Habari

Dk Salmin: Msikubali Mapinduzi kufutwa Zanzibar

Dk Salmin: Msikubali Mapinduzi kufutwa Zanzibar
NA MWINYI SADALLAH
3rd July 2013

Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar walipo mtembelea nyumbani kwake Migombani na kusisitiza umuhimu wa kulinda misingi ya Mapinduzi ya Zanzibar.Picha na Mwinyi Sadallah, Zanzibar

Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour Juma, amewataka vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kusimama imara katika kulinda uhuru na mapinduzi matukufu ya Zanzibar, ili kupinga nadharia aliyosema ya kinyang’au inayokumbatia ukoloni.

Dk. Salmin alitoa kauli hiyo nyumbani kwake Migombani, Zanzibar jana, mara baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, kumaliza ziara yake ya siku sita katika mikoa mitatu ya Unguja.

Rais huyo mstaafu alisema, uhuru wa watu hupatikana mara moja hivyo vijana ambao ni kizazi kipya wana jiukumu la kuulinda uhuru ulioletwa na TANU pamoja na kuyatetea Mapinduzi ya ASP.

“Ingawaje kazi ya jumuiya yenu ni kuimarisha chama, kazi muhimu ya bidii ni kupambana na manyang’ au wanaotaka kupora uhuru wenu au kuyatekeketeza Mapinduzi ya Zanzibar” alisema Dk. Salmin maarufu kwa jina la Kamandoo.

Alisema nchi za Kiafrika, Marekani na Ulaya zilikataa kutawaliwa baada ya vijana wao kujitolea kupingana na ukoloni hadi pale uhuru kamili dhuluma na udanganyifu viliipoondoshwa na watu kuanza kujitawaliwa na kujiamlia mambo yao wenyewe

“Kina Mahatima Gandhi, Martin Luther King Jr, Lenin, Karl Max na wengine, walikikataa kutawaliwa katika nchi zao hadi walipopata tunu ya uhuru, hebu inukeni, simameni pia lindeni uhuru wenu, ukipotea hamtaupata milele” aliwaasa vijana.

Akizuingumzia mabadiliko ya mfumo wa kisiasa nchini, alisema ni vyema vijana wakatambua kuwa huko nyuma kulikuwa na mfumo wa chama kimoja ambao ulitoa nafasi ya wananchi na viongzi wao kuwa na misimamo ya pamoja kuliko ilivyo sasa.

“Sasa kuna vyama vingi, hilo ni jambo jema, indhari yangu kwenu mfumo huo usitoe mwanya na ruksa ya kuwaachia wenye mawazo ya kukumbatia wakoloni wakapenya na kutimiza malengo yao, msikubali kuitupa nchi yenu” alisisitiza Dk. Salmin.

Share: