya maamuzi yangu.

Mimi ni mtu nilietolea maisha yangu marefu katika kupigania haki ya Zanzibar na wazanzibari bila ya tamaa ya kupata malipo yoyote na huo ni msimamo ambao kwangu hauwezi kubadilika milele hata iwapo nitakua katika chama tofauti na CUF, niliishi na msimamo huu kabla ya CUF, nikaishi nao ndani ya CUF, na nimekua naishi nao sasa nje ya CUF na msimamo huo ndio ulionifanya kutofautiana na baadhi ya watu ndani ya ADC.

Wanaodhani kwamba naweza kununulika wajiulize kwa nilivyokua ndani ya CUF lau ningelitaka umaarufu nisingelipata? lau ningelitaka cheo nisingelipata? lau ningelitaka fedha kwa kua ama mbunge au mwakilishi nisingelipata? Lakini katika maisha yangu yote ndani ya CUF sikuwahi kugombea hata udiwani zaidi ya uongozi ndani ya chama ambao haukua na mshahara.
Nimekua kiongozi wa daraja ya juu ndani ya CUF kwa kipindi kirefu mno, nilikuwa Mkurugenzi wa vijana taifa, ambapo wakati huo chama kilikabidhiwa vijana na mimi nikiwa kiongozi wao alie kikabidhi alikua Maalim Seif kwa wakati huo akiwa ndie Makamu Mwenyekiti wa CUF Taifa, kwa heshima nilipohamishiwa katika idara ya Blue guards chama kikakabidhiwa BG nikiwa kiongozi wao, aliekikabidhi alikua Profesa I.H.Lipumba ambae alikua ndie Mwenyekiti taifa kwa wakati huo, nimekua katibu wa kamati ya ulinzi na usalama taifa ndani ya CUF hadi nilipojiuzulu mwenyewe na kadhalika, yote hayo yalifanyika kutokana na imani waliyokuwa nayo viongozi na wanachama wa CUF kwangu, hivi ilikua bado nini kwangu ndani ya CUF?

Nimeitoa nafsi yangu mara kadhaa katika kupigania umma kwa waliokua ndani ya CUF wanaelewa haya, vigingi nilivyopita mimi ni vigumu kupata wa kunifanananisha nae ndani ya CUF.

Kupigwa hadi kutangaziwa kufa,kuwekwa ndani mara kadhaa (jela), kuzuiwa kutoka nje ya mkoa wa DSM na mahakama kwa zaidi ya miaka miwili na nusu na kutengwa na familia yangu, na mengine mengi mazito ambayo kimsingi hayawezi kufidiwa au kulipika (Ku-compensation).

Yote hayo yalikua ni kwa ajili ya kuwapigania wanyonge ndani ya nchi hii na hasa wazanzibari, nilifikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi zote za uongozi ndani ya CUF, baada ya kutokuridhishwa na mwenendo wa chama na nilipoondoka katika uongozi ndani ya CUF, hakuna aliejua maana sikupiga kelele, na kwa imani waliyokuwa nayo viongozi wangu miaka miwili baadae tokea nilipo jiuzulu waliniomba kushiriki nao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 huku nikitwishwa jukumu zito la kua meneja wa kampeni, kushindana mikakati na watu kama kina Abdulrahman Kinana, ambae kwa wakati ule alikua ni Meneja wa kampeni wa CCM.
Baraza kuu la CUF kwa ujumla wao waliniamini kunipa jukumu hilo nikiwa nje ya uongozi wa chama kwa muda mrefu nami nikalipokea na kulitekeleza. Nilipo maliza nikarudi katika shughuli zangu pamoja na baadhi ya viongozi na wanachama kuniomba nirudi katika uongozi sikukubali sababu yaliyonifanya niondoke katika uongozi wa CUF niliona kuwa bado yapo.

Baadae tulianzisha ADC, pamoja na tofauti za kimtazamo na kiitikadi bado uongozi na wana CUF walidiriki kunialika hadi katika mkutano wao mkuu uliofanyika pale Ubungo Plaza na kuamini kunipa kiriri (Plat form) ili nihutubu nami nikafanya hivyo wala hatukutofautiana na naamini walishangazwa na hotuba niliyoitoa siku ile, siasa si uhasama!
Nikiwa kiongozi wa ADC na hata nilipoachana na ADC, bado sikukata mawasiliano na wahisani wangu ambao wako CUF akiwemo Profesa Lipumba mtu ambae tunaheshimiana sana hadi leo, Maalim Seif Sharif ambae kisiasa kwangu ni mtu ninaemuamini na kumkubali kuliko mwanasiasa yoyote Tanzania, pamoja na kwamba kama binaadamu ana mapungufu yake, na kwa sababu hio ndio maana anapokosea sisiti kumsema.

Jambo ambalo wengi hawawezi kuliamini ni kwamba hata katika mgogoro huu wa CUF unaoendelea nimewahi kukutana na Maalim faragha kwa takriban dakika 55 kwa mazungumzo maalum, kadhalika nilitaka kufanya hivyo kwa Profesa Lipumba na nikamfata hadi ofisini Buguruni, nikakuta akiwa kwenye kikao nae akanipigia simu siku hio usiku karibu saa nne na nusu baada ya kupewa taarifa ya kwamba nilimfuata, Profesa aliahidi kua atanitafuta lakini wakati ule kulikua na pirika za uchaguzi katika kata mbali mbali na tokea muda huo hajatulia, nami sikuwepo nyumbani, ila naamini kwamba akipata wasaa atanitafuta tuu na akinitafuta nitakwenda kwa roho safi.

Yote haya ni kwa ajili ya kuona mzozo huu hauwaathiri wanyonge usio wahusu na hili ni jukumu letu kama wadau kuwashauri wahusika badala ya kuwachochea.

