Wazanzibari waja juu kwa mafuta

Written by  //  27/10/2009  //  DIRA  //  Zima maoni

suala hili khasa. Au wizara hizi zimekwisha kuunganishwa, Bara na hapa?”

“Khalafu anakataa kuwa hakuhudhuria sherehe za utiaji saini wakati sote tunakumbuka kumuona katika TVZ akiwekwa amewekwa pembeni kabisa huku wakubwa wakitiliana saini,” alisema Milo

Alimuomba Rais Amani aliangalie tena suala hili ili haki itendeke kwa Zanzibar.

Mkaazi mmoja wa Chuini, Unguja, Mzee Suleiman Makame, ambaye amesema amefanya kazi katika utafiti wa awali wa maliasili ya mafuta Zanzibar, uliofanyika kijiji cha Kama katika miaka ya Khamsini, aliliambia Dira kuwa ameshangazwa sana kusikia mafuta ni suala la Muungano.

“Yote hii ni ghilba ya

kutaka tubaki maskini. Mbona dhahabu, almasi na mengine hayamo katika Muungano?” aliuliza, na kuongeza, “Lengo ni kutubana Zanzibar na kwa hili Wazanzibari lazima tushikamane kulipinga.”

Ustadh Mohamed Salum Aley, mfanyabiashara maarufu wa Darajani, amesema Wazanzibari hawako tayari kuona mafuta ya Zanzibar yanachimbwa na watu yasiyowahusu.

“Tutatetea rasilimali yetu kwa hali yoyote ile na tutahakikisha inainufaisha Zanzibar,” alisema.

Mfanyabiashara mwengine wa Marikiti, Zanzibar, Mohammed Abdalla, alisema mafuta yalikuwepo kabla ya Muungano kama yalivyokuwepo madini ya Bara. “Siyo busara kufanya hadaa dhidi ya Zanzibar.”

Aliongeza: “Tunasema

wazi, bora tumalizike sote. Tunayaambia makampuni ya mafuta yaliyojiingiza katika suala hili yaachane kabisa na mpango huo, isipokuwa kama watafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Serikali ya Zanzibar, sio na Serikali ya Muungano.”

Mkaazi wa Mbuyuni, Salma Magram, naye alimwambia mwandishi wetu kwamba mafuta ya Zanzibar hayajawahusu Bara. “Hatutaki, hatutaki, hatutaki,” alisema kwa msisitizo mkubwa.

Alisema, “Hata hao Wafalme hawakuthubutu. Walionesha imani zaidi kwa Zanzibar. Walitunga sheria kulinda maliasili ya visiwa hivi. Leo iweje Rais Karume awaachie ‘pwaa’! Hataki hata kufuata nyayo za baba yake?” aliuliza Salma.

Akifafanua alieleza: “Baba

yake alifika kutwambia ‘nyinyi watu wa Zanzibar utajiri wenu mkubwa kuliko watu wa Arabuni’. Aliyajua haya na ujasiri wake ukazidi kwa Zanzibar aliposema Azimo la Arusha mwisho Chumbe. Leo vyereje simba mtoto anayaachia mafuta yetu kiulaini?”

Hapo hapo Mbuyuni, Zahra Kombo alilishukuru Dira kwa kufichua mambo mengi na kulitaka liendelee na wajibu huo. “Msitishwe wala msibabaishwe,” alisema, “Sisi wazalendo tuko pamoja na nyinyi.”

Aliendelea kusema, “Kama kuna kitu kikubwa kilichogusa hisia zetu ni hii nakala ya Dira toleo Na. 009. Tunasema kwa kinywa kipana, ‘Uchungu wa mwana aujuaye mzazi; uchungu wa nchi aujuaye mwananchi’. Hatutaki hasama na wenzetu, lakini liso

budi hutendwa. Mafuta yetu watuachie tusimamie wenyewe uchimbaji.”

Naye Asha Salim Baashut wa Mchangani alisema, “Muungano si utumwa. Hatutaki nguvu zetu zende Bara. Kila kukicha ndugu zetu wa Bara wanazuka na mbinu mpya ya kuimaliza Zanzibar. Sasa wanadhamiria kuichukua rasilimali yetu ili ikatumiwe na wao. Hatuko tayari. Tutaandamana wakati wowote kuonesha hisia zetu.”

Ofisa mmoja mwandamizi wa SMZ, ambaye, kwa sababu zinazofahamika, hakutaka kutajwa jina gazetini, alithibitisha kwamba yote yaliyoandikwa na Dira ni kweli.

Alisema suala hili lilizungumzwa kwa kina katika Baraza la Mapinduzi na aliyekuwa Rais wa Zanzibar wa Awamu ya Tano, Dk. Salmin Amour alisimama kidete kukataa mafuta kuchimbwa na Bara. “Aliona hatari ya kumwagika damu, kwani wananchi wasingekubali hata kidogo.”

Alisema Dk. Salmin aliepusha hatari hiyo kwa mbinu mbali mbali.

Kutoka Pemba, Khamis Juma Seif wa macho mane Chake Chake aliliambia Dira kwa njia ya simu kwamba ameshtushwa sana na habari alizozisoma katika Dira kuhusu mafuta ya Zanzibar kuchimbwa na Bara.

Alisema maelezo marefu na ya kina yaliyotolewa na gazeti hili yanaweka wazi kwamba hili suala ni la kweli na sio uvumi tu.

Alisema hayuko tayari kuona mafuta hayo ambapo uchunguzi unaonesha mengi yako Pemba, yanachimbwa kwa misingi ile iliyoelezwa na Dira. “Tutasimama kutetea rasilimali hii na kuona inafaidisha Zanzibar baada ya mkasa wa karafuu.”

Kwa upande mwengine Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Burhan Saadat Haji, katika mazungumzo na vyombo vya habari, ambapo kama desturi yake hakualika mwakilishi wa Dira, alikanusha vikali habari hizi.

Alisema habari hii ni ya siku nyingi (kama ilivyosema Dira kuwa ilianza wakati wa Awamu ya Tano) na “Serikali bado haijatoa uamuzi, ingali inatafuta ushauri wa kitaalamu”. Aidha alikanusha kuwepo hafla ya kutiliana saini baina ya Serikali ya Muungano na Kampuni ya Antrim Energy. Huo ni uzushi, aliongeza..

Lakini mkaazi mmoja wa Bububu, Ali Mohamed Versi, alilisifu Dira kwa kuifichua habari hii kwa kusema, “Kwa vile Dira ni gazeti la ukweli limeweka na website (mtandao wa kampuni hiyo). Tumefuatilia na kukuta ni kweli, tena kweli tupu.”

Versi alisema Waziri Sadaat alipaswa kukanusha taarifa ya Antrim Energy kwani wao ndio walioutangazia ulimwengu habari hizo. Alisema, “Hatukubali hata

kidogo. Lazima sheria za tokea 1924 ziheshimiwe na SMZ isione haya kuyasimamia hayo.”

Habari zilizochapishwa na Dira zilieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ya Awamu ya Sita chini ya Rais Amani Abeid Karume imeridhia Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuchimba maliasili ya mafuta yalioko katika visiwa vya Zanzibar.

Habari hizo zilisema kwamba Shirika la Kuendeleza Mafuta Tanzania (TPDC) la Serikali ya Muungano limeshatia saini mkataba na kampuni ya Antrim Energy yenye makao makuu yake nchini Canada kuiruhusu kampuni hiyo kuanza kuchimba mafuta hayo.

Ikitumia mtandao wa kampuni hiyo ya Canada (www. antrimenergy.com) kama chanzo chake cha habari, toleo hilo la Dira Nam. 009 limesema Serikali ya Rais Karume ilitoa idhini hiyo mwezi Aprili, mwaka jana.

Hii ilirahisisha kazi ya kutiliana saini mkataba kati ya TPDC na Antrim Energy.

“Kampuni ya Antrim Energy inasema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyoitoa Aprili, mwaka jana kuwa ina furaha kutangaza kuwa imeondoshewa kipingamizi cha kuingia Zanzibar kilichokuwa kimewekwa mwaka 1998 na hivyo sasa inaweza kuanza kazi zake za uchimbaji,” linasema toleo hilo la Dira, likionesha na ramani iliyotangazwa na kampuni hiyo katika mtandao wake.

Kipingamizi hicho (force majure) kilichokuwa kimewekwa na Serikali ya Awamu ya Tano ya Dk. Salmin Amour kiliondolewa Apiril 17, mwaka jana na Serikali ya Rais Amani Abeid Karume.

Comments are closed.