Habari

SMT na SMZ kujadiliana uchimbaji gesi

Wanasheria wa Serikali za Muungano (SMT) na Mapinduzi Zanzibar (SMZ) pamoja na wataalamu wa nishati wameanza majadiliano kuuwezesha kila upande kutafuta na kuchimba gesi asilia na mafuta yake.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –Muungano Samia Suluhu Hassan, aliliambia Bunge jana wakati akiwasilisha bajeti ya ofisi hiyo .

Alisema: “Wanasheria wakuu wa SMT na SMZ wanaongoza kamati za wataalam wa sekta ya nishati kuandaa utaratibu wa mapendekezo ya kubadilishana sheria zinazohusu utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili.

“Hatua hii inachukuliwa ili SMZ iwe na fursa ya kuanza kujiandaa kwa kazi hiyo, katika misingi ya kisheria na, sera na matayarisho ya kitaasisi.” Alisema hayo ni miongoni mwa mambo yaliyofanyiwa kazi na sekretariati ya kuondoa changamoto za Muungano.

Alisema mengine ni kufahamu hisa za SMZ zilizokuwa katika bodi ya ya sarafu ya Afrika Mashariki kabla haijavunjwa na kuanzishwa Benki Kuu (BoT).

Alisema Mawaziri wa Fedha wa pande mbili hizo wamepitia nyaraka zenye taarifa hizo kuona hali ilivyokuwa na kiwango cha fedha kilichohamishiwa BoT.

Samia aliliambia Bunge kuwa maamuzi ya jinsi ya kugawana mapato yatokanayo na faida ya BoT yatatolewa baada ya kufahamu na kukubaliana kuhusu hisa za SMZ kwenye bodi hiyo ya sarafu.

Pia alisema kero nyingine ya Muungano iliyoshughulikiwa ni kuondoa vikwazo vya kuingiza na kusajili vyombo vya usafiri kutoka upande mmoja wa Muungano kwenda mwingine .

“Kero zitaondoka kupitia kutungwa sheria mpya ya usafiri wa barabarani kwa upande wa SMT itakayoondoa vikwazo vilivyomo kwenye sheria ya usafiri barabarani ya 1973 na kanuni zake za mwaka 2001,” alisema.

Samia alisema ofisi ya Makamu wa Rais imepitia katiba za mataifa kadhaa yakiwamo Trinidad na Tobago, Umoja wa Falme za Kiarabu na Uingereza.

Mengine ni Ethiopia, Marekani, Ujerumani na India ambazo zinafuata mfumo wa muungano –shirikisho ili kulinganisha utendaji wa vyombo vyake na vya SMT.

“Lengo ni kulinganisha mamlaka za utendaji, kutunga sheria na utoaji haki, aidha masuala ya kifedha na uchangiaji gharama za uendeshaji na maoni yamewasilishwa kwenye tume ya mabadiliko ya katiba.”

MAONI YA KAMATI
Taarifa ya kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala Bora kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais-imesema Watanzania wengi hawaelewi masuala ya Muungano.
CHANZO: NIPASHE

Tagsslider
Share: