Tumewacha yetu … tumevamia ya watu
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 29/10/2009 // DIRA // Zima maoni
Na Ben Wazir
Nataka kubariz katika maudhui yanayohusu utamaduni, mila na desturi zetu, mambo ambayo yanaonekana sio kwamba yanakwenda mrama, lakini yanaelekea kuzama.
Nimeona nizungumzie mengi ambayo yanaleta tafash na ambayo kama yataendelea bila ya kuingiliwa kati na wahusika, pamoja na jamii kwa jumla basi yatazusha balaa kubwa.
Nimeamua niliandikie suala hili kwa vikataa viwili, kimoja wiki hii ambacho kitataalak zaidi juu ya kumomonyoka kwa maadili na kitakachofuata kitagusia mengi ambayo nionavyo mie kama khatua mnasaba hazitachukuliwa basi jamii yetu kama Wazanzibari tujue fika kuwa ipo khatarini.
Inatulazim tujuwe kuwa tutakuwa arijojo tena, ile arijojo ya burtangi, ambayo baada ya kukatika uzi, ikawa inapaa na kuelekea pasipojulikana ikiwa tutakwenda na tabia hizi zilizotugubika. Taib! Huenda nionavyo sivyo uonavyo, lakini sio lazima sote tuone sawa, na ingekuwa sote tunaona sawa basi hata utabibu wa macho ungekuwa haupo na neno miwani lingekuwa nje ya msamiati wetu.
Nionavyo ikiwa hatutosimama kidete kupambana na utamaduni wa kigeni, uliojaa baa na belwa, basi tujue tutakuwa ni taifa lisilokuwa na utamaduni.
Sisemi ulevi umeanza kunywewa Visiwani jana au leo. Laa, hasha! Tangu azal mvinyo ukinywewa, tena na watu wengine ambao wakishikilia dhamana za juu, lakini huko nyuma wanywaji wakikata leseni na pindipo huna leseni ujijue ukikamatwa utapigwa faini au utaelekea korokoroni.
Sasa ya leo yakoje? Hayasemeki. Sehemu za kuuzia pombe ni kila kona na mnywaji ni pesa zake tu, na hata watoto wadogo wakiamua kuelekea kwenye disco, basi akitamani beer, hakuna wa kumkaripia, “Wee mtoto huna adabu, kwanza hapa umekuja kutafuta nini, hujui kuwa haya ni maeneo ya watu wazima?”
Nionavyo ni kuwa tumejisahau. Tumewacha yetu na kuyavamia ya wengine, chembilecho watu, cha kunguru kuwacha mruko wake na kuuiga wa ndege wengine, na mwisho wake kujikuta nusura kuondolewa kwenye kundi la ndege kwani mruko wake ni wa kibega bega tafauti na ndege wengine. Yaliomkuta kunguru sio jengine lolote lile ila ni wigo na huo wigo alifikia khatua ya kukataliwa, lakini mwisho wenzake wakamkubali, sijui sisi itakuwaje? Nionavyo ni bora turejeshe leseni za pombe haraka na wageni wanaokuja Visiwani mwetu wapewe vipande maalumu vitavyoonyesha wao ni rukhsa kunywa pombe na kila pombe atayobugia isajiliwe kwenye kipande, na atapoondoka akirejeshe kipande. Kipande hicho kitakuwa ni njia mjarab ya kukusanya takwimu.
Huenda ukaona hicho kitakuwa ni kitendawili, lakini mwenzangu nikupashe hiyo itakuwa ni njia rahisi ya kutujulisha namna pombe inavyonywiwa na wenyeji na wageni.
Pombe huleta madhara na nionavyo ikiwa hali hii itawachiwa igaregare, kama ilivyo, basi tujue fika miaka ijayo hatutokuwa na taifa la watu wenye afya nzuri kwa kufanya kazi na kusukuma mbele dira ya maendeleo, ila tutazungukwa na wagonjwa. Huo utakuwa mzigo thakili kwa Serikali, na uzalishaji utakuwa wa chini na hapo taifa badala ya kwenda mbele litarudi kinyume nyume na mwishowe ni kuanguka.
Jengine linalonikereketa, na wala sitaki kuwa mkereketwa. Aah, tunapoteza Kiswahili. Badala ya kusema mshabik, anakuwa mkereketwa, anayekereketwa huchafukwa na roho, lakini mshabiki anaweza kuwepo kwenye hali mbili, moja kati ya hali hizo akawa kwenye furaha au karaha. Lakini kukereketwa ni karaha tupu, nawacha hapo sitaki kuwa bingwa wa lugha, nilitakalo ni kutoa dondoo nilizo nazo.
Kivazi tukivaacho kwa jumla, nionavyo ni kuwa sasa ingawa hatujasema kuwa tuna kivazi cha Ki-Zanzibari lakini tuvaavyo sivyo wazee walivyokuwa wakivaa na ndipo hapa inakuwa vigumu pale unaposafiri ukaingia maeneo ya Mrima watu kukutafautisha wewe kama Mzanzibari au mtu kutoka wapi huwa sio rahisi.
Wazee wetu baada ya kuvua khaki za kwendea kazini, na tarbushi inapofika jioni ilikuwa utawaona wakivaa fulana ya ndani na kikoi cha Jabir na kofia ya lasi pamoja na kanzu za darzi kwa wanaume.
Mabanati wao huvaa buibui la kamba na ndani huoni kitu, hujui binti aliye mbele yako au aliyokupitia kavaa nini, sio haya mabuibui ya leo, baada ya kuvaa buibui binti akawa yumo ndani ya stara leo uvaaji wa mabuibui umekuwa kama maonyesho. Buibui ni stara, leo buibui limekuwa ndio la kuondoa stara.
Tena bado sijasema kivazi kinachoitwa fundi kasahau, nacho ni kile cha mpasuo, kanzu imepasuliwa na unaona mpaka visotakiwa kuonekana, gongo wazi, fua linakwita lipo wazi, linakwambia njoo! Halafu huelezwa kuwa ubakaji umeshtadi. Doooh! Wala hautopungua kwa namna tuendavyo, asiokuwa shetani analazimishwa kuwa jini.
Nionavyo sheria ya kivazi, bora irudi. Kwanza sheria hii haijafutwa na ni kuamua tu kuwa tunairejesha. Huenda msomaji ukaruka, ama huyu mwandishi kapitwa na wakati, bora ya hayo kupitwa na wakati kuliko kwenda na wakati huku, kunakotupotoa na kutuangamiza.
Kila nchi ina misingi yake inayojiwekea na misingi hiyo hukubalika. Kuna nchi imeendelea tena pakubwa kwa vipimo vya kuendelea, lakini hairuhusu kinywaji chochote kile kukitia kwenye kopo, kwa nini? Kwa sababu vikopo huelezwa kuwa ni kazi nzito kuvitokomeza kwenye mazingira, na kazi hiyo huwa ni ghali mno.
Watu hao kwa kufanya hivyo hawajakuwa wajinga walipojiamulia, kwani waliona gharama ya kuvirejeza (recycling) ni kubwa, na kujiuliza kwa nini wang’ang’anie kitu kinachowapa mzigo? Hakuna waliowacheka, wameamua, na sisi tuamue.
Nionavyo turudi tunakotoka na tujue kuwa siku hizi kila mtu duniani anapoharibikiwa hugeuka nyuma na kutizama ya kale, na kuamua kujirekebisha. Sasa sisi tumekuwa wa kwenda mbele pasi kutaka kurudi nyuma mfano wa nguruwe? Tujuwe hali hiyo inakuwa rahisi kujeruhiwa na dharba zake zimetufikisha kule kutojijua na kutojulikana.
Naona ipo haja ya kuunda chombo kitakachoangalia kumomonyoka kwa maadili na namna ya kuyarejesha, lakini isiwe tumesema twayataka haya, kikaundwa chombo wakatumbukizwa masarahangi hata kuogolea hawajui.
Nitaomba kiundwe chombo ambacho hakina hata uledi, kila mmoja ni nahodha akiumwa au akisinzia nahodha mkuu, mwengine ataongoza sawa sawa.
Nilitakalo kulisema ni kuwa hicho chombo ninachoomba kuasisiwa kiwe ni chombo kitachowakusanya na kuwahusisha watu wajuzi waliyoyaona yaliopita na ambao wana hisia za Ki-Zanzibari na kuona tunapotea na kupotoka.
Watu wa aina hiyo wataweza kuja na mashauri mjarab ya kutupeleka tulipopata kuwepo na kuwa Wazanzibari, badala ya kuwa kama tulivyo hivi sasa – vikaragosi kankula tembo.



