Habari

Polisi yamkingia kifua Mwalimu anayedaiwa kusababisha kifo

JUNE 18, 2017 BY ZANZIBARIYETU

Siku chache baada yako cha Mwanafuzi wa Shule ya Laurante Internation Kisiwani Pemba Saleh Abdallah Masoud kufariki dunia kutokana na kipigo cha Mwalimu wa shule hiyo, Jeshi la Polisi la Mkoa wa Kusini Pemba limeibuka na kuisafisha shule hiyo na tuhuma hizo.

Shule hiyo ambayo imefungwa hivi sasa kutokana na sakata hilo wakati serikali ikifuatilia kwa kina suala hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Sheikhan Mohammed Sheikhan amesema kifo cha Saleh Abdallah Masoud (11) aliyekuwa Mwanafunzi wa Skuli hiyo iliyopo Ole Kianga Mkoa wa Kusini Pemba hakikutokana na kupigwa na Mwalimu kama inavyodaiwa bali kimechangiwa na kuumwa kutokana na maradhi mbali mbali.

Sheikhan amesema Mwanafunzi huyo alikuwa na ugonjwa wa Figo, Ini pamoja na uvimbe katika shingo yake na hivyo kifo chake hakitokani kipigo cha Mwalimu alichokipata shuleni hapo..

Akizungumza na wandishi wa habari jana huko ofisini kwake Madungu Chakechake Pemba amesema mnamo tarehe 30/05/2017 majira ya saa 5: 00 asubuhi walipokea taarifa ya kifo cha mwanafunzi huyo na ndipo walipochukua hatua za haraka kufika skulini hapo kuwahoji walimu pamoja na wanafunzi wa skuli hiyo na katika taarifa za awali uchunguzi ulibaini kwamba mwanafunzi huyo alipata adhabu baada ya kuharibu midoli ya kufundishia wanafunzi wa chekechea skulini hapo.

Shekhan amesema, Mwanafunzi huyo kabla ya hapo awali alipata kuanguka chooni na kuumia sehemu ya bega la mkono wa kulia na alianza kupatiwa matibabu ya awalii na daktari wa skuli hata hivyo hali haikua nzuri na kulazimika kupelekwa hospitali ya Chakechake na Mwanamashungi kwa matibabu zaidi.

Amefahamisha kuwa 25.05.2017 baba wa mtoto huyo alifika skulini hapo kwa ajili ya kumchukua na kwenda nae nyumbani kwa lengo la kumpeleka hospitali ya Wete kwa matibabu zaidi aliruhusiwa kurudi nae nyumbani na ilipofika 29/05/2017 alirejeshwa tena hospitali ya Wete na kulazwa na hatimae majira ya saa 8:00 alifariki dunia.

Amesema kutokana na uchunguzi wa daktari aliyemtibu katika hospitali ya Wete aligundua kuvimba kwa shavu la kulia , uvimbe usio na maumivu mbeleni mwa shingo, uvimbe kwenye mguu wa kulia, umanjano wa macho na hakua na jeraha lolote wala sehemu yeyote iliyotoka damu wala mkwaruzo au alama zisizo za kawaida.

Pia vipimo vingine vilionesha kuwa alikuwa na upungufu wa damu, kuumwa na Figo pamoja na Ini na sio kujeruhiwa na kupelekea hali yake kuwa mbaya na hatimae kufariki dunia.

Aidha amesema kwa sasa wanawashikilia watu saba na uchunguzi ukikamilika watapandishwa mahakamani kwa kujibu shtaka la uzalilishaji pomoja na uzembe na sio shitaka la mauaji.

Akizungumza na DW siku tatu baada ya kifo cha Manafunzi huyo Mama wa Mwanafunzi huyo Bi Maryam Saleh Mabrouk anayeishi Wete Kisiwani Pemba alisema Mwanafunzi wake alipigwa na Mwalimu Shuleni na kwenda kuchukuliwa kupelekwa hospitali na kutibiwa na hatimae kufariki dunia.

Bi Maryam alisema Mwanawe aliletwa nyumbani kwake hali ya kuwa amebadilika macho yake na mwili kuwa na maumivu makali ambapo anapoguswa viungo hulalamikia machungu anayoyapata.

Chanzo cha kipigo hicho kinaelezwa kwamba alichana boxi la mwalimu kwa kubandua solatep na kwenda kubandika katika gororo lake lililokuwa limechanika mfuko wa plastiki (cover) kabla ya kifo cha Mwanafunzi huyo Mama yake alisema ameacha ujumbe wa kutaka auliziwe kwa wlaimu wake waliompiga kisa cha kupigwa kiasi hicho.

Zanzibar Yetu

Share: