Habari

JAJI FRANCIS MUTUNGI NDIYE CHANZO CHA VURUGU ZINAZOENDELEA NDANI YA CUF

TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI

JAJI FRANCIS MUTUNGI NDIYE CHANZO CHA VURUGU ZINAZOENDELEA NDANI YA CUF HANA USAFI WA MAADILI (MORAL AUTHORITY AND MORAL EXCELLENCE) ASIWADANGANYE WATANZANIA:

Tarehe 24/4/2017 Msajili wa Vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi ametoa tamko la kulaani vurugu zilizofanywa na Walinzi wa Lipumba lenye kichwa cha habari “MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KULAANI VURUGU ZILIZOTOKEA KATIKA MKUTANO WA WANAOSEMEKANA KUWA NI VIONGOZI WA CUF NA WAANDISHI WA HABARI” katika tamko lake hilo anadai eti kusikitishwa na kilichojitokeza na kutaka Wanachama wazingatie Sheria za Nchi, kulinda tunu za Taifa Amani na Utulivu na kwamba wasubiri amewataka wadau wana-CUF kuwa na subira na uvumilivu kwa sababu shauri linaendelea Mahakamani, amedai kuwa uvunjifu wa sheria kwa kufanya vurugu kunaleta sura mbaya mbele ya Jamii. Kwa bahati mbaya Jaji Francis Mutungi ndiye chanzo cha vurugu zinazoendelea ndani ya CUF, hana usafi wa Maadili (Moral Authority and Moral Excellence) wa kujitokeza hadharani kulaani kitendo ambacho kimeasisiwa na mikono yake. Historia inatuonyesha kuwa machafuko makubwa yaliyotokea sehemu mbalimbali Duniani yamesababishwa na mfano wa maamuzi ya hovyo kama haya ya Jaji Mutungi. Jaji Mutungi akiwa ni sehemu ya Washtakiwa/walalamikiwa katika mashauri kadhaa yanayoendelea Mahakamani ameendelea kutenda vitendo vya hovyo na hata kudharau maamuzi ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam katika Shauri la Madai Na.6 la mwaka 2003 baina ya Emmanuel Nyenyemela and Another Versus Registrar of Political Parties and Others lililokuwepo mbele ya Mheshimiwa Jaji Mihayo. Mahakama ilimuonya Msajili na Ofisi yake kwamba haina mamlaka ya kuingilia utendaji wa shughuli za ndani ya Vyama kwa kubariki au kupinga maamuzi ya vikao vya Chama husika. ilieleza kama ifuatavyo kwenye ukurasa wa pili wa hukumu: “…The reliefs sought in this matter do not fall under section 20 of the Political Parties Act. They cannot therefore be sought by way of judicial review. In the same vein, I do not see anywhere in the Political Parties Act where the Registrar has power to bless or condemn meetings of political parties or decisions that they make”.

Tunapenda Msajili Mutungi atambue kuwa uamuzi na muongozo huo wa Mahakama Kuu ya Tanzania haukuwahi kutenguliwa na Mahakama yoyote ile na hivyo tunaamini kuwa Mutungi akiwa ni sehemu ya Majaji ambaye hajastaafu (Sitting Judge) wakati wowote anaweza kufanya kazi ndani ya Mahakama Kuu yeyote Tanzania akipangiwa kufanya hivyo, hatukutaraji ajiondoe ufahamu kiasi hiki katika uweledi wa taaluma ya sheria na kuhuujumu muhimili ambao yeye ni sehemu. Tukio la Tarehe 22 Aprili, 2017 katika Hoteli ya Vina, Mabibo Dar es Salaam, zilitokea vurugu zilizosababishwa na walinzi wa Lipumba, huu ni muendelezo wa matukio kadhaa yanayotokana na maamuzi ya Jaji Mutungi aliyoyatoa Tarehe 23/9/2016 kinyume na matakwa ya sheria. Ifuatayo ni orodha ya matukio na dosari zilizomo katika Tamko lake ambazo Jaji Mutungi ameyafanya kwa makusudi ili kuchochea Vurugu ndani ya CUF kwa maslahi yake binafsi na au waliomtuma kufanya hivyo;

1. Jaji Mutungi amekuwa mfuasi wa Lipumba mkereketwa kuliko wana-CUF wenyewe. Wakati timu ya Lipumba inakiri kuwa Mhe. Juma Mkumbi ni Mwenyekiti Halali wa Wilaya ya Kinondoni na ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Mutungi hajui na hataki kukubali hivyo, anaandika katika Tamko lake eti “….VURUGU ZILIZOTOKEA KATIKA MKUTANO WA WANAOSEMEKANA KUWA NI VIONGOZI WA CUF…” hii inajidhihirisha ni kiasi gani alivyo na chuki zilizopitiliza na kila asiyekubaliana nae.
2. Jaji Mutungi amemuandikia Mkuu wa Jeshi La Polisi –IGP ampe ushirikiano wa kila hali Lipumba kila inapohitajika na asikilizwe kwa kila anacholielekeza Jeshi hilo. Ushahidi wa hili kwa yanayoendelea hauhitaji tochi.
3. Jaji Mutungi ameziandikia Benki mbalimbali nchini ikiwemo Benki ya NMB Tawi la Ilala imfungulie akaunti yenye jina la CUF itakayosimamiwa na Lipumba ili aweze kumuingizia fedha za Ruzuku ya Chama, ilipobainika njama hiyo na kuzuiliwa, sote tunajua nini kilijitokeza January 5, 2017 kwa kiasi cha Tshs 369 milioni kuingizwa katika akaunti ya wilaya ya Temeke tawi la Benki ya NMB na baadae fedha zote kuingizwa kwa akaunti ya mtu binafsi Masoud Muhina, kutolewa zote siku moja na kwa kutumia mifuko ya Rambo na mabegi zikapelekwa nyumbani kwa Lipumba. Hili linafanyika hali akijua kuwa Muwajibikaji Mkuu wa masuala ya fedha ni Katibu Mkuu ambaye yeye anamtambua na kwamba tayari alishatoa maagizo mawili Moja kukitaka Chama kipeleke ofisini kwake Akaunti maalumu itakayopokea fedha za Ruzuku pekee bila kuchanganywa na fedha zingine za Chama. pili, amemuandikia Katibu Mkuu kumjulisha kuwa hatoweza kutoa fedha za Ruzuku ya Chama kwa sababu CUF kina mgogoro wa uongozi kwa madhumuni ya kuzilinda fedha za umma ni bora kusitisha mpaka hapo Mgogoro utakapoisha. Jaji Mutungi amempa Lipumba fedha na yeye akapatiwa mgao wake kamili huku akijua kuwa shauri lipo Mahakamani na anakiri kuwa mgogoro upo.
4. Jaji Mutungi ndiye aliyepanga na Lipumba baada ya kuonekana mambo yao yanakwama na kesi zimewakalia vibaya kumtaka Lipumba aunde Baraza Kuu FAKE na kisha kuteua Bodi ya Wadhamini FAKE na vyombo vyote hivyo FAKE Mutungi amevitambua na kuzijulisha mamlaka mbalimbali eti kuwa vyombo hivyo ndivyo halali. Ameiandikia na kuishinika RITA iitambue bodi ya Lipumba ili anusuruke katika kesi zilizopo mahakamani waendelee na wizi wa fedha za umma, ameiandikia Ofisi ya Bunge wakati wa uchaguzi wa EALA kumuhalalisha Mgombea wa Lipumba ambaye ameshafukuzwa uanachama na tawi lake na eti kumtambua rasmi Magdalena Sakaya kuwa KAIMU KATIBU MKUU WA CUF hali akijua kuwa KATIBU MKUU Maalim Seif Sharif Hamad yupo Ofisi Makao Makuu ya Chama na anatekeleza majukumu yake na kwamba kesi zipo Mahakamani zinaendelea. Huyu ndio mtu mwenye hadhi ya Ujaji anayeitwa Francis Mutungi.
5. Jaji Mutungi anajua na amejikoroga mwenyewe. Anatambua kuwa kwa mujibu wa sheria yeye si Mlezi wa vyama vya siasa. Na katika andiko lake amekili hivyo kwamba Ulezi wake kwa vyama ni ufahamu wa Jamii lakini si matakwa na ulazimu wa kisheria. Sio kweli kuwa eti ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa na hata Jeshi la Polisi lipo kushughulikia malalamiko yoyote yanayohusu uendeshaji na shughuli za chama chochote cha siasa. Hapana.
6. Jaji Mutungi Wahalifu ni washtakiwa wenzake katika mashauri yaliyopo mahakamani na wenyewe wamekiri kuhusika na uvamizi huo. Kama kweli una chembe ya uadilifu katika nafsi yako basi unapaswa kumuonya Lipumba na genge lake na wala si kufanya propaganda na upotoshaji wa kile kilichojitokeza.
7. Jaji Mutungi ndiye chanzo cha yanayoendelea ndani ya CUF kwa kuasisi kutengenezwa makundi yanayoitwa Mazombi(wavicha sura-Ninja), Mungiki, Wavamizi, Wabeba bastola na Mapanga walioshiriki katika matukio ya utekaji wa wanachama na viongozi wa CUF, kupiga watu visu mahakamani…n.k.
8. Jaji Mutungi ndiye aliyesababisha na mlezi wa vitendo vya kihalifu vinavyoendelea ikiwemo uvamizi wa Afisi Kuu ya Chama Buguruni Dar es Salaam, Tarehe 24/9/2016, uvamizi na kuvunja ofisi za Chama katika wilaya mbalimbali hapa nchini kunakofanywa na Lipumba na genge lake, uzuiwaji wa kufanyika kwa vikao halali vya Chama kwa Viongozi wa CUF Taifa na Wabunge wa CUF maeneo mbalimbali kwa lengo la kumlinda Lipumba na kusudio la kutaka kukigawa Chama.

Mwisho:

The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) hakikubaliani na kilaani tamko la kinafiki lililotolewa na Jaji Francis Mutungi na tunamtaka avunje ushirikiano hasi wa kukihujumu Chama alioujenga kati yake Lipumba na Jeshi la Polisi. Ni mtazamo wa CUF kuwa Francis Mutungi amepoteza hadhi ya kuwa Jaji na anaivunjia heshima nafasi ya UJAJI, Mutungi amepoteza sifa ya uadilifu. Historia itamkumbuka milele kwa uovu huu aliouasisi na kuusimamia. CUF haitakubaliana na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kwa Chochote kile ambacho kipo kinyume na matakwa ya sheria na kwa msingi huo HAITOTISHIKA NA JAMBO LOLOTE LILE ANALODHANI MUTUNGI ANAWEZA KULICHUKUA DHIDI YA CUF. Kama ‘hakusita kuchukua hatua anazodhani kuwa ni stahiki kwa mujibu wa sheria za wizi wa fedha za umma Tshs 369’ tunamtaka aendelee kuchukua hatua anazoona yeye zinastahiki dhidi ya CUF. Jaji Mutungi hatokwepa kuwa mshtakiwa namba moja katika Mahakama za Kimataifa pale yatakapotokea machafuko makubwa ya kisiasa nchini.

CUF ni Taasisi Imara ya kisiasa nchini yenye Viongozi Makini, itaendelea kujenga mahusiano na ushirikiano mwema na wadau wote wenye dhamira ya dhati ya kustawisha na kuchochea uwepo wa misingi ya Demokrasia ya kweli nchini, Utawala wa Sheria, kulinda na kutetea Haki za Binadamu, Amani na Kuwaunganisha Watanzania wote.

HAKI SAWA KWA WOTE

……………………………………………………..
SALIM BIMANI
MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA
MAWASILIANO: 0777 414 112/ 0752 325 227

Imetolewa leo Tarehe 26/4/2017

Share: