Kumuomba radhi binaadamu mwenzako
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 29/10/2009 // DIRA // 1 Comment
Na Aboud Maalim
JANA tulizungumza juu ya mtu kutoogopa kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu kwa makosa aliyoyafanya. Asihisi mtu kafanya makosa akaona aibu ya kuyabeba makosa yale kwenda kwa Mwenyezi Mungu kuomba maghfira.
Tukasema namna gani kwa ushahidi wa aya mbali mbali na hadithi za Mtume namna Mwenyezi Mungu alivyo mwepesi sana kuwasamehe waja wake waliomkosea, alumuradi tu kwanza wakubali wamekosa; pili, wakubali Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye uwezo wa kuwasamehe na kuwakubalia toba zao.
Lakini hakuna ugumu wa Mwenyezi Mungu kusamehe, kwa sababu Mwenyezi Mungu hafaidiki na kitu kwa kumtesa mja wake, wala hapungukiwi na chochote kwa kumpa thawabu mja wake. Mtume (SAW) anasema:
Mwenyezi Mungu yuko tayari kupokea toba ya mja wake muda wa kwamba ile roho haijafika milingano ya kutoka (balaghat l’hulkuk). Haijafika, akaomba dua ya msamaha, atapata tu msahama. Jinsi alivyokuwa karimu Mwenyezi Mungu. Sasa tusiogope..
Lakini kama hivyo ndivyo, Mwenyezi Mungu mwepesi kiasi hicho wa kusamehe, anahimiza waja wake waliomkosea waende kwake kuomba msamaha, na sisi tunabaki na matumaini tukiomba msamaha tutakubaliwa, basi wajibu na wewe kujifunza kuwasamehe waliokukosea.
Tumesema huko nyuma katika mazungumzo yetu jambo moja gumu ni mwanadamu kutekeleza agizo la Mwenyezi Mungu kutoa. Tukasema jambo hili mwanadamu anaona gumu sana : ” Nitowe changu mwenyewe nilichokichuma kwa shida na taabu!”
Na ndio shetani anakuwa mwepesi kumzaini mwanadamu asitekeleze agizo la Mwenyezi Mungu.
Basi kama ilivyo kutoa ni jambo zito kwa mwanadamu, hivyo hivyo binaadamu kumsamehe aliyemkosea nalo si jepesi; si jepesi kabisa. Na mtu anayefanya hivyo basi ujue kafanya jambo kubwa sana na hana budi kupata malipo kwa Mwenyezi Mungu. Mtume, S.A.W, anasema:
Mtu anayepewa akashukuru kwa kupewa; akajuwa kwamba wahitaji wanaotaka kupewa wako wengi, Mwenyezi Mungu akamchagua yeye akampa, kama hajashukuru basi yeye kabisa si mja wa shukurani.
Wenye haja wengi; sasa wewe akakuchagua akakupa, unasema basi umepata kwa nguvu zako. Kweli hayo?
Kushukuru mpaka ukubali kuwa kinatokana na mwengine, sio nguvu zako. Qarun alikuwa mstari wa mbele katika ibada. Taurati akiisoma vizuri na kwa ghaibu. Lakini alikuwa maskini na dhalili. Akaombewa dua na Nabii Mussa, akapata mali nyingi sana . Matokeo yake akawacha ibada zake alizokuwa akizifanya. Isitoshe akawa jeuri, basi watu wake wakamuambia:
Ewe Bwana, usiringe na hii mali uliyopewa, kwa sababu Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kufanya maringo. Na hichi ulichopata kitumie kwa ajili ya kujijengea nafasi nzuri huko uendako. Ufanye hivyo bila kusahau nafasi yako ya kustarehe hapa duniani.
Mtume amesema:
Mwenye kushughulika na akhera peke yake tu akaisahau dunia sivyo; mwenye kushughulika na dunia peke yake tu akaisahau akhera sivyo. Dunia imeumbwa kwa ajili ya binaadam na akhera iko kule kwa ajili ya binaadam. Basi kwa hivyo lazima huku na kule.
Sasa wakamuambia atumie hicho alichonacho kwa ajili ya kujitengenezea makaazi mema akhera atakokwenda kuishi milele, bila kusahau nafasi yake ya hapa duniani. Tumia pesa zako kwa kula vizuri, owa wanawake wazuri, safiri duniani uone mambo mbali mbali; haikatazwi. Kinachokatazwa usitafute kuleta uharibifu ndani ya ardhi, kwani hakika Mwenyezi Mungu hapendi uharibifu, wala hawapendi wenye kuharibu.
Maneno kama hayo mazuri, ushauri wa busara kama huo aliopewa Qarun, anasema ” Unadhani hii nimeipata bure mimi? Nimeipata kutokana na uwezo wa Elimu na ujuzi na utaalam nilio nao”.
Alisahau kwamba katika dunia kuna wajuzi kuliko yeye; kuna wataalamu kuliko yeye; kuna wenye sifa nyingi na bora zaidi zinazowafanya wastahiki kupata kuliko yeye na hawakupata, kapata yeye.
Basi nasema hakushukuru baada kupewa. Na kushukuru ni kusema ‘Alhamdulillahi’. Moja. Lakini kubwa zaidi ni kutumia neema aliyokupa Mwenyezi Mungu katika njia inayoelekezwa na kukubalika.
Mtume, S.A.W., anazungumzia mtu mwenye kupigwa mtihani akasuburi. Madhal binaadam yuko hapa duniani hana budi kupambana na mtihani wa namna moja au nyengine; mkubwa au mdogo. Kusema utakwenda zako moja kwa moja tu, huna mtihani, haiwezekani.
Na mitihani ya Mwenyezi Mungu ni mingi. Unaweza kuwa mtihani wa mali , wa nafsi au hata wa khofu. Anaweza mtu akaingiwa na khofu, hajijui, kila kitu anakiogopa. Mwisho hata kivuli chake akakiogopa, labda watu wanamfuata.
Kuna mtihani wa njaa. Una pesa huna cha kununua. Au kinakuja chakula huwezi kukila; kila ukitaka kiteremke kooni hakipiti; njaa inakusakama.
Unaweza kupigwa mtihani wa upungufu wa fedha. Unataka fedha kukidhi mahitaji yako huna na mambo yamekubidi.
Unaweza ukajikuta huna watu, wanakuondokea watu wa karibu nawe sana , walio wapenzi kwako sana na wewe huwezi kuwazuwia.
Mwenyezi Mungu anataka yote haya uyakubali na usubiri.
Unaweza kuwa umelima, umepanda, yanakuja matumaini ya kuvuna, yanapotea. Tunagharamia fedha na nguvu, lakini tunanyimwa mavuno. Mtihani
Basi Mwenyezi Mungu anasema lazima binaadamu atafikwa na lolote katika haya, lakini,
Wape habari njema wale wenye kusubiri
Wape bishara nzuri kabisa, wale msiba unapokuja wakasema, ” Ah, huu unatoka kwa Mwenyezi Mungu, sisi wa Mwenyezi Mungu na kwa Mwenyezi Mungu tutarejea.”
Wakakubali hivyo, wakawa hawapayuki. Msiba ukija wanapayuka baadhi ya watu, mpaka wanajisahau, wanasema Mwenyezi Mungu kawaonea: Mtoto wangu ndiye huyu huyu amekufa, yule jirani ana saba angepunguziwa mmoja asingehisi, lakini anakuja kunichukulia mimi hii chongo yangu niliyonayo.
Ndio, hiyari yake Mwenyezi Mungu. Wewe ndiye aliyekuchagua kukupa mtihani; hakuchagua kumpa yule mtihani huo; yule atapewa mtihani wa aina yengine.
Basi wenye kusubiri ndiwo wenye kupata rehema. Na Mtume kasema nusra haiji mpaka usubiri. ” Baada ya dhiki faraja.”
Hizo ni sifa mbili ambazo Muislam ametakiwa awe nazo; akipewa ashukuru na akikosa astahamili. Mtume ameitaja sifa ya tatu kama mtu mwenye kudhulumiwa kusamehe.
Hapa ndio inatuleta kwenye yale maudhui yetu, yakwamba ikiwa Mwenyezi Mungu kaahidi kusamehe waja wake, huo ni mtihani kwamba na wewe ukikosewa hebu samehe.
Man dhulma faghafara
Aliyedhulumiwa asamehe. Mtu akakufanyia yasiyofaa; ya uonevu, ya jeuri, lakini wewe ukasema ” Basi Mwenyezi Mungu, msamehe.”
Pamoja na kwamba unapofanyiwa jeuri, unapofanyiwa dhulma, provision imo ndani ya Qur-an kuwa wewe ukilipiza hakuna lawama, Mwenyezi Mungu anasema mwenye kusamehe, akafanya wema, malipo yake atayapata kwa Mwenyezi Mungu.
Sasa wewe hiyari yako, unafanyiwa ubaya unalipa ubaya, au unawacha Mwenyezi Mungu akulipie.
Hatari ya kuchukua jukumu la kulipa mabaya wewe mwenyewe ni kwamba Mwenyezi Mungu amesema unapofanyiwa ubaya ukirudisha urejeshe kwa kiwango kile kile ulichofanyiwa. Si rahisi. Mtu aliyekufanyai ubaya, siku ya kumpatia nafasi ya kumlipa unataka kummaliza. Sasa ukizidi ushakiuka mipaka.
Kwa hivyo ruhusu ya kulipiza mabaya kwa mabaya imo ndani ya Qur-an. Lakini pamoja na ruhusu hivyo, umepewa na ushauri wa Mwenyezi Mungu kwamba ukiwacha usilipize, ukamuachia yeye, au ukasamehe kabisa basi wewe uko mbali.
Seyyidina Abubakar bin Sidiq, R.A., alikuwa na jamaa yake akiitwa Mustafir bin Juzaka, akawa anamfanyia wema usio na mfano; alikuwa maskini, fakir, hajimudu kwa chochote. Kila anachokihitajia anapewa na Abubakar bin Sidiq.
Lilipozuka janga katika nyumba ya Sayyidina Abubakar, huyo Mustafiir bin Juzaka ndiyo akavaa njunga akawa anatangaza. Akimuona mtu. ” Unayo habari ya mambo ya nyumbani kwa Sayyidna Abubakar? Mambo makubwa.”
Habari yenyewe ilikuwa uzushi kwa mtoto wa Sayyidina Abubakar, ambaye ni mke wa Mtume, S.A.W., kasingiziwa kuzini. Basi yeye yule Bwana ndio ikawa kazi yake. ” Sheikh Rajab uko wapi? Siku nyingi sijakuona mjini. Ya mjini unayajua? Sikiliza basi nikupe…..”
Na yeye ndio yumo ndani ya nyumba ile, analishwa na kuvishwa na kufadhiliwa kwa kila njia. Mpaka Mwenyezi Mungu akateremsha Aya kueleza kwamba hadithi zote ni uongo na uzushi mtupu na waliokuwa katika mstari wa mbele katika kutangaza mambo hayo ni jamaa zenu wenyewe.
Sayyidna Abubakar akafurahishwa sana kwamba mtoto wake kakoshwa na uchafu na matope aliyokuwa akipakwa. Mtume mwenyewe akafurahi sana kwamba dhana mbaya zilizokuwa juu ya mkewe, mke ambaye alikuwa kipenzi chake, zikaondoka, mapenzi yake yakawa yamerudi. Bibi Aisha mwenyewe ndio hasemeki kwa furaha.
Sasa Sayyidna Abubakar bin Sidiq, R.A., hamaki zake kwa mtu huyu asiyekuwa na ihsani wala fadhila, aliyevaa njuga kutangaza uovu akasema, “Tangu leo huyu bwana hatapata senti yangu, wala sitonyoosha mkono wangu kumsaidia kwa chochote.”
Nani angemlaumu? Nani kati yetu asingefanya kama hivyo? Una nyoka ndani ya nyumba. Basi akamuapia kwamba hampi chochote. Mwenyezi Mungu hakumuacha, pale pale aya imekuja:
Kwa kile kiapo wale wenye uwezo miongoni mwenu kwamba hawatowapa jamaa zao na maskini na wale wanaohama katika njia ya Mwenyezi Mungu wasile kiapo kwa makosa yote yaliofanywa wasemehe, wasahau yaliyopita. Kwani nyinyi hamtaki Mwenyezi Mungu akusameheni mnapokosea? Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe waja wake na mwingi wa kurehemu.
Sayyidna Abubakar ikawa kama aliyechochewa, Mustafir ikawa inammiminikia mvua ya neema kutoka kwa Sayyidna Abubakar. Akaona bora ingetokea tena, kumbe matu akifanya maovu analipwa hivi! Sayyidna Abubakar ikawa anampa zaidi na zaidi kuliko alivyokuwa akimpa kabla, kwa sababu imetoka kwa Mwenyezi Mungu.
Lakini Mwenyezi Mungu mbali ya kusema
Man dhulma faghara
(Mwenye kudhulumiwa akasamehe) pia amesema
Wa Man dhalama fastaghfara
(Na mwenye kudhulumu akomba msahama)
Hili ni gumu zaidi. Mtu akifanya dhulma, akakufanyia jeuri, halafu akakubali kwamba alivyofanya sivyo, akaja akakuomba umsamehe: “Bwana mimi nimekukosea, nilivyofanya, wala sistahiki kufanya mambo kama yale. Naomba unipokee na unisamehe kwa hayo niliyofanya.”
Si watu wengi, wala si rahisi watu kujiteremsha chini kiasi hicho. Yeye kajaza jeuri kwa sababu ya nguvu, kwa sababu ya kukuona wewe mnyonge na dhahili, wala huwezi kufanya lolote pale anapokupitishia jerui ile. Leo arudi aje akupigie magoti kuomba msamaha!
Watu wanafanya; watu wanaomjua Mwenyezi Mungu; watu wanaoamini katika malipo ya Mwenyezi Mungu wanafanya hivyo. Wamewakosea watu wakaenda kuwaomba radhi, wakaomba msamaha.
Abudhar bin L’Khitar alimdhalilisha Bilal bin Rabah. Na Bilal bin Rabal mnamjua, muadhin wa Mtume (S.A.W), lakini alikuwa mtumwa kabla, ni mtu weusi. Akaenda akashtaki kwa Mtume (S.A.W), kwa vile jambo lilikuwa limemuingia rohoni.
Akaitwa Abudhar bin L’Khitar akaambiwa “Wewe bado masalia ya imani ya kikafiri unayo ndani ya moyo wako. Kama ingekuwa imani imetimia usingefanya kitendo hicho cha kumdhalilisha Muislam mwenzako Bilal.”
Akasema, ” Ya Rasula Lllah, mimi nilifanya kwa njia ya maskhara tu, wala sijakuwa nakusudia hivyo. Na kuthibitishia kuwa mimi sijafanya hayo kwa ubaya, namtaka radhi Bilal, na nnalala hapa siondoki Ya Rasula Llah mpaka Bilal anikanyage kwa kiatu uso wangu. Ndipo ntaporidhika mimi, kuthibitisha kwamba sijafanya hayo kwa ajili ya dharau au kumnyanyasa Bilal.”
Kalala chini mbele ya Bilal na Mtume (S.A.W) akamuambia “Nikanyage, nikanyage kwa mguu uliovaa kiatu, kwamba nakutaka radhi.”
Bilal akamsamehe.
Lakini nani hebu fikiri leo atayepitisha jeuri, na jeuri zimejaa siku mbili hizi katika dunia, atayepitisha dhulma, na dhulma ndio tunalala nazo na tunaamkanazo, halafu anasema leo mimi nimekosea nakwenda kutaka radhi. Si rahisi, wala hawapo watu hao siku hizi.
Mtume alipowataja watu hao wanne! Mwenye kupata akashukuru, mwenye kukosa akasubiri, mwenye kukosewa akasamehe na mwenye kukosa akaomba radhi, alinyamaza. Masahaba wakaona Mtume (S.A.W) yale maneno hajamaliza. Basi wakataka kufafanuliwa. Akasema:
Hao ndiwo wenye kupata amani na hao ndiwo wenye kuongoka.
Basi na sisi tujitahidi. Na ukiweza kusamehe dogo na kubwa utaweza kusamehe. Kinyume chake, ukishindwa kusamehe dogo, kubwa ndio litakuwa baa zaidi. Utasema “Mimi sikusamehe mpaka kesho chini ya mkunazi.”
Eh, unalibeba mpaka chini ya mkunazi kesho! Sivyo hivyo. Lazima tuwe na moyo wa kustahamiliana; na tujitahidi kama iwezekanavyo kujitenga na vitendo vya kuwafanyia watu wengine jeuri na dhulma.
Siku hizi jeuri na dhulma zimejaa. Wenye madaraka jeuri na dhulma ndio hazisemeki. Basi wasiokuwa nayo pia nao wanaiga. Labda ana nguvu kidogo kuliko wewe, basi ananyanyasa watu na kutesa watu katika jamii. Uislam uko mbali sana na tabia ya baadhi ya Waislam.
Uislam na Muislam ni vitu tofauti. Ukitaka kuutia dosari Uislam, tazama Uislam wenyewe sio Waislam mmoja mmoja. Uislam sio kuvaa kanzu na kwenda msikitini, ni mambo zaidi. Iko wazi katika kitabu kidogo cha Hidayatul Atfal kilichoandikwa na Al Alam Alamin Mazrui. Anasema Uislamu ni kunyenyekea na kufuata kwa ukamilifu mafunzo yote aliyokuja nayo Mtume S.A.W.
Mimi nilikwenda Amsterdam . Siku hiyo nikachukuliwa na mmoja katika jamaa wa Ubalozini. Akasema twende tukatembee Rotedam. Tukaenda. Ilipofika saa ya chakula tukaenda hoteli. Tukaenda hoteli ya Hilton pale tukala lunch.
Basi kila mtu akaletewa menu, akaagiza chake. Mimi sijajua kaagiza nini. Kumbe yeye kaagiza nguruwe. Muislam, mtu wa Kiunguja. Kilipokuja chakula nikapiga jicho nikamuona mkuu wa meza. Sikustahamili, nikasema, “Sheikh, mbona umeagizia nguruwe?”
Basi aliruka juu ya kiti, mimi nikastaajabu. Akaanza kutizama chini ya kiti na chini ya meza. “Umesemaje? Yuko wapi, yuko wapi, kapitia wapi?”
Nikaona haya maajabu makubwa. “Nikamwambia si huyo hapo?”
“Basi umenitisha, mimi nilidhani kama tumeingiliwa! Kumbe nyama tu bwana? Hii nyama tu.”
Sasa huyu ndio Muislamu wa kumpigia mfano? Habari ya mtu anayoyafanya ni tofauti na habari ya maagizo yanayotolewa ndani ya amri. Wako watu wa namna hii. Ukitaka kuupinga Uislamu upinge kwa maagizo.
Kama anavyotuambia Mwenyezi Mungu
Yote aliyokuleteeni Mtume kukufundisheni kwamba haya ndio barabara yanatoka kwa Mwenyezi Mungu basi yatekelezeni kama yalivyo.
Tena
Yale ya utekelezaji na utumizaji yatekelezeni na muyatimize kwa kadiri munavyoweza.
Ama yale ya kukatazwa, hakuna concession, lazima muyawache moja kwa moja. Hakuna utalewa kidogo; utakula nguruwe kidogo; utachukua wanawake kidogo. Hapana, ya kuwacha unawacha moja kwa moja. Ama ya kutimiza, wewe umepewa nafuu kidogo, kwa kiasi cha uwezo wako.
Tunaambiwa
Zitekelezeni amri za Mwenyezi Mungu zilizowekwa juu yenu kwa kadiri ya uwezo wenu unavokuwezesheni. na kila mmoja kikomo cha uwezo wake anakijuwa mwenyewe. Sasa watu watazidiana katika hichi kikomo, ingawa wengine hawataki tu kufikia kikomo. Kafunga Ramadhani anasema hawezi kufunga sita. Hataki. Halafu anataka alipwe sawa na alietimiza maagizo.
Mtume (SAW) alisema
Hakuna yoyote atakaekuja ila siku ya kiama atajuta; lazima atajuta.
Masahaba wakasema mtu mbaya akijuta inaeleweka; Mtu mwema anajutia nini nae keshafanya mema?
Akajibu Mtume (SAW)
Mtu mbaya atajuta kwa kutotekeleza na mtu mwema atajuta kwa kutokuongeza.




One Comment on "Kumuomba radhi binaadamu mwenzako"
big up jongers,darasa zuri sana ,hongera wazalendo,