Umoja wa Zanzibar-shairi
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 30/01/2010 // Mashairi // Zima maoni
Assalaam Alaykum
kwa wanaoenda mashairi
baada ya dhiki faraja, wakuu wameamua
mambo huenda yakaja, hasama zikapungua
yaliyopita si hoja, udugu waufufua
jana tulihunzunika, leo tunafurahika
Ingawa twajikongoja, kwema twaelekea
mwanzo wa hesabu moja, kuzuri twakaribia
si lazima kwa koroja, mema sasa twasikia
jana tulihunzunika, leo tunafurahika
chuki waziweka nyuma, pamoja washikamana
furaha kubwa adhima, mioyo yatulizana
kamwe hatutosimama, kitete twashikamana
jana tulihunzunika, leo tunafurahika
mzigo wameutuwa, adui anaumia
sasa mambo yatakuwa, ya kale yatarudia
kasheshe zitapungua, jamii itatulia
jana tulihunzunika, leo tunafurahika
wakawa hawazikani, wafu wakiterekezwa
udugu na ujirani, kuyaeleza nashindwa
tafurani mitaani, vyama vikaendkezwa
jana tulihunzunika, leo tunafurahika
serikali ya pampoja, raia wahamasishwe
haki kwa kila mmoja, faraja iwasilishwe
wapemba na waunguja, jamii ziunganishwe
jana tulihunzunika, leo tunafurahika
adui ana unyoge, limemkaa kubwa donge
ilobaki ajinyonge, yakimzidi mazonge
zenji mbele isonge, sio tena kwa vivunge
jana tulihunzunika, leo tunafurahika
wa Shukran
Mohamed Al Aufi



