Habari

TAARIFA KWA VYOMBA VYA HABARI

Imekuwa ni mazowea kila inapojiri kwa Wazanzibari kushikamana katika mwamko wa maslahi ya Nchi, kuwajengea mazingira ya hofu, vitisho, uchokozi, hujuma na kuwaparaganya, kupitia visingizio mbali mbali vya propaganda, vipigo, ubabaifu, na unyang’anyi.

La kusikitisha ni kuona kwamba vitendo hivyo vinahamasishwa na kutekelezwa na hata sehemu ya Mamlaka za Serikali, wakiwamo baadhi ya watendaji wa vikosi vya ulinzi na usalama.

Lengo ni kuondosha utengamano, na kuhamisha fikra juu ya mstari wa maslahi na kuwapeleka watu, ndani na nje ya Nchi, katika ajenda za kisiasa za kistratejia.

Hakuna mwenye busara na mpenda haki, na zaidi aliyeshuhudia, ambaye hataamini kuwa kilichotendeka maeneo ya Darajani Mjini Unguja, Siku ya Jumatano tarehe 12 Juni 2013, majira ya Saa 6.30 mchana, kama si uchokozi wa makusudi wa wahuni na wanavikosi, dhidi ya Wananchi watulivu, wapitanjia, na waliokuwepo katika harakati za kawaida za kujitafutia pato na riziki za halali kwa maslahi ya Taifa kwa ujumla.

Si maadili ya askari, mlinzi, au mwanausalama yeyote aliyefundishwa kutangulia kufyatua risasi, zaidi ya nane, katika mazingira tulivu na mikusanyiko ya kawaida ya binaadamu, bila ya hata hali tete au mzozo wa kiasi kidogo kabisa, pasi na kuwa na ajenda ya siri; na hivyo ndivyo ilivyojiri katika maeneo hayo muhimu ya uchumi na haiba ya Nchi yetu.

Ni lipi, kama lengo siyo kuchokoza, kupora, kufitinisha ili kuharibu, haiba na shaksia tulivu, tena machoni mwa hata wageni wanaotembelea Visiwa vya Unguja na Pemba, ambao sasa wanashuhudia hadhiri na dhahiri yake.

Chama cha Wananchi, CUF, kinaiomba Serikali ichunguze kwa kina mwenendo na wahusika wakuu wa vitendo hivyo, watu wachache, ambao bila shaka wamekosa hikma, uchungu wa maendeleo na wasiojali maslahi ya Nchi ya Zanzibar.
Ni vyema ikazingatiwa kwamba siku zote busara ndiyo njia bora maishani, kulikoni matumizi ya mabavu na mtutu wa bunduki, hasa pale ambapo Mamlaka za Dola na Wananchi, kila upande unamuhitaji mwenzake ili kuleta maendeleo.

Chama cha CUF, kinawaomba wananchi wote kuwa watulivu, wasichokozeke, wakielewa thamani ya sasa ya subira yao, ndiyo malipo ya maslahi mema ya baadae au hivi karibuni, ya Nchi, wakati huu ambao Taifa linaelekea katika mabadiliko makubwa ya kihistoria.

HAKI SAWA KWA WOTE

Imesainiwa na:
Mheshimiwa Salim Bimani,
Mkurugenzi wa Haki za binadamu, habari, uenezi na Mahusiano ya Umma

Tagsslider
Share: