HISTORIA YA PWANI YA AFRIKA MASHARIKI (KWA UFUPI SANA)
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 04/02/2010 // historia // 20 Comments
Audhu biLlahi mna shaytani rajym. Rabby ish rahlysadry wayasirly amry wahlul uqdatan min lisany yafqahu qawly.
Assalamu alaykum,
Ingawa kila baada ya muda inabidi niyarejelee baadhi ya yaleyale niliyokwisha kuyaelezea mara kwa mara, lakini pia hadi inafurahisha hadi kuwaona ndugu zetu wanajishughulisha kwa kusoma khabari za taarikh yao na wanatumia mantik na hoja kuyachuja yasiyoingia akilini na pia kuuliza masuali kwa yale wasiyoyajua. Haya mas-ala ya nani kafika Pwani ya Afrika Mashariki kabla ya nani nimeyaandikia mara kwa mara. Lakini ni muhimu ifahamike kwa uwazi kabisakabisa kuwa kuna utumiaji mbaya wa taarikh uliokuwa ukitumiliwa na wanasiasa ili kuwabagua wananchi wenzao. Kwangu mimi, na nimeshaelezea zamani, kuwa madam mtu ni mwananchi wa nchi yoyote, awe wa asili yoyote ile, ni makosa makubwa kumyima haqi zake kwa kisingizio kuwa ati hana asili hii au ile au kumbagua kwa dhana kuwa wavyele wake walifanya hivi au vile. Iweje iwapo wavyele wa mmoja wamewasili mwambao wa Afrika Mashariki au katika nchi yoyote Duniani jana na wengine juzi! Mwenye-enzi Mungu Anatuambia kuwa:
Enyi watu! Kwa hakika tumekuumbeni(nyote) kwa (yule) mwanamume (mmoja; Adamu) na (yule yule) mwanamke (mmoja; Hawwa). Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbali mbali) ili mjuane (tu basi; siyo mkejeleane). Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi katika nyinyi. Kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye habari (za mambo yote).
AL-HUJURAT(49:13)
Tuje sasa katika suala la kuwasili watu Pwani ya Afrika Mashariki kwa sababu ya taaluma na kuujua ukweli tu wala si kwa kubaguana, maana tumechoka kuona wananchi, khasa wa Zanzibar kubagua na kubaguliwa kwa hoja za kitaarikh ya kusowa na kupaaza.
ASILI YA WASHIRAZI
Ni kweli kabisa kuwa Washirazi walitoka Uajemi (Ufursi/Persia/Iran) kuja pwani ya Afrika Mashariki; lakini jee hilo tuu linatosha kusema kuwa Washirazi wa Afrika Mashariki ni Waajemi? Jawabu ni “la” hilo halitoshi kabisa. Ingawa Washirazi walioko Afrika Mashariki wametokea Uajemi, lakini kabla ya hapo walitokea Arabuni na kwenda huko Uajemi katika eneo linaloitwa “Arabstan” ambako kulitawaliwa na Waarabu zamani, na mpaka leo moja katika lugha kubwa inayotumika huko ni Kiarabu na wana mpaka idhaa zao za redio na runinga (TV). Jee kuna uthibitisho gani unaoonesha kuwa hawa Washirazi wa Afrika Mashariki ni watu wenye asili za Kiarabu? Moja katika ishara kubwa ni jina la kabila. Tukiangalia kabila za waliohifadhi majina ya kabila zao kama vile Mamwinyi Wakuu na Mkamandume tunagundua kuwa kabila zao ni za Kiarabu si za Kiajemi. Kwa mfano, (1) Mkamandume wa Pujani, Pemba – Muhammad bin Abdul-Rahman Addibawy. (2) Mwinyi Mkuu wa Tumbatu – Sultan Yusuf bin Alawy Al-Ahdaly na (3) Mwinyi mkuu wa Dunga ni Muhammad bin Hasan Al-Alawy. Wote hawa kabila zao ni za Kiarabu; na ni kweli kabisa kuwa wavyele wao waliwasili Pwani ya Afrika Mashariki zamani sana kabla ya kuwasili Wabantu; na hata kabla ya kuwasili Washirazi hao, zamani zaidi walitanguliwa na Waarabu kutoka Arabuni moja kwa moja na kuhamia Pwani ya Afrika Mashariki. Kwa hivyo Waarabu hawa na Washirazi ndio khasa “wenyeji” kuliko wanaojinata kuwa ni wenyeji zaidi leo kwa ajili ya “Ubantu” wao. Lakini wapi! Historia imepinduliwa na kumfaya mgeni kuwa mwenyeji wa asili, na mwenyeji mwenye kuujua ukweli, kwa khofu zake alizojazwa, kujiogopea kuelezea ukweli huu wa asili yake. Kwa hivyo Waarabu Waliotokea Arabuni na waliohamia Arabstan kabla ya kuja Afrika Mashariki wamewasili kwa karne nyingi kabla ya kufika Wabantu Pwani ya Afrika Mashariki. Kwa hakika, Waarabu walianza kutambaa Mwambao wa Mashariki ya Afrika karne nyingi sana nyuma.
Kuna sababu nyingi zinazowafanya watu kuhama waliko na kuhamia nchi nyingine, lakini tatu katika sababu hizo ndizo zilizosababisha uhamiaji zaidi, nazo ni kuzidi idadi ya watu mpaka ikawa ardhi haiwatoshi kujipatia vyakula; pili ni ya ardhi kuwa mpovu kwa ukosefu wa mvua na, tatu ni vita na kukhofia kuuwawa au kutiwa utumwani. Sababu kubwa iliyowafanya Waarabu kuhama na kuhamia nchi za rutuba kama Pwani ya Afrika Mashariki mpaka Malasia na Indinisia ni hiyo ya ukami ukifatiliwa na vita baina yao. Ukami umetokea mara kwa mara Arabuni na kwa karne nyingi; kwahivyo tokea zama za zama Waarabu wamekuwa wakihama na kuhamia nchi zenye rutuba.
Waarabu waliunda majahazi tokea siku za kale na walizielewa vizuri pepo za Musim na kusafiri kuelekea nchi mbalimbali. Lakini karibu zaidi kwao ni pwani ya Afrika Mashariki kuanzia Jibuti mpaka Sofala. Ni masafa ya saa chache tu baina ya Yemen na Jibuti na hakuna kilichowazuia kuhamia katika upwa huo. Hawakuwa na haja ya kusema tuwangojee kwanza wafike Wabantu kutoka Cameroon, tuwape nafasi wao kwanza, ikisha ndiyo tuhamie sisi. Ukami na vita hauna subira hiyo ya kichekesho.vya “paukwa pakawa.”
Nikikuambieni kuwa Waomani walifika mpaka Amerika, tena si pwani tu ya Amerika bali ndani kabisa ya bara hilo katika sehemu za Colorado, jee mtaniamini? Tabaan kuna ambao hawataniamini na kusema huyooo naye anatuletea hadithi za kiajabu! Basi nakunakilieni yaliyoajiri hivi karibu, tafadhalini fungueni mtandao ufuatao muuone wenyewe huo ushahidi unavyooneshwa na mabigwa wa taarikh na wa pili mujisomee yaliyoandikwa au andika katika “google search” mameno “Ancient Arabs in Amerika” ujone, usikie na ujisomee mwenyewe ninayokuelezeni.
Video results for Ancient Arabs in Amerika
[youtube]http://www.youtube.com/watch?v=i4qSVm-21gQ[/youtube]
Ilivyokuwa Waomani wameweza kufika mpaka Amerika ndani karne hizo za nyuma, Waomani hao walipitia wapi na bahari gani? Sii watakuwa kwanza wametambaa na upwa wa Afrika Mashariki kabla ya kupitia Afrika ya Kusini na kuingia katika bahari ya Atlantik? Kilichowazuia kufanya maskani katika Upwa wa Afrika mashariki kabla ya hapo ni nini?
Jee kulikuwa na Waafrika Pwani ya Afrika ya Masharika kabla ya kuwasili Waarabu? Naamini sana kuwa walikuwepo Wasomali, Wahabeshi na jamaa zao wngine, na hawa wamekhusiana sana na Waarabu na wako mbali na Wabantu kiasili, kilugha na kimila. Kwa mfano, Wahabeshi ni Wasemiti na vivyo hivyo walivyo Waarabu wa Arabuni. Ni watu wenye asili moja.
KUWASILI KWA WABANTU
Sababu kubwa iliyowafanya Wabantu kuhama kwao Cameroon kama miaka elfu nne nyuma ni kuzidi idadi ya watu pahala pamoja. Lakini tafauti na Arabuni ambako sehemu kubwa ni jangwa, sehemu kubwa ya Afrika kusini ya Sahara ni ardhi ya rutuba na hivyo palipozidi idadi ya Wabantu katika eneo moja, basi hawakuwa na haja ya kuhamia mbali na jamaa zao; masafa mafupi tu huweza kupata ardhi za kilimo na pia kuwa hawapo mbali na jamaa zao ni himaya kubwa kwao kwani panapotokea vita au shida, huwa wanawategemea jamaa zao kuwatetea. Kwahivyo Wabantu walihama polepole na kuhamia masafa ya karibu tu kila mara. Mambo haya nimeelezeya tena na tena katika mtandao huu na kwingineko pia na kuwapa changamoto Watanganyika wenye siasa kali ya “Uafrika mbele” na wafuasi wao walioko visiwani wenye kudai kuwa wao ndio wenyeji zaidi ili kuwabagua wasiokuwa Wabantu watuelezee kitaaluma na taarikhi ya kweli, siyo ya “paukwa pakawa,” ni nani waliofika mbele na kujenga miji yao?
Ukweli ni kuwa Wabantu hawakufika kwenye Maziwa Makuu kabla ya baina ya miaka elfu na elfu na mia tano iliyopita kutoka kwenye shina lalo lililoko Cameroon, Afrika Magharibi, na kutoka hapo, mapote mawili yaliondoka, moja likaelekea Afrika ya Kusini na jingine likaelekea Somalia na wote hawa hawakufika Pwani ya Afrika Mashariki mpaka katika karne ya 16, wakati huohuo walipoanza kuwasili Waportugizi. Wabantu walikuta Waarabu wameshastaqini kwa karne nyingi sana kabla yao na wameshaijenga miji yao. Wabantu (Wazimba) wakawaingilia Waarabu katika miji yao kuanzia kusini ya Sofala mpaka Kaskazini ya Mwambao wa Afrika Mashariki na kuwapiga na kuwageuza vitoweo wenyeji hao waliokuwa Waarabu na wengine kuwachukua mateka kama ni watumwa wao; na huku kutoka baharini Waarabu wakipigwa na Waportugizi na kutawaliwa. Ama Wabantu waliokwenda Somalia walipigwa na kurejeshwa nyuma na wengine kumalizikia kusini ya Somalia na Mwambao wa Kenya. Anatuelezea Mhishimiwa Roland G. Ngala ambaye alikuwa mmoja katika wakuu wa Kigiriama na Waziri katika Sirikali ya Kenyatta katika ukurasa wa 2 wa kitabu chake kiitwacho Nchi na Desturi za Wagiriama, alikichapisha kitabu chake 1949 kuwa: “[...] Yasemekana kwmba ni kama miaka mia tatu tangu wafike nchi ile waliyomo sasa, waiitayo Giriama [...].” Wagiria ndio kundi kubwa la Wabantu walioko Mwambao wa Kenya. Ni miaka mingapi leo tokea walipowasili kwa mujibu wa chifu wao?
Iwapo tunazungumzia kukhusu wenyeji wa Pwani ya Afrika Mashariki basi itakuwa ni Waarabu na jamaa zao wa karibu kama Wahabashi na Wasomali na si Wabantu. Changa moto hii ipelekeni kwa “mabingwa” wa taarikh za alifu layla u-layla wa Tanganyika walioko Chuo Kikuu, Dar-es Salaam waipinge kwa ushahidi na hoja na mantiki kama wanayo.
Uswahili haukuanza kuzuka mpaka hapo walipoanza kuteremka Wabantu Pwani ya Afrika Mashariki katika karne ya 16 na kuingiliana na wenyeji waliokuwa Waarabu (kwanza kwa vita na baadaye kwa njia za salama). Uangalie vizuri Uswahili ulivyo — kilugha, yaani kimsamiati na kinahau; kimila na dasturi na kwa kila namna — utakuta kuwa huwezi kuutoa Ubantu na huwezi kuutoa Uarabu na pia Uislamu ukakabiwa na Uswahili.
Kila la kheri,
Ibrahim
Added following Ashakh’s comment:
REFERENCES:




20 Comments on "HISTORIA YA PWANI YA AFRIKA MASHARIKI (KWA UFUPI SANA)"
so what?boring!!pumba tupu yawn!
Muunguja,
Ahaa! Boring! Ama wewe umekosa fadhila. Baada kazi yote aliyo ifanya Prof Ibrahim Noor, ushahidi wa nukta baada ya nukta, bado wewe unasema boring, wakati amekupa usiyo yajuwa.
Haya lete ya kwako iliyo nzuri zaidi ya hii ili utuelimishe tusio juwa.
@Muunguja
Huyo jamaa hana shukurani ata afanyiwe nini.Ni vyema ukajifunza kuwa na shukurani ndugu yangu, akili yako iko too negative thinking.Unalalama hata kwenye sehemu hazina umuhimu wa wewe kulalama.
Kumbuka shukurani haikugharimu chochote, na hao watu kama Prof.Ibrahim wamepoteza muda wao na kujitolea kuandika na kutoa elimu ya historia ambayo serekali yako imekuwa mstari wa mbele kuipotosha kwa maslahi ya kisiasa.
Mbali na muda Prof.Ibrahim pia muda wangu wa kuichapa hapa.Kumbuka kuwa kila kitu kiko kwa kizalendo, sio kama ni kazi au ajira hii.Ningekushauri ukajifunza kuthamini kazi za watu wengine.
Si matarajia yangu kuwa kila kinachochapishwa hapa ni kwa ajili ya kukufurahisha wewe nafsi yako.Mimi binafsi yangu nachapisha mambo mingi hapa si kwa lengo la kuwa napenda maandishi au kazi hiyo, bali kwa lengo la kuwapatia nafasi wananchi au wazalendo wengine nafasi ya kusoma.
Sasa si busara hivi unavyofanya wewe muunguja, ukiona chapisho liko boring basi jua hilo chapisho si kwa ajili yako ni kwa ajili ya watu wengine.Huu mtandao hautembelewi na wewe pekee au kuwa sisi tupo hapa kwa ajili ya kukufurahisha wewe tuu!!!
muunguja ukiendelea na siasa mbovu humu tutapendekeza utolewe.
Yako wewe sio maoni ni uhuni! Ikiwa umekusudia comedy basi hakuna anayecheka!
Ukiwa hujiheshimu; basi angalau heshimu unakotoka kijana…
Anwani ya ADMINISTRATOR ni admin@mzalendo.net.
Maoni ya kumuondosha yakifikia 3 tuu, atazuiliwa haki za kugusa mtandao huu.Uwezo wa kiufundi wa kukuzuia kugusa mtandao wetu tunao, DONT TEST OUR CAPABILITIES ON THAT!
@Muunguja
You have been warned. We hate going after our users, but it doesn’t mean we will just watch you and do nothing. When we receive complains we work them out.Be aware of that.
Masuala ya historia ya nani alifika mwanzo Zanzibar ni debated topic hata kama itaelezwa na nani. Mie naweza kusema huyo Prof. nadhani anavutia kamba kwake unless kama yeye asili yake ni bantu basi kidogo ningeipa benefit of the doubts hii makala yake. Kwa kweli nakubaliana na hiyo agurment yake kwamba waarabu walikuwa ni watu wa kuhama hama mapema sana kutokana na hiyo hali ya ukame na maendeleo katika usafiri wa baharini, hata hivyo kidogo nahisi kaelezea kishabiki kwamba waarabu wangefika Zanzibar mwanzo kuliko wa bantu.
East Africa kwa ujumla kumevumbulia fossils nyingi sana kuliko sehemu yeyote afrika, hivyo kuna ashiria kwamba ni sehemu iliokaliwa mapema sana. In fact kabla kuandika hii makala nimeperuzi fossils records za afrika hakuna hata moja nilioiona kutoka west afrika au huko Cameroon alikosemea Prof. kwamba wabantu ndio walisalia.
Uvumbuzi wote wa mafuvu kutoka afrika yamepatikana Kenya, Ethiopia, Tanzania, South Afrika na Chad kwa central. Kwa vile pwani ya Bagamoyo ipo karibu sana na Zanzibar kuna uwezekano mkubwa sana kwamba afrika kutoka mainland walifika Zanzibar mapema sana kuliko hao wageni kutoka mbali. Hebu tizama kwamba east africans walifika hadi Madagascar kweli washindwe kufika Zanzibar.
Prof. anatumia kigezo cha majina ya mwinyi wakuu wa Zanzibar ambao hawa ni watu wa karibuni tu kuelezea historia ya washirazi wa Zanzibar wakati visiwa hilikaliwa hata kabla ya hizo chiefdoms. Mie sina mashaka wala ubaya na watu wenye asili ya arabuni waliopo Zanzibar na kwangu naona wao wanahaki sawa sawa na wale weusi kabisa ila kusema kwamba waarabu walifika mwanzo nahisi ni upendeo tu wa kihistoria.
Naweza kukubali kwamba waafrika wengi waliopo Zanzibar hivi sasa basi mababu zao na mabibi zao walikuja Zanzibar karne za karibuni kuja kufanya kazi kwenye mashamba ya waarabu kama watumwa ila napinga kabisa kwamba waarabu au washirazi walipofika Zanzibar hapakuwa na mtu yeyoyote mweusi alie settle kabla yao.
Nawasilisha.
Dont argue with a fool people will never know the diff…..
Nawapongeza wale wote wenye maelimisho.
Ahsante.
Kwa mujibu wa Mgiriki, mwandishi wa kizamani na msafiri aliyewahi kuzitembelea sehemu nyingi za mwambao wa Afrika Mashariki, katikati ya karne ya kwanza (1st century A.D), anasema katika kitabu chake The periplus of the erythrean sea kuwa ameukuta mwambao wote wa Afrika mashariki wakati huo ukiwa umeshahamiwa na watu wa asili ya kiarabu tu, na wanamtambua mfalme wa Yemen kuwa ndiye mtawala wao. Anasema kuwa watu aliowakuta wote ni wa asili za watu wasiokuwa waafrika, na hakukuwa na hata alama ya mtu mweusi kwa wakati huo. Ni hakika kwamba Periplus, inayozungumzia mwambao wa Afrika ya mashariki na kuja chini kusini mpaka Zanzibar, haikuwataja kabisa watu weusi. Geographia ya kiplotemi inawazungumzia (wabantu) na kuwepo kwao mwambaoni, lakini ni kusini kabisa ya eneo hilo ndiko wanakotokea, ambako bila shaka ni kiasi ya kusini ya Msumbiji ya sasa, ukija kwa juu kaskazini zaidi ya eneo hilo (la Afrika mashariki), watu waliokuwepo ni wasomali na wa-Ethiopia watupu (Oliver na Fage 1962: 98). Pia wakati Ibn Batuta, msafiri na mwandishi maarufu, alipoutembelea mwambao wa Afrika mashariki katika karne ya 14 alishangazwa sana alipowaona washwahili kuwa ni watu waliokuwa na nyumba zao nzuri, waliokuwa wakijuwa kuvaa na kula kama walivyokuwa wazungu wa wakati huo. Kwa mujibu wa ukweli huu waarabu walikuwepo katika mwambao wa Afrika ya mashariki na Zanzibar kwa zaidi ya miaka 2000 nyuma..
Ngano nyingi zimetungwa na kusemwa kuhusu wenyeji (wahamizi wa mwanzo) wa visiwa hivi. Wahadimu, wapemba (wadiba) na watumbatu ndio historia inaowaita wenyeji kindakindaki wa vsiwa hivi vya Unguja na Pemba. Hii ni kutokana na kufika kwao mwanzo, kuhamia na kujenga masikani na miji yao katika Visiwa hivi karne nyingi zilizopita huko nyuma. Wahadimu walikuwepo katika kisiwa cha Unguja na walikuwa wakiishi kwa wingi katika maeneo ya Nungwi, Kijini, Muyuni, Pwani mchangani, Chwaka, Bwejuu, Makunduchi, Kizimkazi na Uzi. Mji mkuu, au mji muhimu wa wahadimu ulikuwa ni Dunga. Watumbatu walikuwa wakiishi katika maeneo ya kisiwa cha Tumbatu. Pia watumbatu walionekana kuishi maeneo kama vile Donge, Bumbwini na Mwanda (Ingrams 1962).
Wahadimu hawa, watumbatu na wapemba historia inawaita washirazi, kwa kuwa waliondokea katika mji wa Shiraz- Iran (Persia ya kale) na kufanya masikani yao katika ardhi za visiwa vya Zanzibar. Inaaaminika kuwa wenyeji hawa wa Zanzibar wa mwanzo, asili zao ni kutokea huko Shiraz-Iran. Lakini hapa ifahamike vyema kuwa ushirazi wao huo ni sawa na mzanzibari wa asili ya kibanianii, utamwita mzanzibari kwa uzalendo (watwani wake) wa kuishi Zanzibar kama kwao lakini asili yake itabakia ni banianii vile vile. Pia ni sawa na mnyamwezi aliyetokea mrima, atakuwa mzalendo wa kizanzibari kwa kuwa ameshaifanya Zanzibar kuwa watwani wake lakini asili yake ni mnyamwezi vile vile na ataitwa mnyamwezi. Basi hivyo pia ndivyo walivyo wenyeji hao wa visiwa vya Zanzibar wajulikanao kama washirazi. Msikiti wa Kizimkazi, ni katika mabaki ya kihistoria yaliyo na umri mkubwa zaidi Zanzibar. Msikiti unakisiwa kuwepo hapo si chini ya miaka 900 hivi. Msikiti huu unaakisi ustaarabu wa waarabu au wa-persia (washirazi) ambao walikuwa wameshafanya masikani yao Zanzibar makarne hayo huko nyuma. Kwenye ukuta wa mihrabu wa msikiti huu pameandikwa hivi kwa ki-persia: “hii ni amri ya Kiongozi mtukukufu Sheikh Assayid Abu Imran Musa bin Alhassan bin Muhammad, Mungu ampe maisha marefu na awaangamize maadui wake”. .Kwa kuwa watu hawa walioishi kwa muda mrefu Shirazi-Iran kabla ya kuelekea Zanzibar, basi si jambo la kushangaza kuwa ustaarabu wa kishirazi umeshachangaanyika na ustaarabu wao wa asili wa kiarabu. Ndio maana maandishi ya kwenye mihraab ni ya mchanganyiko wa lugha mbili (maneno yameandikwa kwa kipersia lakini nambari zimeandikwa kwa kiarabu). Staili ya ujenzi wa msikiti huo pia haitofauiani na zile za misikikiti na majumba ya kale yaliyojengwa na waarabu.
Wadiba (wapemba) pia wananasibishwa na washirazi bali ni watu walio na asili zao kutokea katika mji wa Diba. Diba ni mji ulioko baina ya Oman na Sharjah. Inasemekana kuwa uko mji mwengine unaoitwa Diba maeneo ya bara Hindi, lakini hiyo sio Diba ya asili. Diba hiyo ni sawa na miji kama vile Mombasa Unguja, na Taifu Pemba, kwani majina haya ni ya kuazima kutoka katika miji ya asili, yaani Mombasa ya Kenya na Taifu ya Uarabuni. Mitindo yao ya misikiti na majengo waliojenga huko Pemba katika masikani yao katika miji kama vile Pujini na Kengeja ni sawa na ile ya Diba ya Uarabuni. Angalia mabaki ya majengo ya kale na vihame vya Mkamandume unaweza kuthibisha maneno haya.
Watu hawa, yaani watumbatu, wahadimu, wapemba (wadiba) mwanzoni kabisa baada ya uhamiaji wao, walikuwa wakiishi kwa mifumo ya tawala za kienyeji. Waliishi katika tawala zao za kienyeji zinazojitegemea, yaani Watumbatu walikuwa na mtawala wo, wahadimu walikuwa na mtawala wao na wapemba (wadiba) walikuwa na mtawala wao. Mtawala wa kienyeji wa wapemba anaekumbukwa zaidi na historia ni Mkamandume. Baadhi ya wakati tawala hizi zilikuwa na masikizano na baadhi ya wakati zilikuwa na migogoro ya hapa na pale. Tofauti na Unguja ambako kulikuwa na tawala zaidi ya moja, Pemba kulikuwa na tawala moja tu iliyojitambua kama dola kamili ya peke yake, dola ya Mkamandume.
Kuhusu mahusiano ya wazanzibari na Persia (Iran) ni jambo linaloelezewa vibaya na wanahistoria. Ni ukweli usiopingika kuwa upo uhusiano wa wazanzibari na Persia upo. Miongoni mwa dalili muhimu za mahusiano ya wazanzibari na Persia ni ile kumbukumbu ya maneno ya kipersia iiyobaki katika mihraab ya msikiti wa Kizimkazi ambao unakisiwa kuwepo hapo kwa muda wa miaka 900. Pia ni vile kusherehekewa kwa mwaka mpya wa kiajemi yaani Nairooz. Mwaka mpya wa kiajemi (Kiiran) husherehekewa sana na kwa shangwe Zanzibar. Zaidi sherehe hizi zinaonekana yale maeneo yaliokuwa ni ngome kuu za wenyeji hao wa Iran kama inavyonekena kwa wamakunduchi hivi leo. Lakini ifahamike kwamba watu hawa waliitwa washirazi kwa kuhamia kwao katka mji wa Shirazi wakitokea Arabuni, hasa katika sehemu za Oman, Sharjah na Saudi Arabia. Kwa hivyo asili zao zinabakia kuwa ni waarabu. Kwanza asili ya mtu ni kabila lake na sio watwani wake. Hebu tuwaulize hao wasemao watu hao ni washirazi na kuwaita washirazi kabila za watu hao hasa ni zipi? maana ushirazi sio kabila wala asili ya mtu bali ni watwani (masikani) ni sawa na kusema utumbatu na upemba, kwani utumbatu na upemba sio makabila wala asili za watu bali ni masikani za watu hao. Makabila ya watawala (mamwinyi) wa watu hao walioitwa washirazi ndio uthibitisho mkubwa zaidi. Makabila yao ni kama vile Al-alawi, Al-bajuni, Al-addibawy, Al-bahasany, Al-ahdali, Al-attasi n.k. (Issa: 1999).
Wazanzibari na Ubantu
Wabantu ni jamii za waafrika weusi wanaozungumza lugha za kikabila za kiafrika amabo wana asili zao kutokea Afrika ya kati, Afrika ya Kusni na Afrika Kaskazini. Wabantu ni kizazi kilichopatikana baada ya maingiliano kati ya watu mweusi (negros) kutoka maeneo ya kusini mwa Afrika na wahamaiti (hamites) kutoka maeneo ya Afrika Kaskazini. Kwa kweli hakuna tarehe rasmi ya uhakika ni enzi gani wabantu walihamia mara ya kwanza Zanzibar, lakini mpaka mwishoni mwa mwaka wa 700 kabla ya kristo (B.C ) kwa yakini sio Zanzibar tu, bali Afrika mashariki yote kiujumla ilikuwa ishavumbuliwa na kuhamiwa na watu wasio na asili ya kiafrika. Ni vigumu kukisia ni karne ngapi nyuma hasa wabantu walifika katika mwambao wa Afrika ya mashariki na hatimae wakafika Zanzibar na Pemba. Walifika huko baada ya mwambao kwisha kuvumbuliwa tayari na watu waasili zisizokuwa za kiafrika. Mwambao wa Afrika mashariki ulikuwa unafahamika na wenyeji wa Arabuni katika karne ya 8 kabla ya Kristo. Taifa la Kiarabu la Ausan ambalo lilisambaratika mwaka wa 700 Kabla ya Kristo, lilifanya biasharana na bila shaka lilimiliki sehemu ya mwambao (Gray 1962: 10-11).
Tarikhi zinaonyesha kwamba katika nyakati za karne ya 16 (16th century AD) ndani ya ukoloni wa kipotugizi ndipo hasa mababu na mabibi zetu wa asili wa kibantu walipoanza kuingia Zanzibar kwa mara ya kwanza. Tena kuanzia hapo uingiaji wa wabantu kutoka Mrima kuingia Zanzibar ukawa ni wa kawaida na kwa wingi. Hata baharia, mpelelezi wa kiportugizi, Vasco Dagama, aliekuwa akifanya upelelezi sehemu mbalimbali kwa lengo la kuweka ukoloni, mwishoni mwa karne ya 10 (10th century) alifika Afrika ya mashariki na huko aliwakuta watu wa mwambao kuwa ni wale watu wa ustaarabu wa jahazi tu, na akasisitiza kuwa watu hao walikuwa wanauwelewa vyema ustaarabu wa ubaharia wa jahazi (dhow civilization) kama alivyokuwa akiujua yeye (Issa 1999).
Baada ya kuhamia wabantu wakitokea Mrima, walioana na wenyeji wale walioitwa wahadimu, wapemba, na watumbatu na kupatikana watoto machotara. Machotara hawa ndio wale waitwao waswahili. Hata mwinyi mkuu wa Dunga anaonekana nae alihemkwa na mabibi wa kibantu na kuzaa watoto machotara. Angalia picha maarufu ya mwinyi mkuu wa Dunga, Ahmed bin Muhammed bin Hassan Al-Alawi (ambae bado angaitwa Mshirazi) katika vitabu vya historia akiwa na mwanawe. Katika picha hiyo Mwinyi mkuu huyo anaonekana yeye amekozea maumbile ya kiarabu, lakini mtoto wake ni chotara, ameshapoteza ule uarabu wa baba yake na amekozea zaidi ubantu wa mama yake.
@ MUUNGUJA/MPORI-MMPORI
Jamani huyu hamjamjua kama ni mzaramu/mmakondee?
Sababu ya kujiita ‘muunguja’ilukuwa ni
kuweza kujipenyeza humu kupeleleza watu,kwa sababu angejiita KINJENGE-TIRE-NGOMBARE-MWIRU, Ingelikuwa ni rahisi kumjuwa.
hamumuoni ishara zake; kinacho andikwa kwao Tabora/Tanganyika basi mara hukiunga mkono, lakini kinacho andikwa na Wazanzibar basi huwa ni Boring! kwa hiyo si lazima aseme jamani mimi ni ‘MNYACHUSAAA’, Tayari tushamjua kama yeye ni MNDENGEREKO’
Jamani jina lisiku babaisheni wengi hao wakifika znz hubadilisha majina na dadazao hujifundisha kuvaa kanga na kuwacha rubega zao majumbani.
kwa hiyo mimi nashauri MR.frost huyu mtu anaweza akabadili jina lakini tuta muona kwa herufi zake za maandiko anaweza kuji sajili kwa kutumia jina jengine!!
#Anaweza kubadili E-mail address.
mimi nampa chalange’ atutumie picha yake tumuone kama hana ‘CHANJO ZA USO’ HAPO TUTAMJUA KAMA SI MTANGANYIKA.
Na mimi nakuahidi mnyachusa wewe nita ingiza picha yangu watu waseme ni nani Mzanzibari.
A-AA!! USIJE UKAATUANZIA BLA-BLA WEKA PICHA
TUMJUE NANI MJANJA ZAIDI,USIANZE MANA-AKE MANA-AKE- NNCHEJE-IPI NNCHEJE IPI??
KIMAKONDE SISI WENGINE HATUKIJUI.
‘MUNGU IBARIKI ZANZIBAR NA WATU WAKE’
ZNZIBAR KATI YA MWAKA 115 KABLA YA KRISTO NA 525 BAADA YA KRISTO
Katika mwanzo wa karne ya kwanza Baada ya Kristo, Zanzibar ilikuwa sehemu ya Ufalme wa Saba (115 BC-525 CE), pia inajulikana kama Sheba. Washeba walikuwa mabaharia, waliokua na ufalme mkubwa katika Yemen na kutumika upepo wa msimu Monsoon kusafiri mara kwa mara kwenda na kutoka Zanzibar. Wao walisafiri upande wa kusini kati ya Novemba-Februari, wakati wa upepo wa Mansuni wa kaskazi- mashariki, huku wakibeba shanga, vigae vya Kichina na nguo. Kati ya Machi na Septemba, walirudi kaskazini wakati wa Monsoon ielekeayo Magharibi, wakibeba chakula, nafaka, fito za mikoko kwa ajili ya mbao, viungo, dhahabu (kutoka Sofala), pembe na mipingo (Ebony). Waarabu hawa waliijua pwani ya Afrika Mashariki kama “Zinjibar” ambalo lilizaa jina hili zuri la Zanzibar.
Licha ya uhusiano wa kilugha uliopo kati ya Waswahili, Wasumeri, Wababeli na Waajemi pia Wasumeri walileta pembe Zanzibar. Katika makumbusho ya Beit al-Aman (Nyumba ya Amani), kuna pembe mbili kubwa za kale mali ya Mtawala wa kishirazi anayejulikanwa kama Mwinyi Mkuu (Sultani), maana mtu ambaye ana uwezo mkubwa wa uongozi. Kuna picha za pembe za Kibabeli ya kale nyingi katika mawe ya makaburi kama vile juu ya Kaburi la mwanamfalme Haroun lililopo Pemba. Haroun alikuwa mwana wa Mwinyi Mkuu Muhammad bin Abdul Rahman, maarufu kama Mkame Ndume wa Pemba. Hatuna uhakika sana juu ya asili(etimolojia) ya neno Pemba, lakini inafikiriwa ni neno Pembe, kutumiwa na watawala wa Sajjadiyya(Washirazi) Pemba na wawili katika mkoa wa kusini wa kisiwa cha Unguja kama ishara ya nguvu zao. Alama ya pembe kama nguvu, inatajwa katika Agano la Kale kuwa Sedekia ibn Khanaanah alitayarisha pembe mbili na kuashiria nguvu ya Wafalme wa Yuda na Israeli (1 Wafalme 22:11 na 2 Mambo ya Nyakati 18:10). Uwepo wa pembe Zanzibar inaonyesha kuwepo kwa Ustaarabu wa Kiajemi na Kishirazi (Perso-arabo civilization) na Serikali yao, neno la Kiswahili serikali, linalotokana na Kiajemi, hii inaonyesha kwamba ustaarabu wa Kiajemi na Kiarabu ulikuwepo katika visiwa vya Zanzibar kabla ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) lakini nchi kama Afrika ya Kati, Zaire, Bahr al-Ghazal (Kusini mwa Sudan) na Uganda hawana ujuzi wa kutumia pembe kwa uongozi kama ishara ya Zanzibar kabla ya Uislamu.
whatever man.mrfroasty AKA sultani wewe unaweza kunitoa kwenye mtandao wako anytime huna haja kuuliza watu.sikujua kama neno boring ni matusi makubwa kwako samahani.lakini nakukumbusha kitu kimoja usipenda mambo ya kutukuza watu hata kama wana PHD,mtufufu ni mungu peke yake .binadamu hoja zake inaweza kupingwa lakini mola hapingwi.
mzenji inaonekana wazi anaipinga kazi ya professa noor jee na yeye utamtoa kwenye mtandao kwasababu hakuunga mkono aliyoyasema huyo mtukufu wenu professa noor?mimi nahisi ungeandika hapo juu kwamba mtandau huu ni wa cuf members na watu wanao support usultani.
@rasmi huwezi kunilazimisha mimi niwe na mawazo kama yako .wewe unaamini znz ilipata uhuru 1963 na mimi naamini 1964.vile vile unaamini waarabu walifika kabla ya waafrika znz ,wakati mimi naamini kwamba waafrika tayari walikuwepo pale. sasa kama na wewe unaona tafauti yangu inakukera sana kiasi cha kwamba unafikiria ni matusi ya nguoni basi samahani mr sensitive
Mzenji, assalam alaykum!
Mbali ya Sheikh Ibrahim kuwa ni Prof. Mimi nadhani tungeangalia na uadilifu wake katika kazi zake. Kwa vile huu ndio uwanja wake, basi mimi humuamini sana kama ninavyo muamini Prof Ali Mazrui ambaye yupo karibu naye.
Sidhani mtu aweze kuingia kwenye search engine kwa masaa mawili matatu aweze kuja na jibu la uhakika. Lakini mtu akiniambia nimesoma kitabu fulani na fulani, na kutokana na matukio haya na yale, kutokana na majengo haya… basi hapa kuna kitu hiki.
Ndio nakumbuka wiki mbili zilizo pita. Siku ya Ijumaa, Imam kwenye Hutba yake, alikuwa anasema siku hizi kuna Sheikh Google! Huko mtu huingia akitoka huja na fatwa!!!
Prof Ibrahim amezungumzia Cameron. Kwanini? Kwasababu unapozungumza Kiswahili/swahili, basi hii lugha inahusishwa sana sana na kibantu na kiarabu. Hapo una vitu viwili. Kiarabu ambacho kinatokana na Waarabu na Kibantu kinatokana na Wabantu ambao kwao asili ni Cameron.
Hata kishona cha Zimbabwe nacho kinahusishwa na Kibantu, hata makabila makubwa yanahusishwa na Wabantu ama wa-congo.
Majina, majengo, na hata huo usafiri ni vitu muhimu vya kuanzia kutafuta asili ya watu. Ukisikia jina tu Ussi, ama Jecha, basi hapo moja kwa moja inakuambia huyo wa kashakazini. Jeee ukisikia mtu jina lake Mgindo, Kwao, Mwapachu,Mwakanjuki, kabla ya kuambiwa huyu ni mzanzibari, hisia zako zitakupa ni wa wapi huyo?
Tukisomeshwa histroy au hii waitayo his-stroy, tunaanzia kuja kwa Sayd Said kutaka kujenga hoja kuwa ahaa si kaja 1870 tu. Ukitajiwa Mwinyi mkuu utasema aahaa si wa juzi tu, huyo alikuwepo miaka 200 kabla kuja kwa Sayd Said… ni hivyo hivyo. Sasa tafuta asili ya huyo mbantu aliyekuwepo kabla, wapi unaweza kupata kumbukumbu yake aliyo wacha ndani ya Zanzibar? Lakini ukija ya mwinyi mkuu ahaa utapata mambo mengi. Kwani hiyo kazi imefanywa tena si mbali, ni miaka ya 1980′s na kuonekana mambo mengi tu na hata makaburi.
Mtu unaweza kusikia ahaa wametufanya watumwa. Ukimuuliza wewe unakumbuka babu yako yupo aliye wachwa huru kutoka utumwani, basi kwa Zanzibar, mpaka muda huu sijapata kumsikia mtu akiniambia mimi, babu yangu alikuwa mtumwa. Hii haina maana utumwa haukuwepo.
Lakini kama alivyo kusha kusema Prof Ibrahim, baada ya kuonesha Wa-Oman wameweza kuingia mpaka sehemu za colorado, US kwa kuonesha si ajabu kufika East Africa ambako ni karibu na wao. Akauliza nikikumbieni hivyo mutaniamini? Naam kuna wachahce hawato amini na wanaweza kutia mashaka. lakini watakapo soma zaidi na kuachana na his-story watakuja kutambua.
Muunguja!
Prof Ibrahim si mtukufu kama vile dhana za Wa Tanzania bara kwa Nyerere. Juzi moja nilikuwa nasoma commets za watu,baada ya kusikiliza hutuba ya Mwalimu. Basi mmoja anasema huyu ni Nabiii! ahaa!
Hata kama alikuwepo muafrika, kwanini tulazimishwe lazima iwe kutoka Tanganyika? Kwanini haiwezekani kuwa katoka Kenya? Baadhi ya Wakomoro/Wangazija, wengine wanajiita Wamakuwa na wanaweza kukuambia huko Msumbiji tuna mambabu zetu.
Sasa wacha aje mtu Tanganyika aseme, kabla ya Mwinyi mkuuu, alikuwepo chief Sengoro. Tutafurahi, kwani tutakuwa tunajifunza zaidi juu ya histroy yetu.
Sheikh Kassim fatwa zinazopatikana google hazina mushkeli kama zitaambatana na hadith zinazoaminika au aya za Qur-an. Wala hicho si kigezo kwamba imam alishutumu hilo, katika Zanzibar ya leo masheikh wengi wapo shallow hasa kwenye masuala ya fiqh na sharia kwa ujumla.
Mtu akishahifadhi juzuu zake tano na akaweza kusimama akasema maneno mawili ya kiarabu aliokariri anasubiri afike amma aabad anze kushtumu wenziwe. Kuna elimu kibao kwenye mtandao siku hizi kuliko hivyo vitabu viwili vitatu walivyosoma masheikh wetu. Masheikh wanalaani google wakati jamii zetu mambo ya bidaa ndio yanapewa kipao mbele ya kiislam hasa yanapuuzwa.
Kuhusu suala la historia ya Zanzibar mie bado naamini kwamba waafrika walikuwepo mwanzo kuliko hao waarabu, inawezekana hao waafrika hawakuwa hao wabantu kutoka cameroon ila bado walikuwa ni waafrika. Utumwa si lazima kwamba hao waafrika walikuwa wanamilikiwa na waarabu ila ndio waliowafanyia kazi kwenye mashaba yao kwa ujira mdogo, nadhan hiyo ndio inaitwa feudalism. We sheikh Kassim unawajua waarabu wangapi Zanzibar waliowapa majina watoto wao mtumwa? Mie babu yangu hakuwa mtumwa kwamba alikuwa akimilikiwa na muarabu ila alikuwa akiwalimia waarabu mashamba yao kwa ujira mdogo huo nao ni utumwa.
Kama nilivyosema awali mie sina tatizo na mtu mwenye asili ya kiarabu manake mie binafsi asili yangu siijui vizuri, ila kusema waarabu walitangulia kusettlee visiwani ni kuwapendelea na kuturudisha kule tusikokutaka kwamba waswahili walifanya udhalimu 1964 na Zanzibar sio yao kwa vile ni wahamiaji wa karibuni.
Nawasilisha.
Mimi nadhani hapa tuelekezane kwa hoja zenye ushahidi na si tu kwa ushabiki au kulingana na asili ya mtu au imani ya kisiasa. Wanaosema waarabu walikuwpo mwanzo walete ushahidi wao tuuone na wale wanaosema wabantu walikuwepo mwanzo pia walete ushahidi tuuone. Ila kulengeana maneno na tuhuma hapa haitosaidia kupata ufumbuzi wa jambo hili ila ni kupoteza muda. Wazanzibari wote awe mbantu awe mwarabu aw mshirazi atabakia kuwa Mzanzibari ilimradi kizazi chake kinatoka hapo. Wengi wetu tuna mchanganyiko wa damu za kiafrika na kiarabu hapa Zanzibari. Hivyo hatuwezi kumbagua mwarabu wala muafrika. Historia ni jambo linalohitaji mtu kufanya utafiti na kusoma vyanzo tofauti na sio tu kuamini mwandishi mmoja au kitabu kimoja kwani wanahistoria wengi huvutia upande wao na kujaribu kuandika historia kwa mujibu wa itikadi yake au asili yake na ndo mana historia hupotoshwa. Hivyo tusibaki kuwa washabiki bali tusome vyanzo tofauti na tutafiti na sio tu kuyachukua moja kwa moja yanayoandikwa na mtu fulani.
Ndugu Muunguja,
Nafikiri niweke sawa baadhi ya mambo kwako, mimi ni mdau mmoja kati ya wadau wa huu mtandao.Usidhani kila maada ninayoichapisha hapa nimeisoma na kuissupport.Unaposema huu mtandao tungeliandika kuwa ni mtandao wa CUF, naona kama bora ungelitizama FAQ.Hilo suali tumeshalijibu, na wala halitorudiwa kujibiwa tena madhali tayari limeshaorodheshwa hapo.
Mimi nikiwa kama mmoja wa kamati ya nidhamu ya huu mtandao, sijaridhishwa na comment kama “boring”.Maana licha ya muda wa Prof.Ibrahim kuandika hiyo makala, pia na mimi imenicost muda kuileta hapa na kuingiza katika system yetu hapa.Wala sidhani kama kusema “boring” ndio umetoa hoja yoyote au kutoa elimu yoyote kwa jamii.Ninachokiona ni kejeli tuu.Ndio nikasema kama huna mchango wowote wa maada, basi usiingie kati kati.Personally mimi sijalisoma chapisho hili na wala sisomi machapisho yote uyaonayo kwenye mtandao huu.Na ndio maana nimenyamaza kimya sijatoa hoja yoyote kuhusiana na historia.Nilichokifanya nilimuomba Prof.Ibrahim atupe rukhsa ya kulichapisha hapa kwa ajili ya wasomaji wengine.
Si kweli kama kila chapisho litawapendezesha watu wote, na wala sijasema kama napendelea kufukuza watu na wala hilo sio lengo.Ni wazi kuwa lengo kuu la MZALENDO.NET ni kupata watembeleaji wengi na kufikisha habari kwa watu wengi zaidi.Nilichokifanya hapo juu nimekufahamisha taratibu.Kuna tofauti kubwa baina ya kutoa hoja na kuonesha kama hukubaliani na hoja iliyopo mezani.Wewe unachokifanya ni kuonesha dharau kwa mchapishaji au mtunzi wa habari hiyo.Hili halikubaliki.
Sasa niliposema kuwa Administrator’s inbox ikipokea malalamiko 3 kuhusiana na mtumiaji mmoja itatulazimu kuchukua hatua.Huo ndio utaratibu wetu na wala lengo sio kuwaomba watembeleaji waandike hayo maombi.Hapo ninachokifanya ni kuelezea utaratibu, kama kutakuwa hakuna maombi uongozi wa mtandao unajaalia kuwa hakuna tatizo na watu wanajadili kistaarabu.
Sasa usijaribu kusimamisha hoja dhidi yangu, maana hapa mimi naplay roles nyingi.Nilichofanya hapo nimekupa hadhari tuu, na kufahamisha kuwa chunga jinsi unavyochangia.Hii haimaanishi kuwa unaambiwa ubadilishe mawazo, bali presentation ya hoja zako hairidhishi.Kwa tarehe ya leo, tayari niliona chapisho jengine ambalo nimechapisha mimi na wewe unaleta kasumba za kuwa mimi sultan nitamfungia huyo mchapishaji.Wakati chapisho hilo ni mimi ndio nilielishapisha….sasa hii ndio nini, umekusudia kutia choko-choko au kugonganisha vichwa watu na kuonana wabaya.
Nafikiria mimi sio wa kwanza kuona kama maoni yako ya mwanzo hayakuwa kwenye heshima.
Natumai utakuwa umenifahamu.
namshukuru muandishi wa makala hii kwa kutupa elimu na sisi
muandishi kwa upana kabisa kasema hivi
“Iwapo tunazungumzia kukhusu wenyeji wa Pwani ya Afrika Mashariki basi itakuwa ni Waarabu na jamaa zao wa karibu kama Wahabashi na Wasomali na si Wabantu. Changa moto hii ipelekeni kwa “mabingwa” wa taarikh za alifu layla u-layla wa Tanganyika walioko Chuo Kikuu, Dar-es Salaam waipinge kwa ushahidi na hoja na mantiki kama wanayo.”
sasa sijui kajiamini kiasi gani huyu mtu bali naomba kama kuna mtu anaweza kutusaidia kutupaia watu wa chuo kikuu tutafurahi sana kwa sababu wengi tunataka tumpinge lakini hatujui tumpinge vipi
Sitaki niseme mengi, lakini hapa nitawapa vitabu ambavyo havikutungwa na Mzanzibar, vinavyoeleza historia ya Zanzibar. Nawaomba vitafuteni mutajifunza mengi kati ya hayo munayopingana.
1. The Land of Zinj (London 1913) – C. H. Stigand.
2. Zanzibar (London 1931) – W. H. Ingrams.
3. Zanzibar, an account of its People, Indeusties and History (Zanzibar 1924).
4. Zanzibar (London 1920) – F. B. Pearce
Nimejaribu kuviongeza kwenye chapisho hivo vitabu.Shukurani kwa reference hizo
Mzenji, assalam alaykum.
Nilipo gusia kuhusu Google, sina maana kila kitu kwenye Database ya Google ni wrong. Kwenye Google, Yahoo, na search nyengine zote, zinajitahidi kuweka mambo mengi tu. Lakini namo humu kunavamiwa na watu.
Imam aliyezungumzia hilo si wa aya mbili tatu, ni mtu aliyekwenda Saudi kupinda goti, akapita na Cairo kwenda kuchukuwa lugha kabla ya kwenda Saudia. Alichosema yeye, fadhila ya kusoma ni kubwa. Anyway hiyo si issue yetu.
Kuhusu wakaazi wa mwanzo, hilo silo alilosema Prof Ibrahim. Anachojaribu kusema, kuwa Waaabu tokea karne fulani tayari walikusha fika Zanzibar na fukwe nyengine za Afrika Mashariki. Ushahidi huo upo, sasa wale Wabantu nao kama wanao waseme tu, kwamba tulikuwepo tokea karne fulani na ushahidi wetu ni huu. Ukisema mreno alikuwepo Pemba, basi utapata ushahidi wa mambo waliyo yawacha kama huo mchezo wa Ng’ombe, sijuwi kurumbizi…
Sheikh Ashakh, ahsante kwa ordha hii ya vitabu:
1. The Land of Zinj (London 1913) – C. H. Stigand.
2. Zanzibar (London 1931) – W. H. Ingrams.
3. Zanzibar, an account of its People, Indeusties and History (Zanzibar 1924).
4. Zanzibar (London 1920) – F. B. Pearce
Wewe ni mfano mzuri. hivi ndio tunavyotakiwa. Tusome na kujifunza mambo ili tuweze kuchambuwa mambo kwa undani. Nadharia tu naona haitoshi. Kwasababu sisi ndio walengwa, basi mtu akiandika inakuwa ni rahisi kufafanuwa mambo.
Huu ulimwengu mpya, kesho kutwa na sisi tukija kuwa na uwezo, basi tutakuwa na ushahidi mpaka wa DNA, kama wafanyavyo wenzetu wa Ulaya na Umarekani. Leo hii watu wa Genealogisty wamekuwa wanatumia Genetic kwenye uchambuzi wao wa kuweza kujuwa nani alifika Ulaya mwanzo na sehemu nyengine.
Haya mambo yana raha zake, manaake tuna Walibiya, Masri, kuna Wa-Algeria, Kuna Watunusia nk nk haya vipi na huku?