Anaswa akiwanga kweupee!

Written by  //  04/12/2009  //  Mengineyo  //  Zima maoni

  • Eti kavaa kofia chini mtupu!
  • Polisi wamdaka

Mtu mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mara baada ya kudaiwa kukutwa akiwanga kwenye choo cha shule moja, huku akiwa amevalia kofia kichwani ilhali mwilini akiwa mtupu kama alivyozaliwa.
Mtu huyo ambaye alinaswa hivi karibuni katika Kijiji cha Kibasuka mkoani humo na kunusurika kuuawa na wananchi wenye hasira, ametambuliwa kwa jina la Robert Mzee, mkazi wa kijiji jirani na kile alichonaswa cha Tegeruka Mpango.
Taarifa toka katika eneo la tukio na ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa Maalum wa Kipolisi Tarime – Rorya, Costantine Massawe, zinadai kuwa Mzee alikutwa akifanya vitendo vya kishirikina huku akiwa hana nguo mwilini katika choo cha shule ya msingi ya kijiji hicho cha Kibasuka.
Inadaiwa zaidi kuwa mtuhumiwa huyo wa vitendo vya kishirikina, alidai kufanya hivyo baada ya kuletwa katika kijiji hicho cha Kibasuka na mwalimu mmoja wa shule hiyo, lengo likiwa ni kumuwangia mwalimu mwenzake aliyetajwa kwa jina la Mwalimu Marwa waliye na uhasama naye kwa muda mrefu.
Akizungumza na mwandishi, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Kerimani Nyakiha, amesema Mzee ambaye pia anadai kuwa ni mganga wa kienyeji, alikamatwa akiwa tayari ametumbukiza damu na vichwa kadhaa vya kuku katika matundu mawili ya choo, huku akiwa hana nguo hata moja mwilini na kichwani akiwa amevalia kofia ambayo ni ya Mwalimu Marwa Samson, anayedaiwa kuwa hasimu wa mwalimu aliyemfikisha mchawi huyo shuleni hapo.
Akaeleza zaidi Mwenyekiti Nyakiha kuwa awali, mtuhumiwa alijitetea kuwa alikuwa hapo akifanya kazi aliyotumwa na mwalimu huyo aliyemleta, baada ya kumleta kijijini hapo Novemba 30 mwaka huu, ambayo ni kufanya dawa itakayomdhuru hasimu wake Mwalimu Marwa.
Aidha, Mwenyekiti Nyakiha akasema kuwa hali aliyokutwa nayo mtuhumiwa huyo iliwastua mno, hasa baada ya kumuona akiwa hana nguo mwilini na tena amebeba vitu visivyokuwa vya kawaida na ambavyo vinahusishwa na mambo ya kichawi.
Akasema baada ya kunaswa ‘live’ na kisha wananchi kukusanyika eneo la tukio, watu walitaka kumdhuru kwa kipigo baada ya habari kuenea kuwa alikuwa na viungo vya albino.
“Ukweli ni kwamba hakuwa na viungo vya albino, bali hali halisi aliyokutwa nayo iliwafanya watu wastuke sana na mwishowe ikapendekezwa kuwa apelekwe polisi na si kujichukulia hatua za kisheria mikononi mwao,” akasema Mwenyekiti huyo.
Akaeleza zaidi kuwa Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, Otieno Onyango, alipiga simu kituo cha polisi Nyamwaga na askari ambao nao walifika mara moja na kumnusuru mtuhumiwa kwa kumdaka na kisha kuondoka naye.
Walimu waliodaiwa kutajwa katika tukio hilo hawakuweza kupatikana na mwandishi, lakini
Kamanda Costantine Masawe, amekiri kukamatwa kwa mtu huyo aliyekutwa bila nguo na kueleza kwamba wanaendelea kumhoji.
Aidha, Kamanda Masawe amesema kuwa mtuhumiwa hakukutwa na viungo vya albino na kwa maelezo ya mtuhumiwa mwenyewe, alidai kuwa alikwenda shuleni hapo kumtibia mwenyeji wake (Jina tunalihifadhi).
Hata hivyo, akasema kuwa walimhoji Mwalimu huyo na kumuachia baadaye huku uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo ukiendelea.

CHANZO: ALASIRI

Comments are closed.