Habari

Maninja wa Lipumba wavamia mkutano wa CUF Dar es Salaam

Pichani: Mtu aliyekumbana na nguvu ya umma miongoni mwa watu wanne waliyovamia mkutano wa ndani wa CUF na kuwajeruhi viongozi wake na waandishi wa habari jana katika Hoteli ya Vina Mburahati, Dar es Salaam.

Na Mary Geofrey – Nipashe Jumapili
23 Aprili 2017

WATU wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) – (anayetambuli na msajili wa vyama vya siasa), Ibrahim Lipumba jana walivamia mkutano wa ndani wa CUF na kuwapiga na kuwajeruhi viongozi wa chama hicho na waandishi wa habari.

Sakata hilo lilitokea katika hoteli ya Vina iliyopo Mburahati, Dar es Salaam wakati viongozi wa CUF Wilaya ya Kinondoni walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu mgogoro unaoendelea ndani ya chama kati ya pande hizo mbili.

Mwezi uliopita, Lipumba alitangaza rasmi kumwondoa Maalim Seif katika wadhifa wake wa Katibu Mkuu kwa madai ya kutohudhuria vikao muhimu vya chama.

Aidha, Lipumba alitangaza nafasi hiyo kuchukuliwa na Magdalena Sakaya, ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Tanzania Bara.

PICHA ILIVYOANZA
Mnamo majira ya saa 5:30 asubuhi wakati Mwenyekiti wa CUF Kinondoni, Juma Nkumbi na viongozi wengine wa wilaya hiyo, wakiwaeleza waandishi wa habari kile walichowaitia, ghafla watu wanne waliokuwa wameziba nyuso zao kwa kuvaa soksi maalum za usoni, walivamia na kuanza kushambulia viongozi waliokuwa meza kuu kwa kuwapiga kwa mikanda na marungu.

Maninja’ hao walifika kwenye hoteli hiyo wakiwa na magari matatu aina ya Toyota Land Cruiser Prado yenye bendera za CUF na kuingia mapokezi na kujitambulisha kama wafuasi wa chama hicho na kuuliza eneo ambalo mkutano unafanyika.

Watu hao walifika mapokezi wakiwa wamevaa nguo za kiraia jambo lililowafanya wahudumu wasiwatambue kama ni wahalifu, hasa kutokana na magari yao kuwa na bendera za chama hicho.

Baada ya kuelekezwa wakati wakipandisha ngazi kwenda ghorofa ya nne, ndiko wanakodaiwa walivaa soksi maalum ili kuficha nyuso zao.

WALIVYOTINGA UKUMBINI
Wakati mkutano baina ya viongozi wa CUF wilaya ya Kinondoni na waandishi wa habari ukiendelea, ‘maninja’ hao wanne waliingia wakiwa wameshikilia mapanga, fimbo, mikanda na bastola na kwenda moja kwa moja meza kuu na kuanza kuwashambulia viongozi hao.

Taharuki hiyo iliwafanya viongozi waliokuwa meza kuu kusimama na kupambana nao kwa kuzuia kudhuriwa zaidi na silaha walizokuwa wameshika wenzao.

Katika hali isiyotarajiwa, mmoja wa ‘maninja’ hao alitoa bastola aliyokuwa ameihifadhi maungoni na kuinyooshea upande waliokuwa wamekaa waandishi wa habari ikiwa ishara ya kuwatishia kufanya kazi yao.

Kitendo hicho kilizua taharuki kwa waandishi na kusababisha baadhi yao kuumia kutokana na kukimbia bila tahadhari.

Kutokana na mazingira ya ukumbi huo kuwa mdogo na wenye mlango mmoja wa kutokea nje ya jengo hilo, baadhi ya waandishi walikimbilia mlango wa kwenda varanda ya ukumbi na kusababisha mmoja wao kutaka kujirusha, kitendo ambacho kiliwasababishia wenzake, kumvuta na kumuokoa.

Wakati wajumbe wa mkutano huo, wanaomuunga mkono Maalim Seif, wakiendelea kupambana, ‘maninja’ hao waliwashambulia kwa kuwapiga mateke na makofi huku, baadhi ya waandishi ambao baadaye walifanikiwa kutoka nje ya ukumbi kwa kupitia mlango mkuu.

WAANDISHI WAOKOA
Waandishi waliokuwa kwenye varanda ya ukumbi huo, walipiga kelele ambazo ziliwashtua watu waliokuwa chini ya jengo, ambao walijaa kutaka kujua nini kimetokea.

Baada ya kelele hizo, ndipo maninja hao walitoka na silaha zao na kushuka hadi eneo la mapokezi ambako huko walikutana na msimamizi wa hoteli, wahudumu na walinzi ambao walikuwa wamefunga mlango ili kuwazuia.

Kutokana na kitendo hicho ‘maninja’ hao waliwashambulia na kuwajeruhi maeneo mbalimbali ya mwili na kufanikiwa kufungua mlango na kutoka ndani ya hoteli.

WANANCHI WAWAKOMESHA
Baada ya kutoka kwenye jengo hilo walikutana na wananchi ambao walikuwa tayari wamejiandaa kuwakabili na wakati wakikimbilia kwenye magari waliyokuwa wamefika nayo hapo, wananchi waliwashambulia kwa mawe na kuvunja vioo vyote vya magari hayo.

Vipigo vya mawe kutoka kwa wananchi vilisababisha ‘maninja’ wawili kati ya hao walioingia ukumbini kuachwa na magari kukimbizwa na wananchi na wafuasi wa CUF na kufanikiwa kumkamata mmoja katika mtaa wa Mburahati Motomoto.

Mtu huyo alishambuliwa na wananchi na kujeruhiwa kwa kukatwa kwenye kisigino cha mguu wa kulia.

Akihojiwa na wananchi eneo la tukio, mtu huyo alidai kuwa si mfuasi wa CUF isipokuwa alishawishiwa na wenzake kwenda kufanya kazi hiyo ya uvamizi. “Jamani si mimi jamani nisaidieni mimi nimebebwa tu.

“Wamenaimbia nije nifanye hiyo kazi ila sijui chochote…Siyo mimi jamani, siyo mimi mmenikata mguu,” ilisikika sauti ya kijana huyo aliyekuwa katikati ya kundi la wananchi akijitetea.

Mmoja wa hudumu wa hoteli hiyo, alieleza kuwa hakufahamu kama ni wahalifu kutokana na kujitambulisha kuwa ni wanachama wa CUF.

KILICHOPONZA VURUGU
Kabla ya kuanza kwa vurugu hizo, Nkumbi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa lengo la mkutano huo ni kuzungumzia tofauti zilizopo kati ya wafuasi wa Maalim Seif na Lipumba.

Aidha, alieleza kutokuutambua uongozi wa CUF wilaya ya Ubungo, ambao unamuunga mkono Lipumba kwa madai kuwa si kiongozi wa chama na hakuna kikao halali kilichowateua na hawatatoa ushirikiano kwa jambo lolote litakalofanyika.

Pia, walisema wanaunga mkono tamko lililotolewa na wanachama wa matawi 20 ya Mkoa wa Dar es Salaam la kumkataa Lipumba na kundi lake waondoke kwenye Ofisi za CUF za Buguruni.

Share: