Zanzibar bila Dira

Written by  //  29/10/2009  //  DIRA  //  Zima maoni

Na Ali N. Sultan

WAZANZIBARI wameshazoea kusoma gazeti la Dira kila Ijumaa kuanzia saa 4.00 asubuhi, takriban kwa mwaka mmoja sasa.

Tuangalie kinyume cha mambo, ile hadith ya Bwana Msa. Fikiria itakuwaje maisha ya wasomaji/Wazanzibari pale itapofika Ijumaa bila ya kusoma Dira? Bila ya kuwepo Dira mitaani, kama amri ya Serikali inayofikiria kulifungia gazeti la Dira ama kwa kutumia sheria ya usajili wa magazeti na majarida au amri ya mahkama, itatimizwa?.

Kwa mujibu wa tahrir ya Dira, na habari zilizopatikana baadaye, SMZ iko mbioni kulifungia gazeti hili. Lakini nani atafaidika na uamuzi kama huo?

Sababu ya msingi hakuna, lakini ni kwa kuwa tu wakubwa hawapendezwi na mada zinazochapishwa na gazeti hili.

Kwa kigezo cha aina yoyote ile, Dira imeweza kuwafumbua macho wananchi kama sehemu ya chombo chochote cha habari duniani, ikiwemo kuelimisha na kukuza utawala bora.

Wananchi sasa wanasoma habari zinazoandikwa na Dira kwa mujibu wa mnasaba wao. Wazanzibari watalikosa gazeti la Dira, pamoja na “dira ya mambo yao “. Kwa kipindi cha mwaka mmoja, “ujumbe kutoka gazeti la Dira, kuelekea dira yetu umepatikana”. Sasa hata kama litafungwa, itakuwa kazi bure tu – kufungwa kwa Dira hakuwezi kufuta ukweli wa mambo, zaidi kutaonyesha na kuhakikisha mahusiano ya watawala-watawaliwa yako vipi!

Zaidi, Dira halijaandika kitu kikubwa au mada ya kutisha au kuhatarisha amani na utulivu; au kile kinachoelezwa kuwa “kukumbusha yaliyopita”, kama wanavyodai watendaji wa SMZ akina Said Shaaban, aliyejitambulisha kama Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Kiongozi, na anayeshughulikia mambo ya habari; pamoja na Bwana Enzi Talib, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), katika maelezo yao mbele ya Baraza la Habari la Tanzania (MCT).

Maafisa wote wawili (Enzi na Shaban etal) walipotakiwa kuthibitisha mbele ya MCT ni “wapi Dira limeandika mambo ya hatari, au kuvunja amani na utulivu, au kuvunja Muungano”, bahati mbaya walishindwa, badala yake walitishia kuwa “dola inaweza kulifungia Dira”.

Badala ya hoja, tulisikia maneno kama absolute terms yanatumika katika kikao, bila ya kujua yametokea wapi! Tusisahau wale waliowafundisha watendaji wa serikali na chama maneno kama absolute terms ni wakoministi wa Ulaya ya Mashariki.

Sasa hawapo tena, na wao wamebadilika na wamebadilisha mitazamo ya nchi zao kuwa nzuri zaidi kisiasa (demokrasia) na uchumi wao umekua. Sisi tumeganda pale pale tukiendelea kuimba nyimbo yao ya wakati ule: absolute terms. Ama kweli, wakati wenzetu wakikimbia, sisi tunazidi kutambaa!

Ni kweli gazeti la Dira limeleta uamsho wa hali ya juu katika jamii ya Zanzibar ; lakini hiyo isiwe sababu ya kulifungia kwa sababu ya kufanya wema.

Kwa upande wa SMZ, hapa inanikumbusha ile tamthiliya ya William Shakespear alipoandika much ado about nothing, yaani kujishughulisha na jambo linaloonekana kuwa kubwa, kumbe si chochote si lolote.

Imekuwa ndio kawaida ya watendaji wote wa umma hapa kwetu. Wanaumiza vichwa vyao kwa kutaka kulishughulikia gazeti la Dira huku wakiacha mambo ya msingi ya kiutendaji serikalini.

Wameacha kushughulikia huduma kama ya maji; huduma za afya, na kushughulikia gazeti la Dira, ambalo halina jipya zaidi ya kuwafumbua wananchi macho wajue haki zao za kimsingi; tena zilizoelezwa ndani ya Katiba ya nchi. Na kinachofanywa na Dira ni jukumu lililokuwa la wajibu kwa serikali ilotakiwa iwe mbele, wengine wafuate.

Tusisahau kitu kimoja: kukubali kujikosoa na kukosolewa ni jambo muhimu sana katika jamii/nchi kama inataka kupiga hatua na kuendelea. Sasa vipi serikali ya kisasa (modern government) inayodai kuchaguliwa kihalali na inayoongozwa kwa misingi ya kidemokrasia na utawala bora, inakataa au kukasirika pale inapokosolewa?

Uvumilivu wa kisiasa na kukosolewa ndio kigezo muhimu cha kupima aina ya utawala wowote duniani. Gazeti la Dira limewapa ukurasa mzima waandike “kuelimisha wananchi” juu ya mtizamo wao au kusahihisha kilichopotoshwa na wameshindwa kutumia nafasi hiyo na wanabaki na absolute terms.

Ukisoma historia ya namna udikteta ulivyoanza na tawala mbali mbali zilizopita, utaona kuwa hata wale despots, watawala wa kidikteta waliokubuhu, walikuwa wanakaa na washauri wao, na walikuwa wanapokea zaidi pale wanapokosolewa.

Tuangalie matukio mbali mbali duniani, na tupitie safu za magazeti juu ya, mfano, vita vya Iraq , na matukio kama ya Septemba 11, 2001. Angalia mfano wa magazeti kama The New York Times, The Washingtonpost, The Daily Telegraph n.k, au vituo vya televisheni kama BBC, Fox News Network, n.k. Takriban vyombo vya habari hivyo, kwa namna moja au nyengine vimekuwa vikikosoa sera, au vitendo vya utawala wa Bush-Blair kwa Iraq.

The New York Times (www.nyt.com) ndio imekuwa mbele katika kukosoa au hata kupinga vita vya Iraq, tena wazi wazi. Gazeti hili pia limekuwa mstari wa mbele kupinga kutiwa watu kuzuizini huko Guantanamo Bay , Cuba .

Sijawahi kumsikia George Bush au wasaidizi kulisema The New York Times kwa vibaya hadharani au kulifungia au “kunyimwa kibali” cha kuandika. Bush au Blair, badala ya wao kuchukua mbinu za kishupavu kupambana na vyombo vya habari, wanatumia wasaidizi wao (spin doctors) wa Idara za Mawasiliano (communication and media departments) kuelezea ujumbe wa serikali.

Tuangalie mfano mwengine. Mahusiano ya vyombo vya habari vya Uingereza na Kasri ya Mfalme ya Buckingham Palace . Prince Charles amekumbwa na kashfa hivi karibuni, na kumekuwa na mfululizo wa kashfa kama hizi zinazoendelea kumkumba. Wanatumia amri za mahkama na mbinu nyengine za busara/kisheria, na kupitia idara zao za mawasiliano.

Hatujawahi kusikia mapambano baina yao na gazeti kama la The Sun au The Mirror. Magazeti haya yanaendelea kuandika kashfa hizi na zile hata kama Buckingham Palace imepeleka mahkamani ombi la kutaka kashfa hizi isichapishwe. Hatujasikia gazeti kufungwa au kunyimwa kibali cha kuchapisha gazeti, wala mhariri kuambiwa “sio raia”.

Zanzibar tunayo idara/kitengo cha mawasiliano Ikulu, ambayo moja kati ya kazi zake ni kuipa haiba nzuri serikali, kujenga mawasiliano mazuri baina yake na raia (watawala-watawaliwa). Bahati mbaya sana, idara hizi ndio zimeanzisha mapambano ya kihabari baina yao, serikali na vyombo vya habari au kuishia kuandika press statements tu. Tujifunze kwa wenzetu, na tukubali kujifunza, kukosolewa, kujikosoa na hata kuelekezwa au kuiga mazuri kutoka kwa wenzetu.

Tukumbuke kuwa hakuna hata wakati mmoja katika historia ya binadamu, aina yoyote ya ubabe ndio umeimarisha jamii, badala yake demokrasia na utawala mzuri wenye mahusiano mema ndio umeonyesha nuru katika jamii — busara na fikra njema ndio zitawale.

Katika fani ya habari kitu kimoja muhimu sana ni kujiamini: “…changing the news won’t change the situation. Improving the situation will change the news…”, yaani kutoa au kubadilisha aina fulani ya habari kwa ihsani ya upande mmoja haiwezi kubadilisha hali ya mambo, muhimu tubadilishe hali yenyewe, na hapo habari zitabadilika zenyewe.

Kwa mfano, tubadilishe hali ya upatikanaji wa maji Zanzibar, au katika hospitali ya Mnazi Moja, tuone kama kutatokea mwandishi atayeandika kuwa “Zanzibar au hospitali ya Mnazi Mmoja hakuna maji”? Lakini kama tatizo la maji linawakabil wananchi na hakuna hata maelezo zaidi ya yale “kuendelea kuwa wastahmilivu na mipango iko mbioni kutatua tatizo hili”, sidhani kama itasaidia kuwafanya waandishi – iwe wa Dira au wengineo wanaotumia akili zao kuacha kuandika habari hizo.

Kwa wale wanaojiita wasomi, naomba wafumbue macho, na kuona ulimwengu unavyokwenda, ikiwezekana, waishauri serikali na kuilekeza kuwa na mtazamo mpya wa kisasa. Majungu, fitna, ushawishi na kuweka ukereketwa mbele wa huyu mwenzetu na yule si mwenzetu kuliko kazi na majukumu ya umma, havisaidii Zanzibar wala hao wanaotia ushawishi na kupika majungu.

Sasa tuangalie uwezekano wa kulifungia Dira, na kwa sababu gani za msingi. Kutakuwa na mantiki nyingi za kuangalia. Kwanza ile dhana ya kufungia gazeti au kunyang’anya leseni. Unaponyang’anywa leseni – iwe ya kuchapa gazeti au kufanya biashara inalazimika ziwepo sababu.

Muhimu sana inakuwa mmiliki wa leseni ya kufanyia biashara amekiuka au amevunja masharti aliyopewa. Je, kuna sababu zozote zitazoweza kushawishi na kubainisha kuwa Dira limekiuka masharti ya leseni?

Ninavyofahamu kidogo ni kuwa gazeti linapewa kibali cha kuchapisha kwa idhini ya Idara ya Habari Maelezo Zanzibar (Bara kadhalika). Masharti ya kunyimwa kibali/leseni yapo mengi, lakini la msingi ni kuwa “kama gazeti limesajiliwa; lakini limeshindwa kuchapisha hata kopi moja angalau kwa kipindi cha mwaka mmoja”.

Hapo inaweza kuangaliwa upya [sio kunyimwa moja kwa moja]. Kutokana na hali kama hiyo, inawezekana kuwa uwezo wa kifedha na utendaji wa menejimeti ya gazeti unatiliwa shaka. Je, hali kama hii inapatikana katika gazeti la Dira? Jawabu: hapana.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za wachapishaji, Dira limeanza na kutoa nakala 3,000 kila wiki na; sasa Dira inachapisha nakala karibu 15,000. Maana yake ni kuwa Dira limechota wasomaji wengi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kuliko gazeti lolote la wiki au la kila siku. Hilo sio gazeti la kufungia kwa sababu kwanza linasomwa na wengi, na linauza, linauzika na linanunulika, tafauti na yale ambayo baadhi yetu tunayakumbatia na watu hawataki kuyasoma.

Katika mtafaruk huu wa Dira v.s SMZ inanikumbusha mambo matatu muhimu: (i) matatizo ya gazeti la Daily News la Zimbabwe . Gazeti hili limekabiliwa na hali sawa sawa inayoikabili Dira, kwa sababu linaikosoa serikali ya Robert Mugabe, na haikubaliani na vitendo vyake.

Gazeti hili limezuiliwa kuchapishwa chini ya sheria ya Zimbabwe ya vyombo vya habari – sheria ambayo dunia nzima imeilaani kwa sababu ina sura ya ukandamizaji wa uhuru wa habari. Kichekesho ni kuwa mahkama ya Zimbabwe imetoa ruhusa ya uchapishaji tena wa gazeti hilo kupitia kampuni yake ya Associated Newspapers of Zimbabwe (ANZ), lakini amri hii imepingwa kwa mlango wa nyuma na mahkama kubwa zaidi (supreme court).

(ii) Jambo la pili katika mkasa huu wa Dira v.s SMZ ni hotuba ya George Bush, Jr. ya wiki mbili nyuma aliposema na kulaumu kuwa “nchi za Kiislamu hakuna demokrasia na lazima wabadilishe hali ya mfumo wa kisiasa, iwe ya demokrasia zaidi”. Binafsi nakubaliana naye.

Naamini kuwa Zanzibar ina Waislamu wengi lakini yale mambo muhimu katika Uislamu tunayotakiwa tuyafanye hatuyafanyi. Naamini kuwa demokrasia ni mali yetu Waislamu, lakini imeshatutoka.

Uislamu umeruhusu uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa mahkama, utawala bora, kuchagua viongozi kwa njia za busara na kidemokrasia. Sasa tuangalie baina ya “sisi” na “wao”. Nani mwenye mtazamo mzuri wa demokrasia na kutenda haki?

(iii) Inanikumbusha hotuba ya Dk. Mahathir Mohammed, Waziri Mkuu mstaafu wa Malaysia alipokuwa akiwaaga Wamalaysia na kustaafu pale alipotulaumu Waislamu na mataifa ya Kiislamu kuwa tumekosa muelekeo wa maisha yetu.

Kutaka kulifungia Dira na kulipa tough kila wakati ni dalili za kutosha kuwa tumekosa huo muelekeo anaouzungumza Dk. Mahathir.

Wanaoongozwa Zanzibar wengi ni Waislamu, takriban viongozi wote wa juu ni Waislamu. Leo vipi wanaiwacha hali kama hii iendelee katika jamii, vipi wanaruhusu watu kutotendewa haki. Vipi wasomi, masheikh wa Wakf, Kadhi Mkuu, Mufti Mkuu n.k na viongozi wengine wa Kiislam wameamua kubaki kimya.

Inafaa kujiuliza mengi hapa: Nini jukumu la wasomi katika jamii? Vipi wasomi wa Zanzibar wasiweze kuishauri serikali kwa nasaha ili kupunguza makali kwa amri zake dhidi ya Dira. Hii inawezekana, lakini wasomi wetu, pamoja na wanasheria wetu wameamua kubaki bila ya kuwa na muelekeo (huo aliouzungumza Dk.Mahathir).

Eid Mubarak!

Comments are closed.