Mara kadhaa nimekua nikiwaonya siri na dhahiri baadhi ya watu niwajuao wanao watukana na kuwakashifu viongozi wa CUF mitandaoni eti kwa sababu hawako katika mtazamo mmoja na hili kwa kweli sio tuu halisaidii katika kutuliza munkar wa mgogoro huu, bali linaonyesha ni kwa kiasi gani chama hiki cha CUF kilivyoingiliwa na watu wabaya kwa kutumia kisingizio cha mgogoro uliopo, nao wanakamilisha mipango yao katika kuua demokrasia, kwani wanajua fika kwamba CUF ni taasisi imara na ikibogojoka upinzani utatepetepwa pia!
Nimekua nikisoma maendeleo ya mgogoro wa wanaCUf kupitia vyombo mbali mbali vya habari na mitandao ya kijamii kwa kipindi kirefu bila ya kujihusisha nao hata pale ambapo ningeliweza kunena jambo nilinyamaa kimya kusudi kulinda heshima yangu, wapo walio nijumuisha (kuni-tag) katika makala zao humu sura kitabu (Face book) japokua wengine siwajui na wala sijawahi hata kuwaona lakini niliwaheshimu na katu sikujibizana nao, wengine nilizuilia maandiko yao angalau yasitokee katika ukurasa wangu tuu bila ya kuwambia neno kwa sababu sikufurahishwa na maneno yao makali, ya jeuri, laana na matusi kwa watu ambao nawaheshimu, kwangu mimi kumtusi mtu kama Maalim Seif au Profesa Lipumba bila kosa hadharani ni aibu.
Kwa kitendo hicho wapo walio nidhania niko na hawa ama wale, leo nimesikia na kuona fuku fuku, tetesi, minon’gono na hata wengine kunipigia simu na kunieleza kinaga ubaga kwa mitazamo tofauti kwamba eti nimeombwa na Profesa Lipumba kuwa Naibu katibu mkuu wa CUF! Wengine wakifurahishwa na wengine wakihuzunika.
Akili za kuambiwa changanya na zako, kwani ni lini nimekua tena mwanachama wa CUF? Mimi ni mwanasiasa huru nisie na chama chochote, hivyo siwezi kugombea uongozi wala kuteuliwa kuwa kiongozi wa chama chochote nchini na iwapo nahitaji kujiunga na chama chochote kile nikiamua nitaujulisha umma ili uelewe, wala sina haja ya kupitia mlango wa nyuma! Na hili naamini uongozi wa CUF katika makundi yote mawili wanalielewa.

Nilipoondoka CUF pamoja na matatizo yake niliiacha ikiwa moja tena yenye nguvu, natamani kuiona ikirudi kuwa moja iliyo imara na sio vipande vipande ili kuwaenzi walio ifia na wanao itesekea.
Hivyo wale wanaoeneza uvumi huu yawapasa kutambua kua uongo wao hauna mashiko maana mimi si mwanachama wa chama chochote na sishabikii mpasuko uliopo katika CUF kwa vyovyote vile maana jambo hilo kwangu halina tija yoyote.

Zaidi ni kwamba kwa mtazamo wangu ni kua CUF imegawanyika sehemu kubwa mbili hivyo kwa mtu kama mimi siwezi katu, kukubali kujiingiza katika mgogoro ambao haunihusu ndewe wala sikio na kujifanya ni sehemu yake, ninachoweza kufanya ikiwa hapana budi ni kusaidia ikiwezekana kutafuta ufumbuzi wa tatizo liliopo na sio kuwa sehemu ya tatizo hilo!

Nawaheshimu wote waliofanya maamuzi yao kuhusiana na mgogoro huu kwa kuonyesha kushabikia upande fulani lakini hilo si suluhisho linaloweza kuwasadia maelfu ya watu waliopoteza maisha yao, walio dhalilika, waliopoteza mali zao, waliopatwa na ulemavu, waliofungwa magerezani, walioondokewa na wapendwa wao, waliotumia sehemu ya mali na wakati wao kwa CUF na kadhalika kwa ajili ya CUF hii ambayo leo wanaifia tena kwa peresha ya mpasuko huku wengine wakiumizana na kumwagana damu, kwa ajili ya Maalim Seif, kwa ajili ya Profesa Lipumba au kiongozi mwengine yoyote, hii si sawa kabisa!

Mimi binafsi ni mmoja kati ya viongozi ambao tuliwaongoza wanaCUF kwa kipindi kirefu ambapo wakati wa uongozi wetu walifikwa ma maafa mengi, hivi niwaulize wenzangu katika CUF mmesha yasahau haya?
Mimi si kiongozi katika CUF lakini hapana asieujua mchango wangu ndani ya CUF, muna nini wana CUF? Geukeni mtazame nyuma, jiangalieni mlipo kisha muangalie na mbele muendako iwapo kuna ukweli ndani ya nafsi zenu kwa haya mnayoyasema nyinyi viongozi kwa watu wenu kwani ni lazima mgombanie madaraka? Ivi hamuwezi kuwatetea watu hadi muwe viongozi wa kugombana na kuwapiganisha wao kwa wao? Mmesha sahau jukumu la kudai haki za wanachama na wananchi ambalo walikupeni?

Niko tayarai sana kuisaidia CUF lakini sio vikundi ndani ya CUF.
Abdul Rahman, nakushukuru sana kwa uungwana wako wa kulisikia jambo hili ukuamua kuniuliza mwenyewe tena hadarani badala ya kufanya kama wafanyavyo wengine kulivalia njuga na kusambaza uongo.

Ahsante sana.

FB

Share: