Wapemba washauriwa kusahau yaliyopita

Written by  //  29/07/2010  //  Kitaifa  //  Zima maoni

Wakati Wazanzibari wakijiandaa kupiga kura ya maoni kuamua kama Serikali ya Umoja wa Kitaifa iundwe ama la Jumamosi wiki hii, Mwenyekiti wa Kamati ya Watu sita ya Baraza la Wawakilishi inayofuatilia suala hilo, Ali Mzee Ali, amewataka wananchi wa Pemba kukataa kufitinishishwa kwa sababu za tofauti za kiitikadi.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa madiwani na masheha wa Mkoa wa Kusini Pemba, Ali ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, aliwaambia kwamba siasa za fitina, chuki na uhasama zinahitajika kuzikwa na kujenga mustakabali mpya Zanzibar wenye kuzingatia umoja na mshikamano.

“Msikubali kufitinishwa mkapoteza watu wazuri kama ilivyotokea huko nyuma…nakuombeni sana msikubali kurudi katika balaa, tunahitaji umoja na amani zaidi,” alisema na kuongeza:

Aliwakumbusha viongozi hao na hasa wazee walioshuhudia siasa za zamani Zanzibar na misukosuko iliyoambatana na chuki za kisiasa baina ya wafuasi wa vilivyokuwa vyama vya siasa wakati ule kabla ya Mapinduzi kuwa wapenda amani na utulivu hawatarajii tena kurudi huko.

Mjumbe wa kamati hiyo, Haji Omar Kheir ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema msimamo wa CCM ni kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa, alisema Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yalifanyika kuleta hali za watu sawa na kuondoa aina yoyote ya ubaguzi.

Alisema Pemba imepita katika kipindi kigumu vikiwemo vitendo vya kuhujumiana, kuchomeana nyumba na hata watu wengine kuacha wake zao kwa sababu ya ushabiki wa kisiasa.

“Nilikuja na mke wangu na watoto wangu mwaka 2004 nilipoteuliwa kuwa mkuu wa mkoa, lakini nilishindwa na kuwarudisha nyumbani, nilikuwa nikitembea na askari wanaofika kumi, lakini hayo yote ya nini?” alihoji na kuongeza:

“Umefika wakati wa kusahau yaliyopita na kurudisha nguvu zetu za umoja na utulivu ambao ndio huu.”

Tindwa alisema matukio ya Januari 26 na 27 mwaka 2001 yaliyosababishwa na siasa yamefanya Tanzania kwa mara ya kwanza kuzalisha wakimbizi waliokimbilia Shimoni-Mombasa, Kenya wakitokea Pemba na watu 27 walipoteza maisha.

Masheha na madiwani walisema kwamba wanaunga mkono suala zima la kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar wakisisitiza kuwa wananchi wamechoshwa na migawanyiko inayochangia kuwarudisha nyuma kimaendeleo.

CHANZO: NIPASHE

Comments are closed.