Lipumba amwandikia JK akitaka mdahalo
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba amemwandikia barua mgombea urais wa Chama Chama Mapinduzi, Rais Jakaya Kikwete akimtaka wakae kwenye mdahalo ili kuwaeleza Watanzania sera na mikakati watakayoisimamia watakapopewa ridhaa ya kuiongoza nchi. Katika barua yenye kumb; CUF/DSM/IKL/001/2010 ya Julai 12 mwaka huu aliyomwandikia Rais Kikwete na kusambazwa katika vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Prof Lipumba alieleza kuwa mbali na kampeni zitakazojikita katika ujenzi wa hoja, kunahitajika midahalo mitatu kati ya wagombea hao. Barua hiyo ni msisitizo wa Profesa Lipumba la kutaka mdahalo huo, baada ya kutoa pendekeo hilo wiki kadhaa zilizopita, lakini Rais Kikwete akakingia kifua na Naibu Mkuu wa Kitengo cha propaganda cha CCM, Tambwe Hiza, kuwa hakuna haja ya mdahalo kwa kura Rais Kikwete alishamshinda Profesa Lipumba kwa mbali. Vile vile barua hiyo itakuwa ni kipimo cha utayari wa Rais Kikwete kushiriki mdahalo huo wakati anawania kipindi cha pili na cha mwisho cha urais wake, baada ya kuukwepa mwaka 2005 wakati anawania kipindi cha kwanza. Kiongozi huyo wa CUF alisema mdahali huo utawafanya Watanzania wajue kudai na kupata haki sawa kwa wote, kuhakikisha raslimali na mali ya asili ya Tanzania inatumiwa kwa uadilifu ili kukuza uchumi utakaoongeza ajira na kutokomeza umaskini. Kwa mujibu wa Profesa lipumba mdahalo huo utalenga maeneo matatu ambayo ni sera na mikakati ya kukuza uchumi na kutokomeza umaskini; kuboresha huduma za jamii, utawala bora na ujenzi wa maadili mema ya taifa; na uhusiano wa nchi za nje na ulinzi na usalama wa nchi. “Haya ni mapendekezo ya awali ili kufanikisha midahalo hii, ni vyema vyama vya waandishi wa habari, jumuiya za dini, wasomi na watafiti na asasi nyingine zisizo za kiserikali zipewe jukumu la kuratibu na kuandaa midahalo. “Timu zetu za kampeni zaweza kukutana na kukubaliana asasi au watu watakaoandaa midahalo hiyo,” alieleza sehemu ya barua hiyo. Alieleza kuwa midahalo hiyo itajenga uhusiano mwema baina ya vyama na wagombea, kukomaza demokrasia nchini na kuwapa wapiga kura fursa ya kuwapima wagombea wa urais. “Katika kuhakikisha tunajenga utamaduni mzuri wa demokrasia katika nchi yetu itakayowapa fursa wagombea wa urais napendekeza tuwe na midahalo mitatu. “Ni matumaini yangu utaafiki pendekezo la midahalo ya kampeni na kulipa suala hili kipaumbele ili maandalizi yafanyike mapema,” alisema Prof Lipumba. Katika barua hiyo, Prof Lipumba alimpongeza Rais Kikwete kwa kuchaguliwa na Chama Chama Mapinduzi (CCM) kugombea kiti hicho kwa mara nyingine.
Source: Majira






One Comment on "Lipumba amwandikia JK akitaka mdahalo"
Kwa kibiri cha chama cha mapinduzi Kikwete hatokuwa tayari kufanya mdahalo na CUF kwa kuhisi atajidhalilisha !!