Habari

Kifo cha Mwanafunzi wa Skuli ya Laurent International hakihusiani na Kipigo – Polisi

Jeshi la Polisi mkoa wa Kusini Pemba limekanusha kuhusu tukio la kifo cha mwanafuzni wa skuli ya Laurent International kuwa halihusiani na kupigwa na mwalimu.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Kusini Pemba Mh, Sheikhan Mohd Sheikhan amesema kifo cha Saleh Abdallah Massoud aliyekuwa mwanafunzi wa skuli hiyo iliyopo Ole Kianga Mkoa wa Kusini Pemba hakikutokana na kupigwa na mwalimu kama inavyodaiwa na walio wengi bali kimechangiwa na kuumwa na Figo, Ini pamoja na uvimbe katika shingo yake.

Akizungumza na wandishi wa habari jana huko ofisini kwake Madungu Chakechake Pemba amesema mnamo tarehe 30/05/2017 majira ya saa 5: 00 asubuhi walipokea taarifa ya kifo cha mwanafunzi huyo na ndipo walipochukua hatua za haraka kufika skulini hapo kuwahoji walimu pamoja na wanafunzi wa skuli hiyo na katika taarifa za awali uchunguzi ulibaini kwamba mwanafunzi huyo alipata adhabu baada ya kuharibu midoli ya kufundishia wanafunzi wa chekechea skulini hapo.

Shekhan amesema, mtoto huyo kabla ya hapo awali alipata kuanguka chooni na kuumia sehemu ya bega la mkono wa kulia na alianza kupatiwa matibabu ya awalii na daktari wa skuli hata hivyo hali haikua nzuri na kulazimika kupelekwa hospitali ya Chakechake na Mwanamashungi kwa matibabu zaidi.

Amefahamisha kuwa 25.05.2017 baba wa mtoto huyo alifika skulini hapo kwa ajili ya kumchukua na kwenda nae nyumbani kwa lengo la kumpeleka hospitali ya Wete kwa matibabu zaidi aliruhusiwa kurudi nae nyumbani na ilipofika 29/05/2017 alirejeshwa tena hospitali ya Wete na kulazwa na hatimae majira ya saa 8:00 alifariki dunia.

Amesema kutokana na uchunguzi wa daktari aliyemtibu katika hospitali ya Wete aligundua kuvimba kwa shavu la kulia , uvimbe usio na maumivu mbeleni mwa shingo, uvimbe kwenye mguu wa kulia, umanjano wa macho na hakua na jeraha lolote wala sehemu yeyote iliyotoka damu wala mkwaruzo au alama zisizo za kawaida.

Pia vipimo vingine vilionesha kuwa alikuwa na upungufu wa damu, kuumwa na Figo pamoja na Ini na sio kujeruhiwa na kupelekea hali yake kuwa mbaya na hatimae kufariki dunia.

Aidha amesema kwa sasa wanawashikilia watu saba na uchunguzi ukikamilika watapandishwa mahakamani kwa kujibu shtaka la uzalilishaji pomoja na uzembe na sio shtaka la mauaji.

Pemba News Midea

Share:

3 comments

 1. Mrfroasty (Ufundi) 17 Juni, 2017 at 08:37

  Tunaomba serekali iondoshe mambo ya physical abuse, kumpiga mwanafunzi hakusaidii kumfanya afahamu zaidi wala hakuleti picha nzuri.Kama toto halitaki kusoma lipatiwe adhabu za aina nyengine zikiwamo kufungiwa kwenda skuli kwa muda kadhaa na adhabu za aina hii sio kupigana.

 2. rasmi 17 Juni, 2017 at 15:35

  Nakubaliana nawe mrfroasty, nikikumbuka adhabu za bakora skuli ya utaani enzi za D.O, Killer, Mpangile na waliobaki sioni bakora zile kama zilinisaidia lolote katika kuengeza elimu na nidhamu, labda nidhamu ya woga.

  Ilikua nikienda skuli navaa kaptura nilioshonea kigozi kupunguza kasi ya maumivu ya bakora, kosa dogo kama kukosa namba ya mstari si adhabu hiyo, ikiwemo kulima makoongo jioni.
  Sikuona katika adhabu zile kuzidi kufahamu masomo zaidi ya kumaliza hapo sijui hata kuzungumza kiengereza.

  Aloo bakora hazijengi zabomoa ikiwemo kumkosesha mwanafuzi confidence ya kusimama mbele ya hadhira.

  Waliosoma wakati huo watakumbuka debate siku za Ijumaa ambapo baada ya kukaa munapasiana mpira, unaemsimamia anaambiwa asimame aende mbele akajibu kinachowasilishwa, ilikua mbinde kuukimbia mpira usikuangukie wee! Na D.O ukiupeleka mbio mpira anapiga kengele urudi na adhabu juu ya bakora.

  Bakora hazijengi…

 3. Abdul Zakinthos 17 Juni, 2017 at 19:55

  Mini nafanya kazi CAMHS (Child and Adolescent mental health Service) katika kitengo chetu kimeundwa na Drs,Phsychologist,Support workers,mental health nurse,autisim coordinator na clinicians,
  Tunahusika na kumtathmini mtoto maendeleo yake,kufanya observation sehemu mbali mbali ikiwemo skuli,sehemu za kucheza na nyumbani na pia Hospitali.

  nilipanga kuanzisha huu mradi hapa makwetu kwa njia za kujitolea tu,tuanze kutembelea maskuli yetu,ili tuweze kuwasaidia wanafunzi na kuwatoa hofu,Nikashindwa kwa sababu ili mradi huu uweze kutusaidia,hizi adhabu za bakora kwanza ziondolewe, kisha tudeal na matatizo mengine,

  watoto wetu wanashindwa kufahamu kutokana na hofu ua mikwaju,maradhi ,umasikini kushindwa kupata hata mlo mmoja kwa siku na kushindwa hata pesaa ya skulli.
  Inasikitisha sana kuona bakora zinaendelea,Polisi wamesema ameumwa na shingo imesababisha sasa huoni kubeba godoro tayari peke yake kusababisha kuumwa na shingo au hata kuongeza maumivu?
  nawashauri wazazi watafute haki yao mahakamani wahusika wachukulliwe hatua kali na pia walipwe fidia japo kuwa nafsi hailipiki

Leave a reply