Zanzibar kuwa nchi
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 09/08/2010 // Kitaifa // 18 Comments
na Hassan Shaaban, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inafanya marekebisho ya katiba ya mwaka 1984, ambayo yanaipa Zanzibar hadhi kamili kama nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano.
Marekebisho hayo ya katiba yanatarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoanza leo Zanzibar, ambapo pia yataruhusu kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa rasimu ya marekebisho ya katiba hiyo, sura ya kwanza ibara ya kwanza iliyokuwa ikisomeka, Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefutwa chini ya marekebisho hayo.
Rasimu hiyo ambayo itawasilishwa na Mwanasheria Mkuu, Idd Pandu Hassan, inapendekeza kifungu hicho sasa kisomeke ‘Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguuka na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliitwa Jamhuri ya watu wa Zanzibar’.
Aidha, marekebisho hayo ya katiba yamegusa kifungu cha pili na kueleza kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Marekebisho hayo pia yamegusa mamlaka ya rais katika kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.
Kabla ya marekebisho hayo kifungu cha pili cha Katiba ya Zanzibar kilikuwa kikisomeka ‘kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za serikali, Rais wa Jamhuri ya Muungano akishauriana na rais anaweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa’.
Marekebisho hayo pia yamempa uwezo Rais wa Zanzibar kuteua wakuu wa mikoa bila ya kushauriana na Rais wa Jamhuri ya Muungano, kama ilivyokuwa kabla ya marekebisho hayo.
Marekebisho hayo ya 10 ya Katiba ya Zanzibar iwapo yatapitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi yatamaliza msuguano uliokuwa umejitokeza kuhusu nafasi ya Zanzibar katika Jamhuri ya Muungano, baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kudai kuwa “Zanzibar si nchi”.
Hata hivyo, baadaye Rais Jakaya Kikwete akitoa ufafanuzi wa suala hilo alisema Zanzibar ni nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano, lakini “Zanzibar si nchi nje ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyo kwa Tanganyika. ”
Aidha, marekebisho hayo ya katiba yanampa uwezo Rais wa Zanzibar kuteua makamu wawili wa rais, akiwamo makamu wa kwanza ambaye atateuliwa baada ya rais kushauriana na chama kilichoshika nafasi ya pili katika kura za rais kwenye Uchaguzi Mkuu.
Rais pia atamteua makamu wa pili wa rais ambaye atakuwa ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali ndani ya Baraza la Wawakilishi
Wakati wajumbe wa Baraza la Mawaziri watateuliwa kwa uwiano wa viti vya wajumbe ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Pia mswada huo unafuta wadhifa wa Katibu Mkuu Baraza la Mapinduzi na kuweka Katibu Mkuu Kiongozi, ambapo pia kutakuwa na makatibu wakuu wa ofisi ya makamu wa kwanza wa rais na katibu mkuu ofisi ya makamu wa pili wa rais.
tzdaima






18 Comments on "Zanzibar kuwa nchi"
Kama mzanzibari nimefurahishwa na mabadiliko hayo, nasubiria hao wawakilishi watakao kipinga kipengele hichi!
Msaada huu umenifurahisha sana kwa (1) kumpa rais wa zanzibar uwezo wa kuigawa zanzibar ktk mikoa ya kiutawala bila ya kutaka ruhusa kutoka kwa rais wa jamuhuri ya muungano. (2) kufuta kipengele kinachosema kua zanzibar ni sehemu ya jamuhuri ya muungano na badala yake kusema kua zanzibar ni nchi. Hii ni jawabu kwa akina pinda. Unajua bwana pinda kujipinda pinda mpaka akasema zanzibar si nchi kumetusaidia sana wazanzibari na reactions zake ndio kama hizi kwani kheri hutokana na shari. Kuna siku moja nilikasirika sana hii nisiku ya kufungua soko la pamoja la africa ya mashariki, ulipofika wakati kwa marais wa nchi zinazounda jumuia ya africa mashariki kusalimia wananchi waliohudhuria sherehe ile, marais wote wa unganda,kenya,burundi,rwanda na tanzania walipanda jukwaani kila moja kwa wakati wake kusalimia wananchi waliokuepo lkn cha kusikitisha ni kua rais wa zanzibar mheshimiwa amani alikuepo lkn hakupanda jukwaani kuwasalimia wananchi. Mimi nilihisi ni dharau kubwa kwa zanzibar nzima lkn sikua na lakufanya lkn karibuni hivi na sisi tatukua na rais anaeheshimiwa kama rais. Amin. Hongera rais aman, hongera pia kwa walioshiriki kutunga msaada huu. Nawataka wajumbe wote wa BLW kuupitisha msaada huu kwa kauli moja kwani ni wajibu wenu kuupitisha.
A/A MIMI BADO SIAMINI KAMA RASIMU HIYO ITAIFANYA ZANZIBAR KUWA NCHI KWA SABABU NCHI LAZIMA IWE NA WIZARA YA MAMBO YA NNJE ,MAMBO YA NDANI , ULINZI ,MUWAKILISHI WA UMOJA WA MATAIFA ,PAMOJA NA MABALOZI WAKE KATIKA NCHI TOFAUTI DUNIANI TUTAKAPOFIKA HAPO NITASEMA SASA ZANZIBAR IMEKUWA NCHI KAMA ILIVYOKUWA KABLA YA MAPINDUZI YA 1964 NA MIEZI MITATU YA KWANZA BAADA MAPINDUZI
BUTIAMA USIWE NA HARAKA, BANDU BANDU HUMALIZA GOGO LA MNAZI.
A/A
KWAHAPA TULIPO NAAMINI WAWAKILISHI WETU WAMESHAELEWA NINI MAANA YA UZANZIBARI JITIHADA KUBWA ZIMETUMIKA KUFIKIA HAPA PAMOJA NA MASIMANGO YA WATANGANYIKA WACHACHE WASIOITAKIA MEMA ZANZIBAR YETU NAWAOMBA SANA WAWAKILISHI WAKAZEBUTI KATIKA MUSWADA HUU ILI ULIMWENGU UELEWE KUWA ZANZIBAR NI NCHI TANGU AWALI NA SASA TUNAHITAJI KUJITAWALA WENYEWE:
NAAMINI MAMBO YOTE YATARUDI WIZARA BENDERA VITI VYA UN AU NA MENGINE MAZURI MAZURI KILA KITU KWA HATUA TARATIBU NDIO MWENDO:
RAMADHANI NJEMA
Kwa upande wangu, mimi naungana na Butiama, ingawaje kivyanguvyangu kama ifuatavyo. Naomba munisome vizuri kwa kuzingatia na bila ya jazba, kwani hata mimi natamani Zanzibar tuwe nchi kamili, hata leo hivi:
Chini ya Muungano huu, kwa Zanzibar kuwa nchi (kamili)lazima Katiba ya Jamhuri ya Muungano ITAMKE hivyo. Kwani Katiba ya Jamhuri ya Muungano ndio katiba mama, ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania. Chini ya Muungano ni katiba ya Jamhuri ya Muungano pekee ndio inayoipa nguvu Katiba ya Zanzibar.
Zanzibar kuwa na Serikali yake kamili haimaanishi kuwa tuna nchi kamili wakati bado tuko ndani ya nchi ya Tanzania. Kinachofanyika hapa ni kuwa tutakuwa (labda) na Serikali kamili ndani ya nchi yenye Serikali Kuu. Tujuwe kuwa kuna aina nyingi za Serikali, ukiacha Serikali kuu: kuna Serikali za Mitaa, za Wilaya, Serikali za Mikoa, na Serikali ya Zanzibar. Yanayofanyika huko Wilayani, Mikoani, hata Rais wa Jamhuri anakuwa hajui, mpaka apewe taarifa na wawakilishi wake ambao ndio hao Wakuu wa Wilaya na Mikoa. Hivyo chini ya mfumo huu, Rais wa Zanzibar nae atawajibika hivyohivyo. Zanzibar ambayo imekusanya mikoa 5 itatoa taarifa zake kwa Rais wa Tanzania, badala ya kila mkoa kutoa taarifa zake. Nadhani mtakumbuka juzijuzi kule Dodoma ambapo,baada ya shughuli za mchujo wa Urais wa Zanzibar, Nahoda alitoa ripoti ya utekelezaji wa shughuli za kiuchumi na maendeleo (kwa mikoa mitano ya) Zanzibar kwa kipindi kilichopita. Wenyewe wanaita kanda ya Zanzibar.
Kwa hivyo, mabadiliko haya yatakuwa na maana, na nguvu kisheria IKIWA tu pia Katiba (mama) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nayo itafanyiwa marekebisho, ili kuridhia, marekebisho ya Katiba ya Zanzibar; vyenginevyo ni yaleyale ya kuwa Zanzibar si nchi.
Kisheria, Katiba ya Zanzibar haitakiwa KUPINGANA na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, chini ya mfumo huu Muungano tuliokuwa nao leo.
Ahlan wasahlan waungwana,inshallah mungu yupamoja nasi kwa wakati huu kwani kila kkitu kinataka subra, ama kwa mie naona kama wazanzibari wataukubali ka dhati uzanzibari wao baasi hakuna shaka huu ndio waati muwafaka wa mapinduz baridi, mambo ya vitisho na kupigana na kupoteza roho yalishapita.
Mungu ibariki zanzibar na watu wake.
MLUX.
salaam
Kama nilivyosema awali wasi wasi wangu uko hapa aliposema:
Aidha, marekebisho hayo ya katiba yanampa uwezo Rais wa Zanzibar kuteua makamu wawili wa rais, akiwamo makamu wa kwanza ambaye atateuliwa baada ya rais kushauriana na chama kilichoshika nafasi ya pili katika kura za rais kwenye Uchaguzi Mkuu.
Rais pia atamteua makamu wa pili wa rais ambaye atakuwa ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Suala sasa huyu makamo wa kwanza kama atakuwa kutoka cha upinzani atakuwa na majukumu gani ndani ya serikali hiooooo…..mbona hayajaanishwa au ni BOYA hilooooo?
Pengine ufahamu wangu mdogo hebu nifahamisheni.Kweli tuna haraka na mabadiliko lakini tuwe makini na yanayotenda hivi leo huko nyumbani kama alivyosema profesa Shivji.
Yetu masikio.
Waambileeeeeee.
Sikabona na wenzake tulieni mambo mazuri hayati haraka, tuendeni ado ado tutafika. Huezi ukajitoa kwenye miba kwa papara utajiumiza, muungano ni sawa na senyenge kwetu imetuzonga lazima tuipinzuwe taratiibu, la ukiifanyia haraka basi itakutoa damu.
Na hapo unaposema Katiba ya muungano ndugu yangu kama unasubiri alie juu ashuke basi msubiri, katiba ya zanzibar ikifanyiwa marekebisho basi ndio unailazimisha na ya muungano ijifanyie updates ya Article zake. Unajuwa Zanzibar ilipoanzisha sheria ya vyuo vikuu Tanganyika walikuja juu na wakasema ni sheria haramu, leo hii tuko wapi Mashaallah tunavyo vitatu na watu tayari wameshafikia PHD na walianzia degree kupitia vyuo hivyo hivyo vilivyoitwa haramu.
Kumbukeni maneno ya Hashim yule mfanya Biahara tuliekuwa tukimwita majazba alisema yeye anauhakika Zanzibar ni nchi kwa sababu leo ukivunjika tu Zanzibar iko kamili lakini Tanganyika itabidi ianzishwe upya alif bee. Itawabidi waandae katiba yao, jeshi lipanguliwe, mahakama ya rufaa ipanguliwe, Bunge na kila kitu. Ndipo ukaambiwa Ngoma ikipigwa Zanzibar watu wa Afrika ya kati na kusini ndio wachezaji. Sasa mara hii ngoma tunaanza kuidunda dunda na kuipasha moto na wachezaji watakuwa Watanganyika.
tutaona hapo watakapofika dodoma.wacheni wajufurahishe.hatufurukuti wala nini jiti limezama na halitoki.
Hatua si mbaya na inaridhisha sanaaaaaaaaaaa. HAtua kumi mbele za mabadiliko Zanzibar.
Mzizi mwengine uchimbwe kwenye Muungano ambapo Zanzibar itahitaji kurejeshewa Hadhi ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais(Muungano) na Makusanyo ya Kodi za Zanzibar bila ya kuwashjirikisha Bara
Nawashukuru wote waliotoa maoni yao.
Kwa maoni yangu kwanza ningependa kunukuu maelezo ya mtoa maada aliposema kua.
Marekebisho hayo ya 10 ya Katiba ya Zanzibar iwapo yatapitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi yatamaliza msuguano uliokuwa umejitokeza kuhusu nafasi ya Zanzibar katika Jamhuri ya Muungano, baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kudai kuwa “Zanzibar sio nchi”.
Hata hivyo, baadaye Rais Jakaya Kikwete akitoa ufafanuzi wa suala hilo alisema Zanzibar ni nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano, lakini “Zanzibar sio nchi nje ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyo Tanganyika. ”???
Sasa mnaona mziki huo! sasa still mpaka leo najiuliza kwa nini muheshimiwa kikwete akasema Tanganyika ni nnchi wakati jina la tanganyika wameliua wao wenyewe huko bara?! wakati Wazanzibari mpaka leo wanatumia Zanzibar na hawakuliua jina hilo mpaka leo?
Kwa nini zanzibar isiwe nnchi kimataifa kama ilivyo Tanganyika kama alivyotamka muheshimiwa kikwete?
Pili Tanganyika iliungana na nnchi gani ikapatikana Tanzania kama zanzibar sio nnchi?
Mwisho namalizia kusema ili kuondosha mzizi wa fitina katika visiwa vya zanzibar ni lazima narudia tena ni lazima panga pangua vyovyote watakavyofanya serikali ya mapinduzi Zanzibar Wafanye kura ya maoni tena kama walivyofanya juzi ya kuunda serikali ya umoja kitaifa.
Kuulizwa wazanzibari kua wanautaka muungano au hawautaki tena? hilo ndio suluhisho na ndio demokrasia ya kuukata mzizi wa fitina katika visiwa vya zanzibar.
Nawasilisha.
A/alaikum
Natoa shukurani kwa wachangiaji kwa mawazo yenu mazuri kwa mvuto tufati,na hii ndio challenge na ndio itakayoleta jibu kamili.
BUTIAMA
Butiama nakuunga mkono kwa point chache ulizo ongea( NCHI LAZIMA IWE NA WIZARA YA MAMBO YA NNJE ,MAMBO YA NDANI , ULINZI ,MUWAKILISHI WA UMOJA WA MATAIFA ,PAMOJA NA MABALOZI WAKE KATIKA NCHI ) KWA KUENGEZEA (PASSPORT) VIKOSI VYA JESHI LA ULINZI VYA ZANZIBAR
NANUKUU KWA KAULI YA KIKWETE
Rais Jakaya Kikwete akitoa ufafanuzi wa suala hilo alisema Zanzibar ni nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano, lakini “Zanzibar si nchi nje ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyo kwa Tanganyika.
NACHANGIA
Nanza kwa butiama,zanzibar iwe kama zanzibar ni nchi lazima vitu ambavyo alivyongea butiama na mimi pia nimeongezea,marekebisho ya katika hayaweka kuwa zanzibar tayari imeshakuwa nchi,na kama hapo nilipoo nukuu kwa maneno ya kikwete hapo juu soma,nchi mpaka iwe nchi lazima itambulike kimataifa ndugu zangu,leo kikwete anasema kuwa nje ya tanzania sio nchi vipi ? lakini pia kiupande fulani naweza kusema ni nchi kutokana zanzibar itabakia kuwa jina tu nchi kwani tanganyika imepotea,lakini kimataifa sisi hatutambuliki kuwa ni nchi,wewe ni mtanzania so mzanzibar … tumeelewana hapo. sasa katika ya zanzibar lazima ifanyiwe marekebisho makubwa sana,ili iweze kuleta picha ya zanzibar kama nchi na hiyo katiba ifanyiwe kazi na itimizwe.
Pia ikifanyika marekebisho ya katiba kwa vipengele ambavyo vipo juu,alivyotoa butiama na mimi nikaoengezea,na vikafanyiwa kazi,naamini kuwa tanzibar imeshakuwa nchi,na katika ya tangangika itajirekebisha wenyewe,kwa nini tayari wao wameshakwenda michomo,mana washajifunga wao hii senyenge wakati tushajinasua kidogo kidogo kama alivyo sema mmoja ya wachangiaji kuwa tusiwe na papara tuko katika senyenge lazima ujinasue kidogo dogo,usijitoe ngozi. nafikiri mumenielewa mpaka hapa
MIMI NIMEIANGALIA MADA KUU ILIYOWASILISHWA, NA NIMETAMANI KUSEMA MANENO MAFUPI TU, UKIWA MVUVI WA SAMAKI KWA MISHIPI, NA CHOMBO CHAKO NI KIDOGO AU HAFIFU, SAMAKI AKIWA NI MKUBWA ALIENASA, UKIJARIBU KUMVUTA KWA VISHINDO UTAMKOSA SAMAKI, CHOMBO CHAKO ATAKIZAMISHA NA PENGINE NA HATA WEWE MWENYEWE KUKUZAMISHA NA KUWA MWISHO WA HADITHI KABISA. ZNZ NI NDOGO, WATU WAKE KIDOGO, DOLA YAKE NI NDOGO, INAKOTOKA IMECHOKA KWA MISUKO SUKO YA MATEKE YA KASORO HIZI NA ZILE ZA MUUNGANO AMBAZO ZIMEPELEKEA MISUGUANO ISIYOKWISHA, KAMA TUTAENDA KWA VISHINDO, TULIME LEO HALAFU TUTARAJIE KUVUNA LEO NA KULA LEO LEO, TUTAKOSA YOTE, WACHA TUENDE KWA HATUA, KAMA AMBAVYO KWA MVUVI INABIDI ATUMIE TECHNICS , BUSARA NA KUMPURUZIA SAMAKI WAKE ILI KUMVUNJA NGUVUNA HATIMAE AFANIKIWE LENGO LAKE.
sifahamu kitu yaani hapa ZNZ watu wote ni makamo wa kwanza makamo wa pili watatu kwanza ZNZ watu wenyewe wako wapi hata manafasi haya yakupenyezana2 hivi hapa mimi naona si mabadiliko yakutafuta maendeleo bali niku tafutiana nafasi 2 za ulaji2 tu watu milioni mamakamo mawaziri manaibu makatibu wakurugenzi ofwee jamani mnasema au mna semewa mimi naona ziro kuuubwa lenye macho na masikio lakini twende mbele mtaona asanteni sana
aslm alkum nimefurahi sana kusikia zanzibar yetu imezaliwa upya inshallah mungu atatusaidia tushachoka kukaa ugenini tunataka kurudi nyumbani
@ghalib
kwa kweli hueleweki wala hufahamiki maneno yako yote siku zote naona yanajizonga na hiyo senyenge. hatukufahamu kabisaaaaa!
kimewaka
Nimemaanisha kuwa tumemezwa na tanzania,sasa vipi tutajinasua,tumemezwa kijeshi la tanzania,vipi tutajinasua,zanzibar haina kauli,vipi itakuwa na kauli,ndoko kuzongwa na senyenye huku,lazima tuende kwa taratibu,ili tuweze kujizongoa,mambo yanakwenda hatua kwa hatua.