Habari

Tani 700 za unga mbovu Z’bar kuteketezwa Juni 15

Tani 700 za unga mbovu Z’bar kuteketezwa Juni 15

NA MWINYI SADALLAH
18th May 2013
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema unga mbovu uliopo bandari ya Malindi Zanzibar utakuwa umeondolewa ifikapo Juni15, mwaka huu.
Amesema unga huo upatao tani 700 umechelewa kuondoshwa na kuangamizwa kutokana na mvutano kati ya msambazaji na muagiziaji wake.

Akizungumza na wajumbe wa kamati ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi (BLW) inayosimamia ofisi za viongozi wakuu wa Serikali ofisini kwake Migombani, amesema baada ya mazungumzo ya muda mrefu wahusika hao wamekubaliana kushirikiana na serikali zote mbili kuuteketeza.

Hivi karibuni Mawaziri wanaohusika na mazingira wa Zanzibar Fatma Abdulhabib Fereji, Dk. Terezya Huvisa wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Afya Juma Duni Haji, walikutana na kutembelea eneo hilo na kukubaliana juu ya namna ya kuuangamiza.

Kwa upande wao wajumbe wa kamati hiyo mpya ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Saleh Nassor Juma wamewaomba watendaji wa ofisi hiyo kutoa ushirikiano kwa kamati ili iweze kutekeleza majukumu yake vizuri.

Mapema Makamu wa Kwanza wa Rais aliihakikishia kamati hiyo kuipa ushirikiano wa kutosha, ili iweze kufanya vizuri zaidi kama ilivyokuwa kwa kamati iliyopita

Unga wa ngano mbovu tani 780 umeingizwa Zanzibar kutoka nchini Uturuki na mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar, Said Bopar na kuamuriwa kuharibiwa na Bodi ya Chakula na madawa Zanzibar.

CHANZO: NIPASHE
Share: