Polisi wafufua kitengo cha kuchunguza uhalifu mtandaoni
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 23/07/2009 // Teknolojia // 1 Comment
JESHI la Polisi limeunda timu ya kuchunguza matukio ya uhalifu kwa njia ya mitandao, simu za mikononi, ATM za mabenki na huduma nyingine za mitandao cha Ant cyber crime Unity ili waweze kubaini watu wanaotumia mitandao hiyo, kinyume na taratibu.
Hatua hiyo, imekuja baada ya kutokea matukio ya wizi katika ATM za benki, wananchi kutumiana ujumbe wa matusi kupitia mtandao na simu za mikononi na kusababisha usumbufu kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, (DCI) Robert Manumba alisema matukio hayo, yameibuka nchini hivi karibuni na kusababisha baadhi ya wananchi kupata matatizo.
Alisema wananchi wengi wamekuwa wakitumia mitandao hiyo, kinyume na taratibu, na kusababisha upotevu wa fedha.
Alisema kutokana na hali hiyo, jeshi hilo litawashughulikia wananchi wote watakaobainika kufanya vitendo hivyo, kinyume na taratibu.
“Kuna baadhi ya wananchi wanatumia mitandao vibaya, baadhi ya wanatumia ili waweze kuwatukana wenzao, wengine kuiba na kusababisha malalamiko mengi kutokea,” lisema Manumba.
Alisema timu hiyo, itahakikisha wanaofanya vitendo hivyo, wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
Manumba alisema hivi sasa wanaboresha timu hiyo ili iweze kufanya kazi na kwamba anaamini mpango huo, utafanikiwa.
Alisema timu hiyo, ilikuwepo muda mrefu, lakini ilishindwa kufanya kazi kwa sababu matukio ya wizi kwa kutumia mitandao, haikuwepo.
Wakati huo huo, Manumba alisema hivi sasa wanakichunguza chama cha kiislamu kinachojishughulisha na kutetea haki na maslahi ya waislamu nchini.
“Kuna baadhi ya kundi la watu linalojishughulisha na masuala ya siasa ndani ya dini, jambo ambalo linaweza kusababisha mvutano kwa wananchi, kutokana na hali hiyo, tunatakichunguza kwanza ili tuweze kubaini undani wake na kazi wanazozifanya na ikabainika wamekiuka taratibu, watachukuliwa hatua za kisheria,”alisema.
mwananchi





One Comment on "Polisi wafufua kitengo cha kuchunguza uhalifu mtandaoni"
Nimesoma taarifa ya kuanzishwa kwa kitengo hichi kwa mshangao kidogo, ni wazo zuri wakati duni inaondoka katika mfumo wa maisha asilia kwenda katika mfumo wa maisha pepe (virtual life), kwa kuwa katika mfumo wowote wa maisha kutakuwa na wenye kuhalifu, na kwa maana hiyo kuanzishwa kwa kitengo hichi ni dhana nzuri lakini kwa maoni yangu kitakuwa sawa na mbwa mkali asiyekuwa na meno.
Kwa wale wahalifu waliobobea ni tabu itakuwa kuwatia hatiani, kwani sheria tulizonazo haziendani na mwenendo wa matendo ya jinai katika mfumo wa maisha pepe (virtual life) hivyo kabla ya kukurupuka kuunda kitendo tulipaswa kubadilisha mifumo ya sheria zetu hususani hususan sheria ya mwennedo wa makosa ya jinai na ile ya ushahidi unaokubalika mahakamani ikiwa ni pamoja na kuainisha mipaka (jurisdiction) kwani inawezekana mtu akawa Marekani atanda kosa Tanzania kwa kutumia mtandao ambapo kwa sheria tulizonazo mamlaka ya Tanzania itakuwa haina uwezo wa hata kumhoji mtu huyo sembuse kumpeleka mahakamani.
La muhimu kwanza tutafute meno (sheria) zenye kuendana na mfumo wa maisha uliopo (utandawazi)mfano kule Uingereza walipoanzisha kitengo cha namna hii kwanza waliasha sheria moja maarufu Computer Misuse Act 2000 kupambana na makosa sawa na dhamina na kitengo hichi, sambamba na kuanzisha sheri tunapaswa kujenga uwezo wa kitaalamu hii ni pamoja na kuanzisha digital forensics labaratory na kuwa na digital forensics analyst ambao wataisaidia mahakama katika katika mwenendo wa kesi (expert wtinesses, forensics analysis ni muhimu sana katika kujenga hoja ya kesi kwa upande wa mashitaka mahakamani vinginevyo katika kesi 1000 zitakazopelekwa mahakamani kama upande wa utetezi utakuwa na wakili wazuri wanaweza kutumia technicalities zilizo katika Tanzania Evidence Act and Criminal Evidence Procedure Act kufuta kuwepo kwa shitaka, na hivyo ni kazi bure.
Ni muhimu tusikurupuke tuende hatua kwa hatua, na kwanza sheria, uwezo wa kiutendaji, tusomeshe hao digital forensics analyst and cyber law prosecutors kabla ya yote vinginevyo kitengo kitafufuliwa na baadaye kitakufa tena, kitafufuliwa na baadaye kufa tena, tatizo ni kutokuwepo kwa nyenzo, sheria na utaalamu.