Mgombea wa Urais Zanzibar huko Dodoma (Habari za magazeti)

Written by  //  08/07/2010  //  Kitaifa  //  1 Comment

Urais Zanzibar: Dk. Salmin atua Dodoma kutia `ubani`

  • Aondoka ndege moja na Nahodha
  • Aonekana mwenye bashasha nyingi
  • Ameadimika vikaoni muda mrefu

Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi CCM kesho itakutana mjini Dodoma kuwajadili na kuchuja majina ya wanachama 11 waliojitokeza kuomba uteuzi wa kugombea urais wa Zanzibar.

Miongoni mwa viongozi wa kitaifa wanaotarajiwa kuhudhuria kikao hicho ni Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, ambaye kwa miaka kadhaa hajaonekana kati ka shughuli za kitaifa na katika vikao vya CCM vilivyokuwa vikifanyika Tanzania Bara na Zanzibar, kutokana na matatizo ya macho.

Dk. Salmin ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mstaafu, aliondoka mjini Zanzibar jana mchana kuelekea mjini Dodoma.

Dk. Salmin alionekana mchangamfu wakati akiondoka katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar wakati wa kuingia katika ndege ya Serikali ambayo pia ilimchukua Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, ambaye pia ni miongoni mwa wagombea.

Dk. Salmin hakuhudhuria kikao cha Kamati Maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar Jumamosi iliyopita mjini Zanzibar ambacho kilipendekeza majina ya wagombea watano kuwa wanafaa kuteuliwa kushika nafasi hiyo. Kikao hicho kiliongozwa na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

Wagombea waliopendekezwa ni Waziri Kiongozi Mstaafu; Dk. Mohammed Gharib Bilal; Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha; Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna; Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein.

Wagombea wote watano waliopendekezwa waliwasili Dodoma jana kwa nyakati tofauti, wa kwanza akiwa Suleiman, ambaye aliondoka saa 1:00 za asubuhi kwa ndege ya Kampuni ya ZAN AIR akiwa amefuatana na mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mama Fatma Karume, na kufuatiwa na Shamuhuna, Dk. Bilal, Nahodha na Dk. Shein.

“Usione Dk. Salmin kaamua kwenda katika kikao, Zanzibar inapita katika wakati mgumu wa kisiasa na ndio maana ameamua kwenda kuokoa jahazi,” alisema mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka Zanzibar ambaye aliomba jina lake lisitajwe.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz, alisema Kamati Maalum ya CCM NEC Zanzibar tayari imeshakamilisha wajibu wake wa kupokea majina, kuyapitia na kukabidhi CC ambayo itayapitia na kupendekeza majina matatu ambayo yatapigiwa kura na kikao cha NEC kesho.

“Shughuli zote kwa sasa tumemkabidhi Katibu Mkuu wa Chama chetu, kwa upande wetu Zanzibar kazi tumemaliza tunasubiri maamuzi ya mwisho ya vikao,” alisema Ferouz.

Wakati huo huo, jana Mohammed Raza aliandika barua ya malalamiko kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kutokana na kutopokea barua ya mwaliko wa kuhudhuria vikao vya Dodoma.

Kwa mujibu wa barua hiyo yenye kumbukumbu namba 786/7/7/10 ya Julai 7, mwaka huu, Raza alisema baada ya kuhojiwa na Kikao cha Kamati Maalum ya CCM Zanzibar, Mwenyekiti wa kikao hicho, Rais Karume aliwaeleza kuwa wagombea wote watapewa taarifa juu ya kitakachofuatia, baada ya kujieleza na kujadiliwa.

Hata hivyo, alisema tangu kumalizika kwa kikao hicho, hakuna mawasiliano yoyote kati ya wagombea na chama wakati shughuli zote za uchukuaji fomu na urejeshaji zilifanyika kwa taarifa maalumu ya barua, kutoka kwenye chama.

Raza alimueleza Rais Kikwete kuwa baada ya kuona kimya kizito, aliamua kufika Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar na kutakiwa kwenda Masjala kupata mwongozo na kuelezwa kuwa hakuna maelekezo yoyote kuhusiana na suala la wagombea kuhudhuria vikao.

“Kutokana na hali hiyo, nakupa taarifa rasmi kuwa sijajitoa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, isije ikaonekana kuwa nimedharau kutokuja Dodoma kwenye vikao vinavyoendelea, ilieleza sehemu ya barua ya Raza kwenda kwa Mwenyekiti Kikwete.

Hata hivyo, Raza alisema ataendelea kuwa mwanachama muaminifu wa chama hicho na yuko tayari kupokea maamuzi yoyote yatakayofikiwa na CC.

Naye Balozi Ali Karume alisema hadi jana alikuwa hajapokea wito au mwaliko wa kuhudhuria vikao hivyo.

Alisema kwa kuwa yeye si mjumbe wa NEC atalazimika kuhudhuria kama mshangiliaji kwa vile hadi anawasili Dodoma hakukuwepo na mwongozo wowote uliotolewa kwa wagombea wanaowania nafasi hiyo.

Katika hatua nyingine, kikao cha bajeti cha Baraza la Wawakilishi kimeahirishwa hadi Julai 14, mwaka huu, ili kuwapa nafasi wajumbe wa CC na NEC kushiriki katika vikao vya CCM mjini Dodoma.

Kikao hicho kimeahirishwa baada ya kutolewa hoja na wajumbe wengi kuunga mkono ambapo Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho, alitangaza kuwa kikao hicho kitaendelea wiki ijayo.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM anatarajiwa kujulikana kesho baada ya wajumbe wa NEC kupigia kura majina matatu yatakayopelekwa na CC.

Tayari wanachama wa CCM wameanza kupamba maskani ikiwemo kupaka rangi kama matayarisho ya kumpokea mgombea atakayepitishwa huku mjadala ukitaja zaidi majina ya Dk. Bilal, Shamuhuna na Dk. Shein.

Habari kutoka Dodoma zinaeleza kuwa wapambe wa wagombea kutoka Zanzibar wamejaa katika nyumba mbalimbali za wageni wakisubiri hatma ya vikao vya leo na kesho.

Jana, ndege ya Shirika la Ndege la Precision ilikuwa ikitua mara kwa mara na kuondoka huku ikiwa imewabeba wajumbe na wapambe.

Katika ofisi za Makao Makuu ya CCM vijana wengi wa chama hicho jana walikuwa wamekusanyika wakiwa wamevaa sare za chama.

Wagombea ambao Nipashe iliwaona mjini Dodoma jana ni Nahodha, Shamhuna huku majina ya Dk. Shein na Dk. Bilal yakitajwa zaidi na wanachama wa CCM.

Wajumbe wa Sekretarieti walikuwa wakikutana jana kuanzia mchana kwa ajili ya kuandaa ajenda za Mkutano Mkuu unaotarajia kufanyika Jumamosi na Jumapili.

CHANZO: NIPASHE

‘Komandoo’, Nahodha watinga Dom pamoja

RAIS wa Awamu ya Tano ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Salmin Amour Juma, ametua Dodoma kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi kuhudhuria vikao muhimu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), vitakavyofanya uteuzi wa mgombea urais Zanzibar.

Dk. Salmin ‘Komandoo’ alishuka hapa jana mchana akiwa amefuatana katika ndege moja na Waziri Kiongozi wa SMZ, Shamsi Vuai Nahodha, ambaye pia anawania urais wa Zanzibar.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Komandoo kuhudhuria vikao vya juu vya CCM ambavyo ni Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), baada ya kuvikosa kwa miaka mitano kwa sababu mbalimbali.

Mwanasiasa huyo mwenye ushawishi wa juu katika siasa za Zanzibar, amekuwa akikosekana katika vikao hivyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya ugonjwa baada ya kusumbuliwa na macho kwa muda mrefu.

Hata Jumamosi wiki iliyopita, hakudhuria kikao cha Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar, ingawa alikuwapo mjini Unguja, lakini kuja kwake hapa, hakuna shaka kunaashiria jambo na atakuwa msaada mkubwa katika kufikia uamuzi wa nani asimame kwa tiketi ya CCM.

Hata hivyo, jana alishuka katika ndege ya Shirika la Ndege la Precision ATR 72, 5H PWC iliyopewa jina la Mwanza, saa 8.20 mchana, akiwa mwenye afya njema, lakini akitembea polepole.

Alisalimiana na viongozi kadhaa waliokuwapo uwanjani wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, John Tupa, kabla ya kwenda katika chumba cha mapumziko cha watu mashuhuri.

Hakupata fursa ya kuzungumza na wanahabari wachache waliokuwa uwanjani hapo, lakini alisalimia kwa kupunga mkono baada ya kushuka na kisha kusalimia viongozi waliojipanga kuwapokea.

Alisikika akisema, “hamjambo ndugu zangu, na mimi sijambo,” na kusalimiana na Tupa.
Baada ya kushuka kwa Komandoo ambaye kuja kwake Dodoma ni dhahiri kutabadili upepo kwa baadhi ya wagombea miongoni mwa 11 wanaowania kuteuliwa na CCM kumrithi Amani Abeid Karume, alishuka Nahodha.

Nahodha katika ndege hiyo alifuatana na watu mbalimbali zaidi ya 50 wakiwamo viongozi wa CCM Zanzibar, mawaziri, wawakilishi na wakuu wa mikoa.

Walikuwapo Waziri wa Katiba na Utawala Bora, Rashid Abdallah Shaaban, Waziri wa Ajira, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Asha Abdallah Juma na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Shawana Bahati Hassan.

Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa Wazazi Tanzania, Dogo Idd Mbarouk na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi.

Wawakilishi waliokuwamo ni Ame Mati Wadi (Matemwe), Salmini Awadhi Salmin (Magomeni), Ashura Abeid Faraja (Viti Maalumu – Pemba) na Mwenyekiti wa Kwanza wa Wanawake wa ASP, Salama Jabir.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai aliyekuwa kwenye msafara huo, aliwaambia wanahabari uwanjani hapo kuwa Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar imemaliza kazi yake.

Vuai alisema baada ya kikao cha Jumamosi iliyopita cha kupitia majina ya waombaji wa urais, hakuna malalamiko yaliyopokewa, na kwamba kama yupo mwenye malalamiko, anapaswa sasa kuyapeleka kwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.

“Sisi tumemaliza kazi yetu, hakuna ambaye ameleta malalamiko yake na kama yupo anapaswa kuyapeleka kwa Katibu Mkuu kwa sababu tumeshakabidhi kazi yetu. Tumekuja hapa, tayari kwa uamuzi mkubwa,” alisema.

Mbali ya Nahodha, Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein ambaye pia anawania urais wa Zanzibar, aliwasili mapema jana asubuhi kuhudhuria vikao muhimu.

Wote wawili ni wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambayo leo chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, itapitia majina hayo 11 na kutoa mapendekezo yake kwa NEC ambayo kesho itapiga kura, kumchagua atakayebeba bendera ya CCM katika uchaguzi wa Oktoba 31.

Mbali na hao, wengine wanaowania uteuzi huo wa CCM ni aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi Dk. Mohammed Gharib Bilal, Balozi Ali Karume, mawaziri Ali Juma Shamuhuna, Haroun Ali Suleiman na Naibu Waziri katika Serikali ya Muungano, Mohamed Aboud.

Wamo pia Mbunge Omar Sheha Mussa, Hamad Bakari Mshindo, mfanyabiashara Mohammed Raza na Kamishna mstaafu wa Utamaduni, Mohammed Yussuf Mshamba.

Tayari wajumbe mbalimbali wa vikao hivyo vya CCM ukiwamo Mkutano Mkuu wa Taifa utakaofanyika Jumamosi na Jumapili wiki hii, wameanza kuwasili hapa.

Jana Sekretarieti ya CCM ilikutana chini ya Katibu Mkuu Yusuf Makamba, kuandaa makabrasha kwa ajili ya Kamati Kuu leo.

Kama ilivyo katika mchakato wowote wa kuwania uongozi katika CCM, tayari baadhi ya majina yanatajwa kubashiriwa kupenya katika uteuzi wa Kamati Kuu kabla ya kupigiwa kura na NEC kesho.

Nahodha, Dk. Shein na Dk. Bilal ndio wanaotajwa kuwa chaguo la baadhi ya wana-CCM, kwa vigezo na sifa mbalimbali, na haitashangaza kama mmoja wao atasimama kwa tiketi ya CCM kukabiliana na Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, ili kuwa Rais wa Awamu ya Saba ya Zanzibar.

habarileo

Zanzibar CCM presidential aspirants in crucial stage today

THE Central Committee of CCM meets in Dodoma today to pick three members of the party out of 11 who are aspiring to run for Zanzibar presidency in October 31, General Elections for final screening by its National Executive Committee (NEC) on Friday.

The Secretary of CCM Special Committee for Zanzibar, Mr Vuai Ali Vuai, said the three aspirants would appear before NEC members in Dodoma for the final stage of the party’s gruelling nomination process.

NEC members, he said, would secretly vote to pick the party’s presidential candidate in the forthcoming elections.

In the race are the Vice-President, Dr Ali Mohamed Shein, Zanzibar Chief Minister Shamsi Vuai Nahodha, former Zanzibar Chief Minister, Dr Gharib Mohammed Bilal, Tanzania’s Ambassador to Bonn, Mr Ali Abeid Karume and Zanzibar Deputy Chief Minister, Mr Ally Juma Shamhuna.

Others are Zanzibar Minister for Education, Mr Haroun Ally Suleiman, Deputy Minister for East African Co-operation, Mohammed Aboud Mohammed, Zanzibar prominent businessman Mohammed Raza, Legislator Omari Sheha Mussa, Mr Mohammed Yusuf Mshamba and Mr Hamad Bakari Mshindo.

Many observers in Zanzibar speculate that Dr Shein, Dr Bilal and Mr Nahodha are likely to be endorsed by the CC to go to the final round in the nomination race before CCM-NEC on Friday.

The NEC session will be followed by a two-day Special CCM National Congress on Saturday and Sunday.

The Congress is scheduled to receive reports on the performance of the party, the Union and Zanzibar Revolutionary governments during the last five years.

The Congress will reach its climax on Sunday by endorsing the party’s presidential candidate for the United Republic, where the incumbent President Jakaya Kikwete is the sole CCM aspirant. Dr Kikwete is also expected to announce his running mate.

Meanwhile, one of the aspirants for Zanzibar’s presidency, Mr Raza said here that although he would not appear before the CC in Dodoma today for screening, he should be regarded as a serious contender.

In another development, police here said they were investigating on the source of leaflets that were distributed on Tuesday accusing Zanzibar President, Dr Amani Abeid Karume, of backing Dr Shein in the Isles presidential race.

The Urban West Regional Police Commander (RPC), Mr Aziz Juma Mohamed, warned politicians and their supporters to refrain from acts that could disprut peace in the islands.

Dailynews

One Comment on "Mgombea wa Urais Zanzibar huko Dodoma (Habari za magazeti)"

  1. Administrator 08/07/2010 kwa 9:32 um ·

    URAIS ZANZIBAR: Salmin atua Dodoma na Siri moyoni

    WAKATI hatima ya kumpata mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM inaelekea ukingoni mwishoni mwa wiki hii, makundi ya ushabiki yanahaha kuwapigia debe wagombea watatu ambao ni Dk Ali Mohamed Shein, Dk Ghalib Bilal na Shamsi Vuai Nahodha.Jana rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Salmin Amour (Komando) aliwasili mjini Dodoma akiwa katika ndege moja na Waziri wa Kiongozi Vuai Nahodha ambaye ni mmoja wa wagombea.

    Kwa muda mrefu sasa Dk Salmin haudhurii mikutana na vikao vya chama kutokana na kusumbuliwa na macho, hali inayoonyesha kuwa hatua ya sasa ya kumpata mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM ina unyeti wake.

    Makundi hayo yameunda ushindani mkubwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM itakayofanyika kesho, mjini Dodoma.
    Kwa mujibu wa taarifa tulizozipata kutoka Dodoma wakati wajumbe na wagombea wanaendelea kuwasili, kuna mchuano mkali miongoni mwa makundi ya wapambe wao.
    Fununu zaidi kutoka muongoni mwa wajumbe wa CCM zinasema kuna utofuati kati ya wajumbe wa Zanzibar na wa Bara kuhusu uungwaji mkono wa wagombea hao.
    Uchunguzi umebaini kwamba, wafuasi wa vigogo hao wamekuwa wakitambiana na kuelekeza kampeni kwa wajumbe wa Halmashauri ya CCM (Nec), ambao ndio watakaopiga kura kumchagua mtu mmoja atakayeshindana na wapinzani katika kinyang’anyiro hicho.

    Taarifa zinaeleza kuwa ingawa Dk Bilal anatajwa kuwa mshindani mkubwa katika kinyang’anyiro hicho, nafasi yake kuingia tatu bora ina utata kutoka na tuhuma za wafuasi wake kuendeleza kutoa lugha isiyonzuri.

    Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba amedokeza kuwa katika uteuzi huo chama hakitafanya makosa kwa kumteua mtu ambaye watu watamguna na kugoma kumchagua.
    Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni, Makamba alisema Kamati Kuu ya CCM itakutana kesho sambamba na Halmashauri Kuu ambayo itaanza kikao mara baada ya kumaliza kamati ili kuzuia kuvuja kwa maamuzi yaliyofikiwa.

    Akizungumza katika mahojiano maalum na TBC1 juzi, Makamba alisema mgombea urais wa Zanzibar atapatikana kwa sifa zake na jinsi atakavyojieleza mwenyewe mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu (Nec).

    “Hapa hakuna cha mgombea kupita kwa kupigiwa debe wala nini, CCM haiwezi kufanya makosa katika hili kwa kuwa tukimpitisha asiyefaa, watu wataguna na wakiguna ina maana tutashindwa katika uchaguzi; hivyo mgombea atapatikana kupitia sifa tulizozianisha na atakavyojieleza,”alisema Makamba.

    Hata hivyo wakati Makamba akitoa kauli hiyo juzi asubuhi, wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa walisema kulingana na mfumo wa utawala uliopo nchini, rais hawezi kutoka nje ya Baraza la Mawaziri.

    Wasomi hao waliwatabiria kwamba, Dk Shein, Vuai na Bilal kuwa ndio wenye nafasi kubwa ya kuteuliwa na Kamati Kuu.
    Hata hivyo, walionya kuwa kulingana na siasa za visiwa vya Zanzibar, anahitajika kiongozi imara atakayeweza kuimarisha mshikamano baina ya Wazanzibari.

    Mhadhiri Msaidizi wa Kitivo cha Siasa ya Sayansi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema CCM inakabiliwa na changamoto kubwa na kwamba kati ya waliojitokeza kutaka kuteuliwa wapo ambao hawaaminiki kutokana na rekodi na misimamo yao katika uongozi.

    “Lakini katika kinyang’anyiro hiki natoa nafasi kwa Dk Shein, Vuai na Dk Bilal,” alisema Ally.

    Profesa Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostine alisema Zanzibar wamezoea michuano mikali ya kisiasa na kwamba, si mara ya kwanza kujitokeza wagombea wengi katika nafasi hiyo.
    “Mtu ambaye hakuhusika katika mitafaruku hiyo ni Dk Shein na inaonekana ataweza kuwaunganisha Wazanzibari na hata maamuzi ya kumteua yanaweza yasiwagawe Wazanzibari,” alisema Profesa Baregu na kuongeza:

    “Pia Dk Shein hayuko kwenye kambi ya akina Karume wala Dk Salmini, au CCM Asilia na CCM Mtandao, hivyo haya ni mambo yatakayomfanya achaguliwe,” alisema Profesa Baregu.

    Mhadhiri wa Sheria wa UDSM, Dk Sengondo Mvungi alisema idadi kubwa ya wanaowania urais wa Zanzibar imeonyesha kiwango cha juu cha uelewa wao wa katiba ya nchi na haki zao.

    Mwenyekiti mwenza wa Mpango wa Utafiti wa Elimu ya Demokrasia (Redet), Dk Benson Bana alisema: “Kwanza tuwapongeze tu wametambua haki yao na wameonyesha ukomavu wa demokrasia.”

    Wanachama 11 waliojitokeza kuwania urais kumrithi Amani Abeid Karume ambaye amemaliza muda wake ni Nahodha, Ali Juma Shamhuna, Dk Shein, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohamed Aboud na Dk Gharib Bilal.

    Wengine ni balozi wa Tanzania nchini Italia, Ali Karume, Hamad Bakari Mshindo, Omar Sheha Mussa, Mohamed Yusuf Mshamba na Mohamed Raza Dharamsi.

    Wachambuzi wengine wa siasa wanasema sio rahisi kwa Haroun na Shamsi kuingia wote katika tatu bora kwa vile wanatoka katika jimbo moja la Makunduchi.
    Ali Karume ambaye ni mdogo wa Rais Amani Karume amekuwa akitamba kwamba, kutokana na elimu yake na uzoefu katika siasa, ana nafasi kubwa ya kuteuliwa na chama chake kama vigezo vilivyowekwa na vitafuatwa.

    Mohammed Aboud ambaye katika kikao cha kamati maalumu kilichofanyika Zanzibar wiki iliyopita kilimjadili na baadhi ya wajumbe kutoa tuhuma za kughushi vyeti, amekuwa akijitetea kuwa madai hayo hayana msingi na kuwa yuko tayari kutoa ufafanuzi mbele ya vikao vya juu vya chama vyenye maamuzi ya mwisho.

    Mohammed Raza amelalamikia kutoalikwa katika kikao cha CC kinachofanyika kesho na kudai kwamba kutoonekana kwake Dodoma hakumaanishi kujitoa katika kinyanganyiro hicho.

    “Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM nilikwenda katika ofisi zetu za chama kutaka ufafanuzi nikaelezwa niende katika ofisi ya masjala ili kupata utaratibu zaidi kuhusu kwenda katika kikao cha NEC Dodoma,” anasema Raza katika barua yake kwa Rais Kikwete.

    Dk Salmin akilitua mjini Dodoma saa 8:10 kwa ndege ya Shrika la Ndege la Precision akiwa ameongzana na mgombea wa Urais, Nahodha pamoja na Asha Abdalah Juma ambaye ni Waziri na Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala bora, Ramadhani Abdalah, baadhi ya wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
    Komandoo Salmin, alikuwa wa kwanza kushuka na kufuatiwa na Nahodha na viongozi mbali mbali wa serikali na CCM walifika kuwalaki.
    Mgombea mwingine wa Urais wa Zanzibar, Dk Shein aliwasili jana majira ya saa tano asubuhi akifuatiwa na mgombea mwingine, Mohamed Aboud ambaye ni Naibu Waziri wa Afrika ya Mashariki.

    Hata hivyo hadi jana mchana ilikuwa haijafahamika kama Bilal amefika Dodoma ingawa wapiga kampeni wake wameuteka mji wa Dodoma.

    Wakati viongozi hao wakitua, makundi ya wapiga kampeni wa Urais wa Zanzibar kutoka maskani mbali mbali, wamewasili mjini hapa tangu juzi usiku na jana walikuwa wametanda ofisi za CCM na kwenye nyumba za kulala wageni.

    Wengi wa makada hao wa CCM kutoka Zanzibar walikuwa ni Gharib Bilal toka maskani za mikoa mitano Zanzibar wakiongozwa na wajumbe wa maskani kubwa ya Kisonge, ambao walionya kuwa kamwe hawatakubali kusikia vikao vya juu ya CCM vimemwengua.

    Kada maarufu wa CCM Zanzibar na mmoja wa waasisi ya jumuiya ya vijana wa Afro-Shiraz, Baraka Mohamed Shamte, alisema chaguo la Wazanzibar wote ni Bilal na kama CCM Bara ikilazimisha kumleta mwingine kitakachotokea watajuta.

    Shamte alikuwa Katibu wa CCM katika wilaya mbali mbali, ikiwepo Wete Pemba, Unguja Mjini na Pangani mkoani Tanga, kabla ya kurejea Zanzibar.

    “Tangu mwaka 2000 chaguo la Wazanzibari ni Bilal na hadi sasa na kama wanataka CCM iendelee kuwepo Zanzibar waturejeshee Bilal kuwa mgombea wa Urais,”alisema Shamte.

    Wajumbe wengine, Ally Mzee na Mohamed Issa Ramadhani ambao walisema wanajua CCM bara wanamtaka Makamu wa Rais, Dk Shein, lakini wajuwe Zanzibar wanamtaka Bilal au Nahodha.

    Kada Mwingine wa CCM toka Zanzibar, Jamal Ramadhani ambaye alikuwa anaongoza ujumbe wa watu 200 toka Zanzibar alisema, CCM isifanye mzaha katika suala la uteuzi wa mgombea wa Urais Zanzibar.

    Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM Zanzibar, Vual Alli Vuai alimweleza mwandishi wa habari hizi mara baada ya kufika jana kuwa kamati maalum iliyopitia majina ya wagombea Zanzibar imemaliza kazi yake sasa imebaki kazi ya CC na Halmashauri Kuu.
    Habari hii imeandaliwa na Salma Said, Zanzibar, Mussa Juma, Dodoma,
    Sadick Mtulya na Salim Said, Dar

Comments are now closed for this article.