Bwana Msa na urafiki wa magari

Written by  //  29/10/2009  //  DIRA  //  Zima maoni

Na Muhammed Said Abdallah

Bwana Msa alikuwa kasimama dirishani, anachungulia. Nje, gari ndogo imesimama mlangoni kwa jirani yake, na dereva wake kakaa juu ya daraja ya kupandia, watoto wameizunguka, wanafanya ghasia.

Bwana Msa akatulia kimya anatazama tu. Sasa, ukimwona Bwana Msa kakaa kimya, ujuwe akili yake inakwenda kama sinema, na yale mambo hafifu ambayo watu wengine huona upuuzi, kwake yeye humsawirikia mambo mengine mapya. Kwa methali, daima alikuwa akiona katika akili yake, kuwa upo urafiki mkubwa baina ya binaadamu na magari, siku zile. Maana aliona kama urafiki unakuja kwa mazoea basi watu wamezoea basi watu wamezoeana sana na magari. Ilimtulikia Bwana Msa kwamba miaka mingi imepita tangu magari yalipoanza kuingia mjini na watu wakajua raha yao . Hata halafu yake watu wakayazoea, ikawa mtu hawezi kwenda shamba wala kurudi mjini ila kwa gari. Sasa, hapa hapa mjini, Bwana Msa aliona watu wamechaga kutembea na magari, na maadam wanatembea nayo namna hiyo, basi yamekuwa ndio rafiki zao.

Yeye Bwana Msa mwenyewe alikuwa na rafiki zake vile vile: Najum na Ahmed. Na wao kila siku, huja kumchukua wakatembea. Wakifika mlangoni, humpigia kelele, Ëeyha!”naye huitikia Öhhi” kwa sababu marafiki hawachaguliani majina. Lakini hakuweza kujua kama mambo hayo ya usuhuba, ya kuitana majina ovyo ovyo, yapo vile vile katika suhuba yetu ya magari. Maana ikiwa gari na sisi ni marafiki kweli kweli, kama alivyodhani yeye, basi ruli hii lazima iwepo.

Nje, watoto walikuwa katika ghasia zao wameizunguka gari, na dereva alikuwa kasimama karibu na gari lake. Sauti mbili, tatu za kike zilitoka nyumbani kwa jirani zake. Dereva alipiga honi mara mbili; na bibi mmoja ndani alijibu, “Bee! Nakuja!”

Bwana Msa aliruka kwa ghafla, kama mtu aliyestuka usingizini, akaacha kuchungulia. Hata mkewe aliyeingia chumbani wakati ule alistaajabu na akamsikia mumewe akisema, Älaa! Kumbe!” Mkewe alimwuliza nini; lakini badili ya kumjibu, alijitupa kochini kisha akasema, “Ngojea nikufanyie mtihani kidogo”. Lipo swala moja nataka kukuuliza na ukilijibu umepasi. Unajua kwa nini dereva akapiga honi?

Mkewe alijibu rohoni mwake kuwa Bwana Msa umekwisha mjia uhsindani wake wa kilalamishi wa kupindua maneno juu chini, lakini aliona bora kumrai. Akajaribu kujibu kierevu – na huku anajua kuwa aliambiwa sivyo – “Swala lako ni rahisi sana . Labda dereva kachoka kungojea, naye ana haraka, basi kapiga honi kumhimiza huyu bibi, jirani yetu; anakwenda arusini leo, Mwembetanga.”

Bwana Msa alicheka kicheko kikubwa. Kisha akasema “Sijapata kuona dereva mwenye haraka hata mmoja. Kwani “haraka ,” nini? – haraka maana yake “Kwenda mbio.”Ukimtazama dereva, daima utamwona katulia tuli ndani ya gari lake, kazi yake kuifungulia iende naye mbio; na mtu anayekaa kimya, ijapokuwa ni dereva, lakini haendi mbio. Kwa hivyo dereva hana haraka; yeye na abiria wake sawaswa.

Wala haina haja ya kusema kuwa madereva hawakai kutwa ndani ya magari, yao , ila wanapoendesha tu, maana mimi nakwamabia dereva maadam haendeshi gari basi si dereva tena, huwa mtu tu.Lakini dereva kabisa hana haraka. Haraka imo katika gari na hasa katika magurudumu yake. Hebu chungulia nje, yatazame magurudumu ya gari yalivyokaa.

Kwa nini umbo la gurudumu lisiwe la pembe tatu? Au kwa nini lisinyoke kwa urefu? Gurudumu limefanywa kuwa duara makusudi lipite likizuguka upesi upesi majiani. Sasa, haraka iko kwa dereva anayekaa katika gari, au katika gari leneywe? Tazama tena. Kama dereva angekuwa na haraka asingepiga honi, bali angepiga hodi akamwomba abiria wake afanye chapu chapu, maana ana haraka.

Lakini hakufanya hivyo kabisa. Yeye kapiga honi tu kumjuvya abiria wake kwamba “rafiki” yake tayari anamngoja nje; nasi tulivyozoeana na gari, ilipoitwa “Pwom! Pwom!”tu, yule bibi mara alitambua jina alilopewa na rafiki yake, naye akitikia, “bee! Nakuja!”

Makala haya yamechapishwa kutoka Jarida la Mazungumzo ya Walimu katika miaka ya 1948.

Comments are closed.