Habari

Nawaomba Viongozi wa CCM Watafakar

– Kauli zao zitakuja waadhiri

Kumekuwa na maneno ya kurusha yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa CCM, wengi wao kutoka Zanzibar, juu ya mustakbali na khatma ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri za Muungano wa Tanzania. Kama vile viongozi hawa hawajaisoma wala kuifahamu Rasimu hii. Hivyo nachukua fursa hii kuwaomba WATAFAKAR!!!

Tume ya Katiba imewasilisha Rasimu yenye muundo wa Serikali Tatu. Rasimu ilivyo haiwezekani hata siku moja kuleta serikali mbili. Maana yake nini? Rasimu hairuhusu kupenyeza kifungu chenye kutaka serikali mbili. Ukitaka serikali mbili lazima rasimu iandikwe upya kwa kuingiza yale mambo yaliyoachwa kwa ajili ya Serikali ya Tanganyika. Hivyo Bunge la katiba haliwezi kuendelea zaidi ya siku ya kwanza itabidi livunjwe. Kulifanya Bunge la katiba liendelee mukubali kujadili vifungu vilivyomo, si kwengineko. WATAFAKAR!!!

Sambamba na kutoendelea na Bunge la Katiba, pia hakutakuwa na sababu ya kuwepo kura ya maoni, kwani Rasimu haijakamilika. Hakuna cha kuwauliza wananchi. Viongozi wa CCM, WATAFAKAR!!!

Kuirudisha tena Tume ya Katiba kuandika vifungu vipya kwa yale mambo yaliyoachwa ya Tanganyika pia kutazua kizaazaa. Je wajumbe wataridhia mawazo ya watu wachache au wataendelea na kusimamia mawazo ya wananchi wa Tanzania. WATAFAKAR!!!

Ikiwa yote haya ndio yametokezea ni kwamba tamaa ya kupata katiba mpya imeshindikana. Hivyo kwa mujibu wa sheria italazimu turudi na kuendelea kutumia katiba ileile ya zamani. WATAFAKAR!!!

Kurudi kutumika katiba ya Zamani, jee wanafahamu athari zake hasa kwa vile imeshaelezwa kuwa katiba mbili hizi zinapingana? Pale wananchi watakapojitokeza na kufungua kesi Mahakamani, wanafahamu ni kitu gani kinaweza kutokea? WATAFAKAR!!!

Kwa upande mwengine, Bunge la Katiba litakapojadili vifungu vyote vya Rasimu na kuviridhia na kuvipitisha, fedheha kiasi gani itakuwa kwa viongozi hawa wanaoshindwa kujitambua na kutambua kile kilichoandikwa? WATAFAKAR!!!

Pale Bunge la Katiba litakaporidhia Rasimu na likaamua kuipeleka kwa wananchi, wanadhani watakuwa na nguvu gani ya kuizua isipite kuwa Katiba ya Jamhuri za Muungano wa Tanzania? WATAFAKAR!!!

Mtu hufungwa na kauli zake, WATAFAKAR!!!

Share: