HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR DK. AMANI ABEID KARUME

Written by  //  02/08/2010  //  Nyaraka/Vitabu  //  15 Comments

SALAMU ZA RAIS WA ZANZIBAR NA
MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI,
MHESHIMIWA DK. AMANI ABEID KARUME,
KWA WANANCHI BAADA YA KURA YA MAONI
JUMAPILI TAREHE 1 AGOSTI, 2010

Assalaam Aleikum,

Ndugu Wananchi,
Naanza kwa kumshukuru Mola wetu, Subhana Wataala, Muumba Mbingu na Ardhi, kwa rehema zake kwetu zinazotuendeshea mambo yetu kwa salama na amani.

Nachukua fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati na pongezi nyingi kwa wananchi wote wa Zanzibar walioshiriki katika Kura ya Maoni na kutumia haki yao ya kidemokrasia kutoa maamuzi au mapendekezo yao juu ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kushiriki kwao, kwa kupiga kura ya Ndio au Hapana, ni kuthibitisha kupevuka demokrasia na utawala bora nchini kwetu. Zoezi hilo ni la kihistoria ambalo limewapa wananchi wa Zanzibar haki ya kushiriki moja kwa moja katika maamuzi mazito yanayowahusu, na kila alieshiriki ameingia katika historia ya kuendeleza demokrasia, amani na utulivu inayotegemewa kuwa endelevu na msingi mpya wa maendeleo zaidi ya nchi yetu.

Matokeo ya kura hiyo yameshatolewa rasmi na nina wingi wa furaha kuwa kura ya NDIO imechukua nafasi ya juu ikiwa ni asilimia 66.4, karibuni thuluthi mbili ya kura zote zilizopigwa. Nawashukuru na kuwapongeza sana wananchi wote waliochukua uamuzi wa kupiga kura ya NDIO. Kufanya hivyo kumefungua sura mpya ya mfumo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kudhihirisha nia ya Wazanzibari kuishi kwa umoja, kupendana, amani na utulivu. Aidha, nawashukuru na kuwapongeza wale wachache waliokataa mfumo huo kwa kutumia haki yao ya demokrasia na kutoa uamuzi wao.

Kwa vile nchi yetu ni ya kidemokrasia na inafuata misingi hiyo, na kwa kua uamuzi wa wengi umeshafanywa na kauli ya wachache imesikika, sasa ni wajibu wetu sote kushirikiana kuendeleza gurudumu la maendeleo ya demokrasia chini ya mfumo mpya nchini mwetu. Katika hili, hakuna mtu alieshinda wala alieshindwa ila mshindi ni Zanzibar yenye amani, umoja na mshikamano.

Washindi ni wananchi wenyewe kutaka kukuza umoja, demokrasia, utawala bora, amani na maendeleo kwa pamoja. Huo ndio msingi hasa wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Baada ya kura hii ya maoni, wajibu sasa ni wa Baraza la Wawakilishi ambalo linatarajiwa kukutana hivi karibuni kufanya marekebisho ya msingi katika Katiba ya Zanzibar ya 1984. Sisi Zanzibar tutakuwa ni nchi ya kupigiwa mfano kwa chaguzi zitakazokuwa za amani na utulivu ikitiliwa maanani namna ya zoezi la upigaji kura ya maoni ulivyokwenda. Ni matarajio yetu sote kuwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa umoja wao wataheshimu uamuzi wa wananchi wa Zanzibar na kufanya wajibu wao kwa faida ya kila mmoja wetu.

Ndugu Wananchi,
Zoezi hili la kupiga kura ya maoni ili kufanya uamuzi wa mabadiliko makubwa ya mfumo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuliwachia Baraza la Wawakilishi kupitisha Mswada wa Mabadiliko ya Katiba, litaingia katika historia ya maendeleo ya demorasia nchini kwetu na Afrika nzima kwa jumla. Mara nyingi nchi zetu za Afrika zinakutwa na majanga na mizozo kufuatia harakati za uchaguzi. Hali hiyo haipaswi kupuuzwa na ni vyema ikaepukwa kadiri inavyowezekana.

Kwa msingi huo, wananchi wa Zanzibar wameamua kubadilisha sura hiyo kwa kuweka mfano mzuri wa kuigwa na nchi nyengine ili demokrasi iendelezwe kwa kuendesha chaguzi kwa amani na kuwashirikisha wananchi wote katika utawala wa nchi yao.
Ndugu Wananchi,

Bado tuna wajibu wa kuthibitisha kuwa mshindi wa zoezi hili ni Zanzibar na Wazanzibari wote, kwa kuhakikisha kwamba sote kwa pamoja tunaendesha uchaguzi mkuu ujao katika hali ya amani, salama na utulivu, tarehe 31 Oktoba mwaka huu. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kudumisha utulivu na ushirikiano tulionao hivi sasa.

Baada ya hapo tutaingia, Inshaallah, katika kipindi kipya cha kuleta maendeleo makubwa katika nchi yetu katika hali ya umoja na mshikamano. Matokeo yatakuwa ya manufaa kwa wananchi wote na tutakuwa tumejenga Zanzibar Mpya yenye umoja na mshikamano tukiwa sote ni Wazanzibari.

Kwa kumalizia, napenda kutoa shukurani zangu za dhati, kwa mara nyengine tena kwa wananchi wote walioshiriki katika Kura ya Maoni, kwa utulivu na ustaarabu mkubwa. Natoa pongezi za pekee kwa Kamati ya Watu Sita ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Utekelezaji wa Azimio la Baraza kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ambayo Waheshimiwa Wajumbe wake wamefanya kazi kubwa na nzuri ya kuelimisha jamii Unguja na Pemba juu ya mfumo mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo tutaiunda baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Navishukuru vyama vyote vya siasa kikiwemo chama changu CCM, chama cha upinzani CUF, viongozi wa dini, wahadhiri na wanafunzi wa vyuo vikuu, NGOs waliounga mkono hoja hiyo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika kura ya maoni na kuikubali.

Naipongeza na kuishukuru Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), na wafanyakazi wake wote kwa kuendesha zoezi zima vizuri na kwa mafanikio, hasa ikizingatiwa kutokuwepo kwa uzoefu wa muda mrefu katika suala hilo. Tunalishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa – UNDP na washirika wengine wakiwemo Nchi za Jumuiya ya Ulaya na wengineo kwa msaada wao katika kuendesha zoezi hili. Aidha, natoa shukurani maalum kwa Switzerland, Uingereza, Norway na Sweden kwa kua tayari kutupatia uzoefu wao katika mifumo ya utawala wa umoja wa kitaifa na zaidi katika suala la uendeshaji wa kura ya maoni. Mchango wa Switzerland nchi yenye uzoefu wa miaka mingi umetusaidia sana.

Ndugu Wananchi,
Baada ya maelezo hayo, ni wajibu wetu sote kujipanga vyema na kuendesha uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, 2010 kwa ustaarabu na mwenendo huo huo mzuri tuliouonesha katika kura ya maoni. Kwa kufanya hivyo kwa uadilifu, tutapoza nyoyo za wenzetu waliokua na hofu juu ya jambo hilo na bila ya shaka mafanikio yake ni yetu sote. Tuhimizane sote mema na tukatazane maovu. Inshaalla Mwenyezi Mungu atatusaidia.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Mwenyezi Mungu awabariki wote.

15 Comments on "HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR DK. AMANI ABEID KARUME"

  1. kwaomtu 02/08/2010 kwa 9:56 mu ·

    SHEIKH AMANI NAKUOMBEA DUA UMALIZE UONGOZI WAKO KWA USALAMA NA UIACHE NCHI IKIWA KATIKA MISINGI BORA YA KUHESHIMIANA. NAJUWA WAKO WANAOKUONEA CHOYO JUU YA MAFANIKIO HAYA LAKINI WAJUWE TU FURSA WALIIPATA LAKINI WALIJIFANYA HAWAONI WALA HAWASIKII. CHUKI NA FITNA ZIMEWAJAA LAKINI KWA UWEZO WAKE ALLAH SUBHAANA, FEDHEHA ITAWAFIKA HAPA HAPA DUNIANI.

    SASA BAADA YA UCHAGUZI HUU WA OCTOBA TUNATAKA TUPEWE FURSA YA KURA NYENGINE YA MAONI JUU YA MUUNGANO. KWA BAHATI MBAYA JAMBO HILI HALIKUFANYIKA SASA TUNALITAKA ILI TUWAONESHE PINDA NA WENZAKE KUWA HII ZANZIBAR SIO NCHI BALI NI DOLA ILIO IMARA NA KATU INSHAALLAH HAITOSAMBARATIKA.

  2. muhimu 02/08/2010 kwa 10:05 mu ·

    welldone MR president karume

  3. ashakh 02/08/2010 kwa 10:28 mu ·

    @kwamtu, tafadhali nakuomba, kwanza tuachie tuangalie hilo la Octobar. Kwafikra zangu sasahivi ni muhimu kuliko hilo la muungano.

    Nimejifunza kwa hawa wenzetu wazungu, ukiwauliza jee mutachukua kombe? Wanakujibu, la msingi ni kupata hizi point tatu za mchezo unaofuata.

    Najiuliza kuna mantiki gani kusema hivyo. Nimegundua kuwa lengo linakamilika kwa kuligawa sehemu ndogondogo zenye kutekelezeka.

    Zaidi natowa wito kwa wazalendo, kazi iliopo mbele yetu ni kubwa mno. Kwanza, tunataka tufanye uchaguzi wa salama na amani. Pili, tunataka tufanye uchaguzi uwe kigenzo kwa waafrika wote. Tatu, tunataka tuchague kile chama kitakacho ikhuisha Zanzibar, watu, na raslimali zake.

    Hivyo ni wakati wa ku-focus kipindi hichi cha miezi 3, kwenye uchaguzi mkuu.

    @Rais
    Hongera Dr Karume, hii ni aina ya hotuba hata siku moja sijawahi kuisikia kutoka kwa viongozi wetu. Yaani mwananchi kutajwa mwanzo katika itifaki!!! Leo mwananchi yuko juu. Tuendelee kumueka juu pia pale anapoamua kuiondoa serikali yake. Siku zote tumezowea kusikia wanamapinduzi kutajwa mwanzo.

    Nimefarajika saana na msisitizo wako wa kufanyika uchaguzi mzuri zaidi ya kura ya maoni hapo October. Kwa harakaharaka pendekezo langu ni moja juu ya tume yako/yetu ya uchaguzi. Nalo ni hili;
    Imeanzisha “Reporting Centre” kazi yake iwe ni moja tu, kutoa matokeo mojakwamoja kutoka kwa Returning Officer. Sivyenginevyo, kwani nimefuatilia haya matokeo ya kura ya maoni yamekuwa na ERROR. Bilashaka inatokana na sababu nyingi miongoni mwao ni za kibinadamu. Lakini tutakapo tumia utaratibu huu wa Returning officer, error hizi zinaweza kuondoka kabisa.

  4. sale 02/08/2010 kwa 11:18 mu ·

    Wapemba tunasema, Ntoto wa nyoka n nyoka tu.Yule Karume aliye wahamasisha wanamapinduzi kujitoa kwenye ukoloni, akajenga Zanzibar, akawajengea watoto yatima, akawajengea wazee, akasema maji bure, elimu bure,,,Ni sawa na huyo Karume wasasa alieona kuwa Zanzibar inatoweka na kuna watu fulani hawaoni mbali wako tayari kuimaliza zanzibar kwani hawajui historia ya zanzibar, sasa huyu Karume ameshatuonesha njia, kazi kwetu mi na wewe kutomvunja moyo na kuonesha mfano na kurudisha desturi zetu za kizanzibar, kutembelea jirani zako, kumpelekea chakula jirani yako, kutakia kheri jirani yako, kufutari nje we na jirani yako, kumsitiri jirani yako,
    Mungu akujalie kila la Kheri Raisi Karume na akusamehe makosa yako.. “Kila binaadamu ni mwenye kukosea na mbora wa wale waliokesea ni wale wanaotubiya”

  5. kitamli 02/08/2010 kwa 11:59 mu ·

    hutba ni nzuri sana kwa hakika na kama mheshimiwa rais amani alivyosema huu ushindi ni wa zanzibar na wazanzibari wote,kinachotakiwa hapa sasa ni watu kuwa kitu kimoja kwa kuwa na mashirikiano katika kuleta maendeleo ya nchi kwa vile walopiga kura ya hapana sauti yao pia imesikika lakini kwa sababu ya wengi wameshaamua hatuna budi kuheshimu maamuzi ya wengi na waswahili wanasema wengi wape. sasa ndugu zetu wa kisonge hamna budi kustahamili neema zikipatikana tutakula pamoja katika zanzibar mpya.

  6. mohamed soud 02/08/2010 kwa 12:14 um ·

    A kum, kwanza hatuna budi kumshukuru Mw Mungu kwa kutujaalia kupata wingi wa kura ya ndio katika kura ya maoni,sina budi kuwapongeza rais wa zanzibar Dk Amani Abeid Karume kwa ujasiri wake katika mchakato mzima wa kukubali maridhiano na Maalim Seif Shariff Hamad.

    Kama alivyotueleza kwaomtu wako wanaomuonea cheyo rais wetu wa zanzibar Dk Amani kwa mafanikio yake kutokana na nafasi yake lakini kwa roho zao mbaya waliyapuuza maelewano na walikuwa na nafasi sawa sawa na ya rais Karume, kutokana na hili hatuna budi kuwaenzi viongozi hawa Dk Karume na Maalim seif na tuwatambue kama ni Nelson mandela wa zanzibar kwani huu ni mwanzo wa zanzibar kuweza kujitawala na kujiamulia mambo yake mwenyewe baada ya jinamizi zima la muungano kuweza kutukandamiza kimaendeleo, sikusudii kuwa muungano utavunjwa ila naamini utaekwa sawa kwa maslahi ya pande zote mbili na nnamini kuwa kama wenzetu upande wa pili hawatakuwa tayari basi naami huko mbele muungano pia chini ya system mpya ijayo unaweza pia zanzibar tukasema kama ni hivi basi na sisi hatuutaki tena na tukaweza kuuvunja.

    Nawaomba wazanzibari sote tushikamane kwa faida yetu na vizazi vyetu vijavyo sisi vijana wa sasa tunalaumu muungano uwa ndio unaturudisha nyuma ki-maendeleo hivyo lawama haikwepeki kwa rais wa kwanza wa zanzibar Abeid Karume ila kama hatukuwa makini na sisi watoto wetu na wajukuu watakuja kutulaumu sisi kuwa hatukuwajengea future ya nchi yao.

  7. maguvu 02/08/2010 kwa 12:38 um ·

    as/a
    kwanza namshukuru M/Mungu kwa nema hii!
    hongera dr Karume kwa speach yako kwa hatuwezi kuamini kama unaweza kusema maneno mazuri kama hayo tuliyokuwa tukiyaota tu ndotoni. M/Mungu akusamehe kwa yaliyopita amin.

    @ sale comment yako ni nzuri sana lakini tu kama utaondowa kitu WAPEMBA na ukasema sisi waznz wa wa KISIWA CHA PEMBA itakuwa ni vizuri sana kwa kuwa tumeamuwa kuzika tofauti zetu na ku proud kama ss sote ni WAZANZIBAR wacha tukifikia hivi naamini kwa nguvu za M/Mungu na umoja wetu basi hakuna adui atakae pata mwanya wa kutuchezea tena na kutugawa kama tutaondowa hili neno WAPEMBA NA WAUNGUJA.
    nadhani nimefahamika.

  8. sale 02/08/2010 kwa 12:45 um ·

    Maguvu ..Asante kwa kuniweka sawa katika comment yangu kwa kutumia neno Wapemba, na naomba radhi,,,Hongera Zanzibar mpya..

  9. seif 02/08/2010 kwa 3:35 um ·

    Kwaza, nakuombea Dua mwenyezi Mungu akusamehe kwa mambo mengi uliyo yafanya katika utawala

    wako. Pili, Nakupongeza kwa kufikiria Zanzibar na Wazibari kwa ujumla.

    Tatu, nakupongeza kwa hutuba yako mzuri ambayo sijawahi kusikia . Na mwisho, nakuombea

    kila la heri umalize urais wako kwa salama na amani,Amin.

  10. seletochiy 02/08/2010 kwa 4:46 um ·

    a.alaykum
    na mimi pia nataka kuwapongeza viongozi wetu 2 mh.amani karume na mh.maalim seif lakini bila ya kuwasahau wa znz wote waliojitokeza kuiokoa znz.
    mimi binafsi ningeliulizwa kitu gani unataka kiwe znz wakati huu basi ningelijibu hivi:
    kumuomba m.mungu awasameh viongozi wetu hawa na awajaalie maisha marefu na awape hatma njema.

  11. seletochiy 02/08/2010 kwa 5:01 um ·

    a.alayukm
    jamani bado hamjapata matokeo ya kura ya maoni ya ccm kwa ubunge na uwakilishi ?
    kama mmeyapata tupatieni japo jimbo kwa jimbo

  12. mrfroasty 02/08/2010 kwa 6:37 um ·

    Tumetumiwa na Dr.Yussuf electronic copy ya hotuba hio inapatikana katika maktaba yetu hapa:
    http://www.scribd.com/doc/35237763/Hotuba-ya-Balozi-Karume-kura-ya-maoni#fullscreen:on

  13. Yussuf Saleh 02/08/2010 kwa 9:33 um ·

    Sh. Muhsin unakusudia Hotuba ya Rais Karume na sio Balozi Karume ???

Comments are now closed for this article.