Siri ya maridhiano Zanzibar yawekwa hadharani
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 24/08/2010 // Kitaifa // 6 Comments
Na Salma Said,
KATIBU mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad amesema kuwa sifa za maridhiano yaliyofikiwa Zanzibar hazipaswi kuelekezwa kwake wala kwa rais wa Zanzibar, Abedi Amani Karume na kwamba suala hilo lilifanywa kuwa siri kubwa kwa karibu miezi sita kuepuka kuvurugika kwa mpango wa muafaka.
Karume na Seif wamekuwa wakisifiwa kuwa ndio walioasisi suala la maridhiano baada ya kukutana mara mbili Ikulu ya mjini hapa, mazungumzo yaliyofuatiwa na kitendo cha Maalim Seif kutangaza kuwa CUF imeamua kumtambua Karume kuwa rais wa Zanzibar.
Lakini akizungumza na Mwananchi ofisini kwake Vuga Zanzibar mwishoni mwa wiki, Maalim Seif alisema mchakato wa mazungumzo ulianzia siku ya maziko ya kiongozi wa zamani wa CUF, Shaaban Mloo Mei mwaka jana walipokutana yeye, Profesa Lipumba, Khamis Machano na Mzee Hassan Nassor Moyo.
“Tulizungumza kuhusu hali ya nchi inavyokwenda na tukakubaliana kwamba kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka kabisa kuinusuru nchi na tukaona kwamba hakuna haja ya sisi Wazanzibari kuendelea kugombana,” alisema Maalim Seif.
“Kwa hivyo tukasema kwamba pamoja na kuwa tuna timu za makatibu wakuu wa vyama vyetu, hili ni la Wazanzibari zaidi; tunaoumia ni sisi Wazanzibari. Kwa hivyo sisi wenyewe kama hatukuchukua hatua na juhudi maalum hakuna litakalofanyika. Sisi tufanye juhudi, wenzetu watusaidie, lakini kuwategemea wao kwa kweli hatutafika pahala,” Maalim Seif alieleza.
Mloo, ambaye alikuwa katibu mkuu wa kwanza wa CUF na ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM, alikuwa rafiki mkubwa wa Nassor Moyo kabla na baada ya kuruhusiwa kwa siasa za vyama vingi. Pamoja na Mloo kuwa mmoja wa waasisi wa CUF, urafiki wa wawili hao haukufa na Moyo alionekana mmoja wa watu wenye majonzi makubwa kwenye msiba wa Mloo.
Kwa mujibu wa Maalim Seif, baada ya kukubaliana kulivalia njuga suala hilo Mzee Moyo alikwenda kuzungumza na Rais Karume ambaye naye alisema kuwa anaunga mkono juhudi hizo kwa asilimia 100.
Alisema baada ya hapo waliunda timu ya watu sita, watatu kutoka CCM na watatu kutoka CUF, timu hiyo iliongozwa na Mzee Moyo akisaidiwa na Abubakar Khamis kutoka CUF na ilifanya mazungumzo kwa takriban miezi sita na walikubaliana kuwa mazungumzo hayo yaendeshwe kimya kimya.
“Tulikubaliana mazungumzo yaendeshwe kimya, kimya na kila hatua iliyofikiwa mimi na Rais Karume tulikuwa tukipewa taarifa na sisi kutoa mawazo yetu kisha nasi tulipeleka taarifa katika vikao vya juu katika vyama vyetu,” alisema Maalim Seif.
“Sisi CUF tulipeleka taarifa kwenye vikao vya baraza kuu la uongozi la CUF ambalo liliridhia na naamini hata CCM walifikisha kwa Rais Jakaya Kikwete na pia kujadiliwa na kamati kuu na halmashauri Kuu. Hivyo kusema kwamba mazungumzo na maridhiano yale ni ya Seif na Karume si sawa.”
Usiri wa mazungumzo hayo uliwafanya wanachama na wafuasi wa CUF kutoamini tamko la Maalim Seif kuwa chama chake kimeamua kumtambua Karume kuwa mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar kiasi cha kusababisha kiongozi huyo mwenye nguvu kwenye siasa za visiwani humo kuzomewa kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, Maalim Seif alishikilia msimamo wake akisema kuwa harakati za kuondoa siasa za uhasama na chuki visiwani humo, haziwezi kuendelea bila ya kumtambua Karume na ndipo kasi ya maridhiano ilipoongezeka hadi suala hilo kukubaliwa kuwa iundwe serikali ya umoja wa kitaifa na baadaye Baraza la Wawakilishi kupitisha uamuzi wa kupiga kura ya maoni.
Seif, ambaye pia aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, alisema kwa kawaida mazungumzo kama hilo hayawezi kufanywa katika mikutano ya hadhara na umati wa watu, ni lazima watu wachache kwanza waketi, wajadiliane na wapange, na wakifikia mwafaka ndipo jambo hilo hupelekwa kwa watu ili nao watoe ridhaa zao.
“Suala hili lilifikishwa kwenye vikao vya Baraza la Wawakilishi pale mwakilishi wa Mgogoni, Abubakar Khamis alipoliwasilisha kama hoja binafsi; ikajadiliwa na karibu asilimia 100 ya wawakilishi waliipitisha. Hivyo ndio kusema kwamba Wazanzibari waliwakilishwa katika suala hili tena katika hatua za awali kabisa kabla hata ya kura za maoni,” alisema Maalim Seif.
Katika kura ya maoni, watu waliokubali kuanzishwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa walishinda kwa asilimia 66.4 ya kura zote.







6 Comments on "Siri ya maridhiano Zanzibar yawekwa hadharani"
Wazanzibari hatuna budi kuwashukuru watu wote waliokaa na kuitafakari hali ya visiwa vyetu. Hii inaonyesha wazi kwamba hawa WA-ASISI wa Mapinduzi hata kama wengine wanaasili ya kutoka bara (Akina Moyo, Marehemu Mloo,. Wameiyona hali ya Visiwa na hatima yake kua sio nzuri.
Na ndiomaana walifikisha mazungumzo haya, huyu mzee Moyo ndio wale watu waliosema kwamba Karume Juniour na watu wake hawakuhusishwa kwenye mazungumzo ya Muungano hewa. Au wakati mwengine Mh Abeid amani karume aliwahi kumwambia Nyerere kuwa hakumfahamu juu ya Muungano huu.
Lakuomba sasa nikuiyombea nchi yetu (Zanzibar )dua ili uchaguzi ujao upite kwa salama na amani bila ya mauji. Na Ishaallah (ASW) atupe ushindi wanguvu, umoja na wenye matumaini na maendeleo kwa Wazanzibari wote na vizazi vijavyo Amen.
ASW awsambaratishe wale wote waliokua na nia mbaya ya Visiwa vyetu AMEN:
Mungu ibariki Zanzibar, Mungu Wabariki Wazanzibari
MTU MZIMA ZAMKO HIVI WEWE UMEWEZA KUANDIKA MANENO YOTE BILA YA KUFUPISHA ILA HIZI SIFA ZA ALLAH SUBHAANA NDIO UMEONA HAZINA MAANA NA UKATHUBUTU KUANDIKA KWA UFUPI KAMA VILE UMANYOIANDIKA CCM, AU CUF SIO. HEBU KUWENI WAISLAM WAKWELI NA MUINGIENI KATIKA WOTE NA SIO NUSU NUSU. UTAONA MTU ANAANDIKA SIFA ZA ALLAH SUBHAANA, KWA MFANO ALLAH SUBHAANA WATAALA ATAANDIKA ASW/SW KWANI UMESIKIA HIZO SIFA ZAKE NI CHAMA? AU UTAONA MWENGINE ANAANDIKA SIFA ZA KIUMBE MTUKUFU NA MTUME WA DARJA ALIELETWA KUWA NI REHMA KWA ULIMWENGU MZIMA MUHAMMAD SALLA NA AMANI YA ALLAH IWE KWAKE ATAANDIKA SWA ATI NDIO ANAMAANISHA SALLA LLAH ALAYHI WASALLAM, NINI NYIE, KUWENI NA HESHMA NA ASMAAU LHUSNA YA ALLAH AZZA WAJALLAH.
ALLAAHUMMA INNAKA AFUWUN TUHIBBU L-AFWAA FAA’FUANNAA YA KARIIM L-AFWA
Chambilecho chadema na kauli mbiu yao “Mpaka kieleweke” nasi tunasema haturudi nyuma, ni mbele kwa mbele.
Unajuwa watu mara nyingi huwa ni wenye hadhabu kwa hiyo hata pale mtu anapo towa mawazo au kuzungumza kitu hasikilizwi. Maalim Seif alipo kuja London, watu walikuwa wakali sana, kias kwamba hawakuwa na muda kusikiliza hotuba yake. Haya ya timu ya watu sita, alikusha kugusia London, sema hakutaja ni nani na nani. Lakini alisema kuwa kulikuwa na mazungumzo hayo. Mukipata nafasi ipitiyeni tena hotuba yake na mutalisikia hilo. Sisi wengine tunafahamu uwezo wa Maalim Seif wa kushughulika na mambo kama haya, kwa hiyo hatukuwa na pupa.
Mimi niliadha kupata faraja pale nilipomuona Mzee Hassan Nassor Moyo alipo anza kujumuika kwenye mikusanyika kama lile na uzinduzi wa kitabu; Memoirs ya Maalim Seif na Alhajj Ali Sultan. Nikafarajika tena, baada ya Maalim Seif kusema kuwa wao wawili, yaani Maalim Seif na Mzee Moyo hawakuwa ni wenye kusikilizana, kila mmoja alikuwa adui. Lakini si hilo tu, nikakufajika zaidi pale Dr Salim Ahmed Salim naye alipo msifia Mzee Nassor Hassan Moyo kuwa ni muungwana na akatowa sabau zake. Kwani ni moyo ndiye aliye msema vibaya Dr Salim Ahmed Salim kwenye kinyang’anyiro cha kuteuliwa kuwa mgombea wa urais wa Muungano na hata siku za nyuma wakati wa chama kimoja, alimuekea mguu Dr Salim na Maalim Seif pia. Kwa vile watu si wenye kutulia mtu anapo towa maelezo, basi mkutanoule ukaisha kwa kuuliza asuala yakipumbavu kabisa. Kwa mfano Maalim Sif kashasema wao hawana nia ya kuvunja Muungano. Anakujamtu anamuambia Maalim Seif, vipi kuhusu Muungano!
Kwa hiyo huu ni mwanzo tu, kuna mazuri mengi mutayashuhudia mbeleni. Kuna wengi wakupewa tunzo za aina yake kwa kazi hii ngumu waliyo tufanyia. Hawatasaulika abadan ndani ya nafsi zetu. Mtu mzima ni awa.
ni historia pekee ndio itakayojuvya ni nani wa kusifiwa na ni nani wa kulaumuwa.vizazi vijavyo ndivyo vitakavyoona haya na kwa sisi ni bado mapema kwani tumeyaona yalopita lakini bado kuyaona yajayo.
tumuombe mola atupe amani na utulivu katika visiwa vyetu
hivyo vizazi vijavyo watasoma tu kuwa watu walikuwa wakipigwa, wakibakwa nk nk kama vile leo nasikia tu kuwa wakati wa mapinduzi kulikuwa hivi na hivi, kwa hiyo machungu ya mapinduzi mimi siyafahamu kama yule aliyekuwepo wakati husika. Sisi tunawajengea wao na kama tunacho kijenga ni kizuri ni juu yao wao kukiendeleza.
This how goog leaders are! Alhamdulilah, kwa sasa tunamani Zanzibar, kwa hakika kila mtu ni mchunga, na ataulizwa kutokana na alichokichunga, kweli viongozi wetu wamejitahidi kuitoa Zanzibar katika wimbi la machafuko. naamini Wazanzibari walioko Zanzibar kwa kipindi hiki ni watu wenye uelewa na wanaelewa nini wanachokifanya kwa madhumuni gani, tunachohitaji si Uunguja wala Upemba, tunahitaji viongozi wenye kuona mbali, Maalim Seif na Dr Karume wao ni Viongozi na walipaswa kua kimya kama viongozi mahiri. naam, sasa nimeshibitisha mawazo yangu ambayo yaliniingia ktk kipindi cha kwanza cha kukutana Dr. Karume na Maalim Seif nilihisi sio bure, ndio…haikua bure….ilikua kama hivi……Kimya kingi kiliibuka na mshindo mkubwa, hatimae imekua ni historia ya Zanzibar. allah ametuhimiza tuhudhurie Mazishi, harusi na yale yenyekheri nasi, khwani ndani yake kuna ibra kubwa sana, kifo cha Mh. Mloo (Allah Amrehemu) ndio chachu ya mafanikio ya Zanzibar. Mwenyezimungu ni mkubwa. MUNGU IBARIKI Zanzibar watu wake Zanzibar. Nakumbuka mwaka 1993 baba alikua anatuimbia wimbo “……si..si..ni wanaaanchi….. kuendeleza, taifa letu, mabadiliko itikadi yetu…..TUKATAENI KUONEWA….” “A SUCCESSFULL EVENT HAS A PAINFULL STORY AND A PAINFULL STORY HAS A SUCCESSFULL ENDING”