mpinga serikali ya umoja afukuzwa kazi
Written by salma // 31/07/2010 // Habari // 2 Comments
RAIS wa Zanzibar Amani Abeid Karume amemtimu kazi mkuu wa wilaya ya kati Ali Hassan Khamis akidaiwa kufanya kampeni chafu dhidi ya kura ya maoni ambayo itafanyika leo visiwani Zanzibar itakayoamua muundo mpya wa serikali ya umoja wa kitaifa.
Taarifa kutoka ikulu zimesema rais karume ametmfukuza kazi mkuu wa wilaya hiyo kwa mujibu wa kifungu namba 53(b) cha sheria ya Zanzibar ya mwaka 1984 kinachompa mamlaka rais kumfukuza mtu yeyote katika serikali yake.
Hadi sasa hakuna sababu zilizotolewa kuhusiana na kufukuzwa kazi kwake lakini kwa mujibu wa tetesi ziliopo ni kwamba hatua ya rais karume imefuatia kauli yake ya juzi aliyoitoa katika hafla ya kuzindua majenereta ya umeme mtoni mjini Zanzibar amabpo alisema kuna baadhi ya viongozi wa serikali wamekuwa wakiwashawishi wananchi kupiga kura ya hapana.
Akisema ni kitendo kibaya kinachofanywa na viongozi hao ambao wamejisahau kwa kueneza sumu mbaya na kuwadanganya na kuwapotosha wananchi katika suala la kura ya maoni jambo ambalo linapaswa kupuuzwa na wapenda amani.
Kwa mujibu wa maelezo ya watu wlaiokuwa karibu na ikulu zinasema kwamba kufutwa kazi kwa khamis kunatokana na msimamo wake kuuliza mswali mengi yenye kejeli juu ya kura ya maoni wakati kamati ya watu sita ya baraza la wawakilishi wanaosimamia kura ya maoni ilipofanya kikao chake katika wilaya yake Dunga mkoa wa kusini unguja.
Katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na masheha na madiwani mkuu wa wilaya hiyo alionesha wasiwasi wake na kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifahuku akitilia mashaka msimamo wa chama chake katika kuunga mkono suala hilo.
mkuu huyo alisema licha ya kuwa ana mashaka makubwa na utekelezaji wa kura ya maoni lakini pia mshaka yake yapo katika uundwa wa serikali ya umoja wa kitaifa kwa kuwa muda uliobaki sasa ni mdogo sana wa kuweza kuelezwa wananchi suala hilo.
Alisema kwa kuwa suala hilo kwake ni geni atashindwa kuliunga mkono na hangependa kuwashawishi wananchi juu ya upigaji wa kura ya ndio ili kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar.
Alisema kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ni sawa na kuyasaliti mapinduzi ya Zanzibar yaliofanyika 1964 ambayo yamewaandosha watawala wakoloni na kuondosha ubaguzi wa hali zote.
Katika mkutano wake rais karume juzi alichukua sehemu kubwa ya hutuba yake kutoa ufafanuzi juu ya dhana na kura ya maoni na kueleza kwamba inayotokana na maridhiano kati yake na maalim seif katibu mkuu wa CUF.
Karume alionekana kukasirishwa na kauli za kuitwa msaliti na akatumia nafasi hiyo kueleza kwamba yeye anayafahamu vyema mapinduzi ya 1964 na malengo yake ya kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa wazanzibari na akakanusha kwamba yeye hawezi kuwa msaliti wa mapinduzi kwa kuwa baba yake ndio aliyeongoza mapinduzi hayo.
“Mnayatumia mapinduzi kwa maslahi yetu na kujinufaisha binafsi mimi ni mwana mapinduzi na nayajua vizuri mapinduzi moja ya mapengo ya mapinduzi ni kuleta usawa kwa wananchi wote bila ya ubaguzi jee hiki tunachokifnaya sisi ni kibaya cha kuleta umoja na amani katika nchi yetu” alisema karume.
Aidha Karume alikerwa na tabia ya baadhi ya watu wanaomuita kwamba yeye ameuza nchi, na kusisitiza kwamba lengo la mapinduzi ya zanzbar ya mwaka 1964 ni kuweka hali za wananchi wote kuwa sawa bila ya ubaguzi na anachokifanya yeye kwa sasa ni kurudisha amani na sio kuuza nchi kwa kuwa wananchi wote ni ndugu.
‘Mimi nawashangaa sana watu wanaopotosha ukweli wa mambo zaidi watendaji wa serikali….wapo wanaosema kwamba nimeuza nchi..lakini wapo wanaosema kwamba mimi ni msaliti….nimeisaliti nchi wapi?alisema Karume kwa kuuliza.
Alisema muongoza wa chama cha mapinduzi kuhusu serikali ya umoja wa kitaifa upo wazi ukisisitiza kwamba ni kuleta umoja na utulivu wa wananchi wote.
wakati huo huo makaratasi ya chama cha mapinduzi ya kuunga mkono kura ya maoni yaliobandikwa katika maeneo mbali mbali yamebanduliwa na kuchanwa chanwa na kutupwa barabarani.
Mkurugenzi wa tume ya uchaguzi ya zanzibar Salum Kassim alisema maandalizi yote ya kura ya maoni yamekamilika ambapo vipo jumla ya vituo vya kupiga kura vipatavyo 1,295 Unguja na Pemba.
“Maandalizi ya zoezi hili muhimu la kihistoria yamekamilika ambapo tunavyo vifaa vyote vya kupiga kura ikiwemo karatasi ambazo zipo zaidi ya wiki moja kutoka Afrika ya kusini”alisema Kassim.






2 Comments on "mpinga serikali ya umoja afukuzwa kazi"
Ndio muheshimiwa Rais waambie ukweli hao wanaojiita wana mapinduzi lakini hawajui madhumuni ya mapinduzi, ambao wanayatumia mapinduzi kuwa ni njia ya kujinufaisha wao binafsi, ambao wanalitumia neno mapinduzi kuwa ni njia kuwagawa Wazanzibari na ambao wanazitumia nyadhifa zao kupandikiza chuki miongoni mwa Wazanzibari, huo ni mwanzo na mfano mzuri kuwajibishwa viongozi wanajisahau kuwa nyadhifa walizopewa na wananchi ni kwa ajili ya kuwatumikia na sio kuwajengea chuki na kubaguwana, Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, ZANZIBAR DAIMA.
Hakuna haja ya kuwavumilia wasaliti wa nchi yetu. Hawa wanaopinga wote hawana uchungu na zanzibar, wanafaa kuandamwa. Wasitumie vielelezo vya mapinduzi na demokrasia kutuzidishia umaskini.
Nimeskia kuwa masheha 2 pia huko Pemba wamefukuzwa kazi akiwemo sheha wa Shehia ya Gando.
Hatutaki mapinduzi ya njaa, chuki na fitna tunataka mapinduzi ya maendeleo.