Tulivyo SiSi
Written by mseto // 06/02/2012 // Habari // 2 Comments
Nipo juu ya anga la watu hawa nnaowatawala. Walinichagua wakidhani ati nawapenda, wakiwa na matumaini kwamba ntawasogezea maendeleo puani kwao. Japo niliwaahidi kufanya hivyo mara tu wakinipa ridhaa yao ya kuwaongoza, hivyo sivyo nilivyofanya. Na sivyo nitakavyofanya. Kwani hapa nilipo mimi kuna yoyote aliyenisogeza? Si mimi mwenyewe, akili zangu, jitihada zangu, na uthubutu wangu wa kutaka niwe nilivyo ndivyo nikawa? Hata wao wanalijua hili, lakini niliwapata wakati mzuri.
Kama kawaida ya wengi wetu akina SiSi, kabla ya kufanya maamuzi ya kuingia kwenye mchezo huu, husoma (si kusomea) namna ya kuwatawala (si kuwaongoza) hawa God’s bits of wood, kama alivyowaita Sembene Ousmane.
Baada ya kuwasoma na kujua lengo lao la muda mfupi, huwapigia chapuo, tukawatilia shadda na madda kwenye hilo na kuwasahaulisha lile lengo lao kuu, la muda mrefu: ubora wa maisha yao na mustakbali mwema wa watoto wao. Huwapigia magoma, tukawahashua, tukawachonoa, tukawagaia khanga mbili-mbili na fulana za rangi zetu SiSi. Huwapandisha magari ya mbavu za mbwa au makarandinga kwa gharama zao wenyewe walizozichanga bila wenyewe kujua, tukawapeleka kijiji hiki na kile, wakidhani ni jumla ya mapenzi yetu kwao. Lakini siri ya tukitakacho imoyoni mwetu.
Na viumbe hivi, hujiambia mara nyingine moyoni mwangu, ni kama kwamba havina viungo vya hisia. Maana vingekuwa na hisia basi vingekwishagundua ujanja huu ambao mara zote SiSi huurudiarudia. Pale nisimamapo jukwaani, nikawanadia uongo wangu huwahurumia masikini hawa kwa waisvyo na uelewa wa jambo lolote katika dunia hii. Na kwa upumbavu wao kila nnapowaambia uongo mkubwa wao ndio hufurahi zaidi, wakanipigia makofi, mbinja na vigelegele.
Mara moja nilisimama nikiwanadia uongo wangu, nikapigwa na butwaa na majibu yao. Niliwauliza: “Eti hawa wajinga wanasema nyie mna shida, eti kweli mna shida nyiye?” “Hatunaaaa…” walinijibu. Nikawauliza tena: “Muna shida?” Hatuna baba hatunaaaaa…!
Jibu likawa lilelile. Kusema kweli katika hali ya kawaida watu hawa hawakupaswa kuulizwa swali kama hili, kwani sura zao na afya za miili yao ziliweza kuandika encyclopedia ya shida na mashaka waliyonayo bila ya midomo yao kutamka chochote kuhusu shida zao. Lakini wajinga ndio waliwao, na SiSi tulilijua hilo.
Mara nyingine kwa kejeli, inda na inadi zetu tuliwapelekea shehena za majembe na mapanga kuzidi kuonesha upendo wetu kwao. Tulifanya hivyo tukijua ndani ya nafsi zetu kwamba kwa vitu hivyo hawataweza kujikwamua kwenye tego ya umaskini tuliyowatia. Kilimo ndani ya nchi hii tulishakiua zamani, kwa khiyari zetu na kwa shinikizo la wakubwa wetu wa magharibi- la kututaka tuwaangamize hawa wanaojiita wakulima ili wasije wakathubutu kushindana nao kwenye soko la dunia. Masikini. Tumewafanyia zaidi ya tulivyoagizwa. Tumewadamirisha na hawajiwezi kwa lolote wala kwa chochote.
Hivyo madhumuni ya kuwapelekea majembe na mapanga si jingine zaidi ya kuwauwa taratibu (killing them softly), tuwaone wafavyo wakicheka. Mijino nje.
Pamoja na kuwadamirisha huko, lau tungetaka tungeweza kuwavuta mkono tukawasaidia alau kwa kiasi kidogo kuweza kujikimu mahitaji yao muhimu. Lakini hatujataka. Na hatutaki. Kwani unadhani SiSi hatuna uwezo wa kuwapatia trekta moja kwa angalau kila eneo fulani, tukawapumzisha kilimo cha kijembe kongoka mpini? Tunao. Basi tu hatutaki. Hatutaki watukaribie kwa chochote. Si kwa mimeremeto ya nyuso zetu dhidi ya unyaufu wa dashibodi zao, wala ulaini wa ngozi zetu dhidi ya ukwaruzi wa magome yao. SiSi ni SiSi na tutaendelea kuwa SiSi, na wao watabaki kuwa wao. SiSi Daima..
Katika anasa zetu, siku moja moja huamua kupaa juu angani, kuyamulika mashaka na matatizo yao, si kwa lengo la kuyatatua, hasha wa kalla. Walakin litatwmainna quluubana. Kufurahisha nyoyo zetu tu. Raha inapozoweleka huwa si raha sana. SiSi ni kawaida kwetu kupita na migari yetu ya kifahari mitaani mwao, tukawapigia vingora ili kuwatanabahisha kwamba tunapita, walioko ndani wakatoka nje, na walio barabarani wakakaa pembeni na mikweche yao kutupisha SiSi, huku wakiulizana: “Nani uyo”? na wakajibiana kwa kubahatisha kwa kumtaja mmoja wetu au mwengine kati ya SiSi. Yoyote awaye, awe ndie au siye, haibadilishi chochote kwenye ufukara wao. Ila wao hawajisumbui kufikiria yote hayo. SiSi haoo tushapita…
Mara nyingine tulipita katika moja ya vijiji tulivyovifukarisha tukawaona wakaazi wake wakiwa na mahando ya maji vichwani na mizigo ya kuni migongoni. Wakatusalimia kwa nyoyo na kubainisha kwa ndimi na kuashiria kwa kutupungia mikono yao iliyochoka na kukosa siha mithili ya fyagio za chooni. SiSi tukawabeza na kuwadharau, tukajifanya hatuwaoni, tukawaachia vumbi jingi nyuma yetu , hatuna habari wala haja ya salam zao. Basi hayo tushayazowea, na si raha tena sana.
Leo tunapita kwa njia za angani. Raha ya huku ni kwamba hakuna anayetupungia mkono zaidi ya hivi vijitoto vya kimaskini vinavyojiliwaza kwa kuruka na kuimba “ndege ya baba… ndege ya baba…” ha ha ha ha ha.. ati ndege ya baba. Maskhara?
Baada ya SiSi kuvipita vitoto hivi, vyovyo huendelea kuendesha maringi yao, au kimsingi kuendeshwa na maringi yao, ingawa wao ndio walijiona na himaya ya uendeshaji. Uendeshaji wao wa maringi ulikuwa ni sawa na ule wa wazazi wao wa kuendesha maisha yao, ilhali ukweli ni kuwa maisha yaliwaendesha wao. Hawakuendesha, waliendeshwa. Na hivyo hawakuishi, waliishiwa. Na hivyo ndivyo tulivyotaka SiSi.
Kumbe matatizo ya viumbe hawa ni mengi kuliko tunavyoyaona tukiwa barabarani na magari yetu. Tukiwa huku angani, tunawaona wanavyolalamika na kulaani kila uchao, ati maisha yamekuwa magumu. Kwani SiSi si tuliwaambia zamani anaeona maisha magumu ahame?
Alfajiri hii mvua na upepo mkali ukivuma, namuona huyu mzee mwenye watoto sita akijaza upepo baiskeli yake tayari kuelekea kwenye mnada wa samaki –kutukana na kutukanwa- ili apate kununua vidagaa vya kwenda chuuza mitaani kujipatia chochote. Ninavyoiona baiskeli yake ni kwamba huko ilikotengenezwa hata makumbusho haionekani tena, ila kwake yeye hii ndiyo rasilimali pekee aliyonayo ya kuendeshea –au kuendeshwa- na maisha yake na wanawe.
Wanawe bado hawajaamka, ingawa hawajalala. Wapo juu ya kitanda chao cha kamba maarufu kwa jina la “teremka n’kaze” wakiwa wamelala watatu-watatu. Usiku huu wa mvua vitanda hivi vimeshahamishwa sehemu tofauti ili kukimbia michirizi ya maji inayovuja kutoka kwenye paa la mabati ya kuungaunga –matangi ya mafuta yaliyopasuliwa, madebe ya samli, mabango ya matangazo ya biashara, na kila kilichofaa kukidhi haja ya paa. Misumari ya paa hili ni mawe na matofali. Bwana mwenye nyumba hii ni mmoja kati ya wale walionijibu kwa makelele na mabinja siku ile: “hatuna shida baba… hatunaaa!.
Baada ya kuiona hali ya hawa, hisia za uzazi na wana zinaniingia. Nawakumbuka watoto wangu siku nyingi hatujaonana, pamoja na kwamba huwa nawapigia simu kila siku na kuzungumza mpaka simu ikaisha chaji- si pesa. Hii ndio raha ya kuwa kama SiSi. Wakati raia zetu waliojaaliwa kumiliki simu wakibipu tu huangalia salio, SiSi hupiga mpaka simu zikaisha chaji.
Basi namkumbuka mwanangu kipenzi Sifadi. Huyu nilimuhamisha nchi miaka mitano iliyopita kwa utovu wake wa nidhamu. Pamoja na kwamba alikuwa mwana mtiifu kwangu, sikupenda maingiliano yake na watoto wa mtaani. Nilimuhisi kashaharibika akili hasa kwa kukaa na wale akina Mbaruku, Fakihi, Rashidi na Hamadi. Mara nyingi alikuwa akija nyumbani huja na kesi kwamba watoto wa fulani wanaumwa, wengine sjui hawendi skuli, mara achukue pesa ende akale kwa mama ntilie. Nilijuwa yeye kama yeye hawezi kuzaa mawazo haya, lakini wale as-habu zake ndio wanaomchafua mawazo. Nilijitahidi kumfahamisha kwamba kila mbuzi hula kutokana na urefu wa kamba yake, ila hakuoneka kulikubali hilo. Adhabu yake ikawa kwenda kuishi Ulaya.
Mwanangu Tule nae hakuwa akifanya vizuri pale International School nilipo nikimlipia dola elfu moja kwa mwezi. Hivyo nae nikachukua moja ya nafasi zilizoletwa kwa wanafunzi wenye vipaji vya juu nikamuingiza kwenda kuendelea masomo yake Malaysia. Wako wapumbavu wachache waliopiga kelele ati mwanangu Tule hakuwa na sifa ya kupewa nafasi ile, lakini kelele za mpangaji zitanikosesha mwenye nyumba kulala?
Na sasa ni wakati wa kwenda ofisini. Sina kubwa sana la kufanya leo, -kama ilivyo kila siku- zaidi ya kuandaa safari ya kisirikali ambayo nitaihalalisha kwa kuiita “ziara ya kudumisha urafiki baina ya nchi hii na Singapore na Ireland ya Kaskazini”. Nikiwa Singapore baada ya kufanya biashara zangu, ntakwenda Kuala Lumpur kabisa kumuona Tule na nimskilize shida zake. Kisha ntamtumia tiketi Tule anifate Belfast ili tupate kuspend time pamoja alau wiki moja.
Nyinyi kama bado mpo nisubirini. Tutaonana kiririni!
UnaPe




2 Comments on "Tulivyo SiSi"
Hongera sana mwandishi, umeeleza hali halisi ya maisha yalivyo baina ya watawala (SiSi) na watawaliwa. Allah ataleta kheri zake na wanyonge nao wapata nguvu na haki zao ikiwa ni pamoja na neema. Haya yatafikiwa kwa kuwakataa SiSi, na kutokubali tena kusema hawana shida hali ya kuwa paka kalala jikoni na ‘hakieleweki’ nyumbani.
Hili ni darasa tosha kwa wale waliokunywa maji ya bendeara, asaa kheir watafunguka bongo zao.
Akina sisi tunasubiri pia mtwambie mnavyotufanyia kule skuli na mahospitali ambako tunadhani bado kunaitwa hospitali au skuli kwa maana ile ile ya wenzetu wanaojaaliwa na viongozi wao.
Shukrani.