Waangalizi:Ripoti ya JUMAZA
Written by administrator // 01/08/2010 // Nyaraka/Vitabu // 3 Comments
JUMAZA OBSERVER GROUP
RIPOTI YA AWALI
Utangulizi
JUMAZA OBSERVER GROUP ni miongoni mwa Waangalizi wa Ndani walioshiriki kufuatilia Kura ya Maoni iliyofanyika Zanzibar tarehe 31, Julai 2010 kwa kusambaza waangalizi katika majimbo yote 50 ya uchaguzi.
Tulifuatilia hatua zote za Kura ya Maoni ikiwemo matayarisho, elimu ya wapiga kura na kampeni, upigaji wa kura, kuhesabu na utangazaji wa matokeo.
Uandikishaji
Hakukuwa na zoezi jipya la uandikishaji kwa wapiga Kura ya Maoni bali wapiga kura waliosajiliwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010 walithibitishwa kuwa ni wapiga kura halali kwa Kura ya Maoni. Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar wapiga kura halali walioandikishwa ni 407,950. Hata hivyo kulikuwa na malalamiko ya watu wengi wenye sifa kutopewa haki yao ya kimsingi ya kuandikishwa. Hata hivyo, sisi kama waangalizi wa ndani tulishindwa kupata idadi halisi ya watu hao.
Elimu ya wapiga kura na kampeni
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilitoa vipeperushi na kuvitawanya katika maeneo yote ya Unguja na Pemba kuhusiana na utaratibu mzima wa Kura ya Maoni.
Mustakbali wa Zanzibar (MUWAZA) ikishirikiana na Kituo cha Huduma za Sheria, Jumuiya ya Wanasheria Zanzibar, na UAMSHO walifanya Kongamano la Kitaifa la siku mbili tarehe 17 hadi 18 Julai kuhusu Kura ya Maoni.
Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) ilitoa elimu ya ya wapiga kura kwa kupitia kipindi chake cha kila siku cha ujumbe wa asubuhi. Katika kipindi hiki watu walielimishwa juu ya utaratibu wa kupiga Kura ya Maoni ikiwemo kupiga kura kwa usahihi.
REDET waliendesha vikao mbalimbali vilivyoshirikisha vikundi tofauti mijini na vijijini kuzungumzia masuala yanayohusiana na Kura ya Maoni.
Taasisi zisizokuwa za kiserikali zikiwemo ANGOZA, Umoja wa Watu wenye Ulemavu, Theatre for Social Development (THESODE), White Star Society na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake (ZAFELA) waliendesha vikao mbali mbali kuhusu elimu ya uraia na upigaji wa kura. Aidha THESODE walitoa elimu ya Kura ya Maoni kupitia maigizo.
Zanzibar Cable Television, TVZ, Zenj FM, Redio Adhana, FM,Hits, Redio Istqama Pemba na Redio Jamii Micheweni Pemba zilitangaza na kutoa mtiririko wa vipindi vya Kura ya Maoni ambavyo viliwasaidia watu kufahamu nini kinachoendelea Kuhusu kura ya Maoni.
Kamati ya Usimamiaji wa Maridhiano yenye wajumbe sita ilitayarisha ratiba ya kuonana na makundi tofauti katika visiwa vya Unguja na Pemba kuzungumzia kuhusu Kura ya Maoni na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Makundi yaliyoshirikishwa ni pamoja na viongozi wa dini ya Kiislam na Kikiristo, Jumuiya za Watu wenye Ulemavu, wawakilishi wa wanawake, masheha, madiwani, walimu, wanafunzi na makundi ya kijamii.
Waangalizi wetu waligundua makundi mawili makubwa yaliyoshiriki katika kampeni. Kundi la kwanza liliwashajiisha Wanzanzibari kukubali kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kupiga kura ya ndio. Kundi hili lilijumuisha viongozi wa juu ambao ni waanzilishi wa maridhiano Zanzibar Mh. Rais Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad , Tanzania Center for Democracy, wasomi wazalendo wa ndani na nje, viongozi wa dini ya Kiislam, makundi ya jumuiya zisizokuwa za kiserikali na Kamati ya Usimamiaji wa Maridhiano.
Kwa upande mwengine, kundi la pili liliwashajiisha Wanzanzibari hasa wana CCM kukataa kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Kundi hili katika njia isiyo ya wazi lilijitokeza kupitia maskani ya kisonge katika bao la matangazo linalojulikana kwa jina la Sauti ya Kisonge.
Waangalizi wetu waliandika mfano wa ujumbe ulioandikwa na Maskani ya Kisonge uliosomeka “Wana CCM Mseto ni hatari, kura ya maoni Tia hapana hapana hapana”
Pamoja na hayo, kulikuwa na kampeni za chini kwa chini katika kambi zote mbili, inayounga mkono na inayopinga suala hilo. Kwa mfano kulisambazwa vipeperushi vingi sana na watu wasiojulikana katika maeneo yote ya Mkoa wa Mjini Magharibi vilivowashajiisha watu kukubaliana na wazo la kuanzishwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, mfano wa kipeperushi hicho kilisomeka:
“I’M 4 ZANZIBAR VOTE YES 31/7/2010.
Wiki moja kabla ya zoezi la upigaji wa Kura ya Maoni, vipeperushi vilisambazwa na watu wasiojulikana vyenye kuwataka wanachamaCCM kukataa Mseto, kipeperushi hicho kilisomeka:
“PIGA kura ya Hapana kwa sababu”
- Uwokoe nchi yako
- Ulinde Mapinduzi
- Uwokoe chama chako.
Siku moja kabla ya kupiga kura , vipeperushi vingi vilitolewa na Chama Tawala (CCM) vyenye kuonesha picha za viongozi wa juu akiwemo Makamo Mwenyekiti wa CCM, Zanzibar Mh. Amani Karume, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Ali Hassan Mwinyi, Makamo wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Ali Mohd Shein, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmini Amour Juma, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mh. Shamsi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi Mstaafu Mh. Mohamed Gharib Bilali na Naibu Waziri Kiongozi Mh. Ali Juma Shamhuna.
Vipeperushi hivyo takriban vilitawanywa katika sehemu zote za Mkoa wa Mjini Magharibi. Ujumbe wa vipeperushi hivyo ulisomeka:
“HAWA WOTE WAMESEMA NDIO WEWE JEE?
Mwitiko wa wapiga kura katika zoezi hili unaonesha wazi kuwa Elimu ya Wapiga Kura ilitolewa kwa kiwango kidogo sana kwani takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya wapiga kura 100,000 hawakujitokeza katika kupiga kura. Aidha ilidhihirika kuwa mpaka siku ya upigaji wa kura yenyewe wapiga kura wengi walikuwa hawaelewi kwa usahihi dhana za Kura ya Maoni na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Matayarisho ya kupiga kura
Tume ya uchaguzi Zanzibar ilifanya matayarisho yote muhimu kwa zoezi la upigaji wa kura inayojumuisha vifaa vya kupigia kura kama vile fomu za aina tofauti, karatasi za kupigia kura, masanduku ya kura nk.
Makarani wa kura mfano Wapigishaji Kura walichaguliwa kwa kupitia usaili na kupatiwa mafunzo juu ya taratibu za kusimamia Kura ya Maoni. Vituo vya kupigia kura vilipangwa mapema sana kupatiwa vitendea kazi. Karatasi za kupigia kura na vifaa vyengine vilisafirishwa katika Afisi Kuu ya Tume Pemba chini ya ulinzi na baadae kusambazwa katika vituo. Kwa maana hiyo, kwa ujumla matayarisho yalikuwa mazuri na yenye kutosheleza.
Matayarisho ya ulinzi na usalama
Makao Makuu ya Polisi yalifanya matayarisho ya mpango mzima wa ulinzi na usalama hususan kwa siku ya zoezi kupiga Kura ya Maoni. Polisi walisambazwa katika vituo vyote vya kupigia kura pamoja na vifaa vyote muhimu ili kuhakikisha zoezi la Kura ya Maoni linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu na mafanikio.
Siku ya kupiga kura
Takriban vituo vyote vilifunguliwa mapema, ingawa upigaji wa kura ulipangwa kuanza saa mbili za asubuhi. Kabla ya zoezi upigaji kura kuanza, Makarani wa Kusimamia Kura waliwaonesha wapiga kura masanduku ya kura yakiwa matupu kuthibitisha kuwa masanduku hayo hayakuwa na karatasi za kura ndani yake kabla ya zoezi kuanza.
Waangalizi wetu walipewa taarifa kuwa vifaa vyote muhimu vya kupiga kura vilikuwepo na kutosheleza. Kulikuweko na askari wachache wasio na silaha katika kila kituo cha kupigia kua kuweka ulinzi na usalama pamoja na kuweka utaratibu na nidhamu katika foleni za wapiga kura. Hivyo, kinyume na chaguzi zilizotangulia polisi walikuwepo kwa lengo la ulinzi na sio kuwatisha wapiga kura. Kwa ujumla kulikuwa amani na usalama pamoja na mazingira ya utulivu yaliyowawezesha wapiga kura kupiga kura kwa furaha, kujiamini na uhuru. Hakukuwa na aina yo yote ya vitisho na khofu.
Vyumba vya kupigia kura vilipangwa kwa utaratibu wa alfabeti za majina ya wapiga kura ili kuwawezesha wapiga kura kuvitambua vyumba vyao kwa urahisi. Wapiga kura halali wote waliokuwepo katika vituo walipatiwa haki yao ya kupiga kura bila ya usumbufu. Watu wenye ulemevu walisaidiwa kupiga kura wao wenyewe kwa siri kwa msaada wa Makarani. Aidha watu wasioona walipatiwa kifaa maalumu kilichowawezesha kupiga kura wao wenyewe kwa siri, kitendo hiki ni mara ya kwanza kutokea katika chaguzi za Zanzibar.
Aidha wazee walisaidiwa kupiga kura na jamaa zao kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Tume ya Uchuguzi. Kwa ujumla Wazanzibari waliridhika na hali ya hali ya usalama na uhuru uliojitokeza katika vituo vya kupigia kura. Baadhi ya wapiga kura waliwaomba waangalizi wetu kuwapelekea ujumbe ufuatao:
“Wambieni Tume ya Uchaguzi hivi ndivyo uchaguzi unavyofanywa”
Vyama vya siasa vya CUF, TADEA, CCM, JAHAZI ASILIA, na SAU waliweka waangalizi wa vyama, hata hivyo CUF walikuwa na idadi kubwa zaidi ya waangalizi.
Mchakato wa kuhesabu kura
Zoezi la kuhesabu kura lilikwenda vizuri kwani lilifuata taratibu zote za uchaguzi. Kura zilihesabiwa katika vituo na matokeo kupachikwa mbele ya vituo hivyo. Majumuisho ya kura yalifanywa katika Afisi za Tume – Wilaya na baadae kupelekwa Makao Makuu ya Tume kwa kuhakikishwa na kuthibitishwa. Baada ya hatua hizo matokeo yalipelekwa katika Ktuo cha Matokeo – Bwawani kwa kutangazwa rasmi.
Wapiga kura wengi waliohojiwa na waangalizi wetu walisema kuwa wameridhika na mchakato mzima wa upigaji Kura ya Maoni na wanaipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Hali inawapa matumaini kuwa chaguzi zijazo za Zanzibar na Tanzania kwa jumla zitafanyika kwa amani, utulivu na mashikamano wa wananchi.
Msimamo wa kundi
Msimamo wa JUMAZA OBSERVER GROUP ni kuwa pamoja na kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza, zoezi la kura ya maoni limekwenda vizuri na kwa usahihi. Mchakato wote wa uchaguzi ulifanyika vizuri na kwa ufanisi. Kwa hivyo, Kura ya Maoni ilifikia katika viwango vya kutoshelezwa kiutwa Uchaguzi huru na wa Haki.
……………………………………………………………….
MUHIDDIN ZUBEIR MUHIDDN
KIONGOZI WA WAANGALIZI
Download version:





3 Comments on "Waangalizi:Ripoti ya JUMAZA"
Assalam Alaykum Warahmatuh llah Wabarakatuh,
Nimefurahishwa saana na Ripoti iliyotolewa na JUMUIYA YA MAIMAMU ZANZIBAR JUMAZA (JUMAZ OBSERVER GROUP).
Hii ni kuonyesha kuwa Asasi kam hizi za Kidini ndivyo zinavyohitajika kuwa mbele zaidi katika kutetea Umoja na Mshikamano wa Waislamu wote na wale waliokuwa sio Waislamu katika nchi yetu ya Zanzibar.
Kwa ujumla JUMAZA pamoja na JUMIKI na Viongozi wake wote wanastahili pongezi kubwa saana katika mchango wao huo wa kuwambele katika mambo yanayoihusu jamii.
Mimi imani yangu kubwa ni kuwa sasa Zanzibar inaingia katika milango ya maendeleo katika nyanja mbali mbali za Uchumi. Elimu na Jamii kwa ujumla.
Mwenyezi Mungu awabariki viongozi wote wa Jumaza, Jumiki pamoja na Taasisi nyengine za Kidini.
Zanzibar ni nchi yetu sote na sio ya watu maalumu tushirikiane kuleta maendeleo.
Ripoti ya Jumaza imeandikwa kitaalamu kabisa bila ya kuwepo kwa upendeleo wa aina yoyote ile.
Mwisho napendeleo kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mh Dr Amaan Abeid Amaan Karume, pamoja na Al Hajj Seif Sharif Hamad kwa kuonyesha upendo na uzalendo wa kujali zaidi amani na utulivu katika nchi ya Zanzibar.
Wataalam wa Haki za Binaadamu wanasema, There is no development without implementation of Human Rights.
Tudumishe haki za Binaadamu ili tupate maendeleo ya nchi.
Maasalam
Abdul Rahim.
HII NI RIPOTI ILIO NA HADHI YA KIPEKEE. ILA TU HAMUJATUEKEA HIZO KASORO NDOGO NDOGO AMBAZO MUMEZIONA, ILI KWA UCHAGUZI UJAO ZISIJE ZIKAJITOKEZA TENA.
PIA HAMUJATUWEKEA MAWAZO YENU KWA TUME KUILINDA HESHIMA WALIOJIONESHA KWA WANANCHI NA ULIMWENGU MZIMA KUWA UWEZO WA KUENDESHA UCHAGUZI KWA MISINGI ILIYO HALALI WANAWEZA ILA NI UKIRITIMBA TU WA KISIASA UMEWAZIDI.
@JUMAZA INSHAALLAH MULIPWE KHERI ZISIZO NA MFANO HAPA UNIANI KWA KAZI NGUMU MULIOJITWISHA.
@TUME ZEC, MUSIJE MUKAGEUKA MGEMA, MGEMA AKISIFIWA TEMBO HULITIA……. MUHAKIKISHE UCHAGUZI UJAO WA OCTOBER MUKIHARIBU BASI TUTAKULA NA NYINYI SAHANI MOJA KAMA TUNAVYOULA MSETO HII LEO.
FURAHA YA WAZANZIBAR.
NIMEKUSUDIA DUNIANI NA HUKO AKHERA TUENDAKO. AMMIN