Habari

EEZ SI HOJA YA JUSSA NI YA WAZANZIBARI

Mhe. Ismai Jussa Ladhu ambae ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi – CUF na Mwakilishi wa Jimbo la mji Mkongwe ni mwanasiasa makini asiyeyumbayumba, hodari mchapa kazi na mwenye uzoefu wa kutosha katika fani yake ya siasa. Jussa ni bingwa wa kulimudu jukwaa na kumvutia kila anaemsikiiza kwa ufasaha na utamaduni wake wa kuzungumza mambo kwa uchambuzi na kwa msingi wa hoja. Jussa katika harakati zake za kisiasa na hata katika utendaji wa shughuli zake anangozwa na kanuni ya kuweka mbele uwazi na ukweli. Hii ndio maana wasiompenda yeye binafsi au wasiopenda uwajibikaji humuona Jussa ni kipingamizi au mara nyengine adui wa mambo yao.

Mhe Jussa si mtu wa kukurupuka bali ni mtafiti na muweka mbele nguvu ya hoja katika kauli zake, nadharia zake, maoni yake, falsafa zake na hata matendo yake. Hii ndio maana hamasa za wana- CUF mara zote huwa juu pale mwanasiasa huyu anapopanda katika jukwaa. Baada ya kuwa mjumbe wa baraza la wawakiishi ndani ya serikali ya Umoja wa kitaifa ya Zanzibar matumaini ya watu kwa Jussa yametanuka kwa kasi mno kutoka kwa wana- CUF hadi kwa wazanzibari wote baada ya kuamini kwamba mwanasiasa huyu ni mkweli na mtetezi wa maslahi ya wazanzibari kwa ujumla wao na hamugopi yeyote katika kutekeleza majukumu yake hayo. Wazanzibari wote kwa ujumla wao sasa hawana wasiwasi wakifahamu katika chombo chao cha kuwatetea, baraza la wawakiishi, kuna mwanasiasa makini Ismail Jussa ambae huhoji bila woga jambo lote isilokwenda sambamba na matashi ya wazanzibari. Tukisema hivi hatumaanishi hakuna wengine katika baraza la wawakiishi au ndani ya Zanzibar ambao wazanzibari wamejenga matumaini yao, wapo, lakini kwa wanasiasa wa rika lake yeye bado mpaka sasa anabakia kama nyota ing’arayo.

Jussa ni mtaalamu wa siasa kwa nadharia na utendaji na mwenye uzoefu wa muda mrefu. Amekuwa akikiunganisha chama cha CUF na mataifa ya nje kwa muda mrefu na hivyo kuwa mtu mweledi wa siasa za kilimwengu na hivyo kuweza kumudu vyema mazingira yote ya kisiasa pamoja na changamoto za kisiasa za kila nyakati ndani ya nchi yetu na kuzaa fikra za mabadiliko ya msingi katika mwelekeo wa siasa na utawala ndani ya chama na nchi yetu. Jussa ni mweledi wa historia ya ndani ya nchi yetu na ya ulimwengu kiujumla, hivyo si rahisi kumburuza na kumtoa katika uhalisia wa mambo mbali mbali yaliyojiri na yanayojiri ndani ya nchi yetu. Kupitia udadisi wake makini wa kihistoria amekuwa ni mtu anaeifahamu sana Zanzibar. Pia anaifahamu sana Tanganyika na halkadhalika anaifahamu sana Tanzania. Hii ndio maana mara nyingi anapotoa hoja yoyote yenye msingi wa kihistoria, kisiasa au kitaifa basi hupita vyema katika uhalisia wake na sio kukurupuka, hivyo kuibuka kuzipiku hoja dhaifu hata zinazotlewa na watu wenye vyeo vikubwa hapa nchini.

Katiaka makala yake inaysema Jussa: Zanzibar ni koloni la Tanzania? Aliyoichapisha katika gazeti a Mwanahalisi la tarehe 25-31 Januari 2012, Mbasha Asenga ameandika kuhusu Ismail Jussa akimsifu na wakati huo huo akimponda. Lakini haishangazi kwani mwandishi huyu wa makala ni hodari wa kuandika makala zisizo na nguvu ya hoja, zisizo na kichwa wala miguu na zinazoandikwa kwa madhumuni ya kukichafua chama cha CUF na viongozi wake na kukifagilia chama cha CHADEMA. Hivyo basi, mwandishi yupo zaidi kutumikia siasa za CHADEMA na sio kueleza uhalisia wa mambo. Katika Makala yake hiyo mwandishi amepotosha mengi, basi nimeonelea ni vyema nikatumia makala yangu hii kumsahihisha juu ya kile alichokiandika ili yeye na wasomaji wake wapate kuelewa uhalisia wa alichokiandika badala ya kuendekeza ushabiki wake na upotoshaji. Katika makala hii hatutafundishana historia ya Zanzibar, ya Tanganyika wala ya Muungano kwa kuwa sio maudhui yake ila nitazichambua hoja dhaifu za Mbasha Asenga kwa kutumia suala hili hili alilolitumia yeye lililozuka hivi karibuni, ambalo ni hatua ya Jamhuri ya Munngano kupeleka ombi katika Umoja wa mataifa kutaka kuongezewa ziada ya eneo la bahari (Exclussive Economic Zone- EEZ). Mwandishi ametumia suala hilo na kujenga hoja zinazolenga kumchafua Mhe Jussa binafsi na Chama cha CUF kwa maslahi na ushabiki wa chama cha CHADEMA. Lengo la Mbasha Asenga ni kufanikisha kujenga picha potofu kwa Watanzania ya kwamba chama cha CUF na vingozi wake wanaonekana hawaitaki na wanaichukia Tanganyika kama vile CHADEMA ilivyokuwa haiitaki na inaichukia Zanzibar.

Kwa mujibu wa makala yake, Mbasha Asenga anaonekana haijui vyema historia ya Muungano wetu wa Tanzania na kwa maaana hiyo siachi wasiwasi wangu kwamba hajui historia ya Zanzibar nchi ambayo ilikuwepo karne nyingi kabla ya Tanganyika. Kama wasiwasi wangu huu ni kweli basi simshangai Mbasha Asenga kutokukujua kwamba Nyrere na Karume walipounganisha nchi mbili ya Tanganyika na Zanzibar hawakuiweka bahari katika orodha ya mambo ya Muungano. Na hata baada ya Tanganyika kuuchakachua mkataba wa muungano wa kimataifa kati ya Zanzibar na Tanganyika, kwa kuongeza mambo ya muungano kinyemela bila ya kuishirikisha Zanzibar kama nchi mwenza (partner state) katika Muungano ambapo kufanya hivyo ni kosa kwa sheria za kimataifa, suala la bahari bado mpaka sasa lingali si suala la Muungano.

Sasa nije katika hoja zake mwandishi alizozitoa katika makala yake hiyo kama vile 1. Jussa hajafunguka kisiasa, 2. Jussa anaamini katika himaya ndogo ndogo, yaani Uzanzibari na si Utanzania, 3. CUF inapigania Uzanzibari na si Utanzania, 4. Jussa kupinga Tanzania kuongezewa eneo zaidi la bahari na hoja nyengine kama hizo.

Tanzania ni nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar. Nchi zote mbii hizi zina mipaka yake na mamlaka yake. Mipaka na mamlaka ya Zanzibar yameelezwa vizuri katika katiba ya Zanzibar. Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 1 inaeleza, “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar”. Hivyo basi katika Jamhuri ya muungano kuna nchi ya Zanzibar, na ukiitoa nchi hiyo inabaki nchi ya Tanganyika. Kwa bahati mbaya sana upande wa Tanganyika wameikataa nchi yao na kulikataa hata jina lake la Tanganyika na kutunga jina jipya linaloitwa Tanzania bara. Kama suala la upande wa Tanganyika kutupa nchi yao na kufuta jina si la bahati mbaya na linaonekana ni sawa basi kwa upande wa Zanzibar si sawa hata kidogo. Kwa wazanzibari ni kosa kubwa lisilosameheka kwa mtu yoyote kujaribu kuondoa nchi au jina la Zanzibar. Kwa maana hiyo kama Watanganyika hawapo tena basi ni tofauti kabisa kwa upande wa pili. Wazanzibari wapo na ni wazalendo kikwelikweli wa kizanzibari kwanza halafu ndio unafuata Utanzania. Wazanzibari wana utamaduni wao na historia yao tofauti na Tanganyika au nchi nyengine za Afrika ya Mashariki inayopaswa kulindwa na kuenziwa kwa maslahi ya wazanzibari.

Hoja ya kupinga Jamhuri ya muungano kuongezwa eneo la bahari jambo ambalo kimsingi halimo katika orodha ya mambo ya muungano si hoja ya Jussa bali ni hoja ya wazanzibari wote. Mbasha Asenga anaonekana si mfuatiliaji mzuri wa yale yanayojiri Zanzibar kama upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano. Halkadhalika anaonekana hafahamu kama huku Zanzibar kuna Serikali yenye katiba yake, yenye mamlaka yake, yenye Rais wake, yenye Baraza la Mapinduzi (Baraza la Mawaziri la Zanzibar), yenye Baraza la Wawakiishi (Bunge la Zanzibar), yenye Mahakama zake na mambo yote mengine muhimu ya kiutawala. Mbasha hajui kwamba Zanzibar inatunga sera zake za kuendesha nchi, ina bajeti yake, inapitisha maamuzi yake ya kinchi kwa maslahi ya watu wake, yaani wazanzibari na ndio Serikali ambayo wazanzibari wanayoitambua kama mdhamini wa mambo yao yote.

Mwaka 2009 Baraza la Mapinduzi lilipitisha uwamuzi wa kuliondoa suala la mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya muungano, wakati huo Jussa si mwakiishi wala chama chake CUF si mdau wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kuhusu suala la bahari kuu, na Eneo tengefu la kiuchumi (Exclussive economic Zone – EEZ) nalo Baraza la wawakiishi katika kikao chake cha tarehe 08 Aprili, 2009, (Baraza la Saba, Mkutano wa Kumi na Tano), lilikuwa na mjadala mzito wa siku tatu mfululizo kuhusu ‘Taarifa ya Mapendekezo ya Serikali kuhusu Ripoti ya Mshauri Muelekezi juu ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia’ ambapo kutokana na uzito wake, wajumbe 49 wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri wengi wa wakati ule na pia Waheshimiwa Mawaziri wengi tulio nao sasa walichangia mjadala huo, tena kwa hisia kali za kizalendo na mapenzi ya kweli kwa nchi yetu tukufu. Baada ya mjadala huo, hatimaye Mheshimiwa Spika aliwahoji Wajumbe kuhusiana na maazimio matatu yaliyowasilishwa na Serikali. Azimio la tatu lilikuwa ni lile la kutaka “exclussive ecnmic zone” (EEZ) isiwe ya mashirikiano kati ya serikali ya Jamhuri ya muungano na serikali ya Zanzibar bali suala hilo lishughuikiwe na Zanzibar Peke yake. Kwa msingi huo ingetegemewa basi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano isichukue hatua zozote zitakazopelekea kuyafanya maazimio haya ya Baraza la Wawakilishi ambayo ndiyo msimamo rasmi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yakawa hayana maana tena. Kitendo cha kupeleka maombi Umoja wa Mataifa kutaka kuongezewa ukanda wa bahari kuu ambao tayari Zanzibar imeamua kila upande isimamie wenyewe, ni kwenda kinyume na dhamira (spirit) hiyo na hakiashirii kuwepo kwa nia njema.

Masuala hayo mawili yalioamuliwa na mihimii miwili mikuu ya seriakli ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2009 ndio ambayo Jussa alilikumbushia katika Baraza a wawakiishi hivi juzi. Hivyo basi kinachotengua hatua ya Jamhuri ya muungano kuomba eneo hilo katika Umoja wa Mataifa si hoja ya Jussa bali ni uwamuzi wa SMZ. Liko wapi kosa la Jussa hapo kwa hatua yake ya kukumbusha maamuzi ya SMZ ambayo yeye mwenyewe hakushiriki kuyafanya? Kwa nini Mbasha Asenga asiseme seriakali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyotoa msimamo na maamuzi hayo tokea mwaka 2009 ndio inayoamini himaya ndogo ndogo (Uzanzibari ) na kupuuza Utanzania? Baraza la Mapinduzi la Zanzibar la mwaka 2009 lilikuwa na Mawaziri kutoka CCM tu Pale Iilipoamua kuyaondoa mafuta na gesi asilia kutoka katika orodha ya mambo ya muungano, jee CCM hapa haitetei Uzanzibari na kupuuza Utanzania kwa mujibu wa hoja ya Asenga? Jee CCM hapa kwa hoja hiyo hiyo haiamini mamlaka ndogo ndogo? Baraza la Wawakiishi la Zanzibar wakati azimio la EEZ linapitishwa mwaka 2009 lilikuwa na theluthi 2 ya wajumbe kutoka CCM ambao wana uwezo wa kupitisha maamuzi yeyote bila ya kura za wajumbe wa CUF, kinyume na sasa ambapo hakuna chama kati ya CCM na CUF kinachofikisha theluthi 2 za wajumbe katika Baraza hilo. Utawezaje kuuita uwamuzi huo au msimamo huo wa mwaka 2009 kuwa ni wa CUF? Hoja ya hivi juzi ya Mhe Jussa ambayo ndio inayomuumiza kichwa Mbasha Asenga ya kukumbushia lazimio la Baraza la Wawakilishi la mwaka 2009 iliungwa mkono kwa hisia kali na wajumbe 8 wa Baraza la Wawakilishi, kwa uwiano sawa kwa sawa kutoka CUF na CCM, tena inakuwaje hata CUF peke yake katika hoja hii ndiyo inayotetea Uzanzibari na siyo CCM?

Hapa ndipo ninaposema Mbasha Asenga ni mwana propaganda safi wa CHADEMA na sio mchambuzi na wala haelewi kitu katika uchambuzi wa mambo haya ya siasa za Tanzania katika uhalisia wake, na si mwenye lengo la kuwafahamisha Watanzania ukweli. Maoni yangu kwa Asenga asiamini kwamba Wazanzibari wakipigania haki za nchi yao wameukataa Muungano bali kilicho muhimu kwake ni kwamba na yeye aamini kama ni Mtanganyika na hivyo ana kila sababu ya kudai nchi yake iliyofutwa jina lake na Nyerere.

Tagseez
Share: