Uzinduzi wa Nyumba ya watoto Yatima Mazizini

Written by  //  28/08/2010  //  Kitaifa  //  Zima maoni

Salma Said, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar Amani Abeid Karume, amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya ulimwengu na kukua kwa uchumi ipo haja kwa watoto nao kujengewa makaazi bora yenye utulivu na yanayokwenda na wakati uliopo.

Akifungua nyumba mpya ya makaazi ya watoto yatima, iliyopo Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar, iliyojengwa kwa ufadhili wa Jumuiya ya ZAYEDESA, Rais Karume alisema kuwa watoto wana haki ya kuishi maisha bora ambayo yatawasaidia kupata huduma zote muhimu na za lazima ili kuweza kuwaendeshea maisha yao.

Rais Karume alisema kuwa lengo na madhumuni ya ujenzi wa jengo hilo lililojengwa na ZAYEDESA ni kuwasaidia watoto waishi katika maisha mazuri na yenye maendeleo.

Alisema kuwa Rais wa mwanzo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar marehemu mzee Abeid Karume, alijenga jengo la kulelea watoto lililopo Forodhani kwa lengo hilo hilo ambapo kwa sasa jengo hilo limekuwa halikidhi haja sanjari na uchakavu na kutokuwa katika mazingira mazuri.

Kutokana na hatua hiyo ndipo Mama Shadya kupitia Jumuiya yake ya ZAYEDESA kuja na wazo la kujenga jengo hilo jipya na kuweza kuungwa mkono na washirika wa maendeleo wa ndani na nje ya Zanzibar.

Aidha, Rais Karume alitoa wito kwa NGOs nyengine kuiga mfano huo kwa kugawana maeneo ya utendaji kwa kushirikiana pamoja katika kuimarisha maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwasaidia watoto.

Rais Karume alisema kuwa baada ya kuhama watoto hao huko Forodhani jengo hilo kongwe kwa hivi sasa litakuwa ni makumbusho ya Usafiri wa Bahari katika eneo la Bahari ya Hindi kazi itakayofanywa kwa kushirikiana na Jumuiya ya AgaKhan.

Nae Mama Shadya Karume, Mwenyekiti wa ZAYEDESA, alisema kuwa kukamilika kwa makaazi hayo ya watoto ni matokeo ya mashirikiano na misaada ya watu na makundi mbali mbali ndani na nje ya jamii.

Mama Shadya alisema kuwa muasisi wa ulezi huo ambaye ni Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Karume alianzisha nyumba ya kulelea watoto Forodhoni kwa imani na upendo mkubwa wa watoto wa Taifa hili. Na kutoa pongezi kwa Mama Fatma Karume kazi yake kubwa na nzuri na kumuunga mkono mzee Karume katika ulezi wa watoto huko Forodhani.

Mama Shadya Karume alisema kuwa jengo hilo linauwezo wa kupokea watoto 80, ambapo kwa hivi sasa lina jumla ya watoto 48 wakiwemo wanawake 27 na wanaume 21.

Aidha, Mama Shadya Karume alisema kuwa mazingira ya jengo hilo jipya yatatoa fursa nzuri zaidi kwa malezi ya watoto bila ya vishawishi kwa vile vilivyoyazunguka mazingira ya Forodhani.

Alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo hadi kukamilika kwake umegharimu jumla ya Tshs. 8333,826,041, ambayo hiyo ni gharama kubwa ambayo ZAYEDESA pekee isingeweza kuimudu bali ushirikiano wa watu binafsi, wapenzi, wadau mbali mbali na washirika wa maendeleo ndio uliowezesha kukamilika kwa ujenzi huo.

Mama Shadya Karume alitoa pongezi na shukurani kwa wale wote waliosaidia ujenzi huo wakiwemo waliotoa fedha taslim, vifaa na michango mengine mbali mbali.

Nae Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Sultan Mugheiry, alisema kuwa mchango mkubwa unaotolewa na Mama Shadya Karume katika maendeleo ya sekta ya Afya na Ustawi wa Jamii ni kielelezo cha kutosha kuthibitisha jitihada za Mama Shadya Karume katika kuimarisha Ustawi wa Jamii hapa Zanzibar.

Waziri Mugheiry alisema kuwa kuanishwa na kuimarishwa kwa huduma za kuwatunza watoto hapa Zanzibar ni kutekeleza kwa vitendo Azimio la Kimataifa la Haki za Mtoto (Convention of the Right of Child) linalosisitiza umuhimu na haki ya kulindwa na kutunzwa kwa mtoto.

Nao watoto watakaoishi katika jengo hilo jipya walitoa shukurani kwa Mama Shadya Karume kwa kuwajali kwa kuwajengea jengo hilo pamoja na kuwa nao karibu kwa kuwasaidia misaada mbali mbali na kuwatembelea hasa katika siku za sikukuu.

Nyumba hiyo ya ghorofa moja ina vyumba vya kulalia watoto, maktaba, chumba cha kompyuta, jiko la ndani na nje, zahanati,vyumba vya walezi, msikiti, uwanja wa kusomea, bustani, chumba cha kazi za mikono chenye vyarahani,ukumbi wa mkutano na ukumbi wa kulia, mapokezi, chumba cha daktari na sehemu nyengine muhimu.

Picha na Ramadhan Othman, Ikulu.

Comments are closed.