Mabadiliko ya 10 ya Katiba yatiwa Saini

Written by  //  05/09/2010  //  Kitaifa  //  6 Comments

Na Salma Said,

SHERIA namba 9 ya mwaka 2010 ya marekebisho ya 10 ya katiba ya Zanzibar ya 1984 ambayo inaitambua Zanzibar kuwa ni nchi na muundo mpya wa serikali ya umoja wa kitaifa imetiwa saini rasmi na Rais Amani Abeid Karume, Agosti 13, 2010 mwaka huu.

Sheria hiyo imekuja kufuatia kura ya maoni iliyopigwa Julai 31 mwaka huu na asilimia 66.4 ya waliopiga kura kukubali mfumo mpya wa muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar ufanyike baada ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Octoba 31 mwaka huu.

“Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar” imesema sheria hiyo.

Kabla ya kifungu hiki cha kwanza cha katiba ya kwanza kufutwa na kuandikwa upya, Zanzibar ilikuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Marekebisho ya 10 ambayo yamefunua mjadala mkali miongoni mwa wataalamu wa sheria nchini pia imempa mamlaka rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengine kwa kufuata utaratibu uliwekwa na sheria iliyotungwa na baraza la wawakilishi bila ya kuzingatia sheria nyengine.

Vile vile kabla ya marekebisho haya ya 10 rais wa Zanzibar alipaswa kushauriana na rais wa Jamhuri ya Muungano kabla ya kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengine kufuata utaratibu uliowekwa.

Nakala ya sheria mpya hiyo ambayo gazeti hili inayo nakala yake inaeleza kwamba katika kifungu cha 39 (1) (2) kutakuwa na rais wa Zanzibar na makamu wawili wa rais ambayo watajulikana kama makamu wa kwanza wa rais na makamu wa pili wa rais ambao wanatakiwa kuteuliwa kushika nyadhifa hizo ndani ya siku saba mara baada ya rais kushika madaraka.

Kwa mujibu wa sheria hiyo makamu wa kwanza wa rais atateuliwa na rais baada ya kushauriana na chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa rais.

Hata hivyo endapo ndani ya siku saba baada ya rais kushika madaraka, chama kinachostahiki kutoa makamu wa kwanza wa rais kitashindwa kuwasilisha kwa rais jina la uteuzi wa makamu wa kwanza wa rais basi rais atawacha wazi nafasi hiyo na kuteuwa makamu wa pili wa rais.

Makamu wa kwanza wa rais, kwa mujibu wa sheria, atakuwa ni mshauri mkuu wa rais na kutekeleza kazi zake na atafanya kazi zote atakazopangiwa na rais.

Nafasi ya makamu wa pili wa rais itashikiliwa na mtu ambaye atatoka chama kilichotoka rais na kabla ya mabadiliko hayo ilikuwa, nafasi hiyo ikishikiliwa na waziri kiongozi, cheo ambacho kimefutwa kufuatia mabadaliko ya 10 ya katiba ya Zanzibar.

Chini ya mabadiliko mapya makamu wa pili wa rais atateuliwa na rais kutoka miongoni mwa wajumbe wa baraza la wawakilishi na atakuwa mshauri mkuu wa rais katika kutekeleza kazi zake na pia atakuwa kiongozi wa shughuli za serikali katika baraza la wawakilishi.

Sheria imesema makamu wa kwanza wa rais na makamu wa pili wa rais wote watakapokuwa madarakani watawajibika kwa rais na rais atakuwa na mamlaka ya kufuta uteuzi wao.

Aidha katika mabadiliko hayo wakuu wa mikoa Zanzibar hawatakuwa tena wajumbe wa baraza la wawakilishi ambao walikuwa wakiingia kwa nyadhifa zao katika baraza.

Sheria hii haikusema kwamba nafasi za wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya zitateuliwa kwa kuzingatia wingi wa kura zilizopata chama na badala yake rais atateuwa kama anavyoteuwa nyadhifa nyengine.

Kwa mujibu wa sheria hii mabadiliko ya katiba ya Zanzibar ya kufuta Zanzibar kuwa ni nchi hayataweza kufanywa na baraza la wawakiishi mpaka kwanza mabadiliko hayo yakubaliwe na wananchi kwa kupigwa kura ya maoni.

Kitendo cha Zanzibar kupitisha sheria mpya ya marekebisho ya 10 ya katiba kilileta mtafaruku mkubwa na kusababisha wanasheria wa pande zote mbili ya Jamhuri ya Muungano kurushiana makombora kwa madai kwamba Zanzibar imevunja katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Wenye kutamka kwamba katiba imevunja wanadai kwamba Zanzibar haitakiwi kuwa nchi kwa kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndio inayokubalika kuwa ni nchi inayowakilisha Zanzibar na iliyokuwa Tanganyika ambayo sasa inaitwa Tanzania bara.

Aidha wanasheria walidai kumpa nguvu rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar kimikoa. kiwilaya na maeneo mengine kimekiuka katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu mamlaka hayo ni ya rais wa Jamhuri ya Muungano pekee.

Na ikiwa rais wa Zanzibar anataka kuigawa Zanzibar kimikoa au kiwilaya basi kwanza alitakiwa ashauriane na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya kufanya maamuzi.

Kufuatia malumbano hayo ya kisheria waziri wa sheria na katiba wa Tanzania, Matthias Chikawe alilazimika kutoa ufafanuzi wa na kusema Zanzibar haikuvunja katiba kama inavyodaiwa kwa sababu mabadiliko hayo hayakuathiri dola ya Tanzania (sovereign).

Chikawe alisema mabadiliko yaliofanywa na Zanzibar yalikuwa ni kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli zake tu na si vyenginevyo kama inavyodaiwa na wanataaluma wa sheria.

6 Comments on "Mabadiliko ya 10 ya Katiba yatiwa Saini"

  1. Elbattawi. 05/09/2010 kwa 3:29 mu ·

    Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, kutufikisha katika hatua hii ya awali ya kuirudisha Zanzibar katika hadhi yake ya asili.

    Lakini pili sina budi kuwapongeza sana wale wote, waliyokaa na kufikiria na kuanza kuchukuwa hatua za uhakika kabisa za kuirejeshea Zanzibar hadhi yake ya nchi, kama ilivyokuwa kabla ya Muungano wa Aprli 26,1964.

    Na tatu ambalo hili halitaweza kusahaulika ni busara na imani ya dhati kwa Wazanzibari aliyonayo Dk. Amani Karume, kuweza kujiamini na akiwa kiongozi wa juu kuwarejeshea heshima wa utaifa wao Wazanzibari kuwa Zanzibar ni nchi na hapana mjadala.

    Tunakupongeza sana na hasa baada ya kusikia kuwa umesaini sheria ya marekebisho ya kumi ya Katiba ya Zanzibar.

    Historia itachukuwa mkondo wake na kukuheshimu kwa ulichokifanya kwa nchi yako ambayo tayari ilikuwa ndani ya mdomo wa chewa. Mwenyezi Mungu akubariki na atubariki Wazanzibari wote.

    Wakati huo huo kwa maoni yangu, tunapaswa kuwachukulia hadhari kubwa sana watu kama Mizengo Pinda, kwa kudhani kuwa Tanzania ni nchi lakini Zanzibar si nchi. Inasikitisha kuwa Zanzibar ilikuwapo kabla ya Tanzania na wala haijaondoka au kufutika hata dakika moja na wala haitafutika katika ramani ya ulimwengu milele na milele.

    Ila nawashauri na mapema viongozi watakao mrithi Rais wa Zanzibar,anayemaliza muda wake baada ya uchaguzi mkuu hapo oktoba 31, kuwa wasibweteke na hatua hii iliyofikiwa sasa, bali waendelee kurejesha nafasi na haki zote za Zanzibar au ikiwezekana ipo haja ya kuuangalia umpya mfumo mzima wa Muungano.

    Mchakato wa kuutazama Muungano uanze ndani ya siku mia moja (100) baada ya kuapishwa kwa Rais wa Saba wa Zanzibar. Hapa namaanisha kusiwe kulala kwani miaka tuliyokaa katika Muungano inatosha kuwa ni kipimo cha kujuwa hasara na faida.

    Mwisho nawapongeza sana Dk. Amani Karume na Maalim Seif Sharif na wajumbe waote wa Baraza la wawakilishi kwa kazi waliyoifanya kwa muda mfupi sana na pia pongezi maalum ziwaendee waliyopiga kura ya maoni na kuweka asilimia 66.4 pamoja na Wazanzibari wote waliyochangia kwa namna moja au nyengine katika suala la Zanzibari.

  2. WANYUMBANI ZANZIBAR 05/09/2010 kwa 8:57 mu ·

    Hongera za pekee kwa viongozi wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu Zanzibar kwa kutufikisha hapa leo tulipo. Hongera pia Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa Zanzibar kwa kuisaini sheria inayoitambua Zanzibar kuwa nchi kama ilivyokuwa hapo kabla, haya si mageni bali kulitokea tu kuteleza kwa viongozi wetu waliotangulia akina Mzee Karume, Shekhe Jumbe, Mzee wa Ruhsa, Maalim Idriss, Komandoo, Karume wa sasa na Hata Maalim Seif mwenyewe na viongozi wengine wote akina wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya, wawakilishi na wabunge wote waliokuwepo, Masheha na akina Mabalozi wa nyumba kumi na kila Mzanzibari aliyekuwa na akili timamu wakati Zanzibar yetu inapotea.
    Lakini M/mungu amewaonyesha njia, kwani kati ya wote hao waliotangulia mbele ya M/mungu ni wachache mno na waliobaki bado wapo na wameyakubali. Hongereni kwa hili, kizazi cha sasa hatunabudi kuwasamehe
    Hii inaonyesha ni jinsi gani mlivyokubali kuwa mliteleza juu ya hili, hivyo ni wajibu wetu Wazanzibari kuwasamehe kwa moyo na nia safi hasa mukizingatia kuwa Wazanzibari mmewalea katika misingi ya kujirudi wenyewe pale wanapoona wameteleza.
    Hata wale wenye hofu katika nyoyo zao juu ya maendeleo watakayoyapata Wazanzibari baada ya kuungana na kuwa kitu kimoja kwamba watawanyanyasa wengine waondoe hofu hizo Wazanzibari sio watu wa kulipiza kisasi, Wazanzibari ni watu wenye nia safi na kila wenye nia safi na wao, laiti kama Wazanzibari ni wenye kulipa kisasi tusingekwenda Makkah kuhiji na wala tusingetaka kujiunga na OIC kwani hao wote ni waarabu na waarabu walitutawala kwa karne nyingi.
    Msiogope wenzetu hatuna chuki na nyinyi iwapo nanyi hamtakuwa na chuki na sisi.
    OMBI KWA UONGOZI UJAO:
    Sheria sasa inamruhusu Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya watu wa Zanzibar kuigawa Zanzibar kimikoa, hivyo ninaomba zile zote zilizokuwa zikiitwa Wilaya ndogo mfano Wilaya ndogo ya Kojani kule nyumbani Pemba na Wilaya ndogo ya Tumbatu kule nyumbani Unguja sasa zipewe hadhi ya kuwa Wilaya kamili ili tusogeze maendeleo sehemu hizo. M/mungu mwingi wa Rehema na mwingi wa Utukufu ibariki nchi yetu ya Zanzibr Uwabariki viongozi wetu, uibariki ardhi yetu na utbariki wakazi tunaoishi humo, utuongoze daima katika kutenda mema, viongowe vizazi vyetu, viwe ni vizazi vyenye maadili ya Kiislamu daima. Mrehemu na umsamehe Mtume wetu Muhammad (SAW).

  3. rasmi 05/09/2010 kwa 10:34 mu ·

    Hongera Mh Amani kwa kuturejeshea heshima yetu kama Wazanzibari. Tuna hamu na mabadiliko mengine mengi yaje kwa haraka nasi na vizazi vyetu tung’are.

    Nimefurahishwa na para hii:

    “Kwa mujibu wa sheria hii mabadiliko ya katiba ya Zanzibar ya kufuta Zanzibar kuwa ni nchi hayataweza kufanywa na baraza la wawakiishi mpaka kwanza mabadiliko hayo yakubaliwe na wananchi kwa kupigwa kura ya maoni.”

    Power to the people; nasi tuko sholda2sholda na nyinyi viongozi wetu.

  4. Khamis Ayoub Rashid 05/09/2010 kwa 11:17 mu ·

    Ni masikitiko makubwa yalionijaa moyoni kukosa kuona kwa macho yangu mabadiliko ya inch yetu niliokua nikiyasubiri maishani mwangu. Ningependa kuwashkuru wale wote walioanzisha safari hii ya miaka mingi inayoendele ya ukombozi wa Zanzibar yetu, safari ni refu sana lakini inshaaAllah tutafika.Mungu atupe nguvu WAZANZIBARI tuweza kuwa huru na madhalim na mafisdi wa nchi yetu.

  5. Elbattawi. 05/09/2010 kwa 12:03 um ·

    SALAAM MAALUM KWA MHE. MIZENGO PINDA.

    Napenda kumuelimisha kidogo Waziri Mkuu anayemaliza muda wake Mhe. Mizengo Pinda kwamba Zanzibar, ipo karne na karne haijafutika, haijaondoka na wala haijabadilishwa jina na itabakia kuwa Zanzibar milele na milele.

    Sababu Zanzibar ni nchi kamili na jina lake si jina la kubuni. Tanzania ni jina la nchi lakini lililobuniwa tu halina uzito sana wala maana yeyote kwa Wazanzibar. Kwa kufafanua zaidi naamini kuwa sisi Wazanzibari au baadhi yetu hatujisikii na wala hatuoni fahari kuitwa Watanzania Visiwani.

    Unaposema kuwa Zanzibar si nchi ni kuwakejeli na kuwadharau Wazanzibari, hilo haliwezi kuvumilika na kuachiwa kuendelea hivyo, sababu ya Muungano wa chini ya miaka 50. Hivyo watu kama Mhe. Mizengo Pinda, wanapaswa kuwa makini sana na kauli zao.

    Iko wapi Senegambia, hizi ni nchi ziliwahi kuungana – Senegal na Gambia, walipoona upande mmoja wa nchi unajiona kuwa na nguvu na kuchukuwa madaraka na maamuzi ya nchi nyengine, muungano huo ulivunjika kwa usiku mmoja tu. Asubuhi WaGambia walipoamka wanatangaziwa kupitia matangazo ya Redio kuwa Gambia, kuanzia usiku wa manane uliyopita imejiondoa kutoka muungano na Senegal, “very simple”; Kwa Mhe. Mizengo Pinda, anatakiwa kuangalia na kupima zaidi wakati.

    Mwaka 1988 katika ukumbi wa sinema ya Chachani Chake Chake sasa ni ukumbi wa mikutano ya ccm tu, Marehemu Rashid Mfaume Kawawa, wakati huo alikuwa ni Katibu mkuu wa ccm alifanya mkutano pale na walimu wa skuli za Pemba na hasa walimu wakuu na wasaidi wao pamoja na viongozi wa ccm na serikali.

    Nakumbuka aliulizwa swali na Maalim Ali Haji Machano, aliyekuwa maalim mkuu wa Skuli ya Muambe (sasa ni marehemu) kuhusu madaraka ya Chama yaani nafasi za juu za Chama kwanini hayagawanwi sawa na hasa cheo cha katibu mkuu kuwa siku zote kinashikiliwa na watu wa upande mmoja tu.

    Maalim Ali haji machano, aliendelea kumuuliza Kawawa kuwa hivyo Mheshimiwa Zanzibar, hakuna watu wenye uwezo kukamata cheo hicho ila nyie huko Bara tu. Mhe. Kawawa, alionekana kujibu swali hilo kwa hasira na hamaki sana; alisema hivi “ikiwa hapa Pemba, asiyeitaka ccm ahame”.

    Maalim Juma Ngwali wakati huo alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, na yeye alimuuliza,- alimuuliza Kawawa hivi, “Mhe. Kawawa, nakuuliza kwani Pemba na ccm kipi kilichokuja mwanzo?.. kama wamekuja Wapemba mwanzo na hii ni nchi yao, basi nakuhakikishia Pemba ccm itahama kabisa na kama huamini subiri”; Maalim Juma Ngwali, ilikuwa kama kamnywesha haluli Kawawa, inasemekana baada ya hapo Kawawa kutoka katika ukumbi wa Chachani, aliangukia chooni katika Ikulu ya Chake Chake. Na kweli kuanzia hapo ccm Pemba imehama kabisa.

    Hapa naamaanisha kwa Mhe. Mizengo Pinda na baadhi ya viongozi wengine wa Bara wenye muono kama wake kuwa wasicheze na Wazanzibari na nchi yao. Watakusikiliza baada ya hapo watatafuta kukujibu kiani.

    Amma kweli mwenye kusubiri hajuti.

  6. Royal Zenj 05/09/2010 kwa 1:17 um ·

    A/aleykum mimi mwenzenu nadhani niko na mawazo tofauti kidogo :- kama Zanzibar haijapata uwakilishi wa Kimataifa , kuweza kufanya mawasiliano na maamuzi yakuzungumza moja kwamoja na INTERNATIONAL ORGANIZATION ama hapo mimi binafsi siko OK .
    Wakati Maalim Seif alipotembelea hapa London kuna Mzanzibari mmoja alimuuliza suala hili Maalim lakini hakujibiwa vizuri na maalim nadhani ilikua ni mapema mno kujibu , Kwahiyo tufanye kama itakavyowezekana kupatapa uwakilishi wa Kimataifa hii ndio itakayo tupelekea sisi kujuilikana kimataifa , ndio tutakavyo pepea bendera ya Zanzibar .

    Kama nimekosea naomba radhi

    M/Mungu ibariki Zanzibar na Watu wake .

Comments are now closed for this article.