Mchanga wa Kisiwandui -II
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 29/10/2009 // DIRA // Zima maoni
Na Ali Nabwa
MCHANGA wa Kisiwandui ulitanda kuanzia kwa Ali Ahmed Riyami (Ami yake Salim Ahmed) kwenye ‘corner’ kuendea Weles (SAFI Building, pembeni ya Transworld House sasa) hadi muembeni kwa Adu ambapo Ali Ahmed alijenga baadae na kuhama kutoka kwenye ile nyumba ya miasumini, na kwa Dharamsi, mlangi – langini, kwa Bi Panya.
Ukitoka kwa Dharamsi, unapanda kilima cha Kisima Majongoo kuelekea Gongoni. Hiyo ndio Kisiwandui na ilikuwa na mikasa yake na vituko vyake.
Hapo zilikuwa zikipigwa ngumi kati ya Kisiwandui (pamoja na Kikwajuni) na Malindi. Yaani mechi zikipangwa rasmi. Wakipigana mbele ya Msikiti Mabati, pembeni ya Majabalini (nyumba inayotizamana na kibla cha msikiti).
Shujaa wa Malindi alikuwa Ba Manga. Kisiwandui walikuwa Msafiri Rocky na Kaiza. Huyu Kaiza aliwahi kuwa beki wa New King, lakini baadae akawa na mguu mzito (sisi tunasema miguu mizito na mishipa, sio maneno yasiyopendeza).
Kaiza alisifiwa sana kwa kula. Siku moja wenzake walikwenda marikiti kununua kiteweo walimuachia yeye aangaliye viazi vikichemka kwenye debe (la mafuta). Kurudi wakakuta debe tupu, akawaambia alikuwa anaonja.
Siku zote akisema harusi aliyoijua yeye ni moja tu, ya Maalim Mahfoudh, baba yake Said Mahfoudh, kwa sababu alipewa sinia mbili za pilau peke yake.
Siku moja wakati ngumi zinaendelea, alipita jamaa mmoja akajiingiza katikati kama mchuzi wa ugari. Alipigwa ngumi moja na Kaiza akaona vimuri-muri. Alizitimua mbio kuelekea kwa Adu.
Kila akigeuka nyuma anaona mtu kamuandama. Baada ya kupanda kilima, palipokuwa pakiuzwa samaki wakavu, pumzi zikiwa zimempaa, alisimama akamuuliza yule jamaa, “Kwa nini umeniandama mimi tu? Hutafuti kiasi chako kule?”
Yule jamaa akajibu, “Mimi sikufuati wewe. Nimepigwa ngumi na Msafiri Rocky nasikia kizungu-zungu.”
Hebu tuangalie siku yetu wakati ule. Asubuhi nilitumwa maziwa ya mbuzi kwa Bi Maulidi, nyuma ya Bwana Ameir, baba yake Dk. Muchi. Maziwa ya pesa mbili (senti tano) yalitosha kwa chai.
Halafu nilikwenda kwa Baba Hadi kununua majani ya chai pesa mbili, sukari pesa nne na mikate mitatu ya pesa sita sita (senti 15 kila moja). Kwa hiyo, kwa senti 65, chai ilitimia kwa watu watatu.
Baadhi ya wakati tulinunua mbaazi kwa Bi Makiya, bibi yake marehemu Abdul Borafia (kikombe cha kahawa pesa mbili) au samaki wa kukaanga kwa Bi Buluu, mbele ya Msikiti Makuti (paa lake lilikuwa la makuti, kinyume na Msikiti Mabati). Samaki walikuwa pesa mbili, pesa nne na pesa sita (senti 15). Chai ‘maridadi’, ya maziwa, na mbaazi au samaki wa kukaanga, ilikuwa haitimii shilingi moja kwa nyumba nzima.
Chakula cha mchana nilisema katika makala yaliyopita kilikuwa shilingi 1/40. Usiku mikate mitatu, chai na mboga ya kisambu, kama senti 80. Kwa hiyo, kwa shilingi tatu mnakula kutwa mara tatu.
Nakumbuka hata nilipomaliza skuli mwaka 1955 nikawa napata mshahara wa shilingi 147/-, tukila uzuri, tukivaa na katika kipindi cha miezi tisa kabla kuondoka kwenda kusoma Ulaya nilidiriki hata kununua baiskeli ya Raleigh.
Mtoto ukitumwa unaambiwa, “Natema mate, yakikauka kabla hujarudi utakiona cha Mtema Kuni.” Hadi leo sijajua Mtema Kuni alifikwa na mkasa gani.
Wazee wetu wakipenda sana kahawa na kila mmoja alikuwa na muuza kahawa wake. Wakiwajua kwa mlio wa vikombe. Wenye kahawa walikuwa wanachukua madele maalum ya shaba yaliokuwa yakingára , sio mabirika ya kuoshea mikono tunayoyaona leo, na wakivaa seruni na vizibao vya kaki na kofia ya mkono. Wauza kahawa walikuwa washihiri kama walivyokuwa wazegazega. Wakibeba madebe mawili kwenye mzega-zega, sio madumu kwenye marikwama. Labda haya sasa ni maendeleo, lakini Zanzibar ilikuwa na sura yake.
Hata wagonjwa wa akili walikuwa wa aina yake. Wakifurahisha, hawakumkera mtu. Mfano, ‘Al karibu’, mwanamke mdogo dogo ambaye akitembea haraka haraka, na Kichwa Ubuyu. Walikuwa hospitali ya Kidongo Chekundu, lakini wakiruhusiwa kutembea mchana na wakipita Kisiwandui, tukiwasalimia, hasa Al Karibu, ambaye ukimwita akikupungia mkono bila kusimama.Sana sana atakuomba sigara, hata ukiwa mtoto mdogo sana.
‘Mwalimu’ naye akipita na baiskeli yake. Tukimpigia kelele, “Mwalimu!”, anafanya sarakasi yake. Tunampigia makofi, anafurahi, anaondoka.
Bibi zetu wakivaa kimanga, suruali nyembamba na kanzu za urembo mpaka magotini. Leo inaonekana ‘fesheni’. Wakitia behedani (curl kit) na wakijisugua mwili kwa liwa (sio mkorogo). Wakitoga masikio na kutia vigurudumu vya karatasi. Wengine wakipenda mshuku na baadhi wakivuta sigara kali za kusokota, tukitumwa kwa Adu. Wako waliokula na tambuu na popoo, wakitema mate mekundu kwenye matasa.
Siku ya Ijumaa tukenda kusali Msikiti wa Forodhani, khalafu tukenda Palace ambako Seyyid Khalifa akitoa sadaka kwa watoto na maskini. Sisi tukipewa senti kumi.
Lakini Bwana Hamid, muadhini wa Msikiti Mabati, mlemavu wa macho aliyejaaliwa sauti kali (sawa na vipaza sauti vya leo) akipewa nusu shilingi. Yeye alishikwa mkono na kijana akiitwa Nguvu Matata.
Mbele ya nyumba yetu kulikuwa na madobi wawili, Bwan’ Saadi, baba yake Maalim Masururu, na ‘Teacher’. Walikuwa wanafua kwenye vyano vikubwa. Jambo ambalo linanishangaza hadi leo ni kwamba hawakuwa na vipande vya utambulisho (tags), lakini hakuna nguo ya mtu iliyopotea, akapewa mwengine.
Kulikuwa na mikahawa mitatu pale Kisiwandui. Wa Mzee Salmin, ilipo nyumba ya Bi Maryam Hamdan leo, ndio uliokuwa maarufu zaidi kwa maharagwe. Wa Bwana Abdulrahman, pembeni ya Jaffer Building , ulikuwa maarufu kwa mikate ya ajemi, mikavu au ya samli.
Nilipokuwa naishi Mombasa , Kenya , jamaa mmoja aliniambia anaijua Kikwajuni. “Kuna minazi mingi.” kweli, kikwajuni kulikuwa minazi mingi. Nikipenda kumuangalia mkwezi akipanda mnazi akitumia kamba miguuni, sio kuichonga minazi kama wanavyofanya leo. Mkwezi akipanda mnazi alikuwa anaimba nyimbo zikifurahisha. Kuna kitendawili kinachosema alikwenda kuitwa kaja, aliyetumwa hajarudi. Ni nazi na mkwezi.
Kuna mzee mmoja akiuza ngazi. Alikuwa akinadi biashara yake kwa kusema “Mpanda ngazi hushuka, usiingie ujingani.”
Wakati wa Musim, ambapo majahazi ya Malatubi na Wasomali yalijaa Funguni, tukichangishana pesa tukinunua suwela na hanide.
Magharibi tukenda Msikiti Barza kusikiliza darsa za Sheikh Abdallah Saleh Farsi. Maalim Abdallah ‘Muadhini’ akisomesha chuo juu, yeye na Maalim Himid.
Jumapili ilikuwa siku ya kufua Weles, ama kwa sabuni ya chokaa au harita. Zikikauka unapiga pasi kwa mkono vizuri halafu unaweka chini ya mto. Baadae unakwenda kucheza kipande, au kurusha kishada.
Nakumbuka alasiri tukenda Mnazi Mmoja (wakati huo uwanja ukikatwa majani, safi , wakati wote) tukimuona Sayyid Khalifa akipita na gari yake nyekundu. Ilikuwa na ‘Bawabu’ tu mbele. Hakuna askari, hakuna gari nyuma (escort). Njia pia zilikuwa hazufungwi .Ulikuwa wakati wa amani ule.
Mtu akiuwa au akimuingilia mtoto anapandishiwa bendera nyekundu siku ya kesi yake. Lilikuwa tukio kubwa. Leo ni mambo ya kawaida. ‘Utamaduni’ huu umefikaje Zanzibar ? Wazanzibari tutafakar!



