Habari

MAALIM SEIF: KAMA JPM HATAKI MIKUTANO ABADILISHE SHERIA

By Bakari Kiango, Mwananchi

Zanzibar. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Rais John Magufuli amekwenda nje ya madaraka yake kutokana na kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano hadi 2020.

Maalim Seif amesema kama Rais anataka kuiendesha nchi bila ya mikutano ya hadhara na maandamano, apeleke muswada bungeni ili Sheria ya Vyama vya Siasa ibadilishwe.

Maalim Seif, ambaye alikuwa na mahojiano na Mwananchi mjini Unguja, alikuwa akizungumzia tamko la Rais Magufuli la kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa na maandamano kwa maelezo kuwa anataka watu wafanye kazi na hivyo shughuli za siasa zitafanyika mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu.

“Kwa kifupi naweza kusema ame-exceed his powers (amevuka mipaka ya madaraka yake),” alisema Maalim Seif katika mahojiano hayo yaliyofanyika ofisi za makao makuu ya CUF Mtendeni, Unguja.

“Hivi sasa sheria inasema ni haki kwa kila chama kufanya mikutano ya hadhara na maandamano. Rais Magufuli alikula kiapo kuwa atailinda sheria na Katiba ya nchi. Sasa kwa jambo hilo, with all respect (kwa heshima zote), amevunja sheria.

“Kama anataka, apeleke muswada bungeni wa kubadilisha sheria ili aongoze kwa kufuata sheria.”

Hata hivyo, hata Sheria ya Vyama vya Siasa ikibadilishwa na kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa, itakuwa pia ikikiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo inaruhusu mambo hayo.

“Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo,” inasema ibara ya 20 ya Katiba.

Rais alitoa tamko hilo wakati akipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu.

Tangu wakati huo, Jeshi la Polisi halijawahi kuzuia maandamano na mikutano kwa kuwa inakiuka amri ya Rais, bali kwa maelezo kuwa inaviashiria vya uvunjifu wa amani, kushawishi wananchi wasitii serikali yao na wakati fulani ilisema imezuia kutokana na ugonjwa wa ajabu kuibuka mkoani Dodoma na kuua watu sita.

Akizungumzia suala la Katiba Mpya, Maalim Seif alisema endapo angepata nafasi ya kumshauri Rais Magufuli kuwa kama anataka kufufua Katiba, basi arudi katika maoni yaliyotolewa na wananchi.

Maalim Seif alisema Rais Magufuli ameshasema kuwa suala la Katiba mpya halikuwa ajenda yake wakati wa kampeni, lakini akiona lina umuhimu arudi katika Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, badala ya kuendelea na Katiba Inayopendekezwa.

Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitumia fedha nyingi kukusanya maoni ya wananchi na ndiyo Rasimu ya Katiba ndio maoni halali ya Watanzania wengi.

Pia Maalim Seif alitoa tathmini ya mwaka mmoja ambazo Zanzibar imeendeshwa bila ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), akisema hali imekuwa ya mateso kwa wananchi wa visiwa hivyo.

SUK ilikuwa ni matokeo ya muafaka baina ya CCM na CUF baada ya chaguzi mbili za nyuma kutawaliwa na vurugu na kutoaminiana na kwa maridhiano hayo, Maalim Seif alikuwa makamu wa kwanza wa rais huku CUF ikitoa pia mawaziri.

Maalim Seif amesema haoni kilichofanyika tangu Dk Ali Mohamed Shein arejee madarakani zaidi ya wananchi kudhalilika.

Alidai uchumi wa Zanzibar umeporomoka na Serikali haina mapato, kiasi cha wafanyabiashara kukopwa fedha kwa ajili ya kuwalipa mishahara watumishi wa Serikali.

“Hali hii imewachosha hata wafanyakazi ambao baadhi yao wanajikuta wanakwenda kazini, lakini hawafanyi shughuli yoyote kwa sababu fedha za matumizi hakuna,” alisema Maalim Seif.

Pia alisema haoni sababu ya Serikali kuwahamisha wafanyabiashara wadogo, wanaojulikana kwa jina la Juakali ambao hufanyia shughuli zao Darajani, kwa kisingizio kuwa eneo hilo limepata mwekezaji.

Alisema hadi sasa mwekezaji huyo hajafanya lolote.

Alifafanua familia za Kiafrika za wajasirimali kama Juakali, huwa na watu watano hadi sita wanaowategemea, hivyo wakifukuzwa watakosa pa kwenda na badala yake watakuwa wahalifu.

“Kwa tathimini yangu Serikali ya Dk Shein imeshindwa tofauti na ilivyokuwa chini ya SUK. Pamoja na kwamba kulikuwa na kasoro zake kwa sababu jambo hilo lilikuwa jipya, lakini mambo yalikwenda,” alisema.

Alisema kipindi cha SUK kulikuwa na umoja uliosababisha wananchi kusahau tofauti zao za kisiasa na walishirikiana kwenye shughuli za maendeleo bila ubaguzi wa aina yoyote.

Maalim Seif alisema anasikitika kuona umoja huo ukivunjika na kusababisha mgawanyo mkubwa, hasa kwa wafuasi wa CCM na CUF, akidai kuwa ajira zinatolewa kwa upendeleo wa vyama.

Alibainisha kuwa hali hiyo si nzuri kwa masilahi ya Zanzibar na itasababisha kuwapo kwa matabaka ya wenye nacho na wasiokuwa nacho, jambo ambalo ni baya zaidi.

“Tumerudi nyuma badala ya kwenda mbele. Hawa wanaoonewa watavumilia, lakini mwisho wa siku watasema basi,” alieleza.

Maalim Seif alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa ina umuhimu mkubwa kwa sababu inaleta uimara katika nchi na kuwavutia wawekezaji

“Kwa mazingira ya sasa, sioni kama wawekezaji kama watakuja. Mwaka jana chini ya SUK kulikuwa na miradi mingi na tuliisimamia tukishirikiana na wananchi tofauti na sasa,” alisema.

Mbali na hilo, Maalim Seif alisema chini ya SUK wafadhili walikuwa wanajiamini kuisadia Zanzibar kwa kuwa ilikuwa na Serikali inayojali masilahi wananchi hivyo kujiona wana wajibu wa kutoa msaada.

Alipoulizwa kama atakuwa tayari kama SUK itarudishwa, alijibu:“Watanirudisha mimi kwa misingi gani? Kwa sababu Katiba ya Zanzibar ipo very clear (imejieleza vizuri). Mgombea wa chama kitakachopata kura nyingi ndiye rais wa Zanzibar,” alisema.

“Chama kinachofuata kwa wingi wa kura ndicho kitakachotoa makamu pili. Uchaguzi wa mwaka jana nilishinda dhidi Dk Shein,” alisema Maalim Seif.

Matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar na wawakilishi yalifutwa na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha Oktoba 28, siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa mbio za urais. Jambo lililosababisha CUF kususia uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu.
Image may contain: 1 person, sitting and flower

Tagsslider
Share: