Habari

Dr Shein acha kuwadanganya Wazanzibar

Na Rushdy Ahmed

AIBU tena kubwa sana kwa msomi wa PhD kusema kuwa Zanzibar, haikupata uhuru. Mambo mengine ni unafiki na hulka za kishenzi hata kuyasema ni vichekesho na vioja.

Kiongozi kama huyu, ni hatari sana, akiambiwa na watu akina Kikwete na Magufuli kuwa atakuwa Rais wa Zanzibar kwa maisha yake yote (milele) lakini, akubali kuwa kafiri yaani aachane na uislamu, naamini yuko tayari.

Haiwezekani kuwa anajinasibu kuwa ni mzanzibari, tena msomi wa PhD na kwa umri wake naamini anafahamu vizuri tarehe ambayo Zanzibar, ilipopata uhuru wake, leo akaweza kuukana hadharani. Wote ni utamu wa madaraka jamani!!.mmh lazima tujiulize au kashakuwa chizi?.

Akiulizwa na akipewa picha ya Karume (Abeid Amani), Rais wa ‘Afro Shirazi Party’ akiwa katika mkutono wa London, (Lancaster House). Huu ulikuwa mkutano wa kuipa Zanzibar uhuru wake. Hivyo, Karume alikwenda ‘Lancaster House’ na timu yake kufanya nini?.

Hassan Nassor Moyo (Mzee Moyo),’ bado yuko hai na timamu wa akili’ maisha yake yote yuko katika Afro Shirazi na katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, aulizwe, atasema kwamba Zanzibar, ilipata uhuru au haikupata uhuru?.

Mbali na Mzee Moyo, na watu wengine wengi wapo hai bado, waulizwe, wanajuwa ukweli zaidi kuhusu hoja ya uhuru wa Zanzibar.

Asiachiwe huyu mnafiki (chambilicho watu: KINYAGO CHA MPAPURE), huyu rais gani anayepotosha watu kwa jambo ambalo lilitokea na Wazanzibari wanajuwa na dunia yote inajuwa.

Vitabu vya historia vipo na katika mitandao, nenda kwenye GOOGLE, ukipiga tu uhuru wa Zanzibar, umeelezwa A-Z. Google tabaan (mwiko) kuwa na taarifa za uongo.

Anatokea mnafiki anapotosha watu. Ati huyo ni kiongozi wa nchi. Kiongozi gani wa nchi anayefanya hivyo?. Kwa nini anapotosha watu au ni ile dhuluma ya uchaguzi wa Machi 20, inamtesa.

Hivyo, kweli yeye peke yake ndiyo hajui kuwa Zanzibar, ilipata uhuru…basi usomi wake umepigwa na laana na wala hafai hata kuwa rais wa kuongoza hata kuku, achilia mbali kuongoza watu.

Hakuna jambo baya kama dhuluma mwishowe unaangukia kupotosha watu na kuwapotosha watoto wadogo waliyoko maskulini katika masoma. Shein na Mapuri wote kapu moja kwa upotoshaji. Hatari sana watu wa aina hii.

NASHAURI: Watu waliyekaribu naye ‘huyu msomi mjinga’ (Shein) wampelekee kile kitabu cha Dr Harith Ghassany – ‘Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru.’ atajuwa kuwa Zanzibar, ilipata uhuru au la.

Nakumbuka miaka 1980s: Marehemu Aboud Jumbe (Rais wa Zanzibar awamu pili), katika mkutano mmoja wa ndani uliyofanyika katika ukumbi wa ‘Umoja ni Nguvu’, Mkoani alimwambia Bi Ashura Abeid Maftaha (Mwenyekiti wa UWT – Mkoa wa Kusini Pemba)

Nanukuu: “Kunyamaza kimya ni ustaraabu mkubwa…kuliko kusema kitu unachokijuwa ukapotosha watu kwa kukibadilisha ukweli wake, au kusema kitu ilhali hukijui, ukajifanya unakijuwa…wanaojuwa watakudharau na kukucheka na wasiyojuwa wataendelea kuwasimulia wenzao ujinga na hiyo ndiyo hatari.”

Mzee Aboud Jumbe, muda wote aliyokuwa kiongozi wa Zanzibar, sikuwahi kumsikia kukanusha kusema kuwa Zanzibar, haikupata uhuru.

Na sijui kama angesema Zanzibar, haikuwahi kupata uhuru, engeonekana vipi mbele ya macho ya Wazanzibari;
Hata waliyokuja baadaye akina Ali Hassan Mwinyi, Maalim Idriss, Dk Salmin (Komando) na Amani Karume (Junior), sikuwahi kuwasikia kusema kwamba Zanzibar, haikupata uhuru. Isipokuwa huyu ‘Kinyago cha Mpapure.’

Tunaweza tukasema japo walikuwa hawalitaji neno hilo la uhuru wa Zanzibar au hawakupenda kulitaja, lakini walijaribu kunyamaza kimya. Hawakuthubutu kusimama juu ya jukwaa la mkutano wa hadhara, wakaukana.

Lakini, Shein anawapotosha wanafunzi na wazee (ati jamaa zake wa kwao, Mkanyageni) “Zanzibar, haikuapata uhuru na uhuru wa Zanzibar ni mapinduzi ya Januari 12, 1964. Lugha ya kinafiki, iliyojaa ujinga na upotoshaji isiyo stahiki kusemwa kwa mtu aina ya Shein.

Wallahi naapa kwamba, iko siku Dunia itamsuta na kumuhukumu…atadhalilika kutokana na matamshi yake. Dunia uwanja wa fujo. Uhuru wa Zanzibar, Karume wa ASP, alishiriki kuudai, anakuja mtu anasema Zanzibar, haikupata uhuru wake!! ALLAHU AKBARU..

Share: