Habari

Mnazimmoja yakosa umeme kwa masaa 8 Lifti yakwama

Dhamir Ramz

Kufuatia tukio la kuzimwa umeme mchana wa leo kwa karibu masaa manne, katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, mama mmoja alinasa kwenye lift ya taasisi hiyo muhimu ya afya kwa muda mrefu hali iliyopelekea kupoteza fahamu kwa kukosa hewa (suffocation) hadi muda aliotolewa. Kama angechelewa kutolewa basi angepoteza maisha yake kwa kukosa hewa.

Maswali ambayo najiuliza ni haya:
1. Kwamba hospitali kuu ya Zanzibar inakosaje huduma ya umeme wa dharura (back-up power supply) wakati ni sehemu ya kuokoa maisha ya watu?

2. Kama hiyo huduma ipo, tuseme jenereta la dharura, ni nini kimesibu hadi kukakosekana umeme wa dharura ili kuepusha maafa?

3. Wagonjwa ambao wamelazwa ICU, nini kimewasibu kwa kadhia hii?

Tunakazania kuweka jenerators kwenye majumba yetu, lakini sehemu muhimu kama hospitali huduma hiyo hamna. Muliopewa dhamana ya kuendesha taasisi hii, Mungu anakuoneni. Yaliyompata mama huyu na wengine, iko siku yatawafika walio wenu. Acheni ubinafsi na fanyeni kazi mtimize wajibu wenu. Kama hamuwezi ONDOKENI wapisheni wenye uchungu na uzalendo wa taifa hili. THIS IS TOO MUCH!

Inaendelea: Kadhia ya kuzimwa kwa umeme na kunasa kwa mwanamama katika lift ya hospitali kuu ya Mnazi Mmoja:

Muda mfupi uliopita, nilipokea simu kutoka kwa Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, ambae ni Waziri dhamana wa Wizara ya Afya na nimepewa maelezo yafuatayo kwa ufupi kuhusu tukio la leo:

Kwanza, hakuna jenereta inayotosheleza kupatikana kwa umeme wa dharura kwa hospitali nzima. Iliyopo sasa hivi haitoshelezi, na hutoa umeme wa dharura katika vyumba vya Theatre, Makeniki na Neuro-surgery.

Pili, jenerator iliyopo huwekewa mafundi wa zamu, na muda wote inatakiwa awepo fundi mmoja wa zamu ili kukabiliana na dharura. Wakati umeme unazimwa, fundi aliepangiwa kuwepo hakuonekana katika eneo la kazi, na ilibidi atafutwe fundi mwengine kusaidia zoezi la kurejesha umeme wa dharura. Mfanyakazi huyo atawajibishwa kwa uzembe alioufanya.

Tatu, ni kwamba kwa kawaida shirika la Umeme huwasiliana na Wizara ya Afya kila inapotokea dharura ya kuzimwa kwa umeme, lakini kwa siku ya leo hilo halikufanyika kwa sababu hitilafu imetokea kwenye gridi ya taifa. Hivyo hakukuwa na matayarisho ya kukabiliana na hali hiyo.

Zaidi, ni kwamba Serikali inalifuatilia suala hilo kwa karibu zaidi ikihusisha uongozi wa juu. Hivi karibuni, jenereta ya dharura iliyotolewa kwa hisani ya mfuko wa UNFPA itawasili Zanzibar kwa ajili ya kufungwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.

Binafsi, nitoe pole kwa walioathirika na tukio la leo, na pia nimshukuru Mhe. Mahmoud Thabit Kombo kwa kulitolea ufafanuzi jambo hilo ambalo linamgusa moja kwa moja akiwa kama ni kiongozi dhamana wa taasisi hiyo nyeti.

Tujifunze kutokana na makosa. Na pia tusiwache kukosoa pale panapostahiki.

Ahsanteni sana
Dhamir Ramz

Tagsslider
Share: