Viongozi wa soka Z`bar, Bara watinga FIFA

Written by  //  30/08/2010  //  Michezo  //  10 Comments

Mwinyi Sadallah
Rais wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Leodegar Tenga.
Viongozi wa juu wa michezo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar jana waliondoka nchini na kuelekea Geneva, Uswisi kwa ajili ya kuhudhuria mkutano maalumu ulioandaliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jana, mbali na Tanzania kwenda kuomba kupatiwa misaada mbalimbali ya maendeleo, ujumbe huo kwa mara nyingine pia ulikuwa unaenda kukumbushia ombi la kuipatia Zanzibar uanachama wa FIFA.

Kwa upande wa Bara, ujumbe huo unawakilishwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, na Rais wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Leodegar Tenga.

Kwa Zanzibar viongozi wanaokwenda kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Michezo wa Serikali ya Mapinduzi, Ali Juma Shamhuna, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Omar Dadi Sharjak na Rais wa Chama cha soka cha Zanzibar (ZFA), Ali Fereji Tamimu.

Dadi Sharjak alisema ujumbe huo utawasilisha ombi maalum kwa FIFA kutaka Zanzibar iruhusiwe kuwa mwanachama wa FIFA, licha ya kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Aidha, alisema ujumbe huo utakutana na Rais wa FIFA, Sepp Blatter, kuzungumzia masuala mbali mbali ya soka la Tanzania na kutoa shukrani kwa hatua zinazochukuliwa na kiongozi huyo katika kuendeleza soka barani Afrika.

Alisema, kwa hatua ya FIFA kuipa Afrika nafasi ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia, Blatter anastahili kupongezwa kwa vile kitendo hicho, ambacho kimeipa heshima kubwa Afrika.

Alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatarajiwa kumpa Blatter zawadi ya filamu ya dakika 32 inayoonyesha ziara nzima ya Kombe la Dunia, wakati kombe hilo lilipotembelea Zanzibar.

Alisema filamu hiyo anaamini itasaidia FIFA kukubali maombi ya Zanzibar kutaka kuwa mwanachama wa shirikisho hilo.

Suala la Zanzibar kutaka kujiunga na FIFA liliibuka miaka ya nyuma, lakini lilipata kikwazo baada ya kuelezwa Tanzania ni taifa moja na haiwezekani kuwa na wanachama wawili wa FIFA.

Ujumbe huo huo unatarajiwa kurejea nchini Septemba nne.

10 Comments on "Viongozi wa soka Z`bar, Bara watinga FIFA"

  1. Elbattawi. 30/08/2010 kwa 4:31 um ·

    Inshallah ombi likubaliwe lakini kama FIFA wakilikataa ombi lenu itakuwa aibu sana maana huo ujumbe kutoka Zanzibar, una watu wazito sana akina Shamhuna, Naibu waziri kiongozi.

    Mimi maoni yangu ni kwamba ilikuwa wasubiri mpaka Serikali ya umoja wa kitaifa iwe tayari. Naamini Serikali hiyo itakapoundwa na kuanza kazi mambo mengi yatabadilika na hasa baadhi ya sheria na vifungu vya katiba na kero za muungano.

    Kwanini haraka, hawajui kuwa haraka haina mbaraka. Wameshajaribu sana kufai kwa FIFA kuwa Zanzibar ipewe wanachama, FIFA imekuwa ikikataa. Mhe. Shamhuna na Mhe. Jarjak, mjuwe FIFA wakikataa tena ombi lenu, mutakuwa hamna uso ni aibu kwa sababu ninyi ni viongozi serikali wa ngazi ya juu.

    Inshallah ombi lenu likubaliwe.

  2. Bosco 30/08/2010 kwa 5:09 um ·

    Afadhali kidogo alau na zanzibar wamewakilishwa ktk mambo ya nje. Hii inatokana na hiyo kura ya maoni kwani watanganyika sasa wameanza kutuheshemu na kutujua kua na sisi wazanzibari tupo na tuna haki kama wao.

    Alau heshima yetu wazanzibari irudi.

    Mungu ibariki znz na watu wake. Amin.

    ZANZIBAR DAIMA

  3. kijini 30/08/2010 kwa 5:45 um ·

    mimi sipendi hata kidogo kuchanganya2 huyu waziri kiongozi wanini kama hawa wanao itwa wa michezo michezo hawawezi kwenda kuwakilisha basi mimi nitamshauri blata awatimuwe pamoja na zawadi yenu nijuzi tu niliuliza hiyo sirikali inayokuja mawaziri na manaibu wakwanza wapili mpaka mpaka kszigani watafanya matokeo ndio hayo ziara zakijinga jinga walio paniwa hawaziwezi kuna hajigani

  4. Ghalib 30/08/2010 kwa 6:15 um ·

    mimi nauliwa hivi
    ikiwa zanzibar itashiriki katika kombe la dunia,wakati itakapo kubaliwa kujiunga na FIFA,zanzibar itatuakilisha kama wazanzibar jee tanzania itawakilisha vipi ?
    mana tanzania ni tanganyika na zanzibar,tayari imeingia kama taifa moja,labda itoke timu ya tanzania na ingie tanyanyika au vipi ? ndio na sisi tuingia kama taifa la kujitegemea na tanyanyika la kujitegemea ..hebu nifahamisheni..

  5. kwaomtu 30/08/2010 kwa 6:33 um ·

    HAO WAMEENDA KUTEMBEA TU. NA WATARUDI NA FILAMU YAO AU WATAISAHAU HOTELI.

  6. Bosco 30/08/2010 kwa 7:02 um ·

    Jamani mbona siwaelewi? Mara bara wanafanya peke yao. Mukipewa mnaanza kusema hivi na vile.

    Jamani shamhuna ni waziri wa michezo kwa kuna kosa gani kwenda?

    Mbona angela makel anakwenda kuwashangiria wachezaji wake?

  7. ashakh 30/08/2010 kwa 8:41 um ·

    Naona watu tunashindwa kujifahamu. Hoja hapa ni Wazanzibar kuwasilisha ombi lao kwa FIFA. Hizi hoja nyengine zilizobaki zote naona ziko kulekule barazani.

    Jee wazalendo hatujaona Mandela akisimamia South Afrika iandae michuano ya kombe la dunia? Jee hatukumuona Nick Clegg akiukaribisha msafara wa FIFA Downing Street ulipokuwa ukikagua viwanja vya michezo vya Engaland.

    Sasa geni liko wapi kwa Shamhuna kushiriki katika msafara hule. Pia Shajak kuwemo? Basi wazalendo nendeni nyinyi mukatuwakilishe!!!!!!

    Wazalendo, la leo hufanywa leo. Halingojewi kesho. Keshokesho vijana wanakosa haki zao. Nusu karne imetimia vipaji vyetu vinapotea. Nasema ni sawa hasa huu ujumbe ulivyofanya. Nawende hata wakose, si aibu wala fedheha. Tena nawaona mashujaa kwa kutupigania haki zetu.

    La muhimu ni kuwasilisha ombi letu. Ni wao ndio watakao amuwa kuwa ipewe Zanzibar kuweko Tanganyika. Au ipewe Zanzibar kuweko kwa Tanzania. Lakini hatuwezi kukaa vibarazani kama hapa tukaanza kujenga hoja zisizo kichwa wala pembe.

    Sheria zinasema (kama uchambuzi tulioletewa) sidhani kama wanaweza kwenda kinyume na sheria zao. hasa mfano halisi tunao na tunaufahamu kwa kina, yaani Engaland, Scotland, Wales, na Northern Ireland. Na mengine ni hile muandishi aliyotuletea.

  8. MTANGANYAKA 30/08/2010 kwa 10:18 um ·

    @ Ashakh!

    SADAKTA.

  9. stirio 30/08/2010 kwa 11:46 um ·

    inaonesha huyu shamhuna na ujmbe wake hawana kazi ya kufanya

  10. jamaleyl 31/08/2010 kwa 6:21 um ·

    Kwa kweli hii safari ya ujumbe wa serikali na viongozi wa ZFA kwenda Geneva kuonana na Sepp Blatter ni hatua nzuri ya kufurahikiwa na wazanzibari wote.Hata hivyo wakati huo huo inabidi pia tuwe na wasi wasi mkubwa.Kwanini nimesema hivyo,nina wasi wasi mkubwa kuwa safari hii imepangwa bila ya kufanya matayarisho ya kutosha.Matayarisho nikimaanisha ni kujua nini cha kumwambia Blatter,nayo ni nini status ya nchi ya Zanzibar ndani ya Muungano wa Tanzania.Pia wapi tunasimama kwenye tafsiri nzima ya kanuni za FIFA kuhusu wanaoweza kuwa wanachama wa shirikisho hilo.Jee sisi Zanzibar tunaweza kutafautishwa au kulinganishwa vipi na wanachama wengine kama Macau na Hong Kong ambao wako chini ya mamlaka ya China,Montserrat nchi yenye watu elfu nane tu ambayo iko chini ya Uingereza,Aruba,Virgin Islands,Cayman Islands n.k.Nafikiri watakuwa wanafanya kosa kubwa pindipo watajaribu kutumia hoja ya kuwa mbona Scotland,Wales,Northern Ireland na Uingereza ambao ni mamlaka moja wote ni wanachama.Kama tunavyojua sote Shamhuna anataka sifa ya kuwa yeye ndiye alofanikisha Zanzibar kuwa mwanachama wa FIFA pindipo wakifanikiwa.Lakini lazima sote tujue kuwa pindipo Blatter akilitupia mbali ombi lao hilo basi basi hasara yake kwa heshima ya nchi yetu ni kubwa.Vile vile kufanikiwa kwetu kutategemea hao ndugu zetu wa bara nao watatusaidia vipi katika kuifikisha hiyo hoja na upambanuzi mzima wa katiba ya nchi yetu na wapi Zanzibar inasimama.

Comments are now closed for this article.