Nnahum Lamukyadhibuun! Kazi yao kukanusha tu!
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 29/10/2009 // DIRA // Zima maoni
Na Mohammed Ghassany Waziri Burhan Saadat Haji
Si vibaya ikiwa tutadokoa kidogo katika fani ya wenyewe. Katika Falsafa kuna kitu wanakiita Fallacy, ambacho Kiswahili chake kinaweza kuwa Upotofu wa Hoja. Hoja kuambiwa imepotoka haina maana kuwa hoja hiyo haitumiki. Wako mabingwa wa kuzitumia aina hizi za hoja kwa makusudi kabisa, na machoni pa watu zikapata sura ya kuonekana kuwa hoja. Kuna hoja nyengine huitwa potofu, maana huwa zimekosa dira na hivyo huenda kinyume na zinavyotakiwa hoja ziende.
Aina moja ya Fallacy ni ile inayoitwa Argumentum ad Baculum, ambayo ni aina ya hoja ijengwayo juu ya msingi wa wenye madaraka. Kwamba kitu huitwa ndicho kwa kuwa tu walio madarakani wanakiita ndicho, na huitwa sicho ikiwa watawala wanasema sicho. Vijana wenzangu watakuwa wanaukumbuka ule wimbo Ndiyo Mzee, ambao kwa kiasi kikubwa unazungumzia aina hii ya hoja.
Hapa petu si zamani sana tokea hoja ya aina hiyo itumiwe na watawala wetu, ambao, kwa hakika toka hapo si wageni wa kutumia hoja kama hizi. Mzee mmoja wa zamani, aling’aka alipomuona Mheshimiwa Burhan Saadat Haji kwenye TVZ akipapatuwa, akasema: “Innahum Lakyaadhibuun! Kwamba hakika hawa ni wakanushaji tu.
Sikitiko langu ni kwamba jukumu hili mara hii amepewa mtu tunayemuheshimu sana , mzee wetu Sheikh Burhan. Alitumwa – nasema alitumwa, hakuyafanya yale kwa hiari yake – kuja kumpapatuwa bosi wake na aibu na fedheha inayomrandia kuhusu kadhia ya mafuta ya Wazanzibari! Na bado nasisitiza tena na tena matumizi ya neno hili kupapatuwa, maana ndilo nimaanishalo hasa. Naamini, kwa kila hali, kwamba Mzee wangu huyu hakuwa akikanusha habari iliyochapishwa na gazeti hili Toleo Nam . 009: Awamu ya Sita yaridhia Serikali ya Muungano kuchimba mafuta Zanzibar .
Hakuwa akikanusha, maana hii si habari inayokanushika, na hata mtu akijaribu kuikanusha huwa ndiyo anaithibitisha. Kuna baadhi ya habari, wenyewe huziita symmetrical, huwa ni kama vile urimbo, kwamba zinanasa. Na nani asiyejua kuwa ukishanasa kwenye urimbo, huwa hutoki! Unaweza kujipapatuwa, lakini kila hatua moja ya kufanya hivyo, huwa ni kujinasisha zaidi. Hiki ndicho kile kisa cha sungura aliyejifanya mjanja wa kuteka maji ya watu wakati wenyewe hawapo. Kila palipowekwa walinzi wa kukilinda kisima, bado yeye aliendelea kuyateka maji ya watu, maana alikuwa akiwaghilibu wale walinzi kwa kibuyu cha asali na bilauri ya mvinyo.
Siku lilipowekwa sanamu la urimbo, ndiyo siku sungura aliyonaswa. Maana, kwanza tofauti na siku nyengine ambazo alikuwa akitumia ulimi wake kuwalaghai wale walinzi wengine, siku hii alikosa majibu kwa kila suali alilouliza. “Kwani we’ nani eeh?” Kimya. “Unanijuwa mie?” Kimya. “Nikugaiye asali yangu?” Kimya. Mwisho akaona bora ajikaribishe lilipo lile sanamu na alipe mkono, akidhani ni mtu. “Basi rafiki yangu tusalimiane!” Kumgusa tu, akanasa mkono. Alipojipapatuwa na kuona hatoki, akamuuliza: “Kwani mkono mwengine sinao?” Na wa pili ukanasa. “Kwani mguu sinao?” Ukanasa. “Kwani mwengine sinao?” Nao ukanasa. “Kwani kichwa sinacho?” Nacho pia kikanasa. Asubuhi walipokuja wenyewe wakamkuta, sungura ananing’inia kwenye sanamu la urimbo! Sanamu hili lilikuwa ni symmetrical.
Na habari hii kuhusu mafuta ya Wazanzibari kuchimbwa na Tanganyika , nayo pia ina sifa hizo. Na kila anayejaribu kuipinga, huwa ananasa kama alivyonasa sungura wetu kwenye sanamu lisilolaghaika kwa kibuyu cha asali wala kwa bilauri ya mvinyo. Basi katika jitihada za kupapatuwa, Mzee wangu akasema kwamba SMZ haijawahi kufikia makubaliano yoyote na Serikali ya Muungano kuhusu kuyachimba mafuta, na badala yake Serikali bado inatafuta ushauri wa wataalamu kuhusu suala hilo .
Labda aliloshindwa kulijua Mzee wetu huyu, na huyo aliyemtuma kuja kupapatuwa, ni kwamba suala kama hili, ni suala lenye hoja zaidi ya moja ndani yake, watu wa taaluma ya habari huiita Complex Question. Kwa hivyo, si rahisi kiasi hicho kujibika.
Hebu tupige mfano ulio kando kidogo kabla hatujaingia ndani ya kadhia yenyewe. Chukulia kuwa wewe ni kijana wa kiume, ambaye hutaki maisha yako ya faragha yajulikane na wasichana wengine. Kila siku ulikuwa unawaeleza watu kwamba wewe huna mke, ingawa unaye, na ghafla siku moja ukaulizwa: “Siku hizi umeacha kumpiga mkeo?”
Unadhani utatowa jibu gani hapa. Kama unataka kuendelea na msimamo wako wa kujieleza kwa watu kama kapera, basi ni lazima ukatae kabisa kwamba una mke. Uulize mke gani huyo uliyewacha kumpiga na ilhali hunaye. Maana ukiingia kichwa kichwa na kukanusha kwamba humpigi wala hujawahi kumpiga mkeo, utakuwa unaubomoa ule msimamo wako wa mwanzo kwamba wewe huna mke. Utakuwa unautia ulimi wako puani. Maana swali uliloulizwa lilikuwa changamano, kwamba linakueleza kuwa una mke na pili ndiyo linakuhoji kumpiga huyo mkeo.
Pengine mfano huu ni wa kando na wa unyumba zaidi, lakini hivi ndivyo ambavyo mtu anaweza kulizungumzia suala la mafuta ya Zanzibar . Ndani ya habari iliyochapishwa na Dira, mna mambo matatu kwa wakati mmoja. Kwamba kwanza Zanzibar pana mafuta, pili SMZ imeiruhusu Serikali ya Muungano kuyachimba mafuta hayo na tatu kwamba kwa kulithibitisha hilo la kwanza na la pili, basi hata Mzee Burhan naye alishiriki katika sherehe za utiaji saini wa mkataba wa uchimbaji mafuta ya Wazanzibari.
Mzee wangu alitumwa kuyapapatuwa haya mawili ya mwisho, ambayo yenyewe ni matokeo tu ya ile hoja ya kwanza. Basi kwa hivyo ameiwacha hoja ya kwanza kama ilivyo. Hakuigusa, maana haigusiki. Na hivyo, bila ya kujijua ikawa anaithibitisha ile ya kwanza, ambayo ndiyo msingi wa nyengine mbili.
Ndiyo! Maana kupapatuwa tu kwamba Serikali ya Zanzibar haijafikia makubaliano yoyote ya kuyachimba mafuta na Serikali ya Muungano na kwamba hapajawahi kuwa na sherehe ya kutiliana saini makubaliano hayo, ni sawa na kusema kuwa unakubali kwamba Zanzibar pana mafuta. Na kama hivyo ndivyo, hata ule ukweli uliotaka tuuamini katika kauli yako ya pili, nao unaanza kuhojika! Kwa nini? Mheshimiwa Saadat alikuwa anawakilisha ujumbe wa Serikali ya Zanzibar kwa watu wa Zanzibar . Hii ni Serikali ya watu, iliyochaguliwa na watu kwa ajili ya watu. Miongoni mwa majukumu makubwa ya serikali ya aina hii ni kuwataarifu watu walioikabidhi dhamana ya kuwaongoza, kila kitu kinachohusu maisha yao , utu wao, heshima yao na juu ya yote, miliki yao . Pengine wakati alipotoa taarifa hii kwa vyombo vya habari, Mheshimiwa Saadat alikuwa anatekeleza jukumu hilo . Lakini, kwani ni lini huko nyuma ambako Serikali hii hii iliwahi kuwatangazia raia wake kuwa nchi yao ina mafuta? Ninaposema serikali hii hii, isionekane kuwa nazungumzia Awamu ya Sita tu, kwani panapohusika ile dhana ya Collective Responsibility, U-SAT na U-SAS hauna mantiki yoyote ile. Na juu ya yote, hawa hawa walio kwenye hiyo iitwayo SAS sasa, ndio waliowahi kuwamo kwenye hiyo iitwayo SAT. Sasa lini Serikali ilipowahi kunyanyuka na kuwabainishia watu wake kwamba nchi yao ina rasilimali hii na kwamba Serikali yao ilikuwa imo katika jitihada za kuyachimba ili kuuinuwa uchumi wao? Lini ilifanya hivyo?
Pengine nina kumbukumbu mbovu kabisa, na hilo likithibitika, sitaweza kulikanusha. Lakini kwa wengi, taarifa ya kuwepo kwa mafuta Zanzibar , ilipatikana kwa mara ya mwanzo kabisa kupitia katika majukwaa ya mikutano ya wapinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2000. Na kwa bahati mbaya ni kuwa wapinzani waliyasema haya katika siku za kuomba kura, kwa hivyo ile thamani yake, kwa wengi wetu ilionekana kupitia katika kioo cha kuombea kura tu, na si vyenginevyo!
Na ni wakati huo ambapo makini za watu wa Zanzibar angalao zikaanza kudokorwa kwamba: “Nyinyi mna utajiri wa kutosha!” Lakini Serikali haikufanya juhudi yoyote ile ya kuwafafanulia wananchi wake wakati huo – na hadi sasa – juu ya kuwepo kwa mafuta katika nchi yao . Kubwa zaidi lililofanyika, nalo ni kupitia kwa mgombea Urais wa wakati huo, ni kukebehi kauli kwamba Zanzibar pana mafuta. Ikasemwa kwamba ni kuwapotosha watu kuwaambia hivyo, maana ni uzushi. Kukanusha ndio kazi yao ! Hivi sasa miaka mitatu baadaye, huku ikiwa bado Serikali haijapata kuwaarifu watu wake kuhusu kuwepo kwa mafuta katika ardhi yao , inatuzukia na kauli tu kwamba haijafikia makubaliano yoyote na Serikali ya Muungano kuyachimba mafuta ya Zanzibar . Aka! Ilikuwaje? Kwa mtu ambaye siku zote alikuwa akiitegemea Serikali yake kwa kupata habari za uhakika kuhusu maendeleo na mustakabali wa nchi yake, lazima kuanzia hapa atakuwa akijiuliza: Ati nini? Serikali haijaruhusu mafuta kuchimbwa, kwani hayo mafuta yako wapi? Kuanza kujiuliza hivyo kwa raia mtiifu kwa Serikali yake ni kuanza kuijengea shaka na kuanza kutokuiamini. Na Serikali inapoanza kupoteza imani ya raia wake yenyewe, msingi mkubwa wa userikali wa serikali hiyo huanza kuporomoka. Maana userikali wa serikali yoyote ulimwenguni si kuwepo kwake madarakani tu, bali pia kupata imani ya wale inaowaongoza. Na inapofika pahala pa serikali kuwadanganya au kuwaficha raia inaowaongoza, kwenye taarifa muhimu kama hii inayohusu maisha yao , basi sasa ni hatari. Ndiyo, hata kwa raia mtiifu kiasi gani, lazima atasutwa na huo utiifu wake mwenyewe ikiwa atakubali kuimeza tu taarifa hii ya Mheshimiwa Saadat bila ya kwanza kuimung’unya. Na kama ataimung’unya, basi atajikuta ana maswali mkururo ya kujiuliza. Je, ni kweli kuwa Serikali hii haikujua kwamba hapa Zanzibar pana mafuta? Kama ilijua, kwa nini haikutueleza tangu zamani? Ilikuwa inajaribu kutuficha nini sisi raia, ambao ndio wamiliki wa asilimia mia moja wa rasilimali hii? Je, ni mpaka ilazimishwe kujibu hoja, ndipo ifanye hivyo? Nasema hapa kwamba Serikali imelazimishwa kujibu hoja, maana si kwa hiari yake kutoa kauli hii kwa wakati huu. Laiti kama Dira isingeliinuka na kulisema hili hivi sasa, basi mwenendo wa matukio unaonesha kuwa ingelifikia makreni kuletwa hapa na Antrim Energy ikaanza kuyachimba mafuta yetu, kabla ya raia kuelezwa nini kinaendelea. Na hilo ni koseo kwa serikali ya watu, itokanayo na watu na iliyopo kwa ajili ya watu. Pengine kuna baadhi ya mambo, wayaitayo wenyewe Confidential (siri) na pengine wanataka kutuambia kuwa hili la mafuta ni mojawapo, lakini katika ulimwengu kama huu wa mawasiliano, sio tu kwamba ni shida, lakini pia ni aibu kulifanya jambo la kitaifa kama hilo kuwa Confidential ya watu wachache. Hawa raia, ambao ndio wengi, ndio wamiliki wa hayo mafuta yaliyo katika ardhi yao . Kuwaficha hawa au kuwadanganya kuhusu kitu chao wenyewe, mali yao ni kuwaonea na kuwadhulumu. Na baya zaidi ni pale suala linapofikia katika hatua kama hii, kila jambo liko wazi lakini bado Serikali ikaendelea kukana na kukana. Haijuwi kuwa haiwezi kuendelea kuwadanganya watu wote wakati wote? Wakati fulani iliweza kuwadanganya watu wote, na pia wakati wote inaweza kuwadanganya watu fulani, lakini si wakati wote, kwa watu wote!
Na hili pia linamfanya mtu aushuku hata huo ukweli ambao sasa Serikali inajaribu kuutitimiza vichwani mwetu: kwamba haijakubaliana na Tanganyika kuyachimba mafuta ya Wazanzibari. Kwa nini panakuja shaka na shukuki hizi? Nitafafanua kidogo.
Kwanza, ikiwa Serikali ilidanganya katika hoja ile ya kwanza, yaani ya kuwepo kwa mafuta Zanzibar , nani atakayeamini kwamba haidanganyi kwa hii hoja ya pili, ya kuiruhusu Bara kuyachimba mafuta hayo na kwamba Mzee wangu alikuwapo katika kutiliana saini? Kwamba kama iliweza kutuficha katika jambo la msingi na kuja kulikubali baadaye, ni rahisi sana kwake kutuficha katika yaliyobakia na kuja kuyakubali hapo muda ukitimu. Kwamba suala hapa si kwamba serikali inakanusha – maana kama nilivyotangulia kusema kwamba mambo haya hayakanushiki – bali suala ni wakati ambao ukanushi huo unatolewa.
Angalia huu mwenendo wa hoja hapa: katika wakati A, serikali ilikanusha kuwepo kwa mafuta, lakini katika wakati B ikathibitisha kuwepo kwa mafuta hayo. Basi ikiwa katika wakati B inakanusha kuiruhusu Bara kuyachimba mafuta haya, lazima italithibitisha hilo katika wakati C.
Pili, kwa hivyo, ni jambo linalowezekana kabisa kwa Serikali hii hii kutujia tena mwaka mmoja baadaye, wakati huo tayari mafuta ya Zanzibar yameshagidwa na TPDC, na kutwambia kuwa ni kweli kuwa ilitoa ruhusa hiyo, lakini iliwaruhusu kuchimba mapipa milioni moja tu na sio mapipa milioni mia nane na arubaini. Halafu yakishamalizwa hayo mapipa mia nane arubaini, itatuambia kuwa, tuliwaruhusu kuyachimba kweli mapipa hayo, lakini udhibiti na umiliki ni wetu. Alimradi kila muda utakapotimu, Serikali itakuja ithibitishe kile ambacho hapo nyuma ilikikana. Na hapo mtu atajiuliza huo umakini wa Serikali yake adhimu uko wapi?
Wacha nimalize kama nilivyoanza kwa kueleza kwamba kuna upotofu wa hoja hapa. Hata hivyo, hili ni jambo tulilokuwa tukilitarajia, maana si mwanzo leo kutokezea na wala haielekei kuwa hapa itakuwa ndio mwisho wake. Bado Serikali ya watu, itokanayo na watu na iliyopo kwa ajili ya watu inawategemea watu wake kuwa waikubali tu kwa kila inachokisema. Maana kwake hiyo ndio maana ya kuwa mzalendo na kuwa mpenda nchi. Ni kweli kuwa tumo katika jamii iliyolemaa na kulemazwa kwa kupokea habari kutokea upande mmoja tu, lakini kwa nini Serikali ilichukulie jambo hili kuwa ni fursa ya kuwadumaza raia wake yenyewe?
Wanasema kuwa katika Siasa ujinga ni Rehema, na ndio maana mwanasiasa akimuona mtu hajui jambo kuhusu kiti fulani, hutumia kutokujua kwa mtu huyo ili kujinufaisha kisiasa. Lakini huu si msemo wa kuisifu siasa wala wa kuitukuza, huu ni msemo wa kuisuta na kuiaibisha siasa. Ni dhambi kwa mwanasiasa mwenye azma nzuri na fani yake kuutumia msemo huu katika maisha yake ya kila siku. Na hii sio tu kwamba ni dhambi ambayo malipo yake yatapatikana Huko Chini ya Mkunazi na Matongetonge ya Damu, lakini malipo ya mwanzo hutoka kwa umma ambao mwanasiasa huyo anajidai kuutumikia.
Katika ulimwengu huu uliofupika, mambo yanayoweza kuitwa siri ni machache mno, mno sana . Na raia wa nchi hii, hata kama wanaonekana kutokufuatilia, hilo halitokani na ujinga wao. Ni stahamala tu na suala la wakati. Jana walipoambiwa “Hakuna mafuta” waliitikia “Ndiyo Mzee.” Leo wanaambiwa yapo, lakini hayatachimbwa na Bara, bado wanaitikia “Ndio Mzee.” Sasa kesho yatakapochimbwa mapipa milioni, wakaambiwa yamechimbwa mapipa mia moja, nao wakaitikia “Hapana Mzee” tutawafanyaje?
Pata ushahidi kamili dhisi ya taarifa ya Waziri Burhan Saadat katika toleo lijalo.



