Wapingaji wa kura ya Maoni Mafichoni
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 19/07/2010 // Kitaifa // 6 Comments
Na Salma Said,
KAMPENI ya kuhamasisha wazanzibari kujitokeza kwa wingi katika kupiga kura ya maoni itakayoamua kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa visiwani Zanzibar imeanza kwa kasi kubwa huku baadhi ya wanaopinga kura hiyo wakiwa mafichoni.
Wakati kamati ya wajumbe sita wa baraza la wawakilishi ikiendelea kutoa elimu uchunguzi wa gazeti hili umegundua kwamba kumekuwepo na upotoshaji mkubwa wa wafanyao kampeni hiyo ambapo baadhi yao wamekuwa wakitoa elimu isiyo sahihi kwa wananchi mbali mbali katika maeneo ya mjini na vijijini kwa Unguja na Pemba.
Baadhi ya wawakilishi, masheha na viongozi wa ngazi za juu wa serikali wamekuwa wakitajwa kuwa ni miongoni mwa wapotoshaji wakubwa ambao mbali ya kukataa kutoa misimamo yao juu ya kura ya maoni itakayotarajiwa kupigwa Julai 31 mwezi huu lakini pia wamekuwa wakiwataka wananchi kupiga kura ya hapana kwa maslahi yao binafsi.
Hayo yamebainika katika kongamano la siku mbili lililofanyika Baitul Lyamin Malindi Mjini Zanzibar lililotayarishwa na taasisi tatu ikiwemo MUWAZA, JUMIKI, ZLS lililojadili kura ya maoni ya serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar.
Wachangiaji wa kongamano hilo wamesema kumekuwepo na upotoshaji mkubwa ambapo wametaka serikali kuingilia kati kwa kutoa elimu ipasavyo kwa umma ili watu wenye kueneza kampeni chafu dhidi ya kura ya maoni washindwe kufanikiwa na kampeni zao.
Washiriki wa kongamano hilo pia wameshangazwa na wawakilishi ambao wakati wakichangia hoja binafasi iliyowasilishwa na kiongozi wa upinzani barazani Abubakar Khamis Bakari walionekana kuunga mkono hoja ya baraza lakini wanapokwenda majimboni mwao huwapotosha wananchi.
“Ni jambo la kushangaza sana hawa wawakilishi tulikuwa tukiwasilia wakati wakichangia hoja ya baraza kwamba wanaunga mkono kura ya maoni na walikuwa wanajidai wana uchungu mkubwa na hali ya kisiasa inavyokwenda lakini wawakilishi hawa hawa ndio wanaokuja majimboni mwetu na kututaka tuseme hapana siku ya julai 31 sasa hapa sisi tunashindwa kuelewa hivi kweli wana dhamira ya kweli hawa?” alihoji Juma Said Ali katika kongamno hilo.
Wengi wa wawakilishi na wabunge wenye kudaiwa kuendesha kampeni na kataa kura ya maoni wamekuwa kimya na kukataa kutoa misimamo yao wanapofuatwa na kuulizwa iwapo wanamsimamo gani juu ya kura ya maoni itakayopigwa julai 31 mwezi huu.
Ni Mawaziri wawili tu waziri wa elimu na mafunzo ya amali, Haroun Ali Suleiman na waziri wa Maji, ujenzi, ardhi, Mansoor Yusuf Himid ndio waliothubutu kutaja umuhimu wa kuwepo kwa amani na utulivu katika bajeti zao ambapo wamewataka wananchi katika majimbo yao kutoa kura ya ndio ili Zanzibar ipate maendeleo na kumaliza migogoro ya kisiasa yenye kuandamana na chuki zisizokuwa na ulazima.
Kwa upande wa Tanzania bara ukimtoa Rais Kikwete hadi sasa ni mwaziri mmoja pekee anayehubiri serikali ya umoja wa kitaifa ambaye ni Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud Mohammed ambaye kila mara amabpokwenda Pemba kwa ziara huhubiri suala hilo na kuwataka wananchi wa kisiwa hicho kuachana na siasa za chuki na kujitokeza kwa wingi katika kutia kura ya ndio ifikapo tarehe 31 mwezi huu.
Wakati baadhi ya wawakilishi wakiwa wamejificha nyuma ya pazia na kukataa kutoa misimamo yao wakiogopa kupoteza nafasi zao majimboni tayari viongozi wakuu akiwemo Rais Kikwete, Rais Karume, Dk Ali Mohammed Shein, Spika wa baraza la wawakilishi, Pandu Ameir Kificho na Katibu Mkuu wa CUF wameeleza misimamo yao wazi wazi na kuwataka wananchi kutoa kura ya ndio ili kuinusuru Zanzibar na machafuko ya kisiasa.
“Mimi Seif Sharif Hamad nanyoosha mkono wangu wa kulia juu kama alama ya kujitambulisha kwenu na kwa Mwenyeenzi Mungu kuwa nimefikisha ujumbe huu kwa wazanzibari. Naelewa pia Rais Karume na yeye anafanya hivyo hivyo. Nimewafikishia kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Nimewafikishia kuwa hakuna ugomvi usio na mwisho. Nimewafikishia kuwa sisi ni ndugu basi tuuimarishe udugu wetu.Naomba nyote mushuhudie kuwa nimefikisha. Jee mmeshuhudia?” alisema Maalim Seif ufunguaji wa kongamano hilo.
Tayari taasisi mbali mbali zimekuwa zikifanya juhudi za kutoa elimu kwa wananchi ambapo Tanzania Center For Democracy (TCD) imeandaa matamasha mawili makubwa kupitia sanaa za nyimbo kutoa elimu juu ya kura ya maoni kwa Unguja na Pemba.
Kwa upande wao Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imekusanya vikundi vinane kwa ajili ya kutoa burudani na maonesho ya sanaa zao katika kutoa elimu hiyo huku vyombo vya habari vikitakiwa kushiriki kikamilifu katika kuandaa vipindi na makala mbali mbali ya kuelimisha umma juu ya suala hilo.






6 Comments on "Wapingaji wa kura ya Maoni Mafichoni"
Achana nao hao wawakilishi wabovu serikali ya pamoja itashinda tu Inshalla .
A/ALEIKUM HAWA WAWAKILISHI WASIOTOA MSIMAMO WAO NI WANAFIKI CHA KUSHANGAZA ZILE ZAMA ZA KUOGOPANA ZIMEKWISHA NI BORA KILA MTU ATOE MSIMAMO WAKE WAZIWAZI KAMA UNATAKA SEMA NDIO NA KAMA HUTAKI SEMA HAPANA SASA SIJUI NI KITU GANI KINACHOWATIA HOFU AU MNAWAOGOPA KISONGE ?
INSHAALLAH…..Wanafiki wote Mwenyezi Mungu atawaadhirisha; kwa hili la kukataa umoja. Tuendeleeni na juhudi ya kuelimishana na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu InshaAllah atatujaalia kutupa kheri tuliyoikusudia na ambayo kwa miaka nenda rudi ilikuwa tunaitafuta. Pia kwa ushauri na viongozi wa dini watakiwe kusaidia katika kuelimisha jamii yetu juu ya umuhimu wa mariadhiano na haja ya kuunga mkono kura ya maoni ya kukubali kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi. Wengi wa hao wawakilishi na mawaziri wakubwa wanaokataa ni wabinafsi…..Hata hivyo, InshaAllah tunamuomba Mwenyezi Mungu awafedheheshe kwa hili; kwani inaonekana dhahiri ni maadaui wa umoja wa Wazanzibar. Tunamuomba Mwenyezi Mungu asiwape nguvu wale wote wanaoendesha kampeni za kupinga kura ya ndio kwa ajili ya kuunga mkono umoja na mshikamano wa Wazanzibari. Tunamuomba Mwenyezi Mungu pia awabainishe na kuwafedhehesha hadharani maaduni hawa wa Wazanzibari.Mwenyezi Mungu ibariki Zanzibar na Wazanzibari wote. Mwenyezi Mungu tunakumba uwape ilham Wazanzibari wote watie kura ya ndio kuunga mkono Serikali ya Unoja wa Kitaifa Zanzibar …Amini Amini Amini
siku zote kwenye suala la kutoa maoni hapaachi kuwa na upinzani kwani kila mmoja husimama juu ya kile anachoona ni sawa na ndio maana tukapiga kura vinginevyo kuwa watu wote waunge mkono hapana haja ya kupiga kura sasa cha msingi si kuwalaumu kwani ukiwalaumu nao watakulaumu badala yake ni kla mmoja achukue jukumu la kumueleza mwengine umuhimu wa kuwa na hiyo serikali ya pamoja na kumuomba aweke kura ya ndio siku ikifika na ukweli haki ndio itashinda na inabidi tukubaliane nayo hata ikitoke kwamba hapana ndo iloshinda tujue hilo allah ndo katutakia kwa hiyo tuangalie namna gani ya kuimarisha umoja na kufikia lengo kwa sababu hata hiyo kura ya maoni ni moja ya njia lakini ziko njia mbadala endapo haikufaulu hiyo
Hawa wawakilishi wanaopinga kura ya maoni hawatoshindwa kwenye azma yao hiyo tu bali hata kutetea nafasi zao watashindwa kwasababu ya unafiki wao tu.
J
Karume wa mapinduzi baba wa Karume wa leo alisema “umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”