Wazanzibari wamtaka tena Karume – Utenzi
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 23/01/2010 // Mashairi // Zima maoni
UTENZI ULIOSOMWA KATIKA MAANDAMANO YA KUUNGA MKONO PENDEKEZO LA KATIBU MKUU LA MABADILIKO YA KATIBA YA ZANZIBAR, 16 Januari 2010
Naanza hili tamko
Ilahi kwa jina lako
Hitaraji nuru yako
Ndio iongoze njia
Nuruyo itangulie
Mbele iniangazie
Nalo giza likimbie
Lisije kunizuwia
Baraka za Tumwa wako
Zilibariki tamko
Lifike nikutakako
Nako liweze pokewa
Lipokewe kwa hishima
Adabu na taadhima
Sababu tunolisema
Hadhi yake twaijuwa
Ni tamko la kusudi
La nia kuiradidi
Kwamba sasa imebidi
Njia yetu kuamua
Ni tamko la kiapo
Nacho hakitangukipo
Wala hakitaangukapo
Na wala kusalitiwa
Ni tamko la shahada
Ni sehemu ya ibada
Na kwalo sina labda
Ni la hakika twajuwa
Ni tamko la fakhari
Ya kuwa Wazanzibari
Tamko la utayari
Wa lolote litokuwa
Basi Mola twatamka
Na hali tuna hakika
Ni Wewe uliyetaka
Sisi hapa kuzaliwa
Ni Wewe uliyetaka
Sisi hapa kuzalika
Na kwalo twaporomoka
Allah kukusujudia
Vyengine ungeamuwa
Ndivyo hivyo vingekuwa
Kwengine tungezaliwa
Kukawa ni biladiya
Bali wewe Mola wetu
Ulitaka pawe petu
Zinjibari iwe yetu
Ndipo ukatugaiya
Tangu zamani za kale
Zama hizo za wavyele
Ulitaka iwe vile
Kwa mapenziyo Jaliya
Waliotutangulia
Nchi wakatuachia
Na wanaofuatia
Wajibu kuikutia
Ndipo kwa sababu hiyo
Tukasema hii leo
Budi tukunjuwe nyoyo
Na cha ndani kukitoa
Ya kwanza kauli yetu
Kwenu viongozi wetu
Sefu na Rais wetu
Karume mwatusikiya
Hapa tushapofikia
Wazenji tushang’amua
Kwamba linotufalia
Ni umoja na usawa
Sasa tumeshatambua
Kwamba tulizuzuliwa
Adui alitungia
Mapande akatugawa
Sasa tumeshafahamu
Mkoloni ‘liazimu
Tuzimwage zetu damu
Yeye akichekelea
Sasa tumeshazinduka
Tuli wajinga hakika
Kukubali gawanyika
Na mahasimu tukawa
Na sasa tumeshachoka
Kulea khofu na shaka
Za wakoloni vishuka
Walizokituumbia
Waliumba mengi mambo
Ya mijini na viambo
Wakatunga na uongo
Na njia za kulindia
Mkubwa ubaya wao
Walofanya watu hao
Ni kugeuza kibao
Cha tarikhi ya Visiwa
Tarehe ikageuzwa
Ubaguzi ‘katukuzwa
Na chuki kapandikizwa
Kwenye vichwa na vifua
Wakafanya taawili
Ionekane ni kweli
Muarabu ni katili
Waafrika ‘kaua
Mwenye damu ya Mwarabu
‘Kafanywa ajinasibu
Ni yeye mstaarabu
Mfanowe hatokuwa
Washirazi ‘kaambiwa
Peke yao ni wazawa
Na mwengine hatokuwa
Mwenyeji jina kupewa
Tukalazwa usingizi
Wazenji tusimaizi
Kamsahau Mwenyezi
Na dini yake Nabiya
Tukalazwa usingizi
Kwayo kali hino dozi
Mwishowe ni uchafuzi
Nchi ikachafuliwa
Leo nyuma ‘kigeuka
Kuangalia hakika
Lipi tulofaidika
Twajua tulifulia
Sasa miongo minne
Tangu sisi tutengane
Ila hisabu uone
Mangapi yametokea?
Ni lipi tulilotoa
Lipi tulilopokea
Na lipi lilobakia
La sisi kujigambia?
Tumepoteza hishima
Ya pamoja kusimama
Kama si baba na mama
Mmoja alotuzaa
Tumepoteza kauli
Ya mambo kuyaamili
Tukaipeleka mbali
Nako ikachukuliwa
Tumetupa kila kitu
Kale kilokua chetu
Leo mbele ya wenzetu
Twaonekana vichaa
Tumevuna udhalili
Na dharau na kejeli
Za nahari na laili
Za kupwa na za kujaa
Tumepokea mashaka
Mabalaa na wahaka
Nchi kuchwa yaripuka
Na neema yapotea
Tumepokea mzozo
Wa sizo kuzeta ndizo
Na sasa kwenye uozo
Zenji inaogelea
Kipi kilichobakisha
Kuweza kuijulisha
Ingalipo haijesha
Nchi yetu ya uzawa?
Basi sasa tumetubu
Tumeshajua sababu
Na pale tu’poharibu
Twataka kupatatua
Ni umoja peke yake
Wa nchi na watu wake
Utaofanya tutoke
Letu kulisimamia
Tukitaka tuvuuke
Humu topeni tutoke
Lazima tuunganike
Natuwe kitu kimoya
Natuwe kitu kimoya
Ndipo ‘taiona njiya
Tuwezayo ipitia
Pazuri tukafikia
Kauli yetu ya tatu
Watusikie wenzetu
Iwapo nchi ni yetu
Ni sisi wa kuamua
Ni sisi wa kuamua
La kuwa na kutokuwa
Kwamba ndio tunojuwa
Lipi linotufalia
Ni sisi na si mwengine
Mwembamba ama mnene
Atakiwaye anene
Nchi kwa kuelekea
Na ndipo kwa haki hiyo
Na kwa nguvu tulonayo
Twatamka hii leo
Wazenji tushaamua
Hatutaki uchaguzi
Tunataka uongozi
Unao usimamizi
Wa nchi kuikwamua
Ili mawili ya mwanzo
Yapate myega na nyenzo
Na tuepuke mizozo
Lazima kusimamiwa
Lakini msimamizi
Shuruti awe mjuzi
Asiwe ni mrukizi
Kati anayerukia
Na awe ni mwasisi
Asiwe ni mfuasi
Na tumuonae sisi
Karume ndiye afaa
Afaaye ni Karume
Bwana huyu mwanamme
Atafanya isikwame
Nchi nyuma kurejea
Ndilo tushaloamua
Sisi wenyewe raia
Karume kuendelea
Mambo kuyaweka sawa
Tumefanya uamuzi
Nasi tukijua wazi
Katiba ni kizuizi
Wa hili tuloamua
Bali Katiba ni yetu
Mali yetu wenyewetu
Hatutashindwa na kitu
Kubadili ‘kiamua
Ndipo natoa kalmia
Kutoka kwa huu umma
Baraza tunalituma
Kurekebisha sheria
Tunalituma Baraza
Katika siku ya kwanza
Sheria kutengeneza
Kama tushavyoamua
Sheria ibadilishwe
Kipindiche kirefushwe
Karume alazimishwe
Mudawe kuongezewa
Nawe Raisi Amani
Tunakujuwa moyoni
Kurefusha hutamani
Mudao ukiishia
Ila sisi ndio watu
Tulokupa kiti chetu
U mtumwa mbele yetu
Wapaswa tutumikia
Tumika tukutamayo
Kwa muda tuutakao
Na ikimaliza kaziyo
Tutakwambia pumua
Lakini sasa hujesha
Ya nini kuharakisha?
Nchi watakaiacha
Irudi kwenye mabaya?
Zenji unayoipenda
Kuiacha njia panda
Itakuwa ni kuvunda
Uloanza jijengea
Neno nikufahamishe
Mtenda jambo asishe
Mwisho asilifikishe
Bora ‘singelianzia
Na hili ndilo tamko
Na ni kwetu litokako
Amani yako mashiko
Ni huu umma sikia
Ni sisi Wazanzibari
Ambao tunadhukuri
Kwa kheri ama kwa shari
Tuko nawe kwenye njia
Tutakacho ni umoja
Hiyo ndiyo yetu haja
Na ndiyo yetu faraja
Nchi yetu kutulia
Twakataa utengano
Chuki na mifarakano
Na Karume ni mfano
Wa hayo kuyaondoa
Mwisho wa hili tamko
Rabbi twaja tena kwako
Tulinde viumbe vyako
Kama tulivyozowea
Tumezoea ulinzi
Wako Ilahi Mwenyezi
Basi tupe ‘situhizi
Tuepushie balaa
Mlinde Rais wetu
Na Sefu kipenzi chetu
Waongoze nchi yetu
Itoke kwenye balaa
Walinde na mahasidi
Walinde na mafisadi
Walinde na makuwadi
Nchi waloikamia
Rabbi kwa rehema zako
Lilinde hili tamko
Lende mbele nyuma mwiko
Lipe nguvu na satuwa
Lisimamishie kweli
Madhubuti mihimili
Na liwe sauti kali
Isiyodharauliwa
Lipe nguvu ya ajabu
Ulizompa Habibu
Kwenye Badri harubu
Ushindi akachukua
Lipe kila mantiki
Naliwe halipingiki
Naliwe halianguki
Hata linapotishiwa
Lifanye liwe ni hoja
Wapemba na Waunguja
Wote wajile pamoja
Utu wao kutetea
Liwe ni neno la wote
Wazenji wawe popote
Wakiuzwa wasisite
Tamko hili kutoa
Na miye nilitowaye
Ulinzinimo nitiye
Adui ‘sikaribiye
Njia kunizuilia
Salama usalimini
Nisikwame safarini
Uwashinde mafatani
Rabbi Wewe wawajua
Basi tulinde wajao
Kwa kheri ya ulinzio
Na hao tuwambiao
Nao walinde sawia
Utulinde Mola wetu
Tuilinde nchi yetu
Tushinde adui zetu
Hasidi waone haya
Kile kilichobakia
Kwenye yetu Biladiya
Kilinde kisijetwawa
Nacho kikeshapotea
Ilinde na dini yako
Walinde na waja wako
Iwe kwa hili tamko
Mwanzo wa kutuongoa
Ilahi tupe umoja
Wapemba na Waunguja
Tuweze kujenga hoja
Ya nchi kujilindia
Ya Rabbi tupe mapenzi
Tuchukie ubaguzi
Tushikane kama wenzi
Mapacha tuvyozaliwa
Ya Karima Mola wetu
Hupungukiwi na kitu
Ukitupa nchi yetu
Kama vile ‘livyokuwa
Kwako Bwana tuombacho
Sio zaidi ya hicho
Tufumbue yetu macho
Na nuru kututilia
Tuwezeshe kung’amua
Kosa tulilokosea
Kisha tuongoze njia
Ya hapa kujinasua
Lau hii ni adhabu
Kwa mambo tuloharibu
Kwako Ghafuru twatubu
Na toba zetu pokea
Zipokee toba zetu
Ufanye ujira wetu
Ni kutupa nchi yetu
Kama vile ‘livyokuwa
Wewe Bwana hufundishwi
Na wala hurekebishwi
Na wala hulazimishwi
Watenda unoamua
Ukitaka jambo kuwa
Husema “Kuwa” likawa
Sababu u mwenye quwa
Na ilimu iso doa
Lakini hatuna budi
Kukuomba Ya Majidi
Sisi ni wako ibadi
Tunaokutegemea
Kwa rehemazo Wadudi
Na dua za Muhammadi
Tumiminie suudi
Bariki hivi Visiwa
Swala nyingi na salamu
Zende kwa Abu Qassimu
Na sahabaze kiramu
Na wakeze wote pia
Na wote maiti wetu
Wazazi nao wenetu
Warehemu Mola wetu
Kwa Fatiha tun’otia



