Zanzibar Nchi na Uanachama wa FIFA
Written by jamaleyl // 24/08/2010 // Makala/Tahariri, Michezo // 20 Comments
Sasa ni takriban mwaka mmoja tokea ilipotolewa kauli ya kuwa Zanzibar haiwezi kuwa mwanachama wa shirikisho la mpira duniani FIFA.Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo wa FIFA katika ukanda wa Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi.Alisema FIFA haiwezi kuipa Zanzibar uanachama kwasababu ni sehemu ya Tanzania na ni jambo lisilokubalika katika katiba ya FIFA kutoa uanachama kwa vyama viwili vilivyoko katika nchi moja.Aliendelea kwa kusema kuwa FIFA itaendelea kuitambua TFF kwasababu ndio chama kilichosajiliwa kwa jina la nchi kamili, na wao (Zanzibar) ni kisiwa na sio nchi inayojitegemea na inayotambuliwa kama taifa huru.
Kwa kweli sababu kuu ya kuileta mada hii kwenye ukumbi ni kufuatilia haya mabadiliko ya katiba yaliyofanyika hivi karibuni ya kuitangaza rasmi Zanzibar kuwa ni nchi.Hata hivyo kwa kipindi kirefu hata kabla ya mabadiliko haya ya katiba nilikuwa bado naamini kuwa Zanzibar ina haki ya kuwa mwanachama wa FIFA, na kauli hiyo ya Ashford Mamelodi kwa mtazamo wangu ilikuwa na mapungufu ambayo nitayagusia hapo baadae.
Lakini kabla ya kuigusa hiyo katiba ya FIFA kuhusu nani ana haki ya kuwa mwanachama,kuna maswali ambayo yanataka majibu.Kwanza jee Chama chetu cha mpira kilipeleka maombi yake rasmi ya kuomba uanachama FIFA au Ashford Mamelodi alitumiwa na wenzetu kuzima azma hiyo ya ZFA,na hiyo kauli yake ni kauli rasmi ya FIFA, na kama ZFA iliyapeleka maombi hayo jee yalifikishwa kwenye kamati tendaji ya FIFA kujadiliwa na kama yalikatiliwa kiasi kwamba hayakufikishwa kwenye mkutano Mkuu wa FIFA ni sababu gain walizopewa ZFA kukataliwa kwa maombi yao hayo kama taratibu zinavyosema na kama hilo lilifanyika ZFA ilichukuwa hatua gain kuhakikisha inatendewa haki.Pili jee Serikali ya SMZ ilitowa msaada gani katika kulifanikisha hili la kuomba uanachama FIFA?
Hebu kidogo tuiangalie FIFA yenyewe inasema nini kwa chama cha mpira kinachotaka kuomba uanachama, na kwanini nikasema kauli ya Ashford Mamelodi ina mapungufu.Ukiangalia FIFA statues Aug.2009 edition, kifungu cha maombi ya uanachama kinasema ‘Chama cho chote ambacho kina mamlaka ya kuandaa na kusimamia mpira wa miguu katika nchi kinaweza kuwa mwanachama wa FIFA’.Kifungu hicho kinaendelea kwa kusisitiza kuwa neno ‘nchi’ linamaanisha taifa lililo huru na kutambuliwa na jumuia ya kimataifa.
Hata hivyo hili halihusishi vyama vya mpira vinne vya Uingereza ambavyo vinatambuliwa kama wanachama wa kujitegemea ndani ya FIFA.Kwa kumalizia kifungu kinasema chama cha mpira katika eneo ambalo bado halijawa huru kwa mamlaka ya chama cha hiyo nchi ambayo inaitegemea kinaweza pia kupeleka maombi ya uanachama FIFA.
Sasa jee hamuoni wenyewe kuwa kauli ya Ashford ina mapungufu makubwa ukilinganisha na FIFA yenyewe inavyosema kuhusu kuomba uanachama.Hebu tujiulize ni nini kazi ya chama chetu cha mpira ZFA kama si kuandaa na kusimamia mpira wa miguu katika nchi ya Zanzibar?Jee nchi yetu ya Zanzibar siyo taifa huru linalotambuliwa na jumuia ya kimataifa? Kama hayo yote siyo, jee inamaanisha kuwa tunakubaliana na Ashford kuwa Zanzibar siyo taifa huru na tuko chini ya utawala wa Tanganyika? Sawa na tujaalie kuwa sisi tuko kama Ashford Mamelodi anavyosema,bado hakukuwa na kipingamizi cha kupeleka maombi yetu ya uanachama FIFA kama tu hao ndugu zetu TFFwangekuwa na nia njema ya kutusaidia.
Kama nilivyosema hapo mwanzo kuwa ninaamini kuwa tuna haki ya kuwa wanachama wa FIFA, hasa ukiangalia kuwa kuna vyama vya mpira ambavyo ni wanachama wa FIFA ambao maeneo yao hayako huru kama tulivyo sisi Zanzibar.Hebu nitaje baadhi ya hayo maeneo ambayo wengi wenu hamkuwahi kuyasikia ambayo ni wanachama wa FIFA.Hapa mtanisamehe kwa kutumia neno maeneo kwa kuwa sina hakika kuwa na wao ni nchi kama sisi au laa isipokuwa ni kuwa hayako huru.
Kwanza ningependa kutaja eneo linaloitwa ARUBA.Hivi ni visiwa vilivyoko katika pwani ya Caribbean maili kama 27 kutoka nchi ya Venezuela.Kisiwa cha Aruba,visiwa vya Netherlands Antilles pamoja na nchi ya Netherland (Holland) kwa pamoja ndio wanaunda ufalme wa Netherland.Wananchi wa Aruba ni raia wa Holland na wanatumia passport za Uholanzi.Aruba ni wanachama tokea 1988.Visiwa vyengine ambavyo haviko huru na ni wanachama wa FIFA ni British Virgin Island ambavyo vimejiunga 1996 na visiwa vya Cayman ambavyo vimejiunga na FIFA 1992.
Visiwa vyote hivi viko chini ya utawala wa Uingereza. Visiwa vya Aruba ,Virgin na Cayman vyote vimepata uanachama kwa kupitia kifungu kinachosema kuwa chama cha mpira kwa eneo lisilo huru kinaweza kuomba uanachama kwa kupitia mamlaka ya hiyo nchi wanayoitegemea.Kwa visiwa hivyo ni Uholanzi na Uingereza.
Sasa tukiangalia vifungu vyote viwili na mifano ya hapo juu jee ni kweli ndugu zangu ZFA haiwezi kuwa mwanachama wa FIFA?Lakini maombi ya ZFA hayako rahisi kiasi hicho yaani kwa maneno mengine siyo straightforward
.Kwanini nikasema hivyo,nimesema hivyo kwasababu ya huu Muungano wetu ambao kwa wenzetu wa nje hawaufahamu umeundwa chini ya misingi gani na hili limechangiwa kwa kiasi na sisi wenyewe kushindwa kuuleza ulimwengu.Kwasababu ya nia mbaya ya wenzetu maombi yetu ya uanachama FIFA yatafikwa na vikwazo ndani yake,ndiyo maana pale mwanzo nikauliza jee ni kiasi gani serikali ya SMZ imesaidia ZFA katika suala zima la maombi yao FIFA.Hapa namaanisha msaada wa ushauri na fedha.
Kwani SMZ ilitakiwa kujidhatiti kwenye suala hili kwa kujua kuwa wenzetu hawalitaki.Hivyo ilitakiwa kuzishawishi nchi mbali mbali ambazo zina ushawishi FIFA kuunga mkono maombi ya ZFA pindi yakifikishwa huko.Kutumia wanasheria wa mambo ya katiba na michezo pindi pakitokea pingamizi yo yote ya tafsiri ya kikatiba ambayo yanaweza kukwamisha maombi hayo.Vile vile kuwatumia wanasheria hao pindipo ombi hilo likikataliwa kwa kukata rufaa Mahakama ya Upatanishi ya Michezo (Court of Arbitration for Sports) ambayo inatambuliwa na FIFA pindipo hujaridhika na maamuzi yanayotolewa na Shirikisho hilo.Haya yote yanahitaji fedha ambazo ZFA haina na ndiyo maana kunahitajika kwa serikali kutoa mchango wake.
Kwa kumalizia kwa kutilia maanani haya mabadiliko ya katiba ya kuitaja rasmi Zanzibar kuwa ni nchi na tukitilia maanani kuwa michezo si sehemu ya makubaliano ya muungano wetu. Jee ndugu zangu hamuoni kuwa kuna haja kwa ZFA kushirikiana na SMZ wakaliangalia upya suala hili na kama kulikuwa na mapungufu katika maombi ya mwanzo basi yakafanyiwa marekebisho.Au ndiyo tusubiri mpaka hapo tutakapoitisha hiyo kura ya maoni ya kuukataa huu Muungano wa upande mmoja ndiyo tuyapeleke hayo maombi FIFA?Lazima tufahamu katika ulimwengu wa leo njia moja ya kuitangaza nchi ni kwa kupitia michezo hasa mpira wa miguu ambao unafuatiliwa na mamilioni ya watu duniani kote.Kwa kujua hilo ndiyo maana hawa tunaowaita ndugu zetu watafanya kila njia kuhakikisha hatufanikiwi







20 Comments on "Zanzibar Nchi na Uanachama wa FIFA"
Muandishi maneno yako yapo kwenye mstari ila mie nataka kuongezea kidogo tu nini tunacho sisi wazanzibar.
Katika kuchaguwa viongozi au wafanyakazi sehemu tusiangalie usoni vyama vyote wafanyakaziwa serikali yetu muna watu hawana qualification yoyote ila wamo katika nyazima kubwa kubwa.
Na hicho chama chetu cha mpira Zanzibar ni sawa sawa wachache ndio wenye muelekeo na uwezo wa kufanya kitu inabidi pia watu wenye uwezo wa kuongoza wagombee nyazifa tofauti tofauti katika vyama tofauti si tunaangalia siasa tu (CUF na CCM).
Ila mie kama wiki tu niliwahi kuulizia hilo jambo kwa wataalamu wakanambia hilo jambo halia mjadala kabisa kwani akanitolea mfano wa nchi tofauti ambazo wa mfumo wa serikali yetu lakini wamo katika uwanachama wa FIFA, mie nafikiri serikali pia itafute watu wenye uwezo katika masuala ya michezo na wanasheria ili walifatilie zaidi jambo hili.
Mwandishi
Shukran kwa jitihada zako za kulisukuma mbele taifa la Zanzibar.
Hii mada ni mujarab kabisa. Angalau umeweza kushitua roho.
Wasiwasi wangu mkubwa nikuwa ZFA hawakupeleka maombi yao. Nadhani walipo sikia kutoka kwa wenzetu “hamustahiki” walivunjika moyo. Ikawa sasa ni story ya paukwa pakawa. Haya ndio matatizo yetu hatuwi Wanyamwezi kungojea ushahidi kamili.
Ikiwa CAF iliweza kutupa sikuona sababu ya FIFA wasitupe.
Suala la viongozi pia nalo linaumuhimu wake. Tunaye Sh Ally Saleh kwenye ZFA. Lakini Mzee wetu Tamim Ferej bora angewaachia kizazi kipya. Vilevile watu wenye ikiwa wanajiona hawana uwezo hakuna sababu ya kujiweka kimbelembele kugombea hizo nafasi.
Haya ni mambo ambayo mtu mwenyewe anatakiwa ajitathmini, anao uwezo au laa.
Ndugu Wail, Fahamu kuwa huwezi kufikia huko FIFA, kama hujaanzia kwenye siasa. Kwa taarifa yako, Waziri wa Elimu Mh Haroun Suleiman, aliwahi kulitekenya hili suala na likafikia hatua kubwa, lakinimwishowe ikanekana Zanzibar kweli ni nchi, lakini imepoteza mamlaka yake ya nje. Hebu someni kwa wanao juwa. Juzi humu ilitiwa mahojiano ya Mh Jussa na Zenji FM, na amelezea vipi kuhusu hili na nchi….
Na haya si kwa FIFA tu, hata kwa FIDE. Wengi wenu sijuwi kama munafahamu kuna kitu kinaitwa FIDE. Labda kwa wale walio wahi kushiriki mchezo wa Chess miaka ile ya mwishoni mwa thamani na mwanzoni wa tisini. Kulikuwa na Zanzibar Chess Asscociation. Kilikuwa kinatabulika serikalini a kilikuwa kinatengewa pesa yake kama ZFA, japo pesa wenyewe ndio hivyo hivyo, mkia wa mbuzi. Lakini waliweza kutowa wachezaji machachari na kwa mara mwanzo walishiriki Tournament ya Kenya na kupata washindi wa pili kwa junior A and B na wakapata fursa ya kuenda Botswana na Greece kwa International tournament. Lakini haikuwezekana kwa sababu kamahizo za FIFA. Ndipo kulipo undwa Tanzania chess Association kwa msukumo wa ZCA. Bara wakati ule hawakuwa na tournament yeyote ya chess. Kwa hiyo sasa hivi tunaingia kama Watanzania.
Mtowa mani unasema kuna nchi kama Zanzibar ambazo zimo kwenye FIFA, sijuwi nchi gani yenye mfumo kama wetu. Kwasababu huu mfumo wetu wengin unawapa taabu kuwa hakuna mfumo kama huu. Ninavyo juwa mimi kuna nchi kama Zanzibar nadhani kama cyprus na nchi nyengine ambazo nao hufanya mashindano yao na ndio maana miaka hii karibuni Zanzibar imekuwa ikishiriki. Walikuwepo Turkey, miaka ya karibuni, wakafika cyprus nk nk.
Kwa hiyo lazima ufahamu, kwenye siasa kuna mengi huko.FIFA na wengine wote wanaangalia katiba zenu a katiba ndio hizo siasa…
Nimesoma kwa makini na kwa hakika nimevutiwa na makala kuhusu uwezekano au juhudi za Zanzibar kujiuunga na FIFA.
Utafiti wa mwandishi ni mzuri na umefanywa kwa kila aina ya umakini.Ukweli ni kuwa Zanzibar haijakata tamaa katika hili. Juhudi bado zinaendelea kwa sababu kama alivyosema mwandishi kuna taarifa nyingi zilizopatikana ambazo huko nyuma hazikuweza kupatikana.
Ally Saleh
Moved by Admin
Ndugu Kassim ningependa urejee tena kuisoma hiyo mada ilivyoandikwa ili ufahamu kuwa kuna nchi ambazo zinatawaliwa na baadhi zimetajwa hapo juu na ni wanachama wa FIFA, tuchukulie na sisi tunatawaliwa na hao Tanganyika basi pia uwezekano upo wa kuwa wanachama wa FIFA kama wenzetu wangekuwa na nia njema.Kama una nafasi hebu soma hiyo statutes ya FIFA inasema nini kwenye suala zima la admission for membership (www.fifa.com/mm/document/affederation/federation/01/24/fifastatuten2009_epdf).Kama ilivyoandikwa hapo juu suala hilo ni zito na linahitaji political committment kutoka serikali ya SMZ na vile vile kama ilivyoandikwa linahitaji lobbying ya hali ya juu kufanyika hasa kwa nchi zilizo nje ya bara la afrika tukitilia maanani kuwa hawa ndugu zetu wasolitaka hili suala wao wana ushawishi mkubwa katika nchi za kiafrika.Kwa kuongezea ni kama ilivyoelezwa kunahitajika fedha kutoka serikalini kuajiri wanasheria wa katiba wa kuitafsiri katiba ya Muungano na wanasheria wa mambo ya michezo.Narejea tena hilo linawezekana pindipo tu serikali italivalia njuga hilo suala.
Bwana Kassim unataka kujuwa nchi gani yenye mfumo huu angalia mfumo mzima wa United Kingdom then utajuwa kuna nchi inaitwa Wales, Scotland,Ireland and England.
kuna Queen wa nchi nzima, waziri mkuu wa nchi nzima ikisha wabunge katika mabaraza yao kila nchi hakuna waziri mkuu wa scotland wala waziri mkuu wa Wales bora hata hapo Zenji kuna Raisi but tatizo la Tanzania ni moja tu watu wa bara hawawatakii Zanzibar kuonekana kama nchi na kujiendesha wenyewe na kila kitu wanajivutia kwao wakati wenzetu hawana hayo nakubali kama kuna matatizo ya kikatiba kama ulivyosema lakini maneno yangu uyakubali bila ya kupata viongozi madhubuti kwenye vyama vyetu wa kuzungumza basi hakuna liwalo.
KAMA WAZANZIBAR HATUKUJIKAZA NA TUKADAI HAKI ZETU KILA CHOCHORO TUNAYO HISI TUNAZULUMIWA BASI MAJUTO NI MJUKUU?. IKIWA ZANZIBAR SIO NCHI NDIO FIFA HAWAITAMBUWI? JEE SCOTLAND NA WELL NA IRELAND JEE?
A.alaykum jamia,
Nashkuru kusoma makala za aina hii ndani ya zanzinet,kwa kweli muandishi imefanya utafiti na kutupatia nini roho za wazanzibari na wapenda soka zinataka.
Ama kwa kuongezea kama alivyosema mwandishi wa makala sehemu kama Aruba iko chini ya Netherlands,na sisi tuko chini ya Tanganyika.Aruba inashiriki mashindano mengi kama vile beauty pegeants e.g. Miss World, anakuwepo Miss Aruba, kwanini asikuepo Miss Zanzibar!wakati Aruba si nchi kama ilivyo Zanzibar! Kwa mantiki hiyo kama Aruba ni mwanachama wa FIFA basi na Zanzibar inaweza kuwa. Mimi pia naamini juhudi za viongozi wa SMZ plus ZFA zinahitajika wakiwatumia wanasheria wao naamini hili linawezekana. Iwapo watauliza kuhusu muungano wetu basi hapo itakua mwanzo wa wanadunia kufahamu aina feki ya Muungano uliopo baina yetu na ndo ambao unatuzuia sisi kupata uanachama,inaweza ikawa ndo mwanzo mzuri wa kuurekebisha Muungano hasa wakati huu muafaka.
Pili kama kuna watu wapo tayari na wapo Zanzibar tunaweza kufanya kipindi au mahojiano juu ya swala la Zanzibar na FIFA kupitia TVZ au ZAnzibar CAble TElevion kama wanavyofanya vipindi vya sheria ili kuutanabahisha umma wa wazanzibari na SMZ pamoja na ZFA na TFF. Kwanza kwamba TFF ijue kuwa hatujalala na hatujaridhika na wanayofanya na tutapigania haki yetu mpaka tujue moja.
Pili kuwatanabahisha ZFA na SMZ kuwa makini na kulivalia njuga swala hili kwa faida ya wazanzibari na wapenda soka. Tukipata vichwa makini katika mdahalo huu ao ZFA wataanza kujitathmini katika ufanisi wa kazi zao na hasa pale tutakapogusia swala COMMITMENT,POOR LEADERSHIP OR MANAGEMENT, QUALIFICATIONS ZAO n.k na vipi hivi vinaathiri maendeleo za mpira Zanzibar pamoja na kushindwa kuwachallenge TFF kutokana na mapungufu hayo waliyonayo.
IPO SIKU
Maasalam
Kwanza Mtaniwia radhi kwa kuandika ZANZINET badala ya mzalendo.net.
Mdahalo huo utahitaji mtaalamu wa michezo,mwanasheria,mtaalamu wa sayansi ya siasa,mwanahistoria na viongozi wa ZFA na Wizara ya Michezo ikiwezekana.
Mzalendo au wanajamii au jumuiya au Zanzibar Cable TV au TVZ wanaweza kuandaa hilo na sisi tutatoa msaada tuuwezao.
Mambo kama haya jamani yanahitaji kuzungumzwa hadharani. Tukumbuke wanzibari waliowengi hawajui hasa kama kuna Mzalendo.net kwa ajili yao,kwahiyo nashauri mada zinapokua nzuri na zenye faida kwa umma basi zifanyiwe mdahalo kwenye media tulizonazo hasa hapa Zanzibar.
Ninauhakika mambo yatakua mazuri.
Wail, mimi nipo UK, kwa hiyo nafahamu kuwa kuna wales, scotland… Lakini wao kuna mmlaka fulani fulani tu ndio yapo chini ya queen na hilo lipo wazi. Kwetu hakuna kitu hicho. Utakacho gusa utaambiwa hatuna mamlaka ya kufanya hivyo kama Zanzibar. Tulitaka kujiunga na OIC, nini kilitokezea? Hiyo FIFA, wamepiga makelele na tena na tena, mwishowe nini kilitokea? Kwa hiyo narudi pale pale, huko kwenye siasa ndio kwenye utatuzi wa hili. Tukisha kuweka sawa mambo, basi haya yote yatafanikiwa.
Muungano huu unaambiwa wa nchi mbili. Utaambiwa Tanganyika imefutwa, lakini jee kweli Tanganyika haipo? Ni kiili macho tu. Tizama wizara zote za Muungano, jee zina sura ya Ki-Muungano? Balozi zetuhizi zinazo itwa za Tanzania, jee kuna mabalozi wangapi kutoka Zanzibar.
Sasa unanitajia wale, scotland…. Hapo walipo basi bado wanaona wanabanwa na wanataka kuwa huru zaidi.
Salaam za ramadhani ndugu waislamu wote.
Sina budi kumshukuru mtoa mada hii kwa kutukumbusha haki zetu ndugu Wazanzibari. Mada hii inauzito mkubwa na tunapaswa tuivalie NJUGA na UJUMBE uwafike Wazanzibari wote popote pale walipo( haswa Visiwani). Na sio iishie kwenye mtando
Kama ndugu Alwatwan alivosema kwamba kama tutafanya mjadala na utarushwa/ utapitia kwenye Cable TV na TVZ basi ujumbe utawafika watu na vijana tunaowataka. kwani hata Raisi Amani Karume alisisitiza udumishaji wa mpira wakati alipozindua Uwanja wa Amani.
Huu siowakati wakulala, hili linaweza hata likawa ni moja katika campeni za wana Siasa kuwapatia vote. Kwani kupitia michezo ndio nchi hujitangaza. kwani michezo ndio inaunganisha watu wote duniani. Na zanzibar ina haki kuwa mwanachama wa FIFA kama ilivo England,walles,Scotland & Northern Island.Hizi ni nchi ambazo zimo katika (Visiwa) cha Uingereza. Na nchi hizi zimegawana mipaka tu, lakini huwa-wakilisha utaifa wao kwenye Muungano wa United Kingdom.
Sasa itakuaje sisi kila kitu Tanganyika/ tanzania inasema hatuwezi. Hawa watu hawatutakii mema halafu tunasema/ wanasema sisi ni ndugu. Mimi kinachonikera na nikuona kwamba wamekua kwenye FIFA miaka nenda na miaka rudi. Lakini huwa hawafiki popote pale,hata kwenye African Cup of Nation sijawahi kuiona Tanzania/Tanganyika. Na wanashindwa na nchi changa ambazo zilikumbwa na War kama vile Ruanda,Burundi,Zambia n.k
Ujumbe wangu kwa nd. Ally saleh:
Wewe ndio dira yetu hapo, hili jambo tunataka ulifikishe kwa watu watakao litia kwenye mada zao za campeni za Siasa. Tvmedia n.k Ukesha shekh Ally saleh tuletee jibu.
Naam nikweli ndugu zamko hili la kujiunga ZFA kwenye FIFA inabidi liwekwe ktk kampeni za CUF kwani michezo huwavutia watu wote cuf na ccm.
Hawa watanganyika hata iweje hawezi kucheza mpira kwani nguvu hawana hata kidogo na hii inasababishwa na kupenda kwao kunywa pombe kupita kiasi, kupenda kufanya ngono kupita kiasi, njaa nk. Eti mchezaji mpira anakula mihogo ya kukaanga mchana kutwa na siku atakayobahatika basi anakula chipsi kavu. Ah Hapo mtu atapata nguvu?
Bosco, aste aste…
Mimi ninachojuwa Zanzibar kuwa mwachama wa fifa inawezekana,
na kwa nini isiwezekane ndugu zanguni tusiangalieni tofauti
zetu hizi na zile sasa hivi kilichobaki ni kufanya jitihada zetu zote ili kuiwezesha zanzibar ambayo ni nchi kamili kuingia katika fifa hili sio la Cuf wala CCm na hao wanaosema Zanzibar ni sehemu ya T,nzania Naona elimu yao ni fupi sana na ningeliwashauri watafute la kufanya kama hawana
la kuongea au kwa sababu ya posho lao kubwa ndio maana huwa wanajisahau,Z,nzibar wapo vijana wengi tu wenye vipaji vya kucheza Mpira tena kama vile Brazil na uwezo wako nao wa
kuonyesha Nchi nyengine za Mbali vilex2 {so watch your mouth}.Shukraan.
Haya watu wa kandanda, mambo ndio hayo. Mkombozi kashatowa maelekezo… na mambo anaonekana yapo rahisi tu kujiunga na FIFA!
A.alaikum
Natoa pongezi kwa wale wote waliochangia mada hii kwa kutoa mitazamo tofauti,nisoma nakala pamoja na comments ambazo mulokuwa mukiziandika.
Mimi nauliaza hivi …
Vipi zanzibar itajiunga katika FIFA wakati kuna taifa mambalo limewakilisha kama TANZANIA na hii maana ya kuwa zanzibar na tanyangika tumepata TANZANIA,sasa vipi itaweza kuingia tena katika FIFA ?
Ingelikuwa imeingia Tanganyika kisha tukapingwa sisi kujiunga katika fifa hapo sawa,lakini tanzania tayari imeshaingia,nafikiri ipo haja ya kubadilisha katiba kwanza,kutokana na mfumo wanyewe wa uwongozi mpaka ikafikia katika suala la michezo mvurugano.
Sijaona mimi nchi ambazo zimeunga na ikaingia taifa kubwa kisha likaingia taifa dogo,kwa mfano kama Ingiee Tanzania Kisha iingie zanzibar,hapa labda itoke TANZANIA katika fifa ingie tanganyika kisha na sisi tuingie
Ndugu zangu naomba munifafanulie kwa hilo zaidi,tumefunikwa na Tanzania ndioa maana zanzibar haiwezi kungia katika fifa mapaka itoke tanzania.
Katika kuadhimisha siku hii ya Muungano, wadau mbalimbali wa michezo wameangalia miaka 44, ya Muungano na maendeleo ya michezo Tanzania, ambapo hali inaonyesha baada ya Muungano upande mmoja umedidimia na mwingine kuendelea. Rais wa chama cha Soka Zanzíbar ( ZFA), Ali Ferej Tamim anasema baada ya Muungano kufanyika, Zanzíbar imekufa kimichezo. Anasema kihistoria Zanzibar ilikuwa ya kwanza kuunda chama cha mpira mwaka 1926 na Bara wakafuatia mwaka 1930.
Baada ya kuungana na kuwa nchi moja Tanzania, visiwa hivyo vilikubali kwa asilimia 100 kuwa wamoja kwenye masuala ya michezo, ila Bara walikubali au kujitoa kwa asilimia mbili. Muungano huo, chama cha soka cha bara kilibadili jina kutoka Tanganyika Football Associatión na kuitwa Football Association of Tanzania (FAT) ambapo mwaka 1964 walijiunga na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Anasema baada ya Muungano huo, ambao kwa sheria za kimataifa kila nchi inapewa nafasi moja ya kiti katika Shirikisho la soka, hivyo Zanzibar ikawa haitambuliki tena kama nchi.
Tamim anasema baada ya hapo misaada ya kimataifa iletwayo nchini yote huelekezwa FAT, ambapo viongozi wake huifanya ni mali ya soka la Bara bila kuwahusisha Zanzibar hivyo kuwafanya wao yatima.
Anasema ilipofika mwaka 1990, akiwa Mwenyekiti wa ZFA aliona Zanzibar inakufa kimichezo aliamua kutafuta msaada na ndipo akazungumza na FIFA hivyo Zanzibar ikaruhusiwa kushiriki kwenye michuano ya CECAFA (Baraza la Vyama vya Michezo Afrika Mashariki na Kati) kama mshiriki na siyo nchi.
Anasema hata hivyo ushiriki wao baadaye ulileta dosari kwani Sudan walilalamika kwa nini Zanzibar inashiriki wakati siyo nchi, na kwamba wao wanaitambua FAT ambayo inawakilisha Tanzania kama nchi ya Muungano. “Niliposikia hilo, kwa kuwa nilikuwa Makamu Mwenyekiti ndani ya CECAFA, nilizungumza na viongozi wenzangu na hatukutolewa,” anasema Tamim.
Tamim, ambaye hadi leo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Fedha wa CECAFA, aliamua kujitoa mwenyewe mwaka 2002, baada ya mzozo kuibuka na kuibana Zanzíbar isishiriki kwenye michuano ya CECAFA kama nchi, bali kama mshiriki. “Nilijitoa mwenyewe kwenye CECAFA kwa nini niwe kiongozi ili hali Zanzibar hairuhusiwi kushiriki, na huku kwenye Muungano FAT wametutenga?”anasema Tamim.
Anasema tangu Muungano uwepo, Zanzibar wamekuwa wakitengwa kwenye masuala mengi ya kimichezo ambapo hata kwenye misaada itolewayo na FIFA, FAT inaipeleka kwa Bara bila kuigawia Zanzibar. Kadhalika, Rais wa FIFA Sepp Blatter kwenye kampeni zake barani Afrika za kuomba kupigiwa kura kuwa rais wa shirikisho hilo, alisema akiingia madarakani kila mwaka atavipa vyama vya soka barani Afrika dola 250,000 kwa ajili ya kuendeleza soka.
Anasema fedha hizo ni kwa ajili ya masuala ya kiufundi, makocha, kuendeleza vijana na mpira wa wanawake na kwamba ahadi hiyo alianza kuitekeleza ambapo FAT walipewa fedha hizo lakini Zanzibar haikupata gawio lolote kutoka Bara.
“Kwenye kampeni hizo za Blatter nilimwandikia ujumbe ikiwa Zanzibar itapewa fedha, jibu alilotoa ni kwamba wanaitambua FAT, ila kwa kuwa sisi ni Muungano FAT inapaswa itugawie,” anasisitiza Tamim. (FAT kwa sasa ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Anasema hali hiyo ndiyo inayowafanya Wazanzibari kuukataa Muungano kwani unakwamisha maendeleo ya michezo visiwani humo. Hali haikuishia hapo kwani Tamim anasema suala la michezo kwenye Muungano bado ni gumu, kwani viongozi wa FAT wanakumbatia vyama hivyo kama mali yao na kusahahu maslahi ya nchi.
Anasema mfano kwenye misaada ya FIFA ilitoa nafasi za waamuzi, na zilipokuja majina ya waamuzi waliofaulu kwenye viwango wengi walitoka Zanzibar ila majina yalifutwa na kuachwa jina moja, na waamuzi wengi kuchukuliwa wa Bara. Pia mradi wa FIFA Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika ilitaka klabu zitaje zinataka kusaidiwa kujengewa nini na FAT wakasema wanataka uwanja wa Karume ulioko Bara uwekwe nyasi bandia.
Anasema hiyo ni nafasi ya pili ambapo viongozi wa FAT wanaihujumu Zanzibar kwa kutoishirikisha kwenye misaada ya miradi kama hiyo hivyo kufanya Muungano uonekane hauna maana kwao.
Anasema matatizo ya michezo ni mengi Zanzibar kwa kuwa wametengwa na FAT, kana kwamba wao sio sehemu ya Muungano hivyo kuwafanya Zanzibar wategemee misaada kutoka serikalini. “Matatizo ya michezo ni makubwa hapa Zanzibar, viongozi wanahodhi madaraka na kuvifanya vyama vyao, kwa kweli tunaendesha klabu katika mazingira magumu,” anasema Tamim.
Akizungumzia suala la Ligi ya Muungano iliyokuwa inatoa wawakilishi wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, Tamim anasema ligi hiyo imekufa kwa kuwa viongozi wa bara wanataka wafadhili watakaotoa fedha, ili hali kwa upande wa Zanzibar walijiandaa na kununua kombe, lakini kikwazo ni Bara hawataki. Baada ya Zanzibar kupata uanachama wa CAF, Ligi ya Muungano ilikufa, lakini ili kuendeleza Muungano, iliamuliwa timu za Bara na Zanzibar zicheze baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Michezo la Zanzibar, Khamis Ali Mzee, anasema pamoja na kuwapo kwa ushirikiano baina ya Bara na Zanzibar, lakini si wa kuridhisha. Anasema michezo ndio sura halisi cha Muungano, kwani huwaweka watu pamoja kwa kuwa waliunda timu za pamoja ila iko baadhi ya michezo ambayo haina sura hiyo hata kidogo.
Mzee anasema michezo mingi iliyoko Zanzibar haipati nafasi ya kushiriki kwenye michezo ya kimataifa kwa kuwa sura ya Muungano haipo na hayo yanafanywa na viongozi wa vyama ambao wana ubaguzi wa kuchukua wachezaji.
Anasema matatizo makubwa kwenye michezo yanatokana na mvutano baina ya vyama vya michezo vya Bara na Visiwani kwa kuwa sehemu moja inanyonywa kuliko nyingine.
Anasema Zanzíbar wana vyama 26, vya michezo ikiwemo ya jadi, bao na karata na vyote hivyo viko chini ya mwavuli wa Baraza la Michezo la Taifa la Zanzibar (BTMZ), ilhali Bara vipo 30, chini ya Baraza la Michezo la Tanzania (BMT).
Mzee anasema kutokana na mvutano uliopo kwenye vyama hivyo kuhusu uwakilishi wa wanamichezo na misaada itolewayo na FIFA, wamefanya mikutano mbalimbali baina ya BTMZ na BMT, Februari 16, mwaka huu na kuweka wazi maeneo yenye kasoro.
Maeneo hayo yanayofanya Muungano uonekane haufai ni pamoja na mialiko ya michezo nje ya nchi kwa jina la Tanzania, uteuzi wa timu za Tanzania na mgawanyo wa misaada na vifaa vya michezo.
Mengine ni nafasi za masomo zinapokuja zinaleta utata, uwakilishi wa masuala ya kimataifa, taarifa za zimamoto za mafunzo nje ya nchi na malipo ya ada za uanachama katika mashirikisho. Anasema wao wanataka Muungano uendelee hata katika masuala ya michezo ila viongozi wa vyama wanang’ang’ania madaraka kwa maslahi ya umimi na sio kuendeleza Muungano.
Mzee anasema matatizo hayo kwenye michezo yanasababisha sura ya Muungano iwe ya upande mmoja kwa kuwa Machi 16, mwaka huu, vyama vya bara na visiwani waliambiwa wawasilishe kero zao na jinsi wanavyoshirikiana ili kutafuta njia ya ufumbuzi.
Anasema kila mara Bara wanapoambiwa wakae kuzungumzia suala hilo hawataki na hivyo kufanya suala la michezo kuendelea kuwa gumu kwa upande wa Zanzibar.
“Wizara zote Bara na visiwani wana malengo mazuri ila matatizo yapo kwa viongozi wa vyama wanavifanya ni vyao na kusahau maslahi ya nchi,” anasisitiza Mzee. Asema ili michezo ifanikiwe ni lazima ubinafsi ndani ya michezo uondoshwe na kuweka maslahi ya taifa kwanza kwa kuchagua wanamichezo bora kutoka pande zote mbili.
Dah kirinjiko
Jibu umeliweka wazi kabisa kuwa zanzibar haiwezi kujiunga katika FIFA,kutoka na mfumo ambao huu ulitumika wa FAT kuniunga katika fifa, ipo haja ya kwanza kulimaliza tatizo la muungano na kufanya marekebisho ya katiba ya mungano, japokuwa kumefanyika marekebesho zanzibar kuwa ni nchi lakini bado kwa tanganyika kufanyika na tupo katika wakati mgumu.
Kuna mambo yafanye,tanzania ijitoe katika fifa ingingie kama ni tanganyika ndipo nayo ingie zanzibar,hapa kuna kazi kubwa ya kufanya hivyo,mungano huu tuulonao umeturudisha sana sio kimichezo tu kielimu na kimaendeleo, misaada yote mabayo inakuja kutoka katika umoja wa mataifa inaishia tanganyika,ipo haja viongozi kulivalia njuga na kubadilisha mfumo huu,pia hata vyombo vyetu vya habari tutoe ukweli na kuwaeleza wananchi kwa kila nyia ili waweze kusimama kidete na kuwapush hawa viongozi vipofu na walemavu wa akili waliofanya zanzibar kuwa katika wakati mgumu
asalam alaikum ndungu zangu wazanzibar tunatakiwa tufanye kampeni ya kutosha kuwafahamisha ndugu zetu ambao hawajafahamu katika hayo majimbo 8 ili na wao waelewe kama walivyo elewa wenzao na sio kuwalaumu kwani likiwa zuri na wao wamo na likiwa baya nao pia wamo mama yetu zanzibar ndio anatutoka na docter keshasema dawa ipo ya kumponyesha na kurudi kama yali yake ya zamani kwani akija kutotoka mama yetu zanzibar tusije kulia na kuja kujifanya tulikuwa tunampenda mama yetu zanzibar amepewa sumu na jirani yetu nyumba ya pili yeye hufurahiya na hujigamba kuwa atahakikisha dawa ya kumponyesha hapati kwani ameshatoa rushwa kwa madaktari wengi ili mama yetu zanzibar asipate dawa ya kumponyesha sasa tunae daktari mmoja tu ambae huyu hakutaka rushwa na amesema yeye ataweza kumtibu mama yetu zanzibar yeye docter kasema hatotoka kitu chochote atatutibia bure mama yetu zanzibar anacho taka kasema tumsaidie tu kumnyanyua kitandani alipo kwani peke yake hawezi kumnyanyua sasa sisi watoto wa mama zanzibar tumsaidie kwa umoja wetu kumnyanyua mama yetu zanzibar ili na yeye docter awe na nguvu za kumlisha dawa apate kupona na tufurahi na mama yetu zanzibar kwani jirani yetu alompa sumu mama yetu zanzibar yeye hutuambia tuende kwa wanganga wapiga bao tumejaribu kama anavyo taka jirani yetu hatukufanikiwa na madokta wote ameshawapa rushwa ili mama yetu asitibiwe ninalo omba kwenu tumnusuru mama yetu zanzibar kumpa huyu doktari ambae kaonyesha moyo wa huruma kumtibu mama yetu zanzibar japo tuna ndugu zetu wengine ni wakarofi wao wanashirikiana na jirani kutaka wammalize mama yetu zanzibar akisha kufa na wao wajitie kulia na kuhudhunika hapo baadae
Hakuna kitu kibaya kama kutawaliwa kiakili, na hili linajionyesha kwenye huu Muungano wetu na Tanganyika kiasi kwamba baadhi yetu tumejenga imani kuwa hatuwezi kudai haki zetu mpaka uvunjike Muungano.Hao ambao wanadai kuwa hatuwezi kupeleka maombi yetu ya uanachama FIFA ni sawa sawa na wale ambao wanaosema kuwa ukivunjika Muungano Zanzibar itaumia.Mpaka sasa katika wachangiaji wanaosema kuwa hatuwezi kuomba uanachama FIFA,hakuna hata mmoja alotoa jibu la wazi sisi Zanzibar tuna status gani.Jee ni mkoa ndani ya Muungano,ni koloni la Tanganyika au nchi ndani ya huo Muungano.Vile vile tujiulize mpaka sasa ni lipi kwa kupitia ZFA au Serikali ya SMZ lilofanyika katika kudai haki hiyo,nikimaanisha kutumia wanasheria wa mambo ya katiba ambao wangeweza kuitafsiri hiyo katiba na kuifafanua na kuangalia zipi haki zetu katika suala zima la hayo maombi.Kwasababu lazima tukubali kuwa sisi sote kama binadamu tuna mapungufu katika ufahamu wetu wa mambo.Kwa hiyo hata huyo Ali Tamim alietajwa na Kirangiro ana mapungufu yake ya ufahamu wa mambo na hao CECAFA pia wana mapungufu yao.Kama ilivyo mimi na wewe ufahamu wetu wa huu Muungano na tafsiri yake kimataifa ni mdogo basi huyo Ali Tamim na yeye hali kadhalika.Ndiyo maana hii mada imeletwa hapa tuichangie na tuone wapi tunaelekea.Lakini cha kujiuliza vipi Macau na Hong Kong ambazo zote ni majimbo ya kiutawala (administrative regions) ya China ni wanachama wa FIFA.Nchi ya Montserat yenye watu wasiozidi elfu kumi na ambayo iko chini ya USA nao ni wanachama, hali kadhalika US Virgin Island.Sasa hatuwezi kutumia hizo kama vigezo vya kesi yetu?Au tayari tushakuwa na inferiority complex kiasi kwamba tunajiona dhalili wasio na haki, na hivyo kuwapa ushindi maadui zetu.Kwa kumalizia ningependa kuwatahadharisha wale wanaotumia nchi za Scotland, Wales, Northern Ireland na Uingereza kama kigezo cha kudai haki yetu, njia hiyo haitotusaidia kwani status ya nchi hizi nne ndani ya FIFA hakuna nchi nyengine yo yote duniani wanaoifikia.Kwani hawa ni members wa International Football Association Board.Hiki ni chombo chenye mamlaka ya kubadilisha sheria za mpira wa miguu.Bodi hii ina wajumbe wanane,wanne kutoka katika hizo nchi na wanne kutoka FIFA.Kwa hiyo sheria mpya ya mpira itapitishwa na FIFA pindipo tu itapitishwa na wajumbe sita kati ya hao wanane.Ikimaanisha FIFA haipitishi mabadiliko ya sheria yo yote ya mpira pasipo kupata angalau kura mbili ya hizo nchi nne.