Ni Nini Hatma ya Soka la Zanzibar Baada ya Uchaguzi wa Tareh
Nafikiri sote tutakubaliana kuwa mabadiliko katika uendeshaji wa soka nchini mwetu ni kitu cha lazima.Kwani soka kwa sasa linaendeshwa kibiashara,soka linatumika kuitangaza nchi,kupitia soka ajira zinapatikana na soka katika sehemu mbali mbali ulimwenguni linatumika katika kuchangia shughuli mbali mbali za kijamii.Vile vile soka limesaidia wale vijana wenye vipaji kuinua hali zao za maisha katika nchi mbali mbali za ulimwengu wa tatu.Hata hivyo mambo kama hayo hayawezi kufikiwa bila ya kupata uongozi wenye mtazamo wa muda mrefu wa kubadili hali nzima ya uendeshaji soka nchini mwetu.
Hakuna anaekataa kuwa uongozi wa sasa wa ZFA kuna mambo mazuri iliyotenda katika kipindi chao cha uongozi.Hata hivyo ukipima hayo mafanikio yao na hali ya soka nchini mwetu utakuta mezani inalalia upande wa kushindwa kwenye suala zima la uendeshaji wa soka visiwani mwetu.Kipindi cha miaka ishirini kwenye uongozi ni kikubwa kwenye uongozi wo wote ule, hasa ikifikia kuwa yule anaeongoza anasimamia katika kuanguka au kudorora kile ambacho kiko chini ya mamlaka yake.Hali ndiyo ilivyo chini ya uongozi wa sasa wa Rais wa ZFA.
Amesimamia katika kuanguka kwa hali ya soka visiwani mwetu, rushwa ndani ya soka la Zanzibar,kuanguka kwa timu kongwe za mitaani, kupungua kwa mahudhurio katika viwanja vyetu, migongano kati ya chama cha mpira na serikali, na baya zaidi ni kashfa ya hivi majuzi tu ya kuchezesha mchezaji aliyezidi umri katika mashindano ya vijana yaliyofanyika huko Asmara.Kwa kweli kashfa hiyo ni aibu kwa nchi yetu kama aibu ilopata nchi ya Pakistani kutokana na kashfa iliyowahusisha wachezaji wao wa kriketi.Kama ilivyo kawaida yetu hakuna aliyekubali kuwajibika katika kashfa hii.Sasa tujiulize pindipo tungekuwa wanachama wa FIFA na hili la kuchezesha mchezaji aliezidi umri lingefanyika kwenye mashindano yanayosimamiwa na shirikisho hilo, nini athari yake ingekuwa kwa nchi yetu na adhabu ambayo ingetolewa kwa ushiriki wa nchi kwenye mashindano yanayosimamiwa na shirikisho hilo.?
Hata hivyo kutowajibika kiongozi yo yote wa ZFA kwenye kashfa hiyo ni ushahidi mwengine wa kibri cha muda mrefu ambacho kimejengeka ndani ya uongozi wa ZFA.Jeuri na kibri cha kujua kwamba hakuna ye yote ambaye anaweza kuchukua hatua dhidi yao.Hapa inapaswa kufahamu kuwa hiki kibri kitazidi chini ya uongozi huu pindipo nchi yetu itapata huo uwanachama wa FIFA.Kwani kama nilivyoeleza kwenye sehemu ya kwanza, shirikisho hilo haliruhusu chombo cho chote kile kuanzia serikali na hata mahakama kuingilia masuala yanayohusu vyama vya mpira duniani.Athari ya uamuzi huu kwa nchi kama zetu za ulimwengu wa tatu ni kubwa.Mfano mdogo ni kwa hao ndugu zetu Tanganyika, sote tunakumbuka jeuri na kibri alichokuwa nacho Ndolanga alipokuwa akiiongoza TFF.Sasa tujiulize jee kweli inafaa uongozi uliopo wa ZFA kurejeshwa madarakani tukiwa tunaelekea kwenye uwezekano wa kupata uwanachama wa FIFA?
Pindipo tukifanikiwa kuupata huo uwanachama wa FIFA historia itawahukumu kwa kufanikisha hilo, lakini hiyo isiwe sababu ya kupewa dhamana ya kusimamia mpira wa miguu visiwani mwetu.Wasi wasi wangu ni kuwa uongozi wa sasa wa ZFA pindipo ukirudi madarakani na nchi yetu ikapata huo uwanachama wa FIFA,basi sheria zitabadilishwa ili kufanya masharti ya kugombea uongozi ndani ya chama hicho kuwa magumu.Hivyo kuwazuia wengine kugombea na kuhakikisha wao wanaendelea kubaki madarakani kwa kipindi kirefu.
Waswahili wamesema ‘Shetani likujualo halikuli likakwisha’na hiyo ndiyo hali inavyoonekana ndani ya ZFA.Hivi karibuni kulikuwa na tetesi kuwa Rais wa sasa wa ZFA anafikiria kutogombea tena hiyo nafasi baada ya kuwa kitini kwa miaka ishirini mfululizo.Muda haukupita akatokea kiongozi mwengine ambaye ni Katibu Msaidizi wa ZFA akanukuliwa akisema kwamba CAF na CECAFA zimemuomba Rais huyo kufikiria tena uamuzi wake huo wa kutokugombea kwani ataacha pengo katika shughuli za uongozi wa soka.Sasa hapa inabidi tujiulize hili ni kweli na kama ni kweli jee huyu Rais wa ZFA yuko pale kwa maslahi ya soka la Zanzibar au la hayo mashirika? Jee huyu katibu anataka kutuambia kuwa hakuna mzanzibari mwengine ambaye mwenye uwezo na sifa za kushika hiyo nafasi? Mimi ningemfahamu huyu Katibu kama angesema kuwa bado uongozi uliopo chini ya Rais wake kuna programmes na ajenda za kuendeleza soka la Zanzibar ambazo hazijakamilishwa kwa kipindi hicho chote kwa hiyo wanahitaji muda zaidi.Vyenginevyo kwa ufahamu wangu mdogo hapa ninachokiona ni kuwa kuna woga fulani kwa baadhi ya hao viongozi wa ZFA wanaotaka kugombea tena kuwa pindipo Rais aliyepo madarakani wa ZFA akiaachia ngazi huyo atakaekuja hatokubaliana na mwenendo mzima wa chama hicho kinavyoendeshwa na utendaji wa hao viongozi pindipo na wao watarudi madarakani.
Kama nilivyosema hapo kabla na hapa narudia tena kuwa uongozi uliopo yapo mazuri ambayo wamelifanyia soka la Zanzibar.Miongoni mwa hayo ni kuviwezesha vilabu vya Zanzibar kushiriki mashindano ya vilabu yanayotayarishwa na shirikisho la mpira barani Afrika CAF.Kwa hilo lazima tuwapongeze.Hata hivyo sote tumeshuhudia ni kiasi gani vilabu vyetu ushiriki wao umekuwa wa matatizo.Hayo matatizo ni kwa upande wa kifedha na vile vile katika suala zima la ushindani kiwanjani.Hili limetokana na matayarisho madogo.Hapa ninamaanisha kuwa hapo kabla hakujawa na mipango ya muda mrefu ndani ya chama cha mpira ZFA, ni kwa vipi tutakabiliana na suala zima la ushiriki wa vilabu vyetu katika mashindano makubwa kama hayo pindipo tukiruhusiwa. Jee vilabu vyetu vishakuwa na uwezo kifedha na kiufundi kwenda kushindana na siyo kushiriki, ni yepi mapungufu na kipi kinachotakiwa kufanywa.Hayo ni baadhi ya masuala ambayo uongozi wa ZFA ulitakiwa kujiuliza.
Nimelileta hilo hapo kwani nina wasi wasi kuwa wakati tukiwa tuko katika kuomba uanachama wa FIFA,sitegemei kuwa uongozi wa sasa wa ZFA tayari wameliona hilo la kuwa kuna haja ya kuanza matayarisho pindipo tukifanikiwa kupata uanachama wa FIFA,tushiriki kwenye mashindano ya shirikisho hilo kama washindani na siyo wasindikizaji.Kwa uongozi wa sasa ninaloliona wao wanachokifikiria ni hizo safari za mikutano na ushiriki wa mashindano na allowances zitakazopatikana.Tusije tukadanganyika kuwa hatuna wachezaji wenye uwezo wa kushindana.Hilo si kweli juu ya udogo wa nchi yetu, wachezaji wenye vipaji walikuwepo,wapo na wataendelea kuwepo.Kinachotakiwa ni matayarisho yanayoenda na wakati.Kwani si ukubwa wan chi wala wingi wa watu ndiyo unaocheza mpira, ingekuwa ni hivyo basi China na India zingekuwa zinaoongoza katika soka duniani.Najua kuna wengine watakuja na hoja kuwa kuletwa kwa kocha wa soka kutoka Uiingereza ni sehemu ya matayarisho hayo.Kwanza nina wasi wasi kama atamaliza huo mkataba ambao unafadhiliwa na kampuni ya mtu binafsi,ambayo imefanya hivyo ikiwa na ajenda yake ya siri.Huwezi kugharimia kitu pasipo kuwa na tija kwako.Ukweli ni kuwa mfumo mzima wa soka la Zanzibar unahitaji mabadiliko ambayo hayawezi kuletwa na uongozi uliopo sasa pindipo ukirejeshwa madarakani.
Hapa ndugu zangu nimejaribu kuleta hoja ya nini hatma ya soka la nchi yetu baada ya uchaguzi wa tarehe 31/10/2010, na athari za kuurejesha uongozi wa ZFA uliopo sasa madarakani.Najua kwa wengine hoja zangu zina nguvu na kwa wengine hazina nguvu,hilo ni jambo la kawaida kuna kuzidiana akili na jinsi tunavyoyapambanua mambo na ulimwengu tunaoishi.Ningewaomba wale wenzetu ambao wako karibu na wadau wa soka ambao wana haki hiyo ya kuchagua hao viongozi wa ZFA wawasihi kuchagua viongozi ambao watakuja kulinusuru soka la Zanzibar,ambalo sote tunakubaliana kuwa limeanguka.Hoja ya nini kifanyike angalia part 3





One Comment on "Ni Nini Hatma ya Soka la Zanzibar Baada ya Uchaguzi wa Tareh"
kwanza viongozi wazuri wawe wamecheza huo mpira sio muuza urojo akawekwe kiongozi wa mpira .kuushika ule mpira hajui sasa kweli ataweza kuongoza mpira.