Habari

Kwa wageni sheria sio msumeno z’bar

KKTumeambiwa mara nyingi na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kutakiwa tuamini kuwa watu wote visiwani wako sawa na hakuna aliye juu wala chini ya Katiba na sheria za nchi.

Lakini wakati baadhi ya watu wa Zanzibar wakijitahidi kuamini kauli hiyo, wanapata tabu na kujenga hisia kuwa hicho kinachoelezwa si kingine isipokuwa danganya toto. Hii inatokana na wanayoyaona au kuyasikia kuwa tofauti na kinachohubiriwa.

Kwa unyonge kama yatima ambao wamekosa walezi, wamekuwa wanaona watu waliojifunika nyuso zao ‘wakiipiga’ migongo ya wenzao kama ngoma na walipolalamika wakaambiwa waachanane na watu hao kwa kuwa ni kundi la wahuni.

Baada ya malalamiko mengi, yakiwamo ya vyombo vya habari juu ya kundi hili lililopewa jina la “Mazombi”, tuliambiwa suala hilo litachunguzwa na Serikali.

Hata hivyo, hadi leo hatujapewa taarifa ya uchunguzi wala kusikia mmoja wa watu waliosababisha maumivu, majeraha na wengine kuwa vilema, wakikamatwa wala kuwajibishwa kisheria.

Sasa tunashuhudia mengine mapya. Nayo ni ya kuwapo kundi la watu waliopewa kibali cha kuifunika sheria. Kundi hilo ni la wale wanaoonekana kuwa mabwana na mabibi wakubwa ambao ni wawekezaji wa kigeni.

Wakati wavuvi wadogo wa Zanzibar wanakamatwa kila siku, kufunguliwa mashtaka na kutozwa faini au kupelekea jela kwa kwenda kinyume na sheria za uvuvi, baadhi ya wageni wanazivunja sheria hizo kwa raha zao.

Taarifa za karibuni zilizothibitishwa na Jeshi la Polisi ni kwamba baadhi ya hawa wanaoitwa wawekezaji wanapewa vibali vya kufanya uvuvi au michezo ya baharini kwa kutumia bunduki na mishale kuvua samaki, wakati mambo hayo yakifanywa na wazalendo huwa nongwa na hao wanaofanya hivyo kulaaniwa kwamba wanaharibu mazingira ya bahari.

Kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na kupitishwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar (BLW) ya mwaka 2010 uvuvi wa aina hiyo ni haramu na haukubaliki katika bahari inayozunguka visiwa vya Unguja na Pemba.

Lengo la sheria hiyo, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa wakati ilipotungwa ni kulinda mazao ya baharini na uhifadhi wa mazingira ili kupambana na uvuvi haramu visiwani ambao umeathiri kwa kiwango kikubwa mazalia ya samaki, yaani matumbawe.

Tangu kutungwa kwa sheria hiyo ambayo inakataza matumizi ya nyavu zenye matundu madogo zinazonasa samaki wachanga, pamekuwapo na hali inayovutia kwa vile imepunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la uvuvi haramu uliokuwa ukifanyika katika maeneo mengi ya mwambao wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Wakati wazalendo wameitikia wito wa kulinda mazao ya bahari, baadhi ya wageni wanaachiwa kufanya uchafuzi watakavyo kama vile sheria za nchi haziwahusu, yaani kama vile hawa wageni wamekuja kuwekeza kuharibu mali ya bahari ya visiwa vyetu.

Mgeni anaswa, aachiwa

Utafiti ulofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Sayansi za Baharini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (IMS) ulibainisha wazi kwamba uvuvi haramu uliharibu mazalia ya samaki na kupendekeza kuchukuliwa hatua madhubuti ya kuzuia uharibifu zaidi.

Hivi karibuni Jeshi la Polisi Kaskazini Unguja lilimkamata mwekezaji akiwa na bunduki tatu na mishale saba baada ya kupekuliwa nyumbani kwake.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hasina Ramadhani alisema walishindwa kumfikisha mahakamani baada ya kugundua amepewa kibali na Idara ya Uvuvi Zanzibar kutumia zana hizo kuvua kisheria.

Hiyo ina maana kwamba, mwekezaji huyo alipewa kibali cha kuvunja Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2010.

Suala hapa ni kwa nini huyo mwekezaji alipewa kibali hicho wakati sheria ya uvuvi inakataza uvuvi wa bunduki, mishale au vifaa vya umeme?

Hilo siyo jambo jepesi na linamfanya mzalendo ahisi kwamba sheria za Zanzibar ni kwa raia na siyo wageni na kama ni hivyo, kwa nini sheria isiweke wazi kwamba ilikuwa imetungwa kwa raia tu na siyo wageni pia?

Hapa wapo watu wanaopaswa kuwajibika kisheria kwa kuvuja sheria. Hao waliotoa vibali hivyo lazima waeleze wapi walipata mamlaka ya kufanya hivyo.

Kuwanyamazia watu waliotoa kibali hicho ni hatari kwa sababu mtindo huo utaendelea na matokeo yake kutakuwa hakuna haja ya kutungwa sheria za uhifadhi wa bahari na mazalia ya samaki.

Mbaya zaidi ni kujenga dhana kwamba wageni wana haki ya kufanya watakavyo Zanzibar kwa kisingizio cha kuwa wao ni wawekezaji. Siyo ajabu leo wanaachiwa kuharibu bahari yetu na kesho wakapewa vibali vya kuchafua misitu na kuua wanyama watakavyo.

Mwenendo huu wa kuwa na kundi la watu wenye haki ya kuvunja sheria na wengine kulazimishwa kutii ni wa hatari na hauwezi kukubalika katika nchi inayojigamba kuwa na utawala wa haki na sheria.

Mwenendo huo ni lazima ukomeshwe haraka, vinginevyo Zanzibar itakuja kujutia kwa kuruhusu wageni wanaovaa joho la uwekezaji kutuharibia rasilimali za majini na nchi kavu.

Sheria lazima iachwe kwa mapana na marefu kuchukua mkondo wake kwa raia na wageni na pasiwepo kisingizio cha aina yoyote ile kitachowapa baadhi ya watu haki ya kuwa juu ya sheria ya nchi.

Ni kweli kwamba umaskini ndiyo unasababisha kushawishi wageni kuja kuwekeza hapa nchini, lakini tunachotaka ni kusaidiwa kuondokana nao na siyo kututoa kwenye umaskini na kutupeleka katika ufukara.

Watanzania wa Bara na Visiwani tunapaswa kujifunza kwa yaliyowakuta wenzetu katika nchi nyingi za Kiafrika, zikiwamo za majirani zetu walivyoathirika kwa kuwakumbatia wawekazaji waharibifu na kuwaruhusu kufanya watakavyo.

Nchi hizo hivi leo zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa samaki, wanyama na ndege wengi kutoweka misituni. Tunasema tunawakaribisha wawekezaji ili kupata maendeleo ya kiuchumi na siyo kutuongezea umaskini. Tuzisimamie vyema sheria zetu na zitumike kwa watu wote – raia na wageni na wale wanaozivunja lazima wawajibishwe kisheria.

Tukumbuke usemi uliojaa hekima wa wahenga kuwa, “huruma hailei mwana,” na kuelewa kwamba huruma kwa wanaovuja sheria zetu itatuponza leo na baadaye.

Share